Naona nina wajibu kuchangia ktk Suala hili la J.K. kumpigia debe Basil Mramba. Nitangulize kusema kwamba namheshimu na kumwonea huruma sana Rais wangu Kikwete. Nikiri pia kwamba Basil Mramba ni rafiki yangu binafsi wa siku nyingi.
Kwanza, kesi ya Mramba ni ya JINAI. Kama Mramba hangekuwa na wadhamini wa kuridhisha Mahakama, ungekuta sasa ni mahabusu anaishi Keko au gereza lolote la Serikali Tanzania akingojea maamuzi juu ya kesi inayomkabili.
Pili, kesi yoyote ya jinai ni kesi ambayo Serikali inamshtaki mtuhumiwa. Serikali ni taasisi inayoongozwa na Rais, ambaye kwa wakati ule Mramba akituhumiwa ilikuwa ni Kikwete anaiongoza, na hata sasa anaiongoza hadi hapo matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba utakapoamua aendelee au asiendelee.
Tatu, nina hakika kwa mtu mashuhuri kama Mramba, na kutokana na kiasi cha fedha zinazodaiwa Serikali imepoteza kutokana na mkataba Mramba aliosaini (Shs bilioni 12), ni lazima Rais alihusika kwa karibu sana na alikubali kesi ifunguliwe dhidi ya waliohusika: yaani Mramba, Daniel Yona na Gray Mgonja.
Nne, kwa vile Mhe. Kikwete ni Mwenyekiti wa CCM, na alifahamu Basil Mramba alikuwa amemtuhumu (akiwa Rais na kiongozi wa Serikali), angeshauri CCM isimsimamishe kugombea jimbo la Rombo. Kwa hiyo, kwa heshima na taadhima, nasema Mhe. hakutumia uwezo wake na taarifa alizokuwa nazo kupata maamuzi busara kuhusu ugombea jimbo la Rombo. Kama Kamati Kuu ya CCM ilimlazimisha Mwenyekiti wake amkubali Mramba, basi ni cham cha mafisadi kweli!!!!
Tano, hata kama Mramba alikuwa MwanaCHADEMA aliyekuwa na kesi inayomkabili mahakamani, na akapendekezwa na kura za maoni za wanaCHADEMA wa Rombo, sisi katika Kamati Kuu ya CHADEMA, hatungeidhinisha uteuzi wake aendelee na kampeni. Kwa hiyo, kwa Kamati Kuu ya CCM inayoongozwa na Mhe. Kikwete, kuidhinisha mtuhumiwa wa ufisadi agombee ubunge, inadhihirisha CCM kudhalilisha Bunge kama taasisi.
Sita, kwa Mhe. Kikwete wiki hii, kumpigia debe, Basil Mramba, mtu ambaye yeye kama Rais, amempeleka mbele ya Mahakama akimtuhumu kwa kusababisha hasara ya mabilioni ya shilingi, mali ya Serikali, inadhihirisha kutoshauriwa vizuri au yeye mwenyewe kuchanganyikiwa kwa hali ya juu.
Saba, sisi wanaCHADEMA tutaendelea kuwakumbusha wapiga kura wa Rombo kwamba Mramba ni mtuhumiwa na wasimsikilize kwani anaweza kupatikana na hatia na asiweze kuwawakilisha Bungeni. Pia sisi tusisitize kwamba Mhe. Kikwete anashauriwa vibaya au hajui hatua zinazotakiwa kuimarisha utawala bora na kwa hiyo hafai kuchaguliwa kuendelea kuwa Rais.
Mgombea wetu Dk. Willibrod SLAA apigiwe kura.