Kilimo ni ukombozi, japokuwa kwa nchi yetu kinaonekana ni kazi ya walala hoi, isiyo na thamani na inayowahusu watu masikini. Kwa kupitia uzoefu mdogo nilioupata kwenye kilimo, ninadiriki kusema kuwa, kilimo ni fursa, kilimo ni ukombozi, kilimo ni mafanikio kwa watu na nchi. Ni jambo la kawaida mkulima kuwekeza milioni tatu na baada ya miezi mitatu akapata milioni kumi na tano au ishirini. Hii haina maana kwamba hakuna hasara, hasara zipo hasa kwa kilimo chetu cha kutegemea hisani ya mvua.
Kwa sababu za kimaisha na majukumu, nililazimika kuhamia kwenye mkoa wa Dar Es Salaam, na kwa kuwa nilitoka mazingira tofauti, nilikutana na changamoto ya gharama kubwa za maisha ambapo kila kitu hususani cha kula kilipatikana kwa kununuliwa. Nilizungukia masoko karibia yote yanayouza vyakula na kujionea wingi wa bidhaa zinazoingia sokoni kila siku na ifikapo jioni ni kama vile hakuna mzigo ulioingia. Kwangu mimi, hii niliona ni fursa ya kuniwezesha kuongeza kipato na kupunguza ughali wa maisha.
Niliamua kuuzungukia mkoa wa Pwani ili kuona kama ninaweza kupata japo kipande cha shamba ili nilime kwa ajili ya matumizi yangu na ziada iwe kwa ajili ya kuuza. nilivutiwa zaidi na wilaya ya Bagamoyo kwa sababu mbili hasa: Kwanza Ukaribu na Dar Es Salaam ambapo kuna soko kubwa la mazao na pia uwepo wa miundombinu ya usafirishaji ambayo ni mizuri na rafiki. Pili ni urahisi wa upatikanaji wa mashamba tena yenye rutuba ambayo yanaruhusu kustawi kwa mazao mbalimbali kama vile mahindi, alizeti, ufuta, mhogo, viazi vitamu na hata mbogamboga kwa aina zote.
Nilifanikiwa kupata ekari kumi (10) za kukodi, na niliamua kulima mahindi kwa sababu ya urahisi wa kuuzika pindi unapovuna. Na baada ya kuifanya hii kazi ya kilimo kwa takribani miaka kumi(10), kuna mafanikio ambayo nimeyaona japokuwa kuna changamoto zinazotokana na hali ya hewa kama mvua kuwa chini ya kiwango na hivyo kupelekea kupata hasara kubwa. Sera na miongozo ya kiutawala nazo ni sehemu ya changamoto kwani hupelekea kuporomoka kwa bei za mazao ya wakulima wakati mwingine.
kwa sababu ya manufaa, nimepanua eneo la mradi kutoka ekari kumi (10) za kukodi hadi kumiliki ekari arobaini (40) ambazo zote kwa sasa zipo kwenye matumizi. Na ili kuongeza tija, ninatakiwa nitumie mbolea ili kuongeza mavuno. Kwa sasa ninalima pasipo kutumia mbolea na wastani wa mavuno kwa ekari ni kati ya gunia 10 mpaka gunia 16 kwa ekari wakati kwa kutumia mbolea mavuno yalitakiwa kuwa kati ya gunia 25 mpaka gunia 35 kwa ekari. Kwa sasa situmii mbolea kwa kuhofia kuyakaanga mazao pindi mvua ikinyesha chini ya kiwango, ikizingatiwa kuwa ukanda huu wa Pwani huwa haupati mvua kwa kipindi kirefu kama ilivyo kwenye kanda ya Ziwa, kanda ya Kaskazini na Nyanda za juu Kusini. Na pia kilimo ninachofanya ni kilimo cha msimu, yaani, ninalima mara moja kwa mwaka na kusubiri hadi msimu mwingine wa mvua hivyo kuchelewa kupata mafanikio.
