Mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi mmoja, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam,wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe, ameiomba Mahakama Kuu kuamuru zipelekwe silaha ili zifyatuliwe kwenye ukuta wa Posta kwa lengo la kuoanisha matundu yanayodaiwa na upande wa mashitaka kuwa hayakupigwa na risasi za bunduki.
Ukuta huo ndiyo sehemu ambayo Zombe na wenzake wanadai kuwa kulitokea mapambano ya kujibishana risasi kati yao na wafanyabiashara waliouawa.
Zombe alitoa madai hayo eneo la Sinza, jijini Dar es Salam baada ya Mahakama hiyo kuhamishia shughuli zake katika maeneo yanayodaiwa kuuawa marehemu hao ikiwemo Barabara ya Sam Nojuma, msitu wa Pande na Bunju jijini Dar es Salaam.
Zombe alidai kuwa yeye ni mtaalamu wa silaha hivyo matundu yanayoonekana ni ya risasi na kama hawaamini basi zipelekwe SMG zifyatuliwe na matundu yatakayotokea yalinga nishwe na yaliyopo ili kuthibitisha kama yale yanayoonekana yanaweza kuwa ya risasi au la.
``Huu ukuta ni wa zege hivyo risasi haiwezi kupenya moja kwa moja na kama hamuamini waitwe askari wa kikosi cha kupambana na uhalifu hapa wafyatue risasi ili tuone na kuhakikisha kama matundu ni ya risasi au la,`` alidai Zombe.
Hata hivyo, ombi hilo la Zombe lilikataliwa na Jaji Kiongozi Salum Massati, ambaye alisema hakuna haja ya kufanya hivyo na kwamba risasi hizo zitawashtua wanananchi.
Msafara huo ambao ulikuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ulikopita, uliondoka Mahakama Kuu majira ya saa 4: 30 asubuhi ukiwa na magari zaidi ya 20, huku ukiongozwa na magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser zilizokuwa na askari magereza na ving`ora.
Pia kulikuwa na Land Rover Defender nyingine mbili zikiwa na askari kanzu waliosheheni silaha mbalimbali.
Zombe na baadhi ya washtakiwa wenzake walipandishwa kwenye Defender namba STK 1029 na washitakiwa wengine walipanda gari lenye namba STK 1695.
Msafara huo, ulipofika eneo la Sinza C saa 4:50 ambako inadaiwa ndiko marehemu walikamatwa kabla ya kuuwawa, Jaji Kiongozi Salum Massati anayesikiliza kesi hiyo alianza kuendesha kesi ambapo Shahidi wa 30, Emson Mmari, ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora.
Kamanda Mmari aliongozwa na Wakili wa Serikali, Alexander Mzikila wakati akitoa ushahidi wake hadi saa 5:02.
Sehemu ya mahojiano yao yalikuwa hivi:
Mzikila: Shahidi hapa ni wapi?
Shahidi: Hapa ni Sinza nyumbani kwa Alex Ngonyani na Benadetha Lyimo ambao ni shahidi wa kwanza na wa pili katika kesi hii.
Mzikila: Nini madhumuni yenu kuja hapa?
Shahidi: Kupata maelezo kwa Benadetha kama kweli marehemu alikuwa akileta fedha hapa.
Mzikila: Nyumba gani marehemu walipeleka fedha?
Shahidi: Ndiyo hii (wakati huo mahakama ilikuwa nje ya nyumba ya Benadetha).
Mzikila: Gari ya marehemu ilipaki eneo gani?
Shahidi: Ilipaki ng'ambo ya nyumba hii.
Mzikila: Shahidi ulieleza mahakama kuwa kulikuwa na gari ya polisi, je uliambiwa zilikuwa upande gani kwa hapa?
Shahidi: Gari ya ilikuwa imezuia gari waliyokuwanayo marehemu kwa mbele na ilikuja gari ya Bageni kadhalika mshitakiwa wa tatu Ahmed Makelle alikuwa na gari pia. Gari la Polisi Chuo Kikuu lilikuwa linaendeshwa na Koplo Nyangerela ambaye ni mshitakiwa wa tano.
