Mzalendo_Mwandamizi
JF-Expert Member
- Dec 12, 2007
- 1,117
- 4,772
Makala ifuatayo imechapishwa katika toleo la wiki hii la jarida la Raia Mwema ikiwa ni majibu kwa makala yangu katika toleo la wiki iliyopita iliyokuwa na kichwa cha habari "Ni Kweli Mashushushu Huhujumu Uchaguzi?" (Bonyeza HAPA kuisoma)."Raia" mmoja aliguswa na makala hiyo na anaijibu kama inavyosomeka hapo chini
Ningeweza kuandika makala nzima kumjibu "raia mwema" huyu lakini nimeonelea bora kuileta hapa barazani.Of course,kazi mashushushu si kuhujumu uchaguzi kama ambavyo kazi ya JWTZ si kujishughulisha na miradi ya uchimbaji dhahabu (refer Meremeta,etc).Kadhalika,kazi ya serikali si kuwaruhusu watu wakwapue fedha za EPA kisha iwasihi warejeshe,na kazi ya Mhariri wa gazeti la serikali Daily News si utabiri wa matokeo ya uchaguzi wakati hata kura hazijapigwa...My point is,suala sio duties and responsibilities za mtu au taasisi ni zipi bali namna zinavyotekelezwa.
Sina tatizo na "raia mwema" huyo kutumia muda wa kutosha kumjadili mtoa hoja badala ya kujadili hoja husika.Ex-US President George Bush aliwahi kusema ukiongea jambo kisha likaafikiwa au kupingwa then lina mantiki kwani lingekuwa la ovyo ovyo nani angepoteza muda japo kulitaja?
Well,nawasilisha hapa where we dare speak openly
Kazi ya mashushushu ni usalama si kuhujumu uchaguzi
Almasi Kajia
Oktoba 20, 2010
RAIA Mwema namba 155 la Oktoba 13-19, 2010 liliandika makala iliyokuwa ikiuliza kama mashushu hutumiwa kuhujumu uchaguzi.
Makala hiyo iliyochapishwa katika safu hii ya Raia Mwema Ughaibuni ya Evarist Chahali anayeishi Uskochi, ilikuwa na kichwa kidogo cha habari "Dk. Slaa aibua madai fikirishi".
Mashushu ambao mwandishi anaulizia kama wanaweza kutumiwa kuhujumu uchaguzi ni maafisa Usalama wa Taifa wa Tanzania na uchaguzi anaozungumzia ni Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 2010.
Katika makala yake, mwandishi ameanza kwa kujisifu kwamba ana ufahamu wa kutosha juu ya Usalama wa Taifa au intelijensia, ameisomea fani ya Usalama wa Kimataifa na kwamba anaijua vizuri Idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania.
Pamoja na sifa, tambo na majigambo yote haya, mwandishi anasema anachojaribu kuandika hakisemeki au hakizungumziki na anasema kwa kutekeleza kile anachotaka kukifanya lazima tujiulize maswali magumu na pengine ya kuogofya.
Napenda niseme kwamba kuanzia mwanzo kabisa katika kupitia makala yote ya mwandishi huyu hakuna chochote alichoandika ambacho hakizungumziki na hakuna swali lolote gumu wala la kuogofya ambalo amelidhihirisha katika makala yake.
Nilichogundua katika makala yake ni kuwa kama huo si mtindo wake wa kuwavutia wasomaji napenda kuamini kwamba yeye ni mshika bango wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ameendeleza tu yale yanayofanywa na chama hicho yasiyofurahisha kila mtu, ni mambo yanayorandana na afanyayo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mgombea urais kupitia chama hicho, Dk. Willibrod Slaa.
Hata hivyo, ameeleza mambo ya msingi sana katika kuthibitisha kwamba amejifunza fani ya usalama wa kimataifa kwa kusema kwamba uimara wa taifa lolote duniani unategemea uimara wa idara yake ya usalama wa taifa na kulegalega kwa mambo katika nchi yoyote duniani kunaashiria upungufu wa idara hiyo.
Lakini katika hali ambayo sikutarajia, mwandishi anakiri kwamba kwa miaka mingi sasa, Idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania ni miongoni mwa idara bora duniani. Hilo pengine lilitokana na maelezo yake kwamba anaifahamu vya kutosha Idara hiyo.
Wapo waandishi wengine ambao wamekuwa wakiandika habari kama hizo, lakini wakiwa na mitazamo inayotofautiana. Jambo ambalo linanishangaza au pengine linanitia shaka katika makala yake ni kama Idara anayoisifu hivyo imekwishakupoteza sifa hizo na kama ni hivyo je, hiyo ndiyo sababu ya yeye kuanza kuwa na shaka kama Idara hiyo sasa inaweza kutumika kuhujumu matokeo ya uchaguzi?
Amesema idara ya usalama wa taifa duniani kote hufanya kazi kwa siri kubwa kabisa na usiri huo ni sehemu ya utekelezaji wa kazi zake. Anasema usiri ni muhimu kabisa na wa lazima katika ukusanyaji wa taarifa nyeti.
