KIGOMA: Wazazi Kasulu washauri kubadilishana zamu kupunguza Utoro Shuleni

KIGOMA: Wazazi Kasulu washauri kubadilishana zamu kupunguza Utoro Shuleni

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
51
Reaction score
38
Sehemu ya pili ya makala hii iliweka wazi chanzo kikuu cha tatizo la utoro wa wanafunzi zaidi ya 2000 kuacha masomo kila mwaka, ifikapo msimu wa kilimo katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu kuwa ni mitazamo hasi ya jamii juu ya elimu, ikichanganywa na changamoto za kiuchumi, miundombinu na utekelezaji hafifu wa sheria.

Katika makala hii ya tatu, inayohitimisha uchunguzi huu, inaangazia suluhisho zinazopendekezwa na wadau wa elimu, wazazi pamoja na maeneo ambayo tayari yameanza kupiga hatua katika kuboresha mahudhurio ya wanafunzi shuleni, ili kutoa mwanga wa namna tatizo hilo linavyoweza kupunguzwa au kumalizwa kabisa.

Wazazi wapendekeza kubadilishana zamu
WAZAZI wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu wamependekeza suluhisho la kudumu la kubadilishana zamu za kwenda mashambani na kubaki nyumbani wakati wa msimu wa kilimo, kama njia ya kukabiliana na utoro wa wanafunzi uliokithiri wilayani humo.

Wanasema pendekezo hilo linakusudia kuhakikisha watoto hawakosi uangalizi wa wazazi, malezi na usimamizi wa karibu wa masomo, hata wakati wa msimu wa uzalishaji.

Fales Mazina, mkazi wa Nyakitonto, anasema mfumo wa kubadilishana zamu unaweza kupunguza tatizo la kuwaacha watoto chini ya uongozi wa mtoto mkubwa.

“Ni vyema wazazi wakapeana zamu, baba akae shambani wiki mbili, mama abaki nyumbani au kinyume chake, hii inawezekana kama wazazi wataamua,” anaeleza Mazina.

Kwa mtazamo wake, mfumo huo unaweza kusaidia kaya nyingi kuendesha shughuli za kilimo bila kuwaathiri watoto kielimu na kisaikolojia.

Kambi Kinyoma anaona pendekezo hilo linawezekana iwapo wazazi watajiandaa mapema kwa kuweka bajeti ya fedha kwaaajili ya chakula kabla ya msimu mpya wa kilimo kuanza ili kuepuka madhara yatoakanayo na kukosa fedha kwa pande zote mbili.

“Zamu zinawezekana lakini bila bajeti ya chakula na fedha za akiba haitafanikiwa, sisi wanaume tutataka kwenda shambani mara kwa mara kuepuka majukumu ya nyumbani, mke abaki nyumbani, lakini bila posho familia itashindwa kujiendesha,” anaongeza Kinyoma.

Hoja ya Kinyoma inaibua uhalisia kwamba suluhisho la kijamii haliwezi kufanikiwa bila maandalizi ya kiuchumi, hasa katika kaya zinazotegemea kilimo kama chanzo kikuu cha maisha anasema Rashid Shaban.

Shaban anaongeza kuwa, anaona kubadilishana zamu kama njia ya kuokoa kizazi cha watoto ambao, licha ya kumaliza shule ya msingi, bado hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu.

Hata hivyo, Faustina Ndabhona anatoa tahadhari kuwa mfumo huo unaweza kuwa mzigo zaidi kwa wanawake iwapo hautasimamiwa kwa usawa akitoa hoja kuwa wanaume wengi wa mkoa wa Kigoma hupenda kuishi maisha ya kibwana huku wanawake wakipambana na kila kitu.

“Wanaume watakubali kwa maneno, lakini mzigo utabaki kwa mwanamke, malezi, chakula, elimu, kila kitu kitakuwa juu yake kwakuwa wanaume wa humu ni wavivu na wanapenda kufanyiwa vitu na wake zao,” anasema Ndabhona kwa msisitizo.

Anaonya kuwa hali hiyo inaweza kuwaweka wanawake katika mazingira magumu ya kiuchumi na kijamii, jambo linaloweza kuzalisha matatizo mapya badala ya kuyamaliza ya awali.

