Ansbert Ngurumo
KWA mara ya kwanza tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
Baada ya yote yaliyojadiliwa kuhusu yeye, kabla na baada ya kujiuzulu kwake, inatupasa kukubali ukweli kwamba Lowassa ameondoka ili Rais Jakaya Kikwete abaki.
Vinginevyo, ilibidi waondoke wote, kama walivyoingia wote.
Sijui kama walikuwa wanajua kwamba kimsingi, lilikuwa limeanza vuguvugu na bado lipo kwamba Kikwete ajiuzulu ili ufanyike uchaguzi mpya kwa sababu ameshindwa kuongoza nchi.
Katika miaka miwili tu ya utawala wao, ufisadi umekithiri serikalini, huku yeye na mawaziri wake wakiutetea waziwazi, hata kwa kutumia mamilioni ya fedha zetu kuzunguka mikoani kuhadaa wananchi.
Vilio vya wananchi maskini na wanaharakati vimepuuzwa, huku rais mwenyewe akitoa kejeli na kuviita kelele za mlango, ambazo hazimzuii mwenye nyumba kulala. Na wengine wanasema kwamba katika miaka miwili ya Kikwete, umefanyika ufisadi mbaya sana kuliko wa miaka 10 ya Benjamin Mkapa, na kwamba ndiyo maana anawakingia kifua kina Mkapa.
Baadhi wameshaanza kusema: Miaka miwili inawatosha. Kuwaongezea miaka mingine mitatu ni kuzidi kukaribisha uharibifu mkubwa kwa taifa. Waondoke sasa.
Tuishukuru Kamati ya Mwakyembe imewasaidia kuamua na kuondoka, wakiongozwa na Lowassa. Lakini bado amebaki mmoja. Je, kuondoka kwa Lowassa kutambadilisha Kikwete?
Wanaolitazama suala la Richmond kwa haraka haraka wanammwagia shutuma nyingi Lowassa kana kwamba alikuwa peke yake.
Tuseme ukweli. Lowassa alikuwa mtumishi mteule wa rais. Amekuwa akisisitiza si zaidi ya mara moja kwamba anatekeleza mambo mawili Ilani ya CCM na maagizo ya rais.
Tunaijua katiba yetu. Waziri Mkuu hawezi kutekeleza suala lolote kitaifa ambalo hajaagizwa na rais, halafu rais asimfukuze kazi. Ni kweli, mchakato wa Richmond umeonyesha maagizo na shinikizo la Lowassa.
Lakini kwa muda wote huo, kama Lowassa angekuwa amejituma tu bila kutekeleza agizo au makubaliano, asingekuwa madarakani. Angefukuzwa kazi na rais mwadilifu.
Akiwa Waziri Mkuu, Lowassa alikuwa mtekelezaji wa maagizo ya wakubwa wake pia. Alikuwa anasimamia makubaliano, ambayo hata Rais Kikwete aliwaambia waandishi wa habari Ikulu mwaka 2006 katika kuadhimisha mwaka mmoja madarakani.
Rais Kikwete aliitetea sana Richmond, na akatamka kwamba alihusika moja kwa moja katika kuiteua kampuni hiyo baada ya kuridhika kwamba ilikidhi vigezo, hasa vya nafuu ya bei ya gharama ya umeme.
Ripoti ya Mwakyembe imeonyesha udhaifu mkubwa wa utawala wa nchi yetu. Imethibitisha kwamba viongozi wetu wanakurupuka. Wanadanganyika na kutudanganya sisi. Vinginevyo, wanatutumia kutekeleza mambo yao.
Utamu wa kashfa ya Richmond ni kwamba, wote wanaohusishwa na kampuni hiyo feki kwa karibu sana, ni marafiki wa karibu na washauri wa Rais Kikwete ule utatu uliounda na kuongoza mtandao wa Kikwete.
Kama tungeweza kuwatania, tungesema kwamba kwa mujibu ya Kamati ya Bunge, Richmond ni kampuni feki ya vinara wa mtandao!
Yawezekana ndiyo maana rais alishindwa kuwachukulia hatua. Kwa bahati mbaya mambo yanapoharibika, anayewajibika ni waziri mkuu, si rais!
Huu ndiyo mzigo ambao Lowassa amelazimika kuubeba. Na kwangu mimi, huu ndio ushujaa wa Lowassa. Maana ilibidi afe mtu. Amekubali afe yeye ili mkubwa aishi. Amejitoa kafara ili kumnusuru Kikwete na serikali yake. Mdogo lazima awajibike.
Vinginevyo, kama rais hakuhusika kabisa, angekwishamfukuza Lowassa kazi tangu zamani. Wala asingesubiri kamati ya Mwakyembe imueleze la kufanya.
