Katika toleo la jana la gazeti hili, tulichapisha habari kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) upo hatarini kufa kibiashara kutokana na nchi ya Kenya kujenga uwanja mkubwa wa ndege wa kimataifa eneo la Holili-Taveta lililo mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Habari hiyo ilimkariri Balozi wa Kenya nchini, Mutinda Mutiso akisema kuwa uwanja huo unaojengwa sambamba na ujenzi wa bandari ya nchi kavu, unatarajiwa kugharimu Sh10 bilioni za Kenya, sawa na Sh180 bilioni za Tanzania.
Katika uchunguzi wake, gazeti hili limebaini kuwa hali ilivyo sasa, watalii na wageni wengi wanaokuja nchini wanapitia katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyata na kutumia magari madogo kuja hapa nchini wakikwepa gharama kubwa za uwanja wa Kia.
Kuna hofu kuwa kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo mpya na wa kisasa wa Holili-Taveta ulio kilomita mbili tu upande wa Kenya kutoka mpaka mwa Tanzania, kutasababisha watalii wanaokuja nchini kutumia uwanja huo kutokana na ukaribu. Wadau mbalimbali wa utalii na biashara katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambayo ni kitovu cha utalii, wametahadharisha Serikali kuwa kukamilika kwa uwanja huo ndio utakuwa kifo cha uwanja wa Kia.
Gazeti hili limegundua kuwa wageni wengi wanaukimbia uwanja wa Kia kutokana na gharama zake na katika sekta nyingine kuwa kubwa, tofauti na Kenya yenye huduma za gharama nafuu, hivyo mgeni anaona bora ashukie Nairobi ili akodi gari na kuja Tanzania kwa gharama ndogo pia.
Kenya imeamua kuipiku Tanzania kutokana na umakini mdogo wa viongozi wa Tanzania katika biashara na inatazamia kuwa wageni wote waliokuwa wanashukia Nairobi sasa watashukia Holili, kwani watatumia dakika 20 kufika Moshi mjini na kuchukua dakika 50 kwenda Arusha, badala ya kutumia saa tano kutoka Nairobi kwa barabara.
Kama hali itakuwa hivyo, Watanzania tujitayarishe kufanya msiba wa kitaifa, kwani uwanja wa Holili-Taveta moja kwa moja utaiua Kia. Wakati tunajiandaa kwa maombolezo, Watanzania tusimtafute mchawi, kwani mchawi ni sisi wenyewe ambao tumeyaacha matatizo ya Kia kuwachefua na kuwafukuza watalii na wageni wengine.
Ikumbukwe kuwa, katikati ya Oktoba mwaka jana Serikali iliwashutumu wafanyakazi na viongozi wa Kia kwa kuhujumu mapato ya uwanja huo na kusababisha hasara kubwa.
Waziri wa masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo, Deodoras Kamala aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa tayari Serikali ilikuwa inafahamu njia wanazotumia kufuja mapato kwa kutotoa stakabadhi za malipo kwa wasafiri walipotaka viza au kupitisha mizigo. Alisema kulikuwapo malalamiko ya muda mrefu kuhusu urasimu na huduma mbovu katika uwanja huo zilizosababisha wasafiri wengi kuukimbia uwanja huo na kutumia viwanja vingine nje ya nchi.
Alisema Serikali ilikuwa imegundua kuwa baadhi ya mambo waliyokuwa wanafanyiwa wasafiri hao, ikiwamo kuwatoza faini ya dola 50 za Marekani abiria waliokuwa hawana chanjo ya Homa ya Manjano (Yellow Fever), yalikuwa yanawakwaza abiria na mashirika ya ndege kwa kiasi kikubwa, hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa viwanja vingine havina masharti hayo.
Alisema kuwa dunia ya leo yenye ushindani, masuala kama ya chanjo ya homa hiyo katika viwanja vya ndege na mipaka yetu lazima yaangaliwe kwa kutumia busara na uzalendo zaidi kuliko taratibu zilizowekwa kama tahadhari tu, ili wageni waone umuhimu wa kurudi Tanzania.
Baada ya angalizo hilo la kiongozi huyo, watawala wetu waliendelea kupiga siasa zisizo na tija pasipo kuchukua hatua, na ndipo viongozi wa Kenya walipofanya uamuzi wa kujenga uwanja mpya karibu na mpaka wetu ili kuchukua na kuwahudumia wageni tuliowafukuza. Kwa kupitia safu hii, sisi tulitimiza wajibu wetu kwa kuishauri Serikali ichukue hatua haraka lakini iliendelea kuweka pamba masikioni.
Tumeacha Uwanja wa KIA ufe kifo cha mende