HATIMAYE serikali imetangaza kikokotoo kipya cha mafao ya wastaafu, safari hii kukishuhudiwa kuwapo kwa usawa na uwiano kati ya watumishi wa umma na sekta binafsi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu, akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dodoma jana, wakati akitoa taarifa kuhusu kanuni mpya za kikokotoo cha mafao ya watumishi nchini. PICHA: IBRAHIM JOSEPH
Kutangazwa kwa kanuni hizo ni hitimisho la sintofahamu ya mafao hayo iliyodumu kwa takribani miaka nne tangu mwaka 2018 serikali ilipositisha utekelezaji wa kanuni mpya za mafao kwa wastaafu zilizotaka kiwango cha mkupuo kiwe asilimia 25.
Kutokana na kuwapo kwa malalamiko ya wadau dhidi ya kanuni hizo Rais wa wakati huo, Dk. John Magufuli alilazimika kuzisitisha mwaka huo ili kutoa muda kujadili na Mei 14 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliliridhia ombi la wadau wa hifadhi ya jamii kupandisha kiwango cha kikokotoo kutoka asilimia 25 hadi 33.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, mwenyekiti wa kamati elekezi ya kanuni hizo ambaye ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu, alisema waziri wenye dhamana na masuala ya hifadhi ya jamii aliunda kamati hiyo ili kutekeleza maelekezo ya serikali ya kukubaliana kanuni itakayowianisha mafao kwa wafanyakazi wote.
Alisema kamati hiyo ilifanya kazi yake kwa kuzingatia mambo makubwa mawili ambayo ni kuhakikisha kanuni mpya inayopendekezwa inatoa mafao bora kwa wastaafu na pia mifuko inakuwa endelevu kwa manufaa ya wananchi wote.
“Kazi ya kamati ya kuandaa kanuni itakayotumika baada ya kipindi cha mpito imekamilika na kuridhiwa na wadau, kanuni mpya iliyoridhiwa itaanza kutumika rasmi Julai Mosi mwaka 2022,” alisema.
MAFAO YATAKAVYOKUWA
Prof. Katundu alisema kiwango cha mkupuo cha asilimia 33 ni kwa mifuko yote na kikokotoo limbikizi kitakuwa 1/580 kama ilivyokuwa kwa mfuko wa NSSF na ilivyokuwa mifuko ya PPF, GEPF na baadhi ya wanachama wa iliyokuwa PSPF na LAPF.
“Makadirio ya miaka ya kuishi baada ya kustaafu ni 12.5 kama ilivyo kwa mfuko wa NSSF na iliyokuwa mifuko ya PPF, GEPF na baadhi ya wanachama wa iliyokuwa PSPF na LAPF,” alisema.
Alisema mshahara wa kukokotolea mafao ya pensheni utakuwa wastani wa mishahara bora ya miaka mitatu ndani ya miaka 10 kabla kustaafu na umri wa kustaafu kwa lazima utaendelea kuwa miaka 60.
“Pia niwafahamishe kuwa pensheni za wastaafu watakaotumia kanuni hizi zitakuwa zikihuishwa mara kwa mara kwa kuzingatia mfumuko wa bei na uwezo wa mifuko hiyo ya pensheni,” alisema.
FAIDA ZA KANUNI MPYA
Katibu Mkuu huyo alisema kanuni hizo zitaongeza kiwango cha malipo ya mkupuo kutoka asilimia 25 iliyokataliwa mwaka 2018 hadi asilimia 33 kwa wanachama 1,364,050 sawa na asilimia 81 ya wanachama wote 1,690,187 wa mifuko ya pensheni.
Pia alisema inaongeza pensheni ya mwezi kutoka asilimia 50 ya sasa hadi asilimia 67 kwa waliokuwa wanachama wa PSPF na LAPF ambao ni asilimia 19 ya wanachama wote wa mifuko ya pensheni.
