Katika mazingira ya soko huria, kama kuchanganya lugha ndiyo kitu ambacho walengwa wa redio wanakipenda, mtangazaji kuchanganya lugha inawezekana kuwa ni sehemu ya ufanisi wa kazi yake.
Na kwa kweli, kinachotakiwa kumhukumu ni jinsi anavyokubalika na kusikilizwa na jamii, si sheria za umaridadi na uadilifu wa kufuatilia lugha.
Kenya kuna lugha inaitwa "Sheng". Ni mchanyato wa Kiingereza, Kiswahili na maneno ya lugha za asili za Kenya.
Kama mtu anaweza kuanzisha stesheni ya redio ya kuongea "Sheng" na watu wakaikubali, kama wewe hupendi, usisikilize.
Jamaica wana "Patois", ambayo ni mchanganyiko wa Kiingereza na lugha nyingi ambazo watu wa Jamaica wana asili nazo. Watu wa daraja la juu Jamaica wanaiponda sana Patois, lakini ni lugha ambayo watu wa kawaida wanaitumia. Nilikuwa nasikiliza BBC World Service kama kawaida yangu, nikasikia wametafsiri Biblia kwenye Jamaican Patois, kwa sababu watu wanasema Biblia ya King James hawaielewi, kwa sababu hiyo si lugha wanayoongea kila siku.
The link is here
Sasa basi, kama huyo mtangazaji anachanganya lugha, na hivyo ndivyo wasikilizaji wake wanafurahia, muachieni afurahie uhuru wa soko huria.
Kama wasikilizaji hawafurahii, hawatasikiliza, redio itakosa wasikilizaji, itakosa matangazo, itakufa kifo cha asili kwa kutozingatia wanachotaka wasikilizaji.
Ndivyo biashara za soko huria zinavyotaka.
Unaweza kutangaza kwa Kiswahili cha Shaaban Robert, wasikilizaji wasikuelewe, ukawa hujafanya kazi inayotakiwa.
Kuongea lugha nyoofu si sawa na kuwasiliana na watu vilivyo.
Habari hii inanikumbusha habari ya hotuba ya Mfalme Hirohito wa Japan.
Baada ya Japan kupigwa mabomu ya Atomiki Hiroshima na Nagasaki, ilibidi Japan isalimu amri na kukubali kushindwa vita.
Mfalme Hirohito wa Japan alionekana kama Mungu kwa watu wake, na hawakuwahi hata kumsikia sauti yake kwenye redio.
Ila kwa sababu mabomu yalikuwa makubwa sana, na nchi ilitakiwa kukubali kushindwa, mfalme akawa na kazi ya kuwatangazia watu kuwa wanakubali kushindwa.
Mfalme akatoa hotuba kwa watu wake kwa njia ya redio. Wajapan karibu wote wakawa wamekusanyika kwenye redio zao wanamsikiliza mfalme.
Tatizo likawa, Mfalme alikuwa anatumia Kijapan cha hali ya juu sana (classic Japanese) kiasi kwamba, mpaka alivyomaliza kuhutubia, wananchi wakawa wanaulizana, hapo Mfalme kasema nini? Mbona hatujaambulia kitu?
Alikuwa amezingatia kuongea kijapani cha ndani na hali ya juu sana, kiasi kwamba hadhira yake haikumuelewa alikuwa anamaanisha nini. Wengine wanasema alifanya makusudi kuficha aibu, kama anakubali kushindwa vita kwa lugha isiyoeleweka vizuri ili asipate aibu ya kukubali kushindwa kwa lugha inayoeleweka.
Kwa hiyo, kuongea lugha sawia nikitu kimoja, kuwasiliana na hadhira unayotaka nikitu kingine.
Kwa habari zaidi kuhusu speech ya Hirohito, somahapa
NPR Choice page