Na asingesubiri Lowassa mwenyewe aandike barua ya kujizulu. Na kama Lowassa hakujiuzulu, hata Baraza la Mawaziri lisingevunjwa juzi.
Kuna sababu ya ziada. Tangu Serikali ya Kikwete ilipoingia madarakani, imesemwa mno kwamba Lowassa ndiye amekuwa mkono wa kulia wa Kikwete na Rostam Aziz ni mkono wa kushoto wa Kikwete katika kuendesha serikali.
Makamu wa rais hazungumzwi. Kikazi, Lowassa amekuwa mtendaji, Kikwete msemaji, Rostam mshauri. Na inajulikana kwamba mengi ambayo Lowassa alikuwa anayasimamia na kuyatenda hayakuwa yake.
Na kwa jinsi ilivyo katiba yetu, hata makosa ya rais, kama lazima yatekelezwe, ni waziri mkuu anayeyasimamia; na ndiye atakayelaumiwa.
Haya haya yanayomkuta Lowassa leo, yaliwahi kumkuta mzee Rashid Kawawa katika kusimamia makosa ya Rais Julius Nyerere katika kutekeleza sera ya vijiji vya ujamaa.
Kwa hiyo, katika hili, Lowassa atazomewa, Kikwete atashangiliwa. Lakini lao ni moja, na walilitekeleza kwa kuliamini.
Kilichomponza Lowassa zaidi ni hulka binafsi. Si mwoga wa kuchukua uamuzi. Ni mtekelezaji na mara nyingi amesifika kwa kutumia mabavu kuhakikisha anachoagiza kimetekelezwa.
Leo kuna mambo ambayo serikali inajivunia kwamba imeyafanya. Ni lipi lililofanyika bila usimamizi au maagizo ya Lowassa? Kama yapo, ni machache. Kama kuna mafanikio ambayo Serikali ya Kikwete inajivunia leo, tukubaliane kwamba hayawezi kutajwa bila kumhusisha Lowassa.
Kisa? Kwa wadhifa wake na kwa hulka yake, ni mtendaji, msimamiaji na mtekelezaji. Wanaomjua wanasema Lowassa halali hadi alichodhamiria kimetekelezwa.
Utekelezaji na usimamizi ni sifa binafsi inayomtofautisha Lowassa na Kikwete. Hata wale wanaompinga, linapofika suala la kufanya uamuzi na kuusimamia, wanakiri kwamba Lowassa anaweza.
Kwa hiyo, tunapomtazama na kumjadili Lowassa leo, ni vema tutambue kuwa alikuwa mtekelezaji tu; si mwamuzi pekee. Hili ni lao, si lake peke yake.
Katika kusisitiza hulka yake, wapo wengine wanaosema kwamba bahati mbaya ya Lowassa imetokana na tofauti nyingine kuu kati yake na rais; kwamba Rais Kikwete anapenda madaraka, Lowassa anaijua pesa ni mtafutaji.
Na kwa bahati mbaya amekuwa mmojawapo wa watu wanaotafunwa na mzimu wa Mwalimu Julius Nyerere.
Zaidi ya hayo, Serikali ya Kikwete na Lowassa imemomonyolewa na mbinu walizotumia kuingia madarakani zikiwamo kuchafuana majina, matumizi ya pesa zenye kutiliwa shaka, na mengine mengi yanayofahamika kama mbinu za kisiasa, lakini yanayofananishwa na ufisadi.
Leo hii, wapo watu wanasema wazi wazi kwamba watu hawa waliingia kwa ufisadi, wataondoka kwa ufisadi. Kundi hili hili ndilo lilitueleza ufisadi wa Mkapa na Frederick Sumaye. Leo tunapolipima kundi lao na akina Mkapa, nani ni nafuu? Nani anaweza kumcheka mwenzake?
Hata wale waliokuwa wanamtetea Rais Kikwete kwamba ingawa amezungukwa na watuhumiwa yeye ni mtu safi, sasa wanahoji sababu halisi za yeye kujiruhusu kuzungukwa na hao wanaotuhumiwa, ambao anawaamini sana.
Au ni yale yale ya Mkapa wa mwaka 1995, aliyeitwa Mr. Clean? Kilichomaliza usafi wa Mkapa kitauacha wa Kikwete huyu anayezungukwa na kundi hili?
Serikali ya Kikwete ilishazama kaburini. Lowassa ameisaidia kwa kujizulu. Nimesoma kauli yake. Amesikitika. Najua wapenzi wake hawana raha. Rais Kikwete hana raha.
Lakini naamini siku zinakuja ambapo Lowassa atagundua kwamba kitendo alichofanya juzi kujiuzulu, ni ukombozi kwake binafsi na kwa taifa.
Na kwa kiasi kikubwa kwa vigezo vyangu kitendo hicho, licha ya mazingira yaliyokisababisha, kinamvusha daraja na kumwingiza katika kundi la mashujaa wa kisiasa katika Tanzania ya sasa. Kimsingi, Lowassa ndiye aliyevunja Baraza la Mawaziri!
