Kesi dhidi ya JamiiForums: Shahidi adai waliomba taarifa za mteja bila kutaja ni kwa mujibu wa sheria gani

Kesi dhidi ya JamiiForums: Shahidi adai waliomba taarifa za mteja bila kutaja ni kwa mujibu wa sheria gani

JamiiForums

JF Official Account
Joined
Nov 9, 2006
Posts
6,229
Reaction score
5,285
Wakuu,

Leo Kesi namba 456 inayowakabili Maxence Melo na Micke William imeendelea tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu mbele ya Hakimu Thomas Simba kwa kusikilizwa Shahidi wa tatu na wa nne katika kesi hii.

Tayari shahidi wa kwanza kwenye kesi hii alishafanyiwa mahojiano na kutoa ushahidi wake. Alikuwa ni kaimu ZCO, Ndg. Ramadhani Kingai (Soma Yaliyojiri katika Kesi namba 456: Jamhuri dhidi ya JamiiForums - Oilcom na Uchakachuaji/Ukwepaji kodi bandarini Dar na pia soma Sehemu ya II: Jamhuri vs JamiiForums kuhusu Oilcom na Uchakachuaji mafuta/Ukwepaji Kodi bandarini Dar

Shahidi wa pili alisikilizwa wiki iliyopita na unaweza kusoma hapa: Kesi namba 456 (Jamhuri vs JamiiForums): Shahidi akiri mshtakiwa namba 2 yupo kimakosa...

Shahidi wa tatu ni ASP Fatuma Kigondo na ana umri wa miaka 46. Anaapishwa kwa kutumia Quran na anaahidi kuongea ukweli mtupu na kumwomba Mungu amsaidie.

Jamhuri inawakilishwa na Wakili Mutalemwa Kishenyi huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili Peter Kibatala na Jebra Kambole.

Wakili Kishenyi: Unafanya kazi gani?

ASP Fatuma: Mimi kwa sasa ni Afisa Kikosi cha Reli(RCO), kabla nilikuwa Mkuu wa Kitengo cha Fraud katika Kanda Maalum Dar.

Wakili Kishenyi: Unakumbuka nini kilichotokea tarehe 23/02/2016?

ASP Fatuma: Tarehe 23/02/2016 niliingia ofisini 1:30 asubuhi na kwenda Morning Call(kikao cha asubuhi), siku hiyo baada ya kutoka kwenye kikao nililetewa barua, kabla ya hapo nilikuwa nafuatilia Kesi ambayo jalada la uchunguzi lilikuwa linahusu taarifa za mtandao kuwa “Hivi ndivyo mafuta yanavyoibiwa” iliyoandikwa katika Jamii Forum.

Hapa Wakili wa Jamhuri anaonekana kutaka kumsahihisha shahidi kuwa ni ‘JamiiForums’.

Wakili wa utetezi anaingilia…

Wakili Kibatala: Naomba wakili asimtajie Shahidi majibu, Shahidi hajasema JamiiForums, kasema JamiiForum.

… Shahidi anakiri kasema Jamii Forum na si Jamii Forums (yenye S mwishoni).


Shahidi anaendelea…

ASP Fatuma: Ili tupate sehemu ya kuanzia kwenye ushahidi wetu, nikaandika barua ya kuomba kupatiwa kumbukumbu Jamii Forum zinazomhusu Expert member wao, Fuhrer.

Wakili Kishenyi: Shutuma zilizoandikwa mtandao wa JF zilielekezwa kwa nani?

ASP Fatuma: Zilielekezwa kwa Kampuni ya Oilcom

Wakili Kishenyi: Mliwaomba nini Jamii Forum?

ASP Fatuma: Tuliomba kumbukumbu za FUHRER na wao watusaidie kumpata na vielelezo vyovyote vinavyoweza kumpata Fuhrer.

Wakili Kishenyi: Nani alisaini barua hiyo kuelekea Jamii Forum?

ASP Fatuma: Ni mimi niliiandika.

Wakili Kishenyi: Unaweza kuitambua barua hiyo? Na ni kitu gani kitakufanya uitambue?

ASP Fatuma: Ndio naweza, ni kwa sahihi yangu na maudhui ya barua yenyewe.

