‘Muro na wenzake wana kesi ya kujibu' Send to a friend Tuesday, 08 March 2011 20:25
Tausi Ally
JERRY Muro na wenzake Edmund Kapama na Deogratias Mgasa wamepatikana na kesi ya kujibu katika mashtaka matatu yanayowakabili likiwemo la kuomba rushwa ya Sh 10 milioni kutoka kwa Mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Kalori.
Mashtaka mengine yanayowakabili washtakiwa hao ni kula njama, na kujitambulisha kuwa wao ni maofisa wa serikali.
Uamuzi huo, ulitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, Gabriel Mirumbe Mara baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Boniface Stanslaus kufunga ushahidi wao wa upande wa mashtaka.
Stanslaus alifunga ushahidi wa upande wa mashtaka mara baada ya mashahidi sita kati ya 11 waliotarajiwa kutoa ushahidi dhidi ya kesi hiyo, kutoa ushahidi wao.
Akitoa uamuzi kama Muro na wenzake wana kesi ya kujibu au la, Hakimu Mirumbe alisema baada ya kupitia vielelezo na ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa mashtaka washtakiwa wote wana kesi ya kujibu hivyo watatakiwa watoe utetezi wao.
Baada ya hakimu Mirumbe kutoa uamuzi huo, mawakili wa utetezi, Richard Rweyongeza, Majura Magafu na Pascal Kamala waliiomba mahakamani iruhusu wateja wao waanze kujitetea Machi 29, mwaka huu, kuanzia saa 4:00 asubuhi.
Hakimu Mirumbe alikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Machi 29, mwaka huu, Muro na wanzake watakapoanza kutoa utetezi wao dhidi ya mashtaka hayo yanayowakabili.
Wakili huyo wa Serikali Mkuu alifunga ushahidi wao mara baada ya shahidi wa sita, Koplo Lugano Mwampeta (32) kumaliza kutoa ushahidi wake dhidi ya kesi hiyo.
Akitoa ushahidi, Mwampeta alidai kuwa Januari 31,2010 nyakati za jioni akiwa ofisini kwake, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Duwan Nyanda alimpa kazi ya kumsaidia kupekua gari la Muro.
Mwampeta alidai baada ya kupewa kazi hiyo, yeye na Nyanda walilipekuwa gari la Muro na kuwa walifanikiwa kupata miwani na pingu.
Aliongeza kudai kuwa wakati upekuzi huo ukiendelea kufanyika Muro alikuwepo na kwamba yeye mwenyewe kwa hiari yake alimkabidhi silaha aina ya Bastola na magazini inayobeba risasi 10.
Alidai Muro alikuwa ameiweka silaha hiyo kiunoni mwake na kwamba alipomkabidhi alizihifadhi kiofisi.
Hata hivyo shahidi huyo aliiomba mahakama ipokee vitu hivyo kama sehemu ya vielelezo vya ushahidi katika kesi hiyo na mahakama ilikubali baada ya upande wa utetezi kutokuwa na pingamizi navyo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Boniface Stanslaus kutoa ushahidi wake, Mwampeta aliongeza kudai kuwa Februari 2, mwaka jana alichukua maelezo ya onyo kutoka kwa Muro na kwamba katika maelezo hayo, alikana kumtambua mlalamikaji katika kesi hiyo, Michael Kalori.
Muro ambaye ni mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha TBC1 na wenzake Edmund Kapama, maarufu kama ‘Doctor' pamoja na Deogratias Mgasa ambaye anajulikana kama Musa walipandishwa kizimbani Mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 5, mwaka huu.
Awali wakili Stanslaus akishirikiana na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincoln, alidai kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hayo Januari 29, mwaka jana.
Wakili Stanslaus alidai kuwa washtakiwa hao pamoja na wenzao wengine ambao hata hivyo hawajafikishwa mahakamani walitenda makosa hayo ya kula njama na kuomba rushwa kinyume cha kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.
Stanslaus alidai kuwa Muro aliomba rushwa hiyo kutoka kwa Wage katika hoteli ya Sea Cliff Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ili asimtangaze habari zake zinazohusiana na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Aliongeza kuwa siku hiyo hiyo ya tukio washtakiwa Edmund Kapama na Deogratias Mgasa walijipachika nyadhifa zisizokuwa zao kwa kumlaghai Karoli kuwa wao ni maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakati wakijua ni uongo.
Washtakiwa hao wako nje kwa dhamana baada ya kila mmoja wao kusaini bondi ya Sh 5 milioni pamoja na wadhamini wao wawili kwa kila mmoja.
Comments
0
#3 josephjoel 2011-03-09 15:28 Bwana Jerry Muro,usifanyie masihara hiyo kesi ni kitanzi kwako.Ingia magotin kwa mungu umwite atakuitikia.
Quote
0
#2 josephjoel 2011-03-09 15:23 Bw.Jerry hiyo kesi usifanyie masihara itakupoteza.Inabidi uombe sana mungu akusaidie uepuke na kesi hiyo.
Quote
0
#1 mekaki 2011-03-09 13:25 sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa watangazaji wengine
Quote