Nimepita kwa mara kadhaa eneo la Kawe, mkabala na nyumba mpya za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Pembeni mwa barabara inayoelekea Maringo, karibu na msikiti, kuna uchafu uliorundikwa kwa muda mrefu, hii ni wiki ya pili sasa haujazolewa na unazidi kuongezeka.
Najiuliza, katika kipindi hiki cha mvua, hali hii si hatari kwa afya? Nilitarajia kuona magari ya taka yakipita mitaani mara kwa mara kwa ajili ya kuzoa taka, lakini hali ni tofauti. Ikiwa magari hayo hayawezi kufika mara kwa mara, nashauri mamlaka husika ziweke utaratibu wa kuwa na miundombinu rafiki ya kuhifadhia taka kwenye mitaa na pembezoni mwa barabara, badala ya taka kuachwa wazi.
Miundombinu ya aina hiyo itachochea uwajibikaji kwa wananchi na kusaidia kuondoa tabia ya kurundika taka ovyo katika mazingira. Badala yake, taka zitakuwa zinawekwa kwenye maeneo maalumu, jambo ambalo pia litawarahisishia wazoaji kuziondoa kwa urahisi.
Taka zinapoachwa wazi, hasa katika kipindi hiki cha mvua, huongeza uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko. Aidha, wakati mwingine taka hizo husombwa na maji, hali inayosababisha uchafuzi wa mazingira na kuziba kwa mifereji ya maji.
Pia soma ~ Taka zilizorudikwa kwa muda mrefu eneo la Kawe-mkabala na nyumba mpya za NHC zimeondolewa