(Shahidi anaonyeshwa kielelezo na Wakili wa Jamhuri)

ASP Fatuma: Hii ndio barua ambayo niliisaini tarehe 23/02/2016.

Wakili wa Jamhuri anaomba Barua hiyo ipokelewe kama kielelezo baada ya upande wa utetezi kutokuwa na pingamizi. Hakimu anaipokea na shahidi anaambiwa na Wakili wa Jamhuri aisome. Ameisoma (content yake haitaambatanishwa hapa kwa sasa).

Wakili Kishenyi: Nani aliipokea barua hii?

ASP Fatuma: Barua hiyo ilipokelewa na Chrispine Muganyizi ambaye aliandika jina lake, tarehe na sahihi.

Wakili Kishenyi: Baada ya kuomba Jamii Forum, lini mlipata majibu yenu?

ASP Fatuma: Mpaka kesi hii inafunguliwa ina maana hawakutoa majibu yaliyoombwa.

Wakili Kishenyi: Mheshimiwa (Hakimu) ni hayo tu, naomba kuishia hapo.

=========

Upande wa Utetezi unapata nafasi ya kuanza kumhoji shahidi… Wakili Kibatala ndiye anaanza:

Wakili Kibatala: Shahidi, ni kweli mnatekeleza wajibu wenu kwa mujibu wa sheria?

ASP Fatuma: Ndio

Wakili Kibatala: Una elimu yoyote ya Sheria?

ASP Fatuma: Nimesoma na nina cheti cha sheria.

Wakili Kibatala: Vyema sana. Inapendeza kuwa na askari mpelelezi mwenye uelewa wa kisheria. Hebu tuambie - Kipelelezi, kati yako na Kingai nani alikuwa juu?

ASP Fatuma: Kwa cheo yeye ni mkubwa.

Wakili Kibatala: Uliarifiwa kwamba Kingai alishakuja kutoa ushahidi katika kesi hii (shahidi namba moja)?

ASP Fatuma: Nasikia

Wakili Kibatala: Uliambiwa kielelezo ulichokitoa, afande Kingai alitoa barua iliyojibiwa na Wanasheria wa Mkurugenzi wa Jamii Forum?

ASP Fatuma: Mimi nimeitwa kuhusu hii barua.

(Kibatala Anatoa barua ambayo ilitumiwa wakati wa kumsikiliza shahidi wa kwanza na hakimu anaipokea).

Wakili Kibatala: Bosi wako alikiri barua ilipokelewa, ofisi yako ilipata?


Shahidi anaangalia barua kwa muda...


ASP Fatuma: Ni kweli, ofisi ilipokea barua(na anaisoma…)
Hii ni barua iliyojibiwa na wakili wa Jamii Forums ambayo iliomba Kifungu gani cha sheria kinachotumika kuomba taarifa na kosa gani limefanywa na mteja wao.

ASP Fatuma: Kwa kumbukumbu zangu, kuna barua mwezi wa nne ambayo ilijibu barua hii.

Wakili Kibatala: Barua yenu ilijibiwa au haikujibiwa?

ASP Fatuma: Ilijibiwa

Wakili Kibatala: Awali ulisema Jamii Forums hawakujibu hii barua lakini baadaye unasema ilijibiwa, mahakama ikuchukulie wewe ni shahidi wa uongo au ukweli?

ASP Fatuma: Wa ukweli.

Wakili Kibatala: Barua hii (ambayo imeletwa mahakamani kama kidhibiti) ilitaja kifungu chochote cha sheria?

ASP Fatuma: Haikutaja

Wakili Kibatala: Unafahamu kutaja Kifungu cha Sheria ndio uhalali wa Polisi unapotokea?

ASP Fatuma: Ndio

Wakili Kibatala: Haya mambo uliyohitaji(mambo matatu), unafahamu kama yanaangukia kwenye vifungu tofauti vya sheria?

ASP Fatuma: Sifahamu

Wakili Kibatala: Huyu mtu anaiyeitwa Chrispine Muganyizi, ana nafasi gani Jamii Forums?

ASP Fatuma: Kwa mujibu barua, hakuandika title

Wakili Kibatala: Wewe kama mpelelezi mbobezi, unamfahamu?

ASP Fatuma: Mimi simfahamu.