“Faida nyingine ni mifuko ya pensheni ya PSSSF na NSSF itaimarika na kuwa endelevu, pia kwa kuwa kanuni mpya inaimarisha mifuko na kuwa endelevu, mifuko itaweza kuongeza pensheni ya kila mwezi kwa kuzingatia tathmini zitakazofanyika kila baada ya miaka mitatu,” alisema.
Vilevile, alisema wanachama wote wanaochangia kwenye mifuko ya pensheni watatumia kanuni moja ya mafao na hivyo kuweka uwiano na usawa wa mafao baina ya wastaafu.
Katibu huyo alisema serikali imeweka utaratibu wa kutoa elimu kwa wanachama na umma kuhusu kanuni hizo ili kuhakikisha wote wanakuwa na uelewa sahihi na faida zake.
“Nitoe rai kwa wananchi kuendelea kuiamini serikali sikivu inayoongoza na nishukuru wadau wa utatu kwa kazi nzuri ya pamoja iliyofanyika kwa weledi na uzalendo,” alisema.
KAULI ZA WADAU
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, alisema upangaji wa kanuni hizo umekuwa shirikishi na zimeridhiwa na wadau na hakuna eneo walilofichwa.
Alisema pamoja na hayo walikubaliana wasiende chini ya asilimia 35 lakini serikali na wataalamu kutoka nje walishauri kufikia asilimia 33 ili wafanyakazi wasiongeze michango ya kuchangia na mifuko iendelee kuwa endelevu.
“Tulikuwa tunapata asilimia 50 ya mkupuo halafu asilimia 50 nyingine tulikuwa tunapata malipo ya kila mwezi, lakini sasa imebadilishwa asilimia 33 ya mkupuo halafu asilimia 67 tutaipata kwa mwezi, hakuna namna inabidi tulipokee, wafanyakazi zoezi hili limekuwa shirikishi, sekta binafsi tumechukua TUICO wameshiriki ndani,” alisema.
Alisema watumishi wanaochangia mifuko ya NSSF, PPF, GEPF, mkupuo wao umepanda kutoka asilimia 25 na kufikia asilimia 33.
“Kwa wao ni furaha kubwa sana sisi tulikuwa tunapata asilimia 50 tumeshuka na sasa itakuwa asilimia 33, niwasihi tulipokee hili wafanyakazi kwetu sisi ni gumu kumeza lakini ni kwa mustakabali wa uendelevu kwa vizazi vinavyokuja, tusimame pamoja kwenye hili,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Nchini (ATE), Suzanne Ndomba, alisema waajiri, wafanyakazi na serikali walikaa wote kwa pamoja kutengeneza kanuni hizo ambazo zimezingatia utaalamu na wataalamu walikuwa wa pande wote.
“Niwasihi wafanyakazi na waajiri, serikali itaendelea kutoa elimu na wale waajiri wenye maswali waje ATE tutasaidia kuchukua na kupeleka serikalini ili kupata ufumbuzi,”alisema.
Kaimu Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Dinnah Mathamani, alisema jambo hilo limefanyiwa kazi kwa muda mrefu na wameshirikishana.
“Kwa upande wetu ambao kikokotoo kilikuwa asilimia 50 na kushushwa kuwa asilimia 33 nadhani tutapata mshtuko lakini hali ndivyo ilivyo kwa kuwa tumeelezwa kwanini tumefikia hapa, faida zake bila kujali waliokuwa asilimia 50, au asilimia 25 lakini kubwa ni mifuko kuwa endelevu,” alisema.
Aliwaomba walimu wawe na utulivu, watapewa elimu na kueleweshwa, akisema: “Tukipata elimu kwa ujumla hakutakuwa na shida, sisi tumeshirikishwa kwenye kamati elekezi na tumepitishwa na wataalamu, sisi walimu tumelipokea na tutaendelea kutoa elimu kwa ambao hawajaelewa."