Nakala ya KULIKONI katika soft copy
Zigo la tuhuma za Rostam sasa mwiba mkali kwa CCM
*Lowassa, Msabaha, Karamagi walishawajibika
*WanaCCM wastuka yeye kukwepa ya Richmond
MWANDISHI WETU
Dar es Salaam
MBUNGE wa Igunga na mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rostam Aziz, anayekabiliwa na zigo la tuhuma za ufisadi na bado ameshindwa kuzikanusha, anaendelea kushikilia nyadhifa zake hatua ambayo sasa, kuelekea uchaguzi mkuu 2010 inakiweka njia panda chama hicho na Serikali yake.
Tayari CCM imejikuta ikikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi baada ya kushindwa kuchukua hatua kukabiliana na baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi na hatua ya watuhumiwa hao kungangania uongozi si wa mashina au majimbo, bali hata ule wa ngazi za juu za maamuzi.
Rostam ambaye awali mwaka 1994 aliingia bungeni kutokana na uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Igunga uliotokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Chales Kabeho, ndani ya miaka michache aliibuka kuwa mbunge mwenye nguvu na ushawishi mkubwa ndani ya chama na serikali.
Katika muda wa miaka zaidi ya 15 ambayo Rostam amekuwa mbunge, amepanda chati hadi kufikia kuwa mjumbe wa CC, na almanusura aukwae uwaziri mara baada ya Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani, Desemba mwaka 2005, kama minong'ono iliyoenea wakati huo ilikuwa sahihi.
Lakini tatizo la Rostam ni kutajwa kumiliki kampuni zaidi ya kumi, lakini jina lake, uchunguzi wetu, umeonesha, linaonekana katika kampuni moja tu, African Trade Development (T) Limited, katika namna ambayo sasa inazidi kuibua utata juu ya biashara anazofanya mbunge huyo na malengo au mwelekeo wa biashara hizo.
Madai ya Rostam kumiliki kampuni zisizo na majina yake yalianza kujitokeza lilipozuka sakata la yeye kuhusishwa na kampuni kadhaa zenye kashfa ikiwemo ya Dowans na Kagoda.
Kwa mara ya kwanza jina la Rostam kumiliki Kagoda lilitajwa na mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa, mwaka 2007 katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Mwembeyanga, Tandika, Dar es Salaam.
Dk. Slaa aliwaambia umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo, kwamba Rostam amejificha nyuma ya umiliki wa Kagoda kupitia kwa Francis William na John Kyomuhendo 'wamiliki' walioandikishwa kwenye orodha ya Msajili wa Makampuni (Brela).
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Kyomuhendo na William ni wafanyakazi wa Rostam. Hata hivyo, jina la Rostam halionekani katika ofisi za Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA). Mpaka sasa, Rostam hajakanusha madai hayo ya Dk. Slaa.
Naye Wakili wa Mahakama Kuu, Byidinka Michael Sanze alipigilia msumari katika madai kuwa Rostam ndiye mmiliki wa Kagoda baada ya kunukuliwa katika hati ya kiapo, akisema kuwa Rostam ndiye aliyemtaka kushuhudia hati za mikataba ya Kagoda.
Kampuni ya Kagoda ilichota zaidi ya bilioni 40/- katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Si kosa kisheria kumiliki kampuni nyingi nchini, lakini mwenendo wa Rostam wa kutumia watu wengine na wa ndani ya familia yake majina yao kuonekana katika kampuni alizo na maslahi nazo, ndio si tu unashangaza bali una siri nzito nyuma yake ambayo sasa Watanzania wanapaswa kuijua.
Kwa mfano katika kampuni ya Afritainer ambayo inaonekana kuwa na uhusiano na Kagoda iliyohusika na uchotaji wa fedha za EPA mwaka 2000, yamo majina ya watu wengine na/au wanafamilia yake.
