Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,027
UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116539
E-mail: press@ikulu.go.tz
Website: Mawasiliano Ikulu
Fax: 255-22-2113425
PRESIDENTS OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mfumo wa Mawasiliano ya Kompyuta kwa Kiswahili wazinduliwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa jana, Jumanne, Mei 24, 2011 alizindua rasmi Mfumo wa Mawasiliano ya Komptyuta wa Windows 7 Kiswahili Interface Pack unaotumia lugha ya Kiswahili na unaotarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 150 milioni wanaozungumza Kiswahili kote duniani.
Sherehe za uzinduzi wa Mfumo huo wa Mawasiliano zilifanyika kwenye Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa miongoni mwa wageni wengine Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Meneja Mkuu wa Microsoft Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.
Katika uzinduzi huo, Rais Kikwete amesema Mfumo huo wa Mawasiliano kwa njia ya Kompyuta unaotumia Lugha ya Kiswahili, umefungua ukurasa mpya wa historia ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano na ya matumizi ya Lugha ya Kiswahili, kwani kwa mara ya kwanza lugha hiyo inapewa nafasi sawa na lugha nyingine kubwa duniani zinazotumika kwa kupashana habari na mawasiliano kwa njia ya kompyuta.
Rais Kikwete ameipongeza na kuishukuru Kampuni ya Microsoft kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa Lugha ya Kiswahili. Uamuzi wenu huo utasaidia sana katika kukuza na kuendeleza Lugha ya Kiswahili, amesema Rais Kikwete na kuongeza, utawafanya wale ndugu zetu wanaobeza na kutotaka kuendeleza matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika elimu, sayansi, teknolojia na shughuli za serikali na biashara kuwa na mawazo tofauti.
Amesema upatikanaji wa programu ya kompyuta ya Windows 7, utawawezesha watumiaji wa Kiswahili duniani kunufaika na matumizi ya lugha wanayoielewa zaidi katika kompyuta na hivyo kuondokana na kikwazo cha lugha, kwani watajipatia elimu na maarifa kupitia mitandao ya kompyuta na pia kurahisisha mawasiliano kwa njia ya baruapepe.
Mfumo wa Mawasiliano kwa njia ya Kompyuta unaotumia Lugha ya Kiswahili kwa kiasi kikubwa umetengenezwa na Watanzania wenyewe ambao wametafsiri zaidi ya maneno 300,000 ya kiufundi yaliyomo kwenye Microsoft Windows 7 Glossary kwenda kwenye Lugha ya Kiswahili wakishirikiana na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Kampuni yenyewe ya Microsoft. Programu hii ya Kompyuta inategemewa kusambazwa kwenye taasisi zote za elimu hapa nchini.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
25 Mei, 2011