Nilinuia kufanya kilimo cha umwagiliaji, na ili hili lifanyike, ilinibidi niwatafute wataalamu wa maji na umwagiliaji. Kwanza niliwatafuta Drilling and Dam Construction Agency (DDCA) ambao ni taasisi ya serikali iliyowezeshwa kwa utaalam na vifaa ili kuwezesha upatikanaji wa maji kwa kuchimba visima virefu na mabwawa. Nilichoambulia ni kupewa namba za watu binafsi ambao ni wa nje ya taasisi. Kwao ni kama waliona ni fursa badala ya huduma, kwa hiyo sikupata huduma wala msaada kama nilivyotarajia. Changamoto nyingine kwa DDCA, namba zao nyingi zilizopo kwenye website hazipatikani ama hazipokelewi. Nilipowasiliana na taasisi binafsi walifika shambani na kufanya utafiti wa kisima (ground water) na report ikaonyesha maji yatakuwa na kiwango kikubwa sana cha chumvi hivyo hayatafaa kwa mazao badala yake eneo linafaa kwa lambo/bwawa (earthen dam) kwani lina bonde / korongo linalopita kati kati ya shamba hivyo hupelekea maji mengi kupitia pale pindi inaponyesha mvua. Ukubwa wa bwawa lililopendekezwa kwa uvunaji wa maji ya mvua ni; urefu mita 200, upana mita 100 na kina mita 3 (200*100*3 water catchment area) hivyo kuwa na uwezo wa kukusanya na kuhifadhi maji kati ya lita 25,000,000 (milioni Ishirini na Tano) mpaka lita 45,000,000 (milioni Arobaini na Tano) ambazo zinatosheleza kwa mahitaji ya kilimo cha mwaka mzima.
FURSA ZINAZOAMBATANA NA KILIMO NIFANYACHO
Kutokana na mabaki ya mahindi mengi shambani pamoja na wadudu wanaozalishwa kutokana na mabua na magunzi mengi yanayooza, nimeanzisha ufugaji huria wa kuku wa kienyeji. Nilianza na kuku kumi na saba (17) na baada ya miezi minne wapo kuku mia mbili na ishirini (220). Ikumbukwe ninafanya ufugaji huria hivyo hakuna gharama, matarajio ni kuwa na kuku elfu mbili (2000) baada ya mwaka mmoja na nusu.
Fursa nyingine iliyopo na ambayo haijatumika ni ufugaji wa ng'ombe ama wanyama wa jamii yake ikiwa ni pamoja na ufugaji wa kunenepesha, hii ni kwa sababu mabua ya mahindi ni chakula kizuri sana kwa mifugo. Kwa kutokuwa na maji huwa ninalazimika kuyachoma kwani sina matumizi nayo. Hii inatokana na ukweli kwamba huwezi kufuga wanyama bila kuwa na maji kwa ajili ya kuwanywesha na pia kuoteshea majani ya malisho kwa ajili ya kuchanganya na mabua ili kupata ukuaji mzuri wa wanyama.
CHANGAMOTO KATIKA KUWA NA MAJI SHAMBANI
Gharama kubwa za upatikanaji wa maji, mathalani, kwa aina ya bwawa lililopendekezwa pamoja na mifumo na vifaa vyote ya umwagiliaji inatakiwa Tsh 60,000,000/= (Milioni sitini) kiasi hiki ni kikubwa sana kwa mkulima anayejitafuta, hasa ikizingatiwa kinatakiwa kilipwe kwa wakati mmoja.
Niliwasiliana na wizara ya kilimo kupitia mfuko wa pembejeo kuhusu uwezekano wa uwezeshwaji, bahati mbaya ni kwamba, kila mtu niliyezungumza naye alikuwa hana uhakika kama kuna huo utaratibu au haupo, hivyo kubaki nikiwa sina uelekeo. Baadaye nilipata taarifa kuwa serikali imezipatia bank fedha kwa ajili ya kuwakopesha wakulima na wafugaji kwa lengo la kuleta tija kwenye kilimo. Kwa upande wa Bank walisema ni kweli wana huo utaratibu wa mikopo kwa wakulima, lakini kwa miradi ya visima na mabwawa hawana uzoefu nayo, hivyo wao wanakopesha uendeshaji wa kilimo na siyo ujenzi wa miundombinu.
