Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
KHITMA YA IDDI SIMBA ILIPOMREJESHA MUFTI SHEIKH HASSAN BIN AMEIR KATIKA FIKRA
Inaweza sasa kufika zaidi ya miaka 30 siku tulipokuwa tumesimama nje ya Msikiti wa Manyema tukizungumza historia ya masheikh waliokuwa wametangulia mbele ya haki na hapo mimi nikamtaja Sheikh Hassan bin Ameir kama, ‘’Sheikh Mwanasiasa,’’ na nikaanza kueleza mchango wake katika historia ya TANU, uhusiano wake na Abdul Sykes, Dossa Aziz, Nyerere na masheikh wengine wa wakati wake na jinsi alivyowaongoza Waislam wa Tanganyika katika kupigania uhuru wa Tanganyika ndani ya chama cha TANU katika njia ambayo haikuwatia unyonge waumini wa dini nyingine.
Hapo hapo marehemu Sheikh Ali Mzee Comorian akanikatiza akasema, ‘’Sheikh Hassan bin Ameir hakupata kuwa mwanasiasa yeye alikuwa sheikh mkubwa tu.’’
Sikuendelea zaidi na lile ambalo nilikusudia kulieleza kuwa Abdul Sykes mwaka wa 1950 akiwa kijana wa umri wa miaka 26 alimtia Sheikh Hassan bin Ameir na Sheikh Said Chaurembo katika siasa za TAA kwa nia ya kukitia nguvu chama.
Sikuweza kuendelea zaidi nikapingana na Sheikh Ali kwani ingekuwa utovu mkubwa wa adabu kwangu mimi kwa kuwa yeye sote tuliokuwa pale wakubwa na wadogo tukimheshimu kwa elimu aliyokuwanayo katika dini na isitoshe baba yake, Sheikh Mzee Ali Comorian alikuwa kati ya wanafunzi wakubwa wa Shekh Hassan bin Ameir.
Nikabakia kimya.
Jana katika khitma ya Iddi Simba Msikiti wa Manyema watu wengi walipata faida ya kusikia makubwa aliyofanya Iddi Simba kwa siri bila ya kutangaza katika kuusukuma mbele Uislam.
Iddi Simba alifanya haya akitumia fedha zake na muda wake mwingi na wakati mwingine akiwachukua masheikh katika ‘’retreats’’ katika mahoteli makubwa ili papatikane utulivu wa kufikiri na kujadili.
Wakati mwingine ilipobidi alisafiri na kundi la masheikh wakubwa ndani na nje ya Tanzania kwenda kufanya kazi za kuujenga Uislam na maendeleo ya Waislam na kutatua matatizo yaliyokuwapo baina ya viongozi wa Kiislam.
Yote haya akiyafanya kimya kimya.
Sheikh Khamis Mataka alieleza wasifu wa Iddi Simba na kazi alizofanya nchi nzima katika kuwaunganisha masheikh na wasomi wengine wa Kiislam na tija kubwa iliyopatikana hasa katika miji ambayo palikuwa na mikinzano katika misimamo ya mambo kadhaa ambayo yalihitaji mazungumzo kutatua.
Msikiti ulikuwa kimya na baridi watu wakisikia yale ambayo hawakuwa wanayajua na kwa wengine wakawa wamepata kujua kuwa kumbe utulivu na staha iliyoingia kimya kimya haikuja hivi hivi bali kulikuwa na mtu aliyeifanyia kazi kupatikana.
Hakuna asiyejua kuwa kwa miaka mingi Waislam waliipiga pande BAKWATA kutokana na historia ya kuundwa kwake.
Mufti Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali alipokuja kumzungumza Iddi Simba alisema kuwa wasomi wa Kiislam wanyanyue kalamu waandike historia za waja wema kama Iddi Simba na kazi walizofanya katika kuutumikia Uislam.
Mufti Sheikh Zubeir labda kwa kuniona pale msikitini akasema, ‘’Mohamed Said yuko hapa ni kazi yake aandike historia ya watu kama hawa na masheikh kama Sheikh Hassan bin Ameir na Sheikh Kassim bin Juma.’’
Mufti akaeleza jinsi Sheikh Ali bin Hemed alipokuja Dar es Salaam mwaka wa 1955 na kumkuta Sheikh Abdallah Chaurembo wakati huo kijana mdogo anasomesha tafsir ya Qur’an.
Sheikh Abdallah Chaurembo alikuwa mmoja wa wanafunzi wakubwa na hodari sana wa Sheikh Hassan bin Ameir Mufti wa wakati ule.
Sheikh Abdallah Chaurembo alikuja kuwa bingwa wa kutafsiri Qur’an na darsa zake Msikiti wa Mtoro zikijaza wasomaji na wasikilizaji.
Mufti Sheikh Zubeir si mtu wa kutupa maneno yake ovyo na kwa hakika katika miaka mingi nyuma ilikuwa kama vile masheikh wakiogopa kutaja jina la Sheikh Hassan bin Ameir na kutaja tarikh yake na sababu ni ile historia yake.
Kwa Mufti kumuunganisha Iddi Simba na Sheikh Hassan bin Ameir katika kupigania Uislam kwa wengi waliokuwa pale hasa wasomi wa Kiislam waliomjua Sheikh Hassan bin Ameir hili halikuwa jambo dogo na ni kitu kipya hasa kwa kuwa alitangulia kwa kumuadhimisha Sheikh Ali bin Hemed wa Tanga ambae wengi wanamuitikadi kuwa ndiye ‘’Sheikh wa Masheikh,’’ yaani mwalimu aliyewasomesha masheikh waliokuja kusomesha wanafunzi wengi waliokuja kuwa masheikh wakubwa katika historia ya Uislam Tanganyika.
Ningependa kuhitimisha kwa maneno ya Sheikh Abu Iddi aliposema kuwa, ‘’Mtu aliyekuwa na nyadhifa kubwa katika serikali, chama na kwengine kwingi na kuwa mtu mkubwa hawezi kudhurika kwa kuwa karibu na masheikh.’’
Kwa maneno haya Abu Iddi alikuwa anasena kuwa Uislam hata siku moja hauharibu bali unatengeneza mfano wake ukiwa Iddi Simba mtu ambae hakuwa na makuu licha ya nema ya elimu na uwezo wa mali aliojaaliwa na Allah.
Hakika tumeondokewa na hasa sisi nduguze wanachama wa Saigon Club ambao Iddi Simba alikuwa mwanachama shupavu na mhimili wa mengi tuliyomudu kufanya iwe ni kufuturisha kila Mwezi Mtukufu wa Ramadhani au kusoma khitma ya kila mwaka kuwarehemu masheikh ndugu na jamaa waliotangulia mbele ya haki.
Iddi Simba alikuwa nembo ya Saigon na aliwavuta wengi mfano wa yeye kujikurubisha Saigon katika kheri hizi na kuleta umoja na kujenga mapenzi.
Iwe futari au khitma utamkuta Iddi Simba mapema keshafika club anapokea wageni hata pale alipokuwa mgonjwa hakuwa na udhuru akija pale na ‘’wheel chair,’’ kama vile hakuwa anaumwa akielekeza hili au lile lifanyike.
Tunamuomba Allah apokee dua zetu na atulipe mtu bora kama marehemu Iddi Simba au kushinda Iddi Simba.
Amin.