Mwandishi wa Ikulu
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameyaonya mataifa ya Bara la Ulaya kuacha mtindo wa kuwadhalilisha viongozi wa Afrika, kupitia mfumo wa mpya wa utawala wa sheria wa kimataifa unaolenga kuwafungulia mashitaka viongozi wa Afrika, na kuwafikisha katika mahakama za kimataifa.
Rais Kikwete pia amesema kuwa Afrika inaunga mkono, moja kwa moja, mageuzi makubwa katika mfumo wa Umoja wa Mataifa (UN), ili mradi Bara hilo lipewe nafasi mbili zenye kura za turufu katika Baraza la Usalama la Umoja huo.
Mwenyekiti huyo wa AU pia ameutaka Umoja wa Mataifa kuongoza jitihada za kupunguza makali ya bei ya mafuta na bei ya chakula duniani, kama njia ya kuzilinda nchi changa zaidi, hasa zile za Afrika, dhidi ya makali ya bei hizo.
Rais Kikwete ametoa msimamo huo wa Afrika wakati anahutubia Mkutano wa 63 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo (Jumanne, Septemba 23, 2008) kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini New York, Marekani.
Rais Kikwete alikuwa kiongozi wa 12 kuzungumza katika kikao cha mwaka huu cha UN yenye nchi wanachama 192 na alitoa msimamo wa Afrika baada ya ripoti ya utangulizi ya Katibu Mkuu wa Umoja huo, Ban Ki Moon uliofuatiwa na hotuba za Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, Rais George W Bush wa Marekani, Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, Rais Gloria Macapagal-Arroyo wa Philippines na Sheikh Hamad bin Khalifa Al-Thani wa Qatar.
Wengine waliozungumza kabla ya Mwenyekiti huyo wa AU ni Rais Daniel Ortega Saavedra wa Nicaragua, Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia, Rais Abdallah Gul wa Uturuki, Rais Cristina Fernandez de Kirchner wa Argentina, Rais Marc Ravalomanana na Rais Boris Tadic wa Jamhuri ya Serbia.
Katika hotuba yake ya kusisimua, iliyotolewa kwa uchangamfu mkubwa na kupokelewa vizuri, Rais Kikwete ameonya kuwa mtindo wa baadhi ya nchi za Ulaya kuwafungulia mashitaka kwa nia ya kuwakamata viongozi wa Afrika na kuwafikisha kortini kwa sababu mbali mbali ni hatua ya kuwadhalilisha viongozi hao.
Kabla ya kumalizia, ninayo mambo matatu
Jambo la pili ni kuhusu mfumo mpya wa utawala wa kisheria wa kimataifa unaoendeshwa na nchi za Ulaya. Mfumo huu sasa umekuwa na silaha ya kuwadhalilisha viongozi wa Afrika, amesema Raia Kikwete na kuongeza:
Tulilijadili suala hilo katika kikao kilichopita cha Wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika, na tunakusudia kuliwasilisha jambo hilo kwenye Umoja wa Mataifa, ili lichukuliwe hatua mwafaka.
Kuhusu mageuzi ya Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete amesema kuwa Afrika inaunga mkono moja kwa moja mageuzi hayo.
Hata hivyo, Rais ameongeza kuwa AU inaamini kuwa mageuzi katika UN hayawezi kuwa yamekamilisha bila kufanya mageuzi katika Baraza la Usalama la UN.
Kwa upande wa Afrika, tumewaruhusu wawakilishi wetu wa kudumu mjini New York kuanzisha mjadala na pande zote zinazohusika kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama, amesema Rais Kikwete.
Amesisitiza: Hapa sasa nataka kusisitiza msimamo wa Afrika wa kuomba nafasi mbili za kudumu na zenye kura ya turufu, na mbili za kudumu bila kura ya turufu kwenye Baraza hilo. Matakwa yetu lazima yatiliwe maanani kwamba ni kweli kuwa Afrika linabakia Bara pekee lisilokuwa na uwakilishi wa kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama pamoja na wingi wa nchi wanachama wa UN kutoka Afrika.
Kuhusu ongezeko la bei za mafuta na chakula duniani, Rais Kikwete amesema kuwa ni kweli kuwa katika wiki za karibuni bei hizo zimeteremka kidogo, lakini bado ziko juu sana.
Zahama ya bei za mafuta na chakula zikichanganywa na zahama inayokua kila siku katika masoko ya fedha duniani, inatupa kila aina wasiwasi sisi katika Afrika. Hatuwezi kusisitiza kiasi cha kutosha haja ya kusitisha mwelekeo huu. Tunaitaka jumuia ya kimataifa na mataifa makubwa katika uchumi wa dunia kuchukua hatua za haraka kurekebisha jambo hilo. Tunaamini kuwa Umoja wa Mataifa unatakiwa kuongoza mchakati wa hatua dhidi ya zahama hizo.
Rais pia amezungumzia na kujadili kwa undani hali ya kisiasa na usalama katika Afrika ambako ameelezea jinsi Afrika inavyotatua matatizo yake, hali ya Darfur, hali ya Somalia, hali ya Mashariki kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hali ya Zimbabwe, mahitaji ya maendeleo ya Afrika, hali ya Sahara Magharibi na mchakato wa Helsinki, ambao uliongozwa na wanachama wenza, Rais Kikwete na Rais wa Finland, Tarja Halonen.