Watoto washauri wazazi kuzaa watoto wanaowamudu
Marko Edward mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Nyakitonto, anashauri wazazi kuzaa watoto wachache watakaoweza kuwahudumia bila kuwatelekeza akiataja changamoto kubwa hutokea pale wazazi wanapokuwa na watoto wengi na kushindwa kuwalea ipasavyo.

Naye Vumilia John, darasa la tano anasema adhabu zitolewe kwa yeyote anayekiuka utekelezaji a sheria ya elimu ili kumuokoa mtoto ambaye hana maamuzi na sauti yake haisikiki hasa inapokuja kwenye amri itolewayo na wazazi au walimu juu ya mustakabali wa maisha yao.

Suluhisho la kiteknolojia
Ofisa kilimo wa wilaya ya Kasulu, Ntegwa Luziro anasema serikali kupitia wizara ya kilimo imeanza kutekeleza mradi wa kupima afya ya udongo kwa kutumia kifaa cha “Soil Scan” katika wilaya ya Kasulu, hatua inayolenga kuwasaidia wakulima kulima kwa tija katika maeneo yaliyo karibu na makazi yao.

Anasema teknolojia hiyo itapunguza ulazima wa wazazi kuhama na kuweka makambi mbali na familia zao.

“Baada ya kupima udongo, mkulima atajua hali ya udongo na hivyo kujua aina ya mazao ya kupanda sambamba na mbolea sahihi itakayofaa kwaajili ya kupata mavuno mengi kwa kulima katika eneo dogo,” anaeleza Luziro.

Kwa mujibu wake, hatua hiyo tayari imeanza kuleta mabadiliko kwa baadhi ya wakulima waliothubutu kutumia kifaa hicho kwa kutumia maafisa ugani waliopo katika maeneo yao.

Uwezeshaji wa kaya maskini
Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini wilayani humo, Maria Tarimo, anasema kaya maskini 7,171 zimewezeshwa kupitia mpango huo ili kupunguza umaskini na utegemezi wa watoto kama nguvu kazi.

Anasema baadhi ya kaya zilipatiwa ruzuku za masharti kwa ajili ya kuwahudumia watoto wanaosoma, ikiwemo kununua sare za shule.

Hatua hiyo, kwa mujibu wake, imeanza kuonyesha dalili chanya katika baadhi ya maeneo, hasa pale wazazi wanapoweza kumudu mahitaji ya msingi ya elimu.

Mikopo na elimu ya malezi
Mkuu wa kitengo cha maendeleo ya jamii wilayani Kasulu, Victoria Makyao, anasema mikopo inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inalenga kupunguza utegemezi wa kilimo pekee.

“Biashara ndogondogo zinawasaidia wazazi kubaki karibu na familia zao, watoto wanapata uangalizi na wanaendelea na masomo,” anaeleza Makyao.

Anaongeza kuwa halmashauri imeunda vikundi 61 vya elimu ya malezi katika vijiji vyote, hatua inayolenga kubadilisha mtazamo wa wazazi juu ya elimu na umuhimu wa wazazi kutimiza wajinu wao katika malezi.

Miundombinu na maeneo yaliyoanza kupiga hatua
Ofisa elimu wa Wilaya ya Kasulu, Elestina Chanafi, anasema kupitia fedha za ndani na serikali katika mwaka wa bajeti 2025/2026 vyumba zaidi ya 30 vya madarasa vinatarajiwa kujengwa ambapo 24 kati ya hivyo vinaendelea kujengwa na vilivyosaliwa kujengwa kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha.

Vilevile anataja kampeni za uhamasishaji kama “Educate a Child”, kwa kushirikiana na shirika la umoja wa mataifa wa kusaidia watoto (UNICEF), na wadau wengine wa elimu ambazo huzifanya kupitia vyombo vya habari na kupita nyumba kwa nyumba zinaendelea saidia kuwarudisha wanafunzi wengi waliotoroka shule.

“Tulifanya kampeni kupitia redio, nyumba kwa nyumba na mashambani tukihamasisha wanafunzi waweze kurudi shuleni, na wale ambao wanakuwa hawajaripoti kuripoti,” anasema Chanafi.

