Wanabodi wa Jambo Forums,
Kwanza napenda kuwatakia Heri na Fanaka kwa Mwaka Mpya 2008. Napenda pia kuwaasa kufanya tathmini ya kiasi gani malengo mliyojiwekea kwa mwaka 2007 yalitimizwa, na jinsi ambavyo yale mtakayoyaweka kwa mwaka 2008 yatatimizwa.
Baada ya haya napenda kujibu hoja iliyopo hapo juu kwa kuwapa mwanga kuhusu ukweli wa mambo ambayo watendaji wakuu (wengi wao) wa Ikulu, pengine, wasingependa ujulikane.
Kwanza kabisa wengi wenu mnaelewa kwamba kuna utamaduni wa kila rais anayechaguliwa kuweka 'watu wake' kumshauri wakati akiwa kazini. Watu hawa huchaguliwa kutokana na ukaribu/uhusiano alionao (mara nyingi...) au pengine maoni ya baadhi ya 'maswahiba' wa rais, ambao wao wenyewe hawawezi (kwa sababu moja au nyingine) kuteuliwa kufanya kazi Ikulu. Hawa ndio hutoa maoni yao kwa rais nani ateuliwe kushika nafasi ambazo zinakuwa ziko wazi baada ya baadhi ya watendaji wa Ikulu kuondolewa.
Pili, kutokana na utamaduni huu, kinachotokea ni kwamba, wanaoteuliwa kushika nafasi hizo nyeti huwa hawana vigezo vya kiutendaji (professional qualifications, terms of refereence, etc.), hivyo huwa hawajui, kimsingi, wajibu wao na hata sifa zao za kikazi. Hili si jambo la kufanyia mzaha, kwani, kinachotokea ni kwamba wanateuliwa watu ambao hawana sifa au viwango vya kuwa washauri wa rais, au watendaji wa Ikulu. Hii inasababisha mambo mengi kuamuliwa kutokana na uzoefu wao, si uzoefu wa kitaalam kama inavyopaswa iwe.
Tatu, kutokana na watendaji hawa kutokuwa na sifa zinazowahalisha kuwa watendaji wa Ikulu, mara nyingi watu hawa hufanya kazi kwa 'kujipendekeza' kwa rais. Hawana mawazo mapya sembuse fikra za kibunifu, kwa hiyo wanafanya maamuzi ambayo mimi ninayaita 'kuziba nyufa' wakati inatakiwa 'kujenga upya ukuta'. Hawana mawazo mapya, wao ni kurejesha kila walichokikuta humo ndani ya lile kasri kubwa jeupe, na kukileta kikiwa na 'nembo mpya', kumbe rais anapelekewa mvinyo ule ule pasi na yeye mwenyewe kujua. Kwa yeyote ambaye atabisha juu ya hili, ninao mfano zaidi ya mmoja, ya utendaji huu mbovu wa watendaji wa Ikulu.
Sasa wengine pengine mtajiuliza, iwapo mambo ni shaghalabaghala kama haya? Kwa mtazamo wangu, itabidi watu walio karibu zaidi na Rais Kikwete, wamshauri kuangalia upya sifa za kitendaji (professional qualifications) za waajiriwa wa Ikulu, kwani, kama inavyoeleweka duniani kote, Ikulu ni mahali ambapo kila aliyeajiriwa hapo anastahili kuwapo, na hata kama aliitwa hapo kwa matakwa ya Rais, basi, Rais asiwe na mashaka naye hata kidogo. Kwa kila nafasi yake, mtendaji wa Ikulu anatakiwa kuwa na kiwango cha juu kabisa cha uwajibikaji, uzoefu na uadilifu. Asiwe mtu wa kuchukua 'uamuzi mwepesi' kwa kazi ngumu. Asiwe mtu wa kukwepa majukumu, na awe mtu wa kusema ukweli, kumshauri Rais ipasavyo, awe tayari kukataa kufanya kazi ambayo utendaji wake unachangia katika ushauri mbaya kwa Rais, na matokeo yake kuwa mabaya zaidi kwa mustakabali wa nchi husika. Asiwe mnafiki.
Jambo moja ambalo watendaji wa Ikulu (ikiwa ni pamoja na taasisi zote zinazohusiana na Ikulu) hawajalitambua ni kwamba, kisheria na kitendaji, wana nguvu nyingi sana. Wana uwezo wa kumwita mtu yeyote na kumpa kazi yoyote waitakayo aifanye, bila kuulizwa na mtu yeyote au taasisi yoyote. Si uongo, ukiwa Ikulu 'umeula', lakini kama ni 'kuula', basi uwe na uhalali wa 'kuula'. Hatupendi kusikia na kuona utendaji mbovu unaomdhalilisha na kumwaibisha Rais kila uchao; kama kulikuwa na nafasi ya Rais kuwaona Watanzania waishio Marekani, basi, nafasi hiyo ingetumika. Inawezekana watendaji hao wa Ikulu, pamoja na maswahiba zao wa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, waliona kwamba Watanzania wenzetu waliopo Marekani wangewaumbua kwa kutoa dukuduku zao mbele ya Rais iwapo wangepata nafasi ya kuzungumza na Rais, dukuduku ambazo pengine zingepaswa kufanyiwa kazi na watendaji hao wa Ikulu na ubalozini. Lakini wakaamua kukwepa majukumu; mimi namsifu mtendaji anayekubali kukosolewa, kuliko anayekwepa kukosolewa. Utajuaje kama utendayo ni sahihi kama hutaki kukosolewa? Ndio maana Rais Kikwete alisema malalamiko ya upinzani hayamnyimi usingizi, ni matokeo ya demokrasia; kwenye demokrasia lazima upinzani upige kelele, usipopiga kelele si demokrasia! Sijui nani kati yenu alimwelewa Rais Kikwete aliposema hayo.
Kabla ya kupata nafasi ya kufanya kazi (japo kwa mbali) na baadhi ya watendaji wa ngazi za juu za Ikulu, nilidhani kwamba Ikulu ni mahali patakatifu, ambapo kila aliye huko alistahili kuwa huko. Kwa leo, ule utakatifu wa Ikulu haupo tena. Watu wamekwenda huko kwa njia za ki-ajabu-ajabu. Hakuna "professional qualifiations" wala "terms of reference" zinazowawajibisha na kuwaruhusu kuwapo huko. Tutaendelea kufanya mzaha na Ikulu mpaka lini?
Rais Jakaya Kikwete, tafadhali safisha nyumba yako. Kama unahitaji ushauri wa kitaalam zaidi, tupo sisi huku nje, tutakushauri, tuite... tena tutaifanya kazi hiyo hata bila malipo, ili mradi ni kwa manufaa ya Taifa letu! Unastahili kufanya kazi na wataalam, sio watu wanaodhani ni wataalam. Wapo watu wachache sana ulionao huko Ikulu, ambao ni wataalam kweli kweli, lakini wana sauti ndogo kuliko hao uliowapa madaraka ya juu zaidi... hao mimi ninawaogopa... hao ndio wanaokupotosha.
Jambo Forums, tuendelee na kazi yetu. Uzi ni ule ule mwaka 2008! Sikukuu njema!