Wakili Kibatala: Kosa mnalotaka kuchunguza, ni kosa lipi kutokana na kilichoandikwa JamiiForums?

ASP Fatuma: Kosa linabainishwa baada ya kufungua jalada la uchunguzi.

Wakili Kibatala: Kosa ni nini? Kwa hiyo mpaka mnafungua jalada mlikuwa hamjuhi kosa?

ASP Fatuma: Tulikuwa tunachunguza Preliminary investigation.

Wakili Kibatala: Kosa gani?

ASP Fatuma: Kosa ndio hilo jalada la uchunguzi. Kosa linakuja baada ya kuchunguza.

Wakili Kibatala: Taarifa zilizoandikwa na huyo Fuhrer (JF expert member) Ni za kweli au sio kweli?

ASP Fatuma: Mimi nilifungua jalada la hii kesi na wala sio mpelelezi.

Wakili Kibatala: Bado mpaka leo taarifa zinachunguzwa?

ASP Fatuma: Nilihama mwezi Mei mwaka jana.

Wakili Kibatala: Mpaka unahama, bado mlikuwa hamjajua kosa linalochunguzwa?

ASP Fatuma: Niliacha uchunguzi ukiendelea.

Wakili Kibatala: Unaifahamu nchi inaitwa Brunei mji wake mkuu ni Dar es Salaam?

ASP Fatuma: Siifahamu

Wakili Kibatala: Barua yako imesema Dar es Salaam ipo nchi gani?

ASP Fatuma: Jeshi la Polisi lipo hapa Tanzania, ndilo liliandika barua.

Wakili Kibatala: Sio kwenye barua, kwenye post aliandika Dar es Salaam inayoibiwa mafuta, kuliandikwa ni ya nchi gani?

ASP Fatuma: Alisema Tanzania.

Wakili Kibatala: Wapi imeandikwa kwenye barua yako? Msomee hakimu hiyo Dar es Salaam ni ya nchi gani ilipoandikwa kwenye barua yenu!

ASP Fatuma: Oilcom iko Tanzania

Wakili Kibatala: Ni wapi kwenye post wameandika ni Dar es Salaam ya Tanzania?

ASP Fatuma: Haipo.

Wakili Kibatala: Hii kampuni ya Oilcom ya Tanzania, unafahamu imesajiliwaje?

ASP Fatuma: Sifahamu

Wakili Kibatala: Ulifuatilia bandarini ukweli wa tuhuma zilizoandikwa JamiiForums?

ASP Fatuma: Sikwenda (kwa sababu Mimi sio mpelelezi)

Wakili Kibatala: Content zake za hiyo post iliyokuwa JamiiForums unazifahamu?

ASP Fatuma: Kwa wakati huo niliziona, kwa sasa sifahamu.

Wakili Kibatala: Leo huwezi kuzitolea ushahidi mahakamani? Mlipopeleka hiyo barua kwa JamiiForums mliprint content za mjadala husika na kuambatanisha na barua yenu?

ASP Fatuma: Sikumbuki, hatukuweka

Wakili Kibatala: Mpaka unaondoka, ulikuwa unajua wazi kuwa JamiiForums wana taarifa ulizoomba?

ASP Fatuma: Ndio

Wakili Kibatala: Nini kilikufahamisha? Au unahisi tu?

ASP Fatuma: Kwa uelewa wangu mdogo, nilijua wanafahamu, mtu anaweza kuacha namba za simu, email n.k. Kwa hilo nafahamu.

Wakili Kibatala: Unafahamu hatua (steps) anazofuata mtu mpaka anajisajili katika JamiiForums?

ASP Fatuma: Sifahamu.

Wakili Kibatala: Mlichukua hatua gani nyingine kumfikia FUHRER

ASP Fatuma: Mimi nilihama na sikuwa mpelelezi.

Wakili Kibatala: Mpaka unahama, ulichukua hatua yoyote kumfahamu FUHRER?

ASP Fatuma: Mimi sikuchukua hatua yoyote(kwa sababu sikuwa mpelelezi)

Wakili Kibatala: Hii barua ilielekezwa kwa nani?

ASP Fatuma: Mkurugenzi Mkuu.

Wakili Kibatala: Ni nani hasa? (Maana naona washtakiwa wawili)

ASP Fatuma: Simfahamu

Wakili Kibatala: Mpaka unatoa ushahidi, ulifanya chochote kujua Maxence Melo na mwenzake wana uhusiano gani na hicho cheo?

