SoC02 Kilio chetu

SoC02 Kilio chetu

Stories of Change - 2022 Competition

PeterMakrina

New Member
Joined
Oct 29, 2021
Posts
1
Reaction score
1
Kama ilivyo asili yetu Watanzania kupumzika majira ya jioni baada ya shughuli mbalimbali za hapa na pale za kutupatia mlo, kupata wasaa wa kujumiaka na ndugu, jamaa na marafiki zetu (vijiweni).

Ndipo tunapo jadili mambo mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii hasa yanayoendelea katika nchi yetu pendwa ya Tanzania kwani penye wengi pana mengi.

Mjadala kuhusu ongezeko la tozo katika bidhaa na huduma mbalimbali umekuwa moja ya mjadala kafika zaidi siku hizi.

Watu wengi hupata muda wa kujielezea na kutoa mawazo yao kuhusu ongezeko la tozo ikiwemo ni pamoja na faida na hasara zake kwa watanzania ambapo wengi wao wanalalamikia ongezeko hilo na kudai limepelekea kupanda kwa gharama za maisha.

Sio vijiweni tu, la hasha! bali hata katika mitandao ya kijamii mjadala kuhusu ongezeko la tozo umapata nafasi huku watanzania waliopata nafasi ya kuchangia kutoa maoni yenye kuonyesha serikali imewapa mzigo mkubwa wasioweza kuubeba.

Nafuu ya maisha ya watanzania hasa wenye maisha ya kawaida kwa hivi sasa kupitia serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutaipata wapi ikiwa kila huduma muhimu kuna ongezeko la tozo?

Ni miongoni mwa maswali yaliyisikika kutoka kwa wananchi nchini Tanzania baada ya serikali kupandisha tozo katika huduma na bidhaa mbalimbali. Mnamo tarehe 15 Julai mwaka 2021, serekali ya Tanzania ilipandisha tozo ya miamala ya fedha kupitia mitandao ya simu na hivyo kusababisha kuongezeka gharama hasa kwa wananchi wanaotumia mitandao hiyo katika kufanya miamala.

Kwa mujibu wa serikali, ongezeko la tozo katika bidhaa na huduma mbalimbali limewekwa kwa lengo la kuongeza mapato ya nchi ingawa ongezeko la tozo limeonekana kuwa mzigo mkubwa wananchi wa Tanzania
Nukuu “Baadhi ya wataalamu wa masuala ya kodi na uchumi nchini Tanzania wanasema serikali haikufanyia utafiti wa kutosha sheria ya tozo ya miamala ya kielektroniki ya mwaka 2022, na kwamba inakwenda kinyume na kanuni za kimataifa katika masuala ya kodi” (DW. Idhaa ya kiswahili, Maswala ya jamii, 22.8.2022).

Kufika sasa nchini Tanzania kunaongezeko la tozo kwenye bidhaa na huduma mbalimbali mfano tozo kwenye mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, tozo kwenye mita za luku kutokana na jinsi mtumiaji anavyotumia, pamoja na nyingine nyingi.

Ongezeko hili la tozo limewafanya baadhi ya wananchi kutoa mawazo yao mitandaoni na kudiriki kusema hakuna haja ya kutumia njia za mitandao katika kutuma fedha ni afadhali ya kutumia bodaboda au kupakia gari na kupeleka fedha hizo kunakohusika kwani tozo katika miamala inaongeza gharama sana.

Licha ya ongezeko la tozo kuongeza mapato ya nchi, limeleta athari ambazo zinaathiri uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na uchumi wa taifa letu la Tanzania kwa ujumla. Athari hizo ni pamoja na:

•Mfumuko wa bei za bidhaa na huduma na hivyo kuongeza ugumu wa maisha hasa kwa watanzania wa kawaida. Ongezeko la fedha katika miamala ya (tozo), limesababisha kuongezeka kwa gharama za huduma na bidhaa hasa kwa wale wanaolipia kwa njia ya simu.

•Kupungua kwa biashara za mitandaoni. Watu wengi waonafanya manunuzi mtandaoni hulipia kwa njia na simu na hivyo kujikuta wahanga wakubwa wa ongezeko la tozo kwenye miamala ya simu. Hii imeathiri wafanyabiashara hao kwani wateja wao wamepungua kwa kuepuka kuongezeka kwa gharama wakati wa kufanya miamala.

•Mfumuko mkubwa wa bei katika bidhaa na huduma mbalimbali kwa watanzania kutokana na ongezeko la tozo kwenye mafuta ya petrol na dizeli. Mfumuko huu mkubwa wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali unasemekana kuwa matokeo ya madhara ya vita vya Urusi na Ukraine ilihali kwa upande mwingine ni kwa sababu ya ongezeko la tozo mbalimbali.

Mfumuko huu wa bei umewaathiri sana watanzani na kupelekea baadhi yao kushindwa kupata bidhaa na huduma pale wanapozihitaji kwani gharama ni kubwa mno.

Ni wakati sasa wa serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutazama jambo hili la tozo kwa jicho la pili kwani ongezeko la tozo limekuwa kilio cha watanzania walio wengi.

Serikali itafute namna ya kuweza kupata mapato bila ya kuwatoza wananchi wake tozo kubwa kwani tozo kubwa imekuwa mzigo mkubwa unaowaelemea. Kwa kufanya hivyo, wananchi wataimarika kiuchumi na hatimaye kuimarika kwa uchumi wa nchi yetu ya Tanzania.

Serikali ipitie tena sheria ya VAT na kufanya marekebisho ikiwa ni pamoja na kupunguza kodi ya ongezeko la thamani, VAT kutokana na ongezeko tozo ili kuweza kupunguzia wananchi maumivu ya kupanda kwa gharama za kimaisha.

Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na rasilimali nyingi zinazoweza kutumika kama chanzo cha mapato. Serikali iendelee kutumia rasilimali hizi kwa umakini na ufasihi mkubwa zaidi ili zitumike katika kuongeza mapato ya nchi yetu.

Pia tafiti yakinifu zifanyike juu ya namna ya kuweza kupata vyanzo vipya vya kimapato badala kutumia njia zinazowaumiza wananchi.

Nchi inaweza kupata mapato, kujiendeleza na kujiendesha katika shughuli za kila siku hasa katika kukuza uchumi wa nchi na kuwapa wananchi maisha bora bila kuwatoza wananchi tozo kubwa zinazowaumiza na kuwakandamiza.

Tunaomba serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano kufanya mabadiliko na kuwasaidia wananchi wake kwa kupunguza tozo katika bidhaa na huduma mbalimbali.

Kwa kufanya hivyo serikali itakuwa imefuta machozi ya watanzania walio wengi walio elemewa na mzigo mzito wa ongezeko la tozo katika bidhaa na huduma mbalimbali.

Maendeleo ya Tanzania bila tozo kubwa kwa Watanzania inawezekana.

Mwandishi: Makrina
Simu: 0756376302
Baruapepe: makrinasimoni@gmail.com
 
Upvote 2
Back
Top Bottom