Baada hapo mahakama ilihamishia shughuli zaka eneo la barabara ya Sam Nujoma, ambapo ilikuwa saa 5:02 hadi 5:10 asubuhi na baada ya kufika mahojiano yalikuwa hivi:-
Mzikila: Hapa ni wapi?
Shahidi: Ni barabara ya Sam Nujoma, eneo ambalo tuliambiwa lilitokea tukio la uporaji wa fedha za kampuni ya Bidco.
Mzikila: Ni gari gani ilikuwa imeporwa fedha hzio?
Shahidi: Mercedis Benz mali ya kampuni hiyo.
Mzikila: Nani aliwaongoza katika maeneo haya?
Shahidi: Ni Sajini Nikobai ambaye aliwahi kuwa katika timu ya upepelezi ya kwanza kabla Rais hajaunda tume.
Mzikila: Kuna mabadiliko makubwa katika barabara hii, ni kitu gani kinakuonyesha kuwa ni hapa?
Shahidi: Kuna alama ya eneo la Konoike ya zamani na ndio sababu ninapakumbuka vizuri.
Mzikila: Baada ya hapa mlikwenda eneo gani kama timu ya wapelelezi?
Shahidi: Tulikwenda eneo la ukuta wa Posta kunakodaiwa marehemu walipambana na polisi na kuuawa.
Saa 5:16 hadi 5:20 asubuhi msafara wa mahakama ulihamia eneo la ukuta wa Posta.
Mzikila: Hapa ni wapi?
Shahidi: Mtukufu Jaji huu ni ukuta wa Posta niliosema.
Mzikila: Hayo matundu uliyosema yako wapi?
Shahidi: Haya hapa tuliambiwa yamepigwa kwa bunduki aina ya SMG (alionyesha matundu yaliyokuwa katika ukuta huo).
Mzikila: Je, mlifanikiwa kuwahoji watu?
Shahidi: Ndiyo, kwenye gereji hii hapo ng`ambo ya ukuta na mmikili wake namkumbuka kwa jina la Mzuri.
Mzikila: Kuna umbali gani kati ya ukuta na gereji? Piga hatua tujue.
Shahidi alipiga hatua kutoka kwenye ukuta hadi ilipo gereji huku Zombe akihesabu ambapo kulikuwa na umbali wa hatua 15.
Mzikila: Urefu wa ukuta wa Posta ni mita ngapi?
Shahidi: Ni mita mbili.
Mzikila:Nani mwingine mlimhoji?
Shahidi: Muuza maji ambaye alikuwa umbali wa hatua 35 kutoka kwenye ukuta wa Posta.
Mzikila: Madhumuni ya kuwahoji waliokuwa eneo hili ni nini?
Shahidi: Kama walisikia milio ya risasi Januari 14, 2006, ambapo walituambia mimi na timu ya wapelelezi wenzangu kuwa hawakuwahi kusikia.
Mzikila: Nini kiliwafanya mje eneo hili?
Shahidi: Bageni alidai kulikuwa na kutupiana risasi kati ya waliodaiwa kuwa majambazi na polisi.
Mzikila: Katika uchunguzi wenu, polisi walijeruhiwa katika tukio hilo?
Shahidi: Polisi hawakujeruhiwa.
Baada ya mahojiano hayo msafara huo ilianza safari ya kuelekea Mbezi Luis msitu wa Pande saa 5.48 eneo hilo liko kilomita 21 kutoka Ubungo, jijini Dar es Saalaam.
Baada ya msafara huo kufika Mbezi Mwisho watu walikuwa wamejipanga pembeni ya barabara kana kwamba wanasubiri mapokezi ya Rais.
