Umeelewa nini kwenye katuni hii?
Kijana Mtanzania, badili mtazamo
Tuwasihi vijana wetu wagombee nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mtaa kuanzia mwaka huu na hatimaye wagombee uchaguzi mkuu mwakani.
Vijana, kueni na uthubutu. Hapa tunawahitaji vijana wa vyama vyote vya siasa. Nendeni muoneshe makali yenu ya hoja na muweze kuleta mabadiliko kwenye nchi yetu.
Vijana, msikae kulalamika. Msiwaige vijana wa hovyo walioamua kuishi kama wapambe au machawa. Kapambaneni huko, ikishindikana msikate tamaa.
Nchi na hatma yake iko mikononi mwenu. Naamini mkijieleza vizuri mtaaminiwa tu bila tatizo.
Iwe ni nafasi ya mwenyekiti wa mtaa, mwenyekiti wa kijiji, udiwani, ubunge, hata urais. Kagombeeni msiogope.
Vaeni roho za wapigania uhuru na wakataa utumwa kama Mkwawa, Mtemi Isike, Mwami Ntare, Nangwanda. Ingieni kwenye siasa kwa wingi wenu, mtafanya kitu.
Shime shime, nendeni msiogope kitu chochote. Ninyi ni taifa la leo na hazina ya leo na ijayo.