Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
''Kila chini ya paa la nyumba kuna historia,'' maneno haya aliniambia Dome Okochi Budohi mwaka wa 1972 nyumbani kwake Ruiru, nje kidogo ya Nairobi.
Hapo juu ni picha ya Ring Street na Upanga Road miaka ya 1950.
Sasa hapa ni makutano ya Mtaa wa Jamhuri na Mkwepu Street hilo jengo kulia lilikuwa linaitwa Diamond Trust Building.
Hivi sasa pana duka la Bakheresa. Katika miaka ya 1950s hapo lilipo duka la Bakhresa lilikuwa duka la Assanand likiuza vifaa vya muziki kama magita, gramafoni na santuuri zake na vitu vingine vinavyoendana na muziki.
Dome Okochi Budohi aliyekuwa mmoja wa viongozi wa TAA aliyeingia madarakani na Julius Nyerere katika ule uchaguzi wa Arnautoglo 17 Aprili, 1953 alikuwa akifanya kazi katika duka hili.
Assanand alikuwa Muhindi wa Kenya na alikuwa na maduka makubwa ya muziki katika miji yote mikubwa Afrika ya Mashariki.
Duka lake kubwa na maarufu lilikuwa Nairobi River Road na lingine Mombasa Salim Road sasa Moi Avenue.
Haya maduka yapo hadi sasa.
Dome Budohi kadi yake ya TANU ni no. 6.
Nimeieleza historia nzima ya Budohi katika kitabu cha Abdul Sykes kuanzia uanachama wake ndani ya TAA na hatimae TANU hadi kukumatwa kwake akituhumiwa kuwa mmoja wa Mau Mau, kuwekwa kifungoni kwenye kambi ya Mau Mau Handeni ambako Rashid Kawawa alikuwa mmoja wa wafanyakazi kutoka Welfare Department, hadi kurudishwa kwao Kenya ndani ya mabehewa ya ng'ombe yeye na wenzake wakiwa wamefungwa minyororo miguuni na kufungwa jela kisiwani Lamu na kuachiwa kwake kabla ya uhuru wa Kenya.
Historia ya TANU na harakati za kudai uhuru wa Tanganyika ina mashujaa wengi na mambo mengi ambayo bado hayajaandikwa.
Hii ni picha ya mwaka wa 1958 baada ya Uchaguzi wa Kura Tatu ambao mpiga kura alitakiwa kumpigia kura Mzungu Muasia na Mwafrika.
Picha hii inaonyesha Mzungu, Muasia na Mwafrika walioshinda katika uchaguzi ule wakiwa wagombea wa TANU.
Ninapopataka si hapo bali ni Ring Street niliyoitaja hapo juu.
Wakati TANU inatayarisha safari ya pili ya Nyerere UNO mwaka wa 1957, Nyerere alikutana katika mtaa huo na Amir Jamal.
Amir Jamal baada ya kusalimiana na Nyerere akamuambia kuwa alikuwa anamtafuta sana.
Amir Jamal akaingiza mkono mfukoni akatoa fedha akampa Nyerere akamwambia hizi anampa zimsaidie katika safari yake.