NINI KIFANYIKE
Serikali kupitia wizara ya kilimo isimamie ujenzi wa visima na mabwawa kwenye maeneo ya wakulima kutegemeana na nature ya eneo husika ili kukifanya kilimo kisiwe tegemezi kwa mvua badala yake kiwe cha umwagiliaji na hivyo kifanyike kwa kipindi chote cha mwaka. Hii itasaidia kuchagiza uzalishaji na kuleta mafanikio kwa wakulima nchini ambayo yatatumika kama motisha kwa vijana wasomi wanaotafuta ajira. Mradi wa Building a Better Tomorrow (BBT) utekelezwe katika utaratibu wa kuwaunganisha (attach) vijana wageni katika kilimo na watu walioko kwenye sekta ya Kilimo ambao wamewezeshwa kwa kujengewa miundombinu na vitendea kazi, hili lizingatie mgawanyo wa kikanda na mikoa wanaokijua kilimo pamoja na chanamoto zake, hivyo haitakuwa rahisi kwa hawa wakulima wapya kukata tamaa. Vilevile, wakulima waliowezeshwa wawekewe malengo ya uzalishaji, mafanikio na utengenezaji wa ajira mpya kupitia shughuli zao za kilimo.
Mikopo ya kilimo inayotolewa kupitia mabenki ilenge kwenye kukifanya kilimo kuwa ni cha umwagiliaji, endelevu na chenye tija. Utafutwe utaratibu maalum ambao utamfanya mkulima ambaye hana mfumo wa umwagiliaji asipewe pesa mkononi bali zielekezwe kwenye kujenga miundombinu ya umwagiliaji kama visima na mabwawa kutegemeana na eneo husika. DDCA kupitia kanda zake iwe ndiye mdau namba moja kwa kutoa utaalam au kufanya kazi za ujenzi na uchimbaji wa visima na mabwawa kusudi pesa inayolipwa iende kwenye kuongeza uwezo wa taasisi na wakitaalam.
Soko la mazao ya kilimo kama chakula kwenye nchi zinazotuzunguka, iwe ndiyo chachu ya kuongeza uzalishaji na kukifanya kilimo chetu kuwa ni chanzo kikubwa cha ajira na kipato kwa vijana na watanzania kwa ujumla. Ni ukweli usio na shaka kwamba watu hupenda kufanya kazi ambayo wanajua itawaletea mafanikio, na ikiwa kilimo kitakuwa ni chanzo cha mafanikio kwa wakulima, ni hakika kwamba vijana wengi watavutiwa kufanya kilimo, na hii itawezekana ikiwa tu kuna bei nzuri ya mazao. Na kwa kuwa wafanyabiashara toka nje ya nchi hununua mazao kwa bei nazuri, ni budi serikali iweke utaratibu mzuri wa kupata mapato kutoka kwao badala ya kuwazuia kununua moja kwa moja kutoka kwa wakulima. Inapotokea wamezuiwa, huwa kunazalishwa tabaka la madalali ambao siku zote hujiangalia wao na hivyo kumkandamiza mkulima. na pindi hili litokeapo idadi ya watu wanaolima ikiwa ni pamoja na uzalishaji huwa vinaporomoka kwa kasi ilhali bei inapokuwa ni nzuri na yenye kuvutia, idadi ya wakulima pamoja na uzalishaji huwa vinaongezeka kwa kasi. Tuifanye Tanzania iwe ni ghala la chakula kwa nchi za Afrika.
Na kwa kuwa idadi kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini na kilimo ndiyo njia yao pekee ya kukidhi mahitaji yao ya kila siku, hatuna budi kuwa na mtazamo tofauti juu ya kilimo. Ni vyema sote kwa umoja wetu tukajua kuwa, kilimo ni uchumi, kilimo ni maisha na kilimo ni mstakabri wetu kama jamii na nchi, hivyo, yapasa kipewe hadhi na thamani stahiki ili kituheshimishe na kutuletea manufaa ikiwa ni pamoja na maendeleo.

Upvote
5