WAKENYA wanakabiliwa na tisho la kufungwa jela miezi 12 (mwaka mmoja) au kulipa faini ya zaidi ya shilingi milioni 2 za Kenya, sawa na shilingi milioni 40 za Tanzania kwa kukosa la kutomuita Mbunge 'mheshimiwa' endapo mtu anaongea naye nchini humo. Sheria hiyo mpya iliyopendekezwa na wabunge wa Kenya, inalenga kuhakikisha kila kiongozi wa umma anatakiwa kupewa heshima anayostahili na wale watakaokaidi watapatwa na adhabu kali kwa kuvunja sheria hiyo.
Watakaovunja sheria hiyo watapata adhabu kali
Adhabu hiyo itawakuta wale watakaokosa kumpa Rais heshima zake kwa kumuita 'Mtukufu Rais', na kwa upande wa Spika wa bunge, ambaye anapaswa kuitwa 'Mheshimiwa Spika wa bunge'.
Katika mswada huo ambao uliwasilishwa na Mbunge wa bunge hilo, Adan Keynan, jana Alhamisi Aprili 24, mwaka huu, alisema kuwa, umuhimu wa sheria hiyo ni pamoja na kukuza sura ya nchi kwa kuanzisha utaratibu huo ili kuonyesha heshima kwa maafisa wa serikali nchini humo.
"Ni nzuri zaidi kwa lengo la kutoa kigezo cha heshima kwa aajili ya kuwapa maafisa wa serikali sehemu ya kuonyesha picha nzuri ya nchi, na kuwepo kwa mpangilio na maadili mema, '' alisema Keynan. Hata hivyo mzozo kati ya wabunge na magavana ukiendelea kutokota, mswada huo haujapendekeza chochote kuhusu cheo cha magavana ambao ni wakuu wa majimbo na watakavyoitwa kama ilivyopendekezwa mmoja wa wabunge hao.
Ikiwa mswada huo utakuwa sheria, cheo cha Mbunge kitakuwa juu zaidi kuliko cha Gavana, Majaji wa mahakama ya juu, Marais wa zamani na Makamu wa Rais.
Chanzo: FikraPevu