Jambo ambalo wasomaji walitakiwa walijue kutoka kwa mwandishi ni ikiwa usiri wa Idara ya Usalama wa Taifa ndio utakaotumika kuhujumu matokeo ya uchaguzi na kama hilo ndio lengo ni kwa nini Idara hiyo ifanye hivyo, kwa kutumiwa na CCM au kwa utashi wake yenyewe?
Mwandishi amezitaja nchi za Uingereza na Marekani kama mifano kwamba mara chache wakuu wa vyombo vya intelijensia huitwa kutoa ufafanuzi kwa mambo yanayohusu usalama wa Taifa wa nchi hizo.
Kwamba aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Central Intelligence Agency (CIA) ya Marekani, George Tennet aliitwa kueleza juu ya ushahidi kwamba Iraki ilikuwa na mipango ya kutengeneza silaha za maangamizi.
Anasema katika nchi hizo mbali na kuondoa katika orodha baadhi ya mambo ambayo ni siri, mabunge yao yana kamati zinazoshughulikia masuala ya usalama na zinawaita viongozi wa idara hizo kutoa ufafanuzi katika masuala yanayohusu intelijensia pale inapokuwa lazima kufanya hivyo.
Suala hili halifanyiki kwa siri anayoizungumzia mwandishi na kama nia yake ingekuwa ni kulifahamu hilo angemuuliza Dk. Slaa ambaye amekuwa mbunge kwa miaka 15 na anafahamu kwamba ipo Kamati ya Bunge ambayo inafanya kazi kama zile zinazofanywa na mabunge ya Uingereza na Marekani.
Amerejea swali lake kama Idara ya Usalama wa Taifa inaweza kutumiwa na CCM kuhujumu uchaguzi na akaunganisha masuala mengine mawili kwamba; hakuna ofisa usalama atakayefurahi na tuhuma za Slaa zikibainika kama ni uongo na Watanzania watakuwa na hofu kama itabainika kwamba tuhuma hizo ni za kweli.
Swali kwamba Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa wapi wakati ukitokea ujambazi wa EPA na je, Idara hiyo ilikuwa ikifanya nini wakati mikataba ya kifisadi ikitokea. Mwandishi anajihami mapema kwa kusema kwamba maswali haya yatazua uhasama kati yake na idara hiyo.
Labda niseme tu kwamba si maofisa wa Idara ya Usalama tu watakaochukia bali Watanzania hawatafurahi kuona tuhuma hizi za Dk. Slaa ambazo ni za uongo zinazidi kuendelezwa na watu wenye hadhi za kisomi kama mwandishi mwenyewe kwa ahadi ambazo nina hakika hazitatimia.
Wananchi wa kawaida ambao wamekwishakuelewa kwamba Chadema ina tabia ya kuzua mambo na ambao wanaamini kwamba nchi hii ina ulinzi wa kutosha, hawawezi kuingiwa na hofu kwa kutegemea tu propaganda za askari wetu kutoka Uskochi.
Ninachotarajia mimi ni kwamba Idara ya Usalama wa Taifa haitamjibu mwandishi. Nililo na uhakika nalo ni kwamba itanyamaza bila kusema chochote kwa kuwa mwandishi mwenyewe amesema kuwa Idara hiyo inafanya kazi zake kwa siri kubwa kabisa.
Ninahisi kwamba mara zote Idara hii inaacha wajinga wajielimishe wenyewe. Swali kwamba Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa wapi wakati ufisadi wa EPA ukitokea sio la msingi bali jambo la muhimu ambalo Mtanzania wa kawaida anaweza kusema ni kwamba suala la EPA limeshughulikiwa sana na Serikali na baadhi ya wahusika wamefikishwa mahakamani.
Naamini kwamba ufisadi si sera ya Serikali wala ya Chama tawala-CCM- na ni vyema ikubalike kwamba, kwa sasa pengine tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, ufisadi ni suala la mtizamo na hulka ya mtu kuliko kuonekana kama mtindo wa maisha wa baadhi ya Watanzania.
Serikali ya Tanzania inazingatia utawala wa sheria na tungejali sana suala la mtu kumiliki vitu kama gari, nyumba nzuri, vitu ambavyo wengine hawana, mtu huyu akaonekana kuwa fisadi, Watanzania wengi wangeishia jela.
Amezungumza mengi ikiwa ni pamoja na ikiwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye shughuli zake si za siri anaonyesha wazi kuipendelea CCM kwa kuingilia majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hali ikoje katika Idara ya Usalama wa Taifa.
Nilijaribu kuhoji pale mwanzo kama mwandishi alikuwa anahisi nini juu ya usiri aliousifia sana, usiri wa Idara ya Usalama wa Taifa, kama usiri huo ndio utatumika kuhujumu matokeo ya uchaguzi.
