Dar es Salaam, 18/11/2021; -NYOTA wa muziki wa Bongo Fleva, Kayumba Asosie almaarufu 'Kayumba' ameachia rasmi Extended Playlist (EP) yake ya kwanza iliyobeba jina la ‘Sweet Pain’.
EP hiyo imebeba ngoma sita za moto ambazo ni ‘Mapenzi Yanauma’, ‘Bombaa Remix ft Nadia Mukami’, ‘Baishoo’, ‘Move On ft Sharara,’ ‘Coco,’ na ‘Nimegonga Remix ft Marioo’.
Akiizungumzia EP hiyo, Kayumba alisema, “Miezi sita (6) iliyopita nilianza na maandalizi ya kuandaa Albamu yangu ya kwanza, lakini nikaona bora nianze kuachia EP na baadae albam. Msanii hawezi kukamilika bila kuwa na EP au albamu na ukiangalia tayari nina nyimbo kadhaa ambazo zinafanya vizuri sokoni, hivyo ni muda sahihi wa mimi kukamalisha ndoto yangu ya kuachia EP”.
Kayumba aliongeza kuwa wakati wa maandalizi alitamani kuona EP inavuka boda na ndio sababu kubwa ya kumshirikisha msanii Nadia Mukami kwenye Bomba Remix. “Niliona Nadia ni mtu sahihi sana kwa kuwa anafanya vizuri nchini kwao Kenya na vilevile haikuwa na ugumu kumpata kwa kuwa mara baada ya kuachia ‘Bomba’, aliipenda na tukawasiliana kupitia mtandao wa Instagram na tutakubaliana namna ya kutengeneza remix ya wimbo huo.
Pamoja na EP hiyo, Kayumba amewataka mashabiki wake wajiandae kwa ujio wa albamu yake ambayo tayari imeshakamilika kwa asilimia tisini (90).
Katika kuipa promo EP yake, Kayumba amesema kutakuwa na mashindano makubwa mawili. Shindano la kwanza ni ‘#BoomplayBaishooChallenge’ itakayoshirikisha mitandao mitatu ya kijamii yani Instagram, Tiktok na Vskit ambapo kupitia mitandao hiyo kila mshiriki atajishindia kiasi cha sh. 500,000.
Shindano la pili ni ‘Sweet Pain EP Stream & win’ kupitia App ya Boomplay ambapo washindi watatu watakaosikiliza EP kwa muda mrefu zaidi watajinyakulia zawadi ya fedha taslim sh.500,000 kwa mshindi wa kwanza, sh. 300,000 kwa mshindi wa pili na sh. 200,000 kwa mshindi wa tatu.
Lakini pia ameongeza kuwa kuanzia jumamosi atafanya ‘Roadshow’ ambapo atazunguka katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kuwaburudisha wakazi wa jiji na nyimbo zilizopo kwenye EP yake na kugawa zawadi mbalimbali kwa mashabiki watakaoweza kuimba nyimbo zake kwa ufasaha.
‘Sweet Pain EP’ inapatikana Boomplay tu kwa sasa ndani ya muda wa wiki mbili ambapo mashabiki wataweza kusikiliza na kupakua nyimbo zote sita buree.
EP hiyo imetayarishwa na maprodyuza tofauti akiwemo: - Manecky, Mafia, T-Touch, Jay Sterio na Mafeeling kwa ushirikiano wa karibu na Boomplay na Uongozi wa Kayumba.
MWISHO