Wale wanaoendelea kudoubt what i am fighting for should look at this...
Ubelgiji yamuonya JK
MPASUKO ZANZIBAR
na George Maziku
SERIKALI ya Ubelgiji imemtaka Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua za haraka kuumaliza mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar, kwa kuwa unatia doa na kuhatarisha utulivu wa kisiasa nchini.
Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Balozi wa Ubelgiji nchini, Peter Maddens, katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima yaliyofanyika ofisini kwake, Upanga, jijini Dar es Salaam.
Balozi Maddens alitahadharisha kuwa, kama hatua za makusudi na madhubuti hazitachukuliwa na watu wenye mamlaka juu ya mgogoro huo, hususan Kikwete, basi Tanzania inaweza kushuhudia machafuko, ghasia na mauaji kama ilivyotokea hivi karibuni nchini Kenya na hali tete ya kisiasa inayoinyemelea nchi ya Zimbabwe.
Hali ya kisiasa ya Zanzibar inatutia mashaka wote. Kuna kila dalili kuwa mambo yanaweza kuharibika wakati wowote kama hatua madhubuti za kumaliza mgogoro wa kisiasa uliopo hazitachukuliwa, na katika hili tunaamini Rais Kikwete anawajibika moja kwa moja kutokana na madaraka aliyonayo kiserikali na katika chama chake, alisema Balozi Maddens.
Alisema kuwa kwa tathmini yake, baada ya sherehe za Krismasi za mwaka jana, Tanzania ilikuwa inaongoza kwa uthabiti na utulivu wa kisiasa kuliko nchi zingine zote katika ukanda wa mashariki na kusini mwa Afrika, na hata Afrika nzima kwa ujumla.
Lakini alisema kwa sasa hali ya kisiasa nchini ni ya mashaka makubwa, baada ya kushindikana kwa mazungumzo ya muafaka kati ya vyama vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Kwa tathmini yangu, baada ya Krismasi, Tanzania ilikuwa inaongoza kwa uthabiti na utulivu wa kisiasa katika ukanda wa Afrika Mashariki, kusini na hata Afrika yote kwa kuangalia yaliyokuwa yanatokea nchini Kenya na Zimbabwe, lakini leo siwezi kusema hivyo, sababu ipo wazi, mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar unatia doa na kusababisha mashaka makubwa, alisema Maddens.
Kauli hiyo ya onyo kutoka moja ya nchi wafadhili wa Tanzania, imekuwa ya kwanza kutolewa, baada ya kuwepo dalili za wazi za kurudia kuchafuka kwa hali ya kisiasa visiwani Zanzibar, kutokana na hatua ya hivi karibuni ya kukwama kwa mazungumzo ya kutafuta suluhisho la kudumu la mgogoro wa kisiasa visiwani humo.
Balozi huyo anatoa kauli hiyo wakati tayari kukiwa na tamko la baadhi ya wanachama wa CUF waliodai kuwa wako tayari kuanza kujitoa mhanga, kupigania haki zao Zanzibar.
Dalili za mgogoro wa kisiasa wa hivi sasa Zanzibar zilianza zaidi ya muongo mmoja uliopita, hususan baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, ambao matokeo yake yalikataliwa na CUF, ikidai kuporwa ushindi wake na CCM.
Kufuatia kuibuka kwa mgogoro huo, juhudi mbalimbali za kuleta mapatano zilifanywa na watu na taasisi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo Jumuiya ya Madola ambayo ilifanikisha kufikiwa muafaka mwaka 1999, ambao hata hivyo, haukutekelezwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa pili wa vyama vingi mwaka 2000, mgogoro ulizidi kukua baada ya matokeo ya uchaguzi huo kukataliwa tena na CUF.
Wakati huo, mgogoro ulichukua mkondo mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa ule wa kwanza, ambapo makumi ya Wazanzibari wafuasi wa CUF, waliuawa wakati wa maandamano ya Januari 2001 walipokuwa wakikabiliana na vyombo vya usalama.
Tukio hilo lilikwenda sambamba na uamuzi wa baadhi ya Wazanzibari na hususan Wapemba kukimbilia eneo la Shimoni, Mombasa nchini Kenya, walikoishi kwa muda kama wakimbizi wa kisiasa.
Kupuuzwa kwa utekelezaji wa muafaka wa Oktoba 10, 2001, kati ya vyama vya CUF na CCM, kulisababisha mgogoro huo kuendelea hata baada ya uchaguzi mkuu wa tatu wa vyama vingi visiwani humo mwaka 2005.
Akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania mwishoni mwa mwaka 2005, Rais Jakaya Kikwete, aliahidi kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa kisiasa Zanzibar, na akamwagiza Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, kuwasiliana na mwenzake wa CUF, Seif Sharif Hamad, ili waanze rasmi majadiliano ya kutafuta muafaka.
Mwezi Februari mwaka juzi, Makamba na Hamad wakiongoza kamati ya muafaka iliyoundwa na wajumbe kutoka vyama vyao, walianza rasmi majadiliano ya kutafuta muafaka wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar.
Julai mwaka jana mazungumzo hayo nusura yavunjike, baada ya kuwepo kauli za kutatanisha zilizodaiwa kutolewa na Makamba na viongozi wengine wa CCM.
Katika hatua hiyo, Kikwete aliyanusuru mazungumzo hayo kwa kuwasihi CUF kurudi katika meza ya majadiliano, huku akiahidi mazungumzo hayo kukamilika mapema iwezekanavyo.
Mapema mwaka huu, CUF ilitangaza kukamilika kwa mazungumzo na kusema kuwa vyama hivyo vimekubaliana kuunda serikali ya mseto visiwani Zanzibar, kama njia ya kuutibu mpasuko wa kisiasa.
Hata hivyo, mambo yaligeuka wiki chache baadaye, pale Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, zilipokutana Butiama mkoani Mara na kuibuka na pendekezo la kufanyika kwa kura ya maoni kabla ya kukubalika kwa pendekezo la serikali ya mseto kuanzia mwaka 2010. Hilo liliwafanya CUF wahamaki na kuwaona CCM kama watu wa hadaa na chama hicho kikuu cha upinzani visiwani kikatangaza kujitoa katika mazungumzo hayo. Hivi sasa, wakati CCM ikiwa inahangaika kuwarejesha CUF katika meza ya mazungumzo, chama hicho cha upinzani kimekuwa kikiendesha maandamano nchi nzima, kuishinikiza CCM iyasaini makubaliano hayo.