Scandinavia Yaishinda Shell katika Kesi
KAMPUNI ya Scandinavian Express Services Limited, imeshinda kesi iliyofunguliwa dhidi yake na Kampuni ya mafuta ya Shell Limited.
Shell ilifungua kesi ikitaka Scandinavian ifilisiwe ili iweze kulipwa deni lake la sh zaidi ya bilioni moja inazoidai kampuni hiyo ya usafirishaji.
Hukumu ya kesi hiyo yenye kurasa 36, ilitolewa juzi na Jaji wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara, Nathalia Kimaro.
Jaji Kimaro alisema baada ya kupitia hoja za upande wa mashitaka na upande wa utetezi, amebaini kuwa kuifilisi Kampuni ya Scandinavian si jambo la busara.
Alisema anakubaliana na hoja za mawakili wa upande wa utetezi kuwa kampuni hiyo ina mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.
Alisema inasafirisha abiria zaidi ya 2,000 kila siku kwa kutumia mabasi zaidi ya 80.
Mabasi hayo yanafanya shughuli zake katika eneo lote la Afrika Mashariki hadi katika nchi za Malawi na Zambia.
Kampuni imeajiri wafanyakazi zaidi ya 600; ambao Jaji Kimaro alisema kwa hali ya sasa ya ukosefu wa ajira na ongezeko la uhalifu nchini, kuifilisi ni kuleta matatizo zaidi.
Alisema kampuni inatumia sh 69,343,500 kila mwezi kuwalipa wafanyakazi mishahara.
Jaji Kimaro alikubaliana na hoja za utetezi kuwa Scandinavian inao uwezo wa kulipa deni inalodaiwa, na uwezo huo umethibitishwa kwa malipo iliyofanya kwa benki za Euro African, na NBC Limited.
Alikubaliana na hoja kuwa kuyumba kwa Scandinavian kifedha kulisababishwa na mambo kadhaa, yakiwamo ya ajali zilizosababishwa na ubovu wa matairi ya mabasi, na kupanda kwa bei ya mafuta.
Haya ni mambo yanayochukuliwa kuwa ni ya kawaida katika biashara, alisema Jaji Kimaro.
Jaji pia alisema kampuni hiyo, licha ya matatizo ya mtiririko wa fedha yaliyojitokeza siku zilizopita, bado inaendelea na shughuli zake kama kawaida, jambo ambalo linathibitisha kuwa inaweza kulipa madeni yake.
Uamuzi wa kuifilisi utaiua kampuni ambayo ni msafirishaji mkuu wa abiria, mizigo na vifurushi si kwa Afrika Mashariki pekee, bali hadi Zambia na Malawi.
Inasafirisha abiria 2,000 kila siku na imeajiri wafanyakazi 600; pia ni moja ya walipa kodi. Mahakama inajua matatizo ya ajira yanayoikabili nchi yetu ambayo yameongeza vitendo vya uhalifu, alisema Jaji Kimaro.
Alisema hoja zilizotolewa na upande wa utetezi ni za msingi na zinazopaswa kuzingatiwa.
Zilionyesha ni kwa namna gani pande zote mbili zisivyoweza kunufaika kama Scandinavian ikifilisiwa.
Uamuzi wa kuifilisi utaiua, tatizo la ajira litaongezeka, na pia uhalifu. Uamuzi wa aina hiyo hautakuwa na manufaa kwa jamii, alisema Jaji Kimaro.
Katika hukumu hiyo, Jaji Kimaro alitoa miezi tisa kwa Scandinavian na kampuni zinazoidai, kuketi pamoja na kutafuta njia sahihi za kulipa madeni hayo.
Katika kesi hiyo, jopo la mawakili wa Scandinavian liliongozwa na wakili wa kujitegemea ambaye sasa ni Jaji mstaafu, Lameck Mfalila.
Kampuni hiyo ilikuwa ikiungwa mkono na benki za NBC Limited, Standard Chartered, Euro Africa na Kampuni ya Scania Tanzania.
Shell ilikuwa ikiungwa mkono na kampuni za Diamond Motors, Sameer Tanzania Limited na Benki ya CRDB. Mawakili wake waliongozwa na Kennedy Fungamtama.