Kikwete aliyeshindwa mtihani wa kwanza, amepewa mtihani mpya. Amepewa fursa nyingine kujaribu. Akishindwa naye tunamtimua!
Hatutarajii atujazie sura zile zile katika baraza jipya. Tanzania haina upungufu wa watu wenye akili, ujuzi na uadilifu.
Hatutarajii rais atuteulie watu asiowafahamu vizuri, halafu baadaye ajiunge nasi kuwalaumu na kuwasimanga majukwaani kama alivyokuwa anafanya kwa hawa waliopita, huku akiogopa kuwatimua.
Rais ateue wachapakazi, si wapiga porojo na wachekeshaji. Wanaweza kuwa vijana au wazee, lakini asituletee wale wale wanaotuhumiwa kuharibu huko walikotoka.
Na asipoteze pesa zetu kuwapeleka Ngurdoto kuwapa semina elekezi. Imedhihirika kwamba licha ya kutumia mabilioni hotelini, mwalimu wao na wao wenyewe walipoteza pesa yetu hotelini. Hawakujifunza lolote Ngurdoto.
Tunatarajia baraza dogo la mawaziri wachache wachapakazi. Muda wa kugawiana vyeo na kupeana shukrani ya uchaguzi umepita. Kikwete ajisahihishe. Hasara za baraza kubwa zilikuwa nyingi kuliko faida alizotutajia wakati anaunda hili lililovunjwa na Lowassa.
Tayari tumeshaanza kumtazama Waziri Mkuu mpya, Mizengo Pinda. Tunamjua. Na huko alikotoka tunakujua. Hatuna sababu ya kumhukumu kabla hajaanza kazi.
Tutampongeza, lakini ajue kuwa tunajua matatizo ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) alikotoka hasa kwenye halmashauri zetu.
Tumemsikia akiomba kura na kushukuru baada ya kuidhinishwa na wabunge. Tumemsikia akiwataja waliomlea kisiasa. Tunataka kuamini kwamba watu hao hawakumharibu!
Tumesikia ombi lake kwamba tumwambie ukweli kwa mambo yatakayokwenda kombo. Tunaamini limemtoka moyoni. Tutasema.
Amekiri kwamba yeye si mwanasiasa mzoefu. Tunajua. Lakini ni vema ajue kwamba humo alimoingizwa ndimo walimo wazoefu. Asipowashinda, atajiunga nao. Asipowabadili, watambadili yeye.
Napenda kumpongeza Mheshimiwa Mizengo Pinda kwa uteuzi wake. Namwambia kile anachokijua kwamba ameingia serikalini wakati mbaya. Tutampa muda wa kumpima, lakini hautakuwa mrefu.
Na tutaanza hivi karibuni kwa ripoti ya wakaguzi kuhusu ubadhirifu wa pesa zetu katika Benki Kuu. Huu ndio mtihani wake wa kwanza. Likimshinda hilo, tutajua naye ameanza kuwa mzoefu kama hao waliomfundisha siasa.
Anajua Bunge linataka ripoti. Hakuna cha mashauriano na serikali. Bunge likitaka ripoti serikalini, lipewe. Atuonyeshe umakini na ujasiri wake sasa, amwondolee Spika woga uliomfanya aanze kujadiliana na serikali badala ya kuagiza apewe ripoti.
Pili, waziri mkuu amshauri rais sasa ateue watendaji wapya wizarani, hasa katika zile zinazoguswa moja kwa moja na hoja iliyovunja baraza lililokuwapo. Wasipoteuliwa sasa, Pinda ahesabu kwamba naye tayari kaingizwa mjini mapema.
Tatu, asimamie kwa kasi isiyo ya kawaida utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati ya Bunge kama yalivyotolewa na Kamati ya Mwakyembe. Utekelezaji huo uanze sasa kabla hajalewa madaraka na kuharibiwa.
Kama atatoa ushauri wake huo na rais akaukataa, Pinda ajiuzulu mapema, tujue anapinga ufisadi. Tutampongeza.
Ndiyo! Tunachojua kwamba kwa nafasi aliyopewa sasa, Pinda anakwenda kuwa mtekelezaji na msimamizi wa maelekezo ya rais. Na hapo kuna mawili.
Unapokuwa chini ya rais anayeogopa kuchukua uamuzi, huku wewe ukiwa na mamlaka ya kuchukua uamuzi, usipochukua uamuzi, hakuna kitakachofanyika.
Na ukiwa mtendaji, na katika mazingira tata kama haya ya Richmond, ujue yatakupata kama yaliyomkuta Lowassa. Pinda yuko tayari kwa lipi?
ansbertn@yahoo.com www.ngurumo.blogspot.com