Mhasibu amkandamiza Prof Mahalu mahakamani (Mwananchi)
Na Tausi Ally
ALIYEKUWA Mhasibu katika Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, Stewart Migwano (47), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam namna alivyoandaa hati ya Euro 3,098,741.40 kwa ajili ya maalipo ya ununuzi wa Jengo la Ubalozi nchini humo.
Hayo aliyasema jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Sivangilwa Mwangesi wakati akitoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na aliyekuwa Afisa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania uliopo nchini Itali, Grace Martin.
Akitoa ushahidi huo, Migwano alidai kuwa alipokuwa Mhasibu nchini Italia kuanzia Julai 2001 hadi Januari 2007, alikuwa akifanya kazi ya kuandaa maalipo na kupokea fedha zote za maduhuli (mapato) na kwamba alikuwa akifanya kazi hizo kupitia maelekezo aliyokuwa akipewa na aliyekuwa Grace Martin.
Alidai kuwa anafahamu kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa Euro 3,098,741.40 na kwamba aliandaa hati ya maalipo ya ununuji wa Jengo hilo la Ubalozi nchini Italia na kuisaini baada ya kupata barua iliyomuelekeza kufanya hivyo.
Alidai kuwa fedha hizo za ununuzi wa jengo hilo zilitumwa kwa awamu tatu tofauti, za awamu ya kwanza zilitumwa Machi 2002, awamu ya pili Julai 2002 na za awamu ya tatu zilitumwa Agosti 2002.
Alidai zaidi kuwa Septemba 24, 200, Serikali ya Tanzania ilituma Euro 2,065,827.60 kwenda Monaco na Euro 1, 320,913.80 kwenda kampuni ya Ceres inayoendeshwa na Fioreolla Pegliuca kwa ajili ya ununuzi wa jengo hilo na kwamba zote zilifika katika kampuni husika.
Baada ya maelezo hayo, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), Abubakar Msangi alimhoji Migwano kuwa wakati wanafanya mauziano ya jengo hilo kuna mkataba wowote aliyowahi kuuona.
Migwano alijibu kuwa mpaka wanafanya maalipo ya ununuzi wa jengo hilo hakuwahi kuuona mkataba wowote bali ulikuwa unashughulikiwa.
Msangi alimhoji shahidi huyo, kuwa kulikuwa na haraka gani ya kufanya maalipo ya ununuzi kabla ya mkataba.
Naye alisema hafahamu kwanini ilikuwa hivyo na kuongeza kwamba aliwahi kuona barua kwenye mafaili ikidai kuwa taratibu zote za ununuzi wa jengo hilo zimekwisha kamilika bado kusaini mkataba.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuhujumu uchumi kwa kuisababishia hasara serikali ya Euro 2,065,827.60 wakati wakiwa maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Itali.
Ilidai kuwa Septemba 23 mwaka 2002 katika ubalozi wa Italia jijini Roma, washitakiwa wakiwa waajiriwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walisaini vocha yenye namba D2/9/23/9/02 ikionyesha kuwa bei ya ununuzi wa jengo hilo kuwa ni Euro 3,098,741.58 maelezo ambayo yanadaiwa kuwa ni ya uongo na yenye nia ya kumdanganya mwajiri wao.
Katika shtaka la tatu wanadaiwa kuwa Oktoba Mosi, 2002 washitakiwa hao kwa pamoja wakiwa waajiriwa wa serikali kwa pamoja walisaini mkataba wa mauzo na shitaka la nne, wanadaiwa kuwa Oktoba Mosi, 2002, walitumia hati ya malipo ya Euro 3,098,741.58 kwa maelezo kuwa muuzaji wa jengo la ubalozi mjini Rome alipokea fedha hizo huku wakijua kwamba ni uongo.
Katika shitaka la tano, wanadaiwa kuwa Oktoba Mosi, 2002 katika Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, washitakiwa hao kwa pamoja waliiba euro 2,065,827.60 ambazo zilikuwa mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.