Mkuu Mag3 hebu soma hapa chini uone kuwa sio kweli kwamba wananchi wote wanaamini maneno yenu against mama Kilango,
KONA YA KARUGENDO: Mama Socrates wa Tanzania
Padri Privatus Karugendo Julai 2, 2008
ANNE Kilango Malecela, Mbunge wa Same Mashariki, akichangia hotuba ya Bajeti Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo, alijifananisha na mwanafalsafa wa zamani Socrates. Alisema yuko tayari kufa akitetea ukweli.
ANNE Kilango Malecela Socrates alikataa kwenda kinyume na yale aliyokuwa akiyaamini na kuyatetea katika jamii ya wakati wake. Wafuasi wake walimbembeleza akubali kukana ukweli, ili apone kifo. Enzi hizo Socrates, alikuwa muhimu sana katika jamii na alikuwa mwalimu wa kutegemewa na watu wengi.
Hivyo wafuasi wake waliona ni bora, akane ukweli, ili aendelee kuwapo kuwafundisha na kuibua mambo mapya katika ulimwengu wa fikra. Lakini Socrates alikataa kukana ukweli, maana hakuna heshima ya mwanadamu kuzidi mtu kufa akitetea ukweli. Hivyo Socrates, alikubali kufa kwa kunywa sumu! Galileo Galilei, mwanasayansi na bingwa wa hisabati wa kale wa Italia, aliyeshutumiwa kwa mawazo yake kwamba dunia ilikuwa mviringo na inalinzuguka jua, alipata kusema kwamba ukweli mara zote ni rahisi kuuelewa pindi unapougundua; tatizo ni jinsi ya kuugundua. Niongezee hapa kwamba na pindi mtu anapougundua ukweli, na kwa vile mara zote ukweli ni rahisi kuuelewa, ni lazima mtu awe tayari kuufia ukweli huo.
Anayekubali kusaliti ukweli, anausaliti utu wake na heshima yake kama binadamu. Imeandikwa kwenye Biblia, kwamba Musa, alinyosha mikono na jua likasimama.Usiku haukuingia, hiyo ikawasaidia wana wa Israeli kupambana na maadui zao. Uvumbuzi wa ukweli wa Gelileo, ulipingana na dhana hii, maana jua limesimama daima, na kinachozunguka ni dunia. Galileo, alikuwa tayari kufa akitetea ukweli huu. Ameheshimika hadi leo hii, na ukweli umebaki ule ule kwamba dunia ni mviringo na inazunguka jua.
Anne Kilango Malecela au Mama Socrates wa Tanzania, ameugundua ukweli juu ya udhibiti na ulinzi mbovu wa fedha za umma. Na kwamba fedha nyingi ziko mikononi mwa watu wachache. Na kwamba watu wachache hawa wakiendelea kushikilia fedha hizi peke yao, hatuwezi kuendelea. Ametoa mfano wa fedha za EPA, zilizoingia mikononi mwa watu wachache kwa njia za udanganyifu. Ukweli huu unamfanya mama huyu awe tayari kufa, kama alivyosema menyewe, kama watu wengine waliokufa wakiutetea ukweli.
Mwanafalsafa mwingine wa zamani wa Ujerumani, Arthur Schopenhauer, aliyeishi kati ya mwaka 1788 na 1860, alisema hivi ju ya ukweli: ukweli wowote hupitia ngazi tatu. Kwanza, ngazi ya kukejeliwa. Pili, ngazi ya kupingwa na hata ikibidi damu kumwagika. Na tatu, ni ngazi ya kukubalika; kwa kuwa ukweli hujisimamia wenyewe.Hivyo kwa hoja ya Arthur Schopenhauer, haishangazi kuona akina mama Anna Abdalah, Chitalilo na wengine wanamkejeli Anne Kilango. Wanasema anapayuka, wanasema anazungumza kwa mbwembwe, wanasema lengo lake ni kutaka kugombea kiti cha Mwenyekiti wa Taifa wa UWT, wanafikiri anakisaliti chama chake cha CCM, wengine wanakwenda mbali kusema kwamba ana hasira za kushindwa kuingia Ikulu 2005, kwamba mbio za Mzee Malecela ziliishia sakafuni.
Hizo zote ni hatua za kupita katika kutafuta ukweli. Na jinsi hali inavyokwenda, na labda ndiyo maana Anne Kilango, anasema haogopi- inawezekana hata hatua ya pili ya kumwagika damu tukaipitia, (bila hekima, busara na uzalendo) kabla ya ukweli wenyewe kukubalika na kujisimamia.
Ingawa sifahamu vizuri historia ya mama huyu Socrates wa Tanzania, hoja zake zinashawishi na kuwagusa Watanzania wengi wa kawaida. Uchumi wa Tanzania, uko mikononi mwa wachache. Wakati maisha yanaendelea kuwa magumu, bei ya mafuta inapanda, mfumko wa bei unashika kasi ya kutisha, lakini wachache wetu wanaogelea katika ufahari.
Wanafanya manunuzi na matumizi yao nje, wanasomesha watoto wao nje, wakiugua wanakimbizwa India, Ulaya au Marekani. Wamejenga majumba ya kifahari na wanaendesha magari ya bei mbaya. Ipo mifano mingi ya kuelezea jambo hili na Watanzania wengi sasa wanafahamu.
Panahitajika watu wachache wa kusimama na kutetea ukweli. Utafiti wa haraka unaonyesha kwamba idadi kubwa ya Watanzania inashawishiwa na mawazo ya watu kama kina Anne Kilango, kuliko ya Chitalilo na Mzindakaya.
Hoja yangu ni kwamba kila raia mwema wa Tanzania, hawezi kupuuzia msimamo wa kutafuta na kusema ukweli. Mbegu ya kutafuta na kusema ukweli haiwezi kuoza. Ni hekima kwa viongozi kuanza kusoma alama za nyakati.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa S. L. P. 114 Magu, Mwanza. Simu: 0754 633122