Kinachojidhihirisha hapa ni kwamba mwandishi anataka Watanzania waamini kwamba Idara ya Usalama wa Taifa kwa kutumia kigezo cha usiri, inaingilia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama alivyofanya Msajili wa Vyama vya siasa kwa nia ya kuhujumu matokeo ya uchaguzi (kama kweli alifanya hivyo).
Inaonekana anaamini kwamba usiri huu ndiyo utakaotumika kukipatia ushindi CCM kwa kuihujumu Chadema.
Lakini kila mtu anajua kwamba kazi ya Idara hiyo kama chombo cha usalama ni kuhakikisha Usalama wa Taifa ambao ni pamoja na uchaguzi kuendeshwa kwa amani, si kuuhujumu.
Inavyoonekana, mwandishi mara zote anaiangalia Idara ya Usalama wa Taifa kama chombo chenye uamuzi wa mwisho kwa kila kitu na anasema kwamba Idara hiyo inamfahamu mmiliki wa Kagoda, ama kwa njia zisizo rasmi au njia rasmi.
Hivi kama kweli kazi za Idara hiyo ni za siri ni vipi itathubutu kutekeleza au hata kama imetekeleza, ieleze wazi kwamba imefanya hivi na hivi kwa watuhumiwa wa aina yoyote, achilia mbali wa Kagoda.
Binafsi nina shaka juu ya uelewa wake wa usalama wa kimataifa na ufahamu wake juu ya Idara hii ambayo anadai ni moja ya idara bora duniani na inayotenda kazi zake kwa usiri.
Ni utaalamu gani anaozungumzia mwandishi unaoweza kutumika kushinikiza Serikali kwa njia zilizo rasmi na zisizo rasmi. Nimejaribu kudadisi kwa wajuzi wa masuala ya Usalama wa Taifa, nikaambiwa kwamba kazi ya idara hiyo duniani kote ni kutoa ushauri na si kushinikiza kama mwandishi anavyotaka tuamini.
Nilitaka kujua kama ameifahamu Idara hiyo vipi kwa kuhadithiwa au pengine alishawahi kuwa mtumishi kwenye chombo hicho nyeti? Kwa yote mawili nilipata jibu moja kwamba hata kama alihadithiwa au alifanya kwenye Idara hiyo, kulingana na kanuni za usiri ambao ameukiri yeye mwenyewe, hawezi kusimama hadharani na kusema kwamba amekuwa mtumishi wa chombo hicho.
Anasema pia kwamba idara ya usalama wa taifa kote duniani ni kama nusu jeshi (paramilitary) na viongozi wake wanaogopwa kupindukia na uamuzi wao hauhojiwi.
Katika udadisi wangu, niliambiwa mambo mawili kwamba kuogopwa kupindukia kunatokana na usiri wa idara zenyewe na nikaamini kwamba usichokijua ni sawa na usiku wa giza.
Kwamba wanaoiogopa idara ni wasioifahamu na anachotaka kusema mwandishi ni kwamba wasomaji waendelee kuiogopa
Idara yao ya Usalama wa Taifa.
Nafikiri hilo si la lazima kwa sababu wananchi wana haki ya kukifahamu chombo ambacho kwanza kinahakikisha kuwa Taifa ni salama na kinatumia kodi za wananchi katika utendaji wake wa kazi wa kila siku. Hakuna sababu ya kukiogopa, ni chombo chao na ambacho kimewekwa kisheria.
Mwandishi ametaka pia wasomaji wake wapime madai fikirishi ya Dk. Slaa ambayo yametolewa kama tuhuma ikiwa hadithi au ni kitu kinachowezekana. Ukiyavulia nguo maji sharti uyakoge na kwa hilo mwandishi haamini kwamba anachosema Dk. Slaa ni hadithi tu, anaamini kwamba ni ukweli ingawa hoja yake imejengwa katika nadharia tu.
CHANZO: Raia Mwema
Ningeweza kuandika makala nzima kumjibu "raia mwema" huyu lakini nimeonelea bora kuileta hapa barazani.Of course,kazi mashushushu si kuhujumu uchaguzi kama ambavyo kazi ya JWTZ si kujishughulisha na miradi ya uchimbaji dhahabu (refer Meremeta,etc).Kadhalika,kazi ya serikali si kuwaruhusu watu wakwapue fedha za EPA kisha iwasihi warejeshe,na kazi ya Mhariri wa gazeti la serikali Daily News si utabiri wa matokeo ya uchaguzi wakati hata kura hazijapigwa...My point is,suala sio duties and responsibilities za mtu au taasisi ni zipi bali namna zinavyotekelezwa.
Sina tatizo na "raia mwema" huyo kutumia muda wa kutosha kumjadili mtoa hoja badala ya kujadili hoja husika.Ex-US President George Bush aliwahi kusema ukiongea jambo kisha likaafikiwa au kupingwa then lina mantiki kwani lingekuwa la ovyo ovyo nani angepoteza muda japo kulitaja?
Well,nawasilisha hapa where we dare speak openly