Watumishi wawili tata na ambao KULIKONI linafahamu kuwa ni wasiri wakuu wa Rostam, Tabu Omari ambaye ni katibu muhtasi wake wa miaka mingi na Barati Godda ndio walioandikishwa kama Wakurugenzi wa Afritainer Limited kwa haraka haraka bila kufuata taratibu za BRELA ili waweze kufanikisha uchukuaji wa fedha za EPA.
Kampuni ya Afritainer na kampuni nyingine ya familia ya Rostam ya Africa Trade Development Limited ziliwahi kutumia pamoja namba ya simu ya mezani 2861371 na faksi 2861372, namba ambazo hatimaye baadaye ndizo zilizokuja kutumiwa na Kagoda iliyoanzishwa mwaka mmoja kabla ya kuchota bilioni 40/- za EPA.
Baada ya habari za namba hizo kufichuliwa, kina Rostam waliziachia namba hizo ili hatimaye ziweze kutumiwa na mtu mwingine. Rekodi za Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) zinaonesha wazi jinsi namba hizo zilivyotumika kwa muda mrefu tangu wakati Dar es Salaam ikiwa inatumia kianzio cha namba cha 051. Sasa inatumika 022.
Rostam anatajwa tena katika tuhuma nyingine za kuchukua fedha za serikali bila ya kuwa na mkataba akidai kuagiza mahindi, lakini wakaguzi wakabaini kwamba hakukuwa na ushahidi wa yeye kuingiza mahindi nchini. Hata taarifa hizo zilipoanikwa kwa mara ya kwanza hivi karibuni, mwanasiasa huyo hakukanusha.
Kuna utata pia katika kuhusika kwa Rostam katika umiliki wa Dowans. Wakati anuani na barua pepe za kampuni yake ya Caspian Construction zilitumiwa na kampuni hiyo ya Dowans, Rostam mwenyewe alikana kuimiliki lakini walau mfanyakazi mmoja wa Dowans alipobanwa na Kamati Teule ya Bunge, alifikia karibu kidogo na uhalisia pale alipokiri mbele ya Kamati Teule ya Bunge kuwa Rostam na mwanzilishi wa Dowans huko Dubai, ni maswahiba.
Hata hivyo, taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwemo kauli ya mbunge mmoja kutoka kanda ya Magharibi ambaye ni swahiba mkubwa wa Rostam, Dowans Tanzania, iliyokuja kusajili muda mfupi au wakati wa sakata la Richmond ni kampuni ya Rostam.
Eneo moja la kushangaza na kuibua maswali ni la usajili na/au majina yaliyotumika kusajili kampuni ya African Trade Development (T) Limited ambapo kuna Rostom A. Sakarri, Rostam Sakarri, Rustom Aziz Sakarri, Rustam Sakarri na Rustam Sakaari.
Ukiacha kituko hicho, kampuni nyingine zinazotajwa kumilikiwa na Rostam lakini jina lake halionekani BRELA ni pamoja na Africa Tanneries Limited, Tanzania Leather Industries Limited, Manufactures Limited, Wembere Hunting Safaris Limited na Ticts ambayo pamoja na kelele zote kutokana na kushindwa kazi bandarini, hadi sasa kila kiongozi anagwaya kutekeleza azimio la Bunge lililotaka mkataba wake usitishwe.
Katika Ticts jina linaloonekana ni la Gulam Chaka, ambaye katika kampuni ya African Trade Development (T) Limited, nako kuna jina kama hilo, lakini likiandikwa kwa Gulam Chakar.
Haijafahamika kama Gulam Chakar ambaye amejitambulisha kama mwenyekiti katika African Trade Development (T) Limited., ndiye huyohuyo wa Ticts ambaye huko amejitambulisha kama mkurugenzi.