Watu hao walisikika wakisema kuwa yametimia hakuna aliye juu ya sheria, sheria ni msumeno. Sheria msumeno, Sheria msumeno, hakuna aliye juu ya Sheria, waandishi andikeni watu wajue kinachoendelea.
Msafara huo ulifika Pande majira ya saa 6:28 na mara moja mahakama ilianza shughuli zake na mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo.
Mzikila: Shahidi unaweza kutueleza hapa ni mahali gani.
Shahidi: Msitu wa serikali wa Pande.
Mzikila. Nani alikuelekeza hapa?
Shahidi: Mshtakiwa wa 11 PC Rashid.
Mzikila: Lengo la kuja huku ilikuwa nini?
Shahidi: Tulikuja hapa baada ya mshtakiwa wa 11 katika kesi hii Rashid kutueleza kuwa kule Sinza inakodaiwa kuwa wale wafanyabiashara waliuawa si kweli na alisema waliuawa hapa.
Mzikila: Alikueleza waliuawaje?
Shahidi: Alisema walikuwa wakiteremshwa kutoka kwenye gari na kulazwa kifudifudi kisha walipigwa risasi na Koplo Saad.
Mzikila: Eneo hili mlikuta nini?
Shahidi: Tulikuta damu tukaichukua na kuipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi ili kujua kama ni ya binadamu au mnyama.
Mzikila: Zaidi ya damu nini kingine mliona?
Shahidi: Maganda mawili ya risasi na tulipiga picha eneo zima la tukio.
Mzikila: Huyo aliyewaleta aliwaambia nini kuhusu maiti.
Shahidi: Hatukuzikuta, lakini alisema walizipeleka hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mzikila: Baada ya hapa mlienda wapi.
Shahidi: Bunju
Mzikila: Mlienda siku gani.
Shahidi: Siku hiyo hiyo Machi 7.
Baada ya mahojiano hayo, Zombe alisikika akidai kuwa hajawahi kufika eneo hilo la Pande na labda vijana wake ndio wanaopajua.
Hata hivyo, mshtakiwa wa 11 kwenye kesi hiyo, Rashid Lema, alimjibu Zombe kwa jazba akimtaka aeleze vizuri namna walivyosherehekea baada ya kufanya mauaji hayo.
Baada ya majibu hayo ya Rashid, Zombe alikaa kimya na kuingia ndani ya gari na safari ya kuelekea Bunju ilianza.
Mahojiano ya Bunju yalikuwa hivi:
Mzikila: Shahidi tueleze hapa ni wapi
Shahidi: Bunju machimbo ya mchanga
Mzikila: Nani aliwaongoza hadi eneo hili.
Shahidi: Mshitakiwa wa 11 Rashid Lema.
Mzikila: Aliwaeleza madhumuni ya kuja huku ni nini?
Shahidi: Alisema walielekezwa na Bageni (mshtakiwa wa pili) waje kufyatua risasi yeye (Rashid) afyatue tatu na Saad ambaye hajakamatwa hadi sasa alitakiwa kufyatua sita.
Shahidi: Tulipiga picha na kuchora ramani ila hatukupata maganda ya risasi kwa kuwa walishayachukua na kumpelekea Bageni.
Mzikila: Rashid alikueleza huku walikuja na nani?
Shahidi: Alikuwa na dereva, Rajabu na Koplo Saad.
Baada ya maelezo hayo, Jaji Kiongozi Salum Massati aliahirisha kesi hiyo hadi leo asubuhi ili Mmari kuendelea kutoa ushahidi wake.
Mbali na Zombe na Bageni, washtakiwa wengine ni Ahmed Makelle, Jane Andrew, Noel, Nyangerera, Imanuel Mabula, Felix Cedrick, Rashid, Rajabu Hamis na Abeneth.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Januari 14 mwaka 2006, katika msitu wa Pande Mbezi Luis waliwaua kwa kuwapiga risasi Ephraem Chigumbi, Sabinus Chigumbi, Mathias Lukombe na Juma Ndugu