ASP Fatuma: Sikufanya

Wakili Kibatala: Kwa ufahamu wako, Je, kuna kesi yoyote iliyowahi kufunguliwa na Oilcom dhidi ya JamiiForums inayolalamikia kuchafuliwa(Defamation)?

ASP Fatuma: Sijui

Wakili Kiabatala: Hapa mahakamani umetoa uthibitisho wowote kwamba haya yaliandikwa katika JamiiForums?

ASP Fatuma: Binafsi sijatoa

Wakili Peter Kibatala anaamua kuachia hapo, anamwachia mwenzake Jebra Kambole ili aulize maswali machache…

=========


Wakili Jebra: Unakubaliana na Mimi kwamba barua yako haukuomba taarifa husika chini ya sheria ya Makosa ya Mtandao?

ASP Fatuma: Sio kweli (baada ya kubanwa anakubali kuwa barua yake haikuwa imetaja sheria yoyote, hivyo ni kweli hakuomba kwa mujibu wa sheria yoyote).

Wakili Jebra: Barua uliyoandika kwenda Jamii Forum ilikuwa ni OMBI au ni AMRI?

ASP Fatuma: Ilikuwa ni amri.

Wakili Jebra: Chini ya sheria ipi?

ASP Fatuma: Kuhusu sheria gani tulitoa kwenye barua ya pili.

Wakili Jebra: Haipo Kama kielelezo mahakamani kama kielelezo (Hakimu anaingilia na kusema hiyo barua anayoitaja shahidi haipo na haihesabiki kama kielelezo hivyo haihusiki)

ASP Fatuma: Kama ni hiyo barua (iliyo mahakamani kama kielelezo), ilikuwa ni ombi.

Wakili wa Jamburi, Mutalemwa Kishenyi anapewa nafasi ya mwisho kumwongoza tena shahidi:

Wakili Kishenyi: Wakili Kibatala alitaka uonyeshe post, wakili alikuonyesha post yenyewe?

ASP Fatuma: Hajanionyesha

Wakili Kishenyi: Mheshimiwa (Hakimu) ni hayo tu.

ASP Fatuma Kigondo amemaliza kutoa ushahidi na anaruhusiwa kuondoka… Shahidi wa Pili anaitwa.
 
Ndio maana Polisi na hata viongozi huwa wanaagiza washukiwe wanaotofautiana nao kisiasa wapigwe na kudhalilishwa na polisi kwani eti washitakiwa huwa wanajua sheria hivyo wakipelekwa watashinda kesi.

Kwahiyo namna pekee ni kuwajeruhi na kuwadhalilisha hata wakishinda kesi wawe wamedhalilika.

Huo udhaifu wa vyombo vya dola unajionyesha wazi so kipigo kwa watuhumiwa huchukuliwa kama njia sahihi ya kuadhibu watuhumiwa mbele ya Polisi kwani huko mahakamani Polisi hugeuka vituko.
 
Particulars of any charge must disclose essential ingredients of offence - It is now trite law that the particulars of the charge shall disclose the essential elements or ingredients of the offence.

This requirement hinges on the basic rules of criminal law and evidence to the effect that the prosecution has to prove that the accused committed the actus reus of the offence charged with the necessary mens rea.

Accordingly, the particulars, in order to give the accused a fair trial in enabling 3 him to prepare his defence, must allege the essential facts of the offence and any intent specifically required by law.

A charge which did not disclose any offence in the particulars of offence is manifestly wrong and cannot be cured under section 388 of the Criminal Procedure Act, 1985.
 
Hii ni kesi ya kushangazaa sana kwani hawa Polisi wangefanyia kazi ripoti ya mtoa taarifa kwanza na baada ya hapo kama taarifa ni ya uongo ndipo wangechukua hatua nyingine.

Naona nia ya Polisi ni kutaka kujua ID ya members wote wa Jamii Forums hii kesi ina dhumuni kubwa.
 
Aisee Kuna mawakili ukikutana nao mahakamani inakuwa si sehemu nzuri acha kuwa mtuhumiwa, ushahidi tu unaweza kuhenya..
 
Back
Top Bottom