Mchango wa wadau wa elimu:
Aidha, Christine Karungi meneja wa mradi wa Wezesha Binti unaofadhiliwa na Enabel, anasema wamefanikiwa kutoa hema 13 za hedhi salama zinazozunguka (mobile MHM) kama sehemu ya kuwadhibiti mabinti ambao waliacha kwenda shule kwa siku kadhaa kutokana na kuwa katika hedhi

Anasema hema hizo zitatumika pia kama chumba cha kujifunza hedhi salama, haki na wajibu wa wanafunzi pamoja na elimu ya jinsia jambo ambalo litasaidia kupunguza mimba za utotoni.

Kwa upande wake meneja mradi wa shirika la World Vision kanda ya mgharibi, Jackline Kaihura, anasema katika jitihada za kuboresha miundombinu ya shule, shirika hilo limetoa zaidi ya milioni 700 kujenga miundombinu ya vyoo rafiki kwa walemavu, na wanafunzi wengine sambamba na vyumba vya hedhi maalumu kwa watoto wa kike.

Anasema kutokana na tafiti walizofanya waligundua kuwa shule nyingi hazina vyoo bora, na ndipo walipoamua kutenga bajeti ya ujenzi wa vyoo 100 kwa mwaka 2024/2025 ambavyo vimeshakabidhiwa kwa matumizi vikiwa na maji ya kutosha kuimarisha usafi akitaja kuwa miradi kama hiyo ni sehemu ya kupunguza adha ya ujifunzaji kwa watoto na walimu pia.

Mabadiliko ya kisheria:
Ofisa elimu sekondari, wilaya ya Kasulu, Iyogo Isuja, anashauri marekebisho ya baadhi ya kanuni za elimu, hasa waraka unaoruhusu mwanafunzi kutoroka siku 90 mfululizo kabla ya kuchukuliwa hatua.

Milardy Ayo katika ukurasa wake wa instagramu “millard ayo 22 August 2019” aliripoti taarifa iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa elimu Joyce Ndalichako juu wa waraka wa elimu "Waraka wetu wa Wanafunzi utoro Shuleni unamruhusu Mwanafunzi awe mtoro siku 90”

Baadhi ya wadau wa elimu walilalamika juu ya waraka huo wakidai “hii haiendani kabisa na 'Hapa Kazi Tu', asipokuja kazini siku 5 anafukuzwa kazi kwanini mwanafunzi tumruhusu akae nyumbani siku 90 bila taarifa" - WAZIRI NDALICHAKO.

Wakili Hamis Ramadhan wa Shira Advocates anasisitiza marekebisho ya Kifungu cha 35 cha sheria ya elimu ya mwaka 1978 ili kuendana na hali ya sasa, huku akisisitiza juu ya elimu ya sheria kwa watekelezaji wa sheria husika.

Katika ripoti iliyoandika na gazeti la Mwananchi, Agost 29, 2017 (https://www.mwananchi.co.tz/mw/haba...za-kukabiliana-na-utoro-shuleni-bungo-2863588) juu ya mbinu za kukabiliana na utoro katika shule ya msingi Bungo iliyopo manispaa, mwalimu mkuu wa shule hiyo Roman Luoga alsema mbin ua mic chakula cha mchana, vipindi vya michezo ya pete, wa miguu na kikapu pamoja na kuwapatia uongozi wanafunzi wengi wanaopenda kutoroka.

Naye mwalimu wa taaluma wa shule hiyo Rose John anasema walifanikiwa kupitia ziara za kimasomo ndani na nchi ya nje akifafanua kuwa hufanya ziara hizo mara kwa mara kwenda kujifunza katika shule zinazofanya vizuri kuliko wao jambo ambalo lilifanikiwa kwa kiwango kikubwa kupunguza utoto.


ANDIKO LA: Adela Madyane – Kigoma
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.

Pia soma:
: Kambi za kilimo Kasulu zinavyochochea utoro shuleni
:
Mitazamo Hasi juu ya Elimu chanzo cha Utoro Shuleni
 
Back
Top Bottom