Mwanasiasa mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru, amewajia juu baadhi ya viongozi wa Kanisa Katoliki nchini waliodai kuwa yeye ni fisadi na kuwataka wanaodhani kuwa ni wasafi kumzidi, wajitokeze hadharani.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Kingunge alisema wakati anatoa angalizo juu ya Waraka na Ilani ya Kanisa hilo bungeni, hakuwa anatafuta ugomvi na viongozi hao wa kