141 nchi nzima. Genius ni hao tu!?
ZAIDI ya kaunti kumi na sita hazikuwa na mwanafunzi hata mmoja aliyepata alama ya 'A’ (plain) katika matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE).
Miongoni mwa kaunti hizo ni Kakamega, Busia, Meru, Marsabit, Kisumu, Trans Nzoia, Pokot Magharibi, Tharaka Nithi, Turkana, Makueni, Kitui, Taita Taveta, Machakos, Narok, Muranga na Lamu.
Vilevile ilibainika kuwa kaunti mbili pekee ndizo zilikuwa na zaidi ya nusu ya watahiniwa 141 waliopata alama A katika KCSE, na kuwapatia nafasi nzuri ya kupata kozi maarufu zaidi katika vyuo vikuu.
Kaunti hizo mbili za Kiambu na Nairobi zilikuwa na watahiniwa 86 kati ya 141 waliopata A. Kaunti ya Kiambu ilikuwa na watahiniwa 49 na Nairobi 37 waliopata A.
Kulingana na afisa mkuu wa Huduma ya Kutenga Nafasi za Vyuo Vikuu na Vyuo (KUCCPS), Bw John Muraguri, baadhi ya kozi kama udaktari na usanifu majengo, ni maarufu zaidi kwa kuwa ushindani huwa mkubwa.
Hata hivyo, mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC), George Magoha aliondoa hofu hiyo kuwa wenye alama A pekee ndio watapata kozi hizo katika vyuo vikuu.
“Hata wale wenye alama C+ bado wanaweza kufanya kozi hizo zenye ushindani mkubwa,” alisema.
Kaunti nyingine kama Kisii na Nakuru zilikuwa na A sita, Nyandarua (2), Vihiga (1), Embu (2) Migori (1), Kirinyaga (2), Homa Bay (4), Uasin Gishu (3), Nandi(2), Elgeyo Marakwet (1), Nyamira (1) na Bomet (2).
Nyingine ni Nyeri (4), Mombasa (4), Kericho (4) na Bungoma (3).
Lakini wadau wa elimu walipuuza kaunti za Kiambu na Nairobi kutawala katika matokeo hayo na kuwahimiza Wakenya kuangazia matokeo ya jumla ya watahiniwa.