Jambo la kushangaza kuhusu biashara za Rostam ni pale ambapo hata katika ununuzi wa magazeti ya Rai, Mtanzania, The African, Dimba, Bingwa na Chuo cha Uandishi wa HabariMAMET, kutoka kampuni ya Habari Corporation Limited (HCL), hakuna jina la Rostam, hata hivyo inashangaza kuwa hivi karibuni akizungumza na waandishi wa habari Rostam alikiri kuwa yeye ni mmiliki tu wa kampuni, alipokuwa akikana tuhuma za kuagiza kuchapishwa toleo lililokuwa na lengo la kueneza propaganda zisizo na msingi.
Na ni Rostam huyo huyo ambaye haonekani kwenye majina ya kusajiliwa kampuni hiyo ambapo hivi karibuni magazeti hayo, yalitoa picha akiwa anakabidhiwa kombe mojawapo la ubingwa wa mashindano ya NSSF, ambayo moja ya timu za kampuni hiyo ziliutwaa.
Taarifa zinasema kampuni ya HCL iliuzwa kwa kampuni ya Isenegeja Company Limited, kupitia New Habari (2006) Limited (NHL), ambayo Rostam ni mmiliki.
Hata hivyo, jina la Rostam halionekani katika wakurugenzi na wamiliki wa kampuni ya Isenegeja ambayo sasa imethibitika kwamba ndiyo iliyonunua HCL.
Kwa mujibu wa watu wa karibu na Rostam, ameanza taratibu za kuhamisha uwekezaji wake toka nchini na kwenda nchi za nje ambako huko kinyume na anavyofanya nchini, huko atatumia majina yake katika umiliki wa kampuni zake.
Mojawapo ya mambo yanayotajwa ni mfano wa hilo ni kusudio lake la kutaka kuhamisha hisa alizonazo kwenye kampuni ya Vodacom jambo ambalo limekutana na upinzani kutoka kwa wasimamizi wa sekta ya mawasiliano.
Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya kisiasa na kiuchumi wanasema, Rostam ataweza kuhamisha biashara zake iwapo atafanikiwa kuingia katika timu ya kampeni ya CCM katika uchaguzi ujao.
Huko ndiko Rostam anakotengeneza fedha. Ndiyo maana anahaha kutaka kujisafisha hata kwa kutumia majitaka, ili ateuliwe kuwa mweka hazina wa kampeni zijazo za CCM, alisema kada mmoja wa chama hcho anayefahamu vema mwenendo wa Rostam.
Makada mbalimbali waliozungumzia mwenendo wa mambo hayo kutoka ndani ya CCM wamekiri kuwa mwaka 2010 na hata zaidi ya hapo, miongoni mwa watu watakaoikwaza CCM ni mbunge huyo.
Ni wazi kuwa sasa wananchi wamemuelewa, tatizo liko ndani yetu, hatuko tayari kukisafisha chama, tusubiri kuchafuka zaidi chaguzi zijazo, alisema kada mmoja.
Baadhi ya wana CCM sasa wanahoji inakuwaje Rostam bado anashikilia nyadhifa za juu katika chama wakati ambapo wanaCCM wengine waliacha nyadhifa walizokuwa nazo Serikali baada tu ya kutuhumiwa katika sakata la Richmond.
Wakati wanaCCM kama Edward Lowassa, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha waliwajibika kwa nyadhifa zao, Rostam ambaye ushahidi uliomo kwenye Kamati ya Bunge ni mzito dhidi yake yeye anaendekea kuhudhuria Kamati Kuu ya CCM, kikao muhimu ambacho kinapojadili masuala ya msingi kiutawala na kisiasa kitaifa, Rostam moja kwa moja anakosa nguvu ya kimaadili (moral authority) kushiriki au kuamua mambo hayo kutokana na tuhuma nzito na ushahidi ambao hadi sasa hajaweza kuukana.
Swali la msingi ni nguvu zote hizo za kutogusika wala kuchukuliwa hatua anazitoa wapi na kama kwa nguvu hizo ataendelea kuendesha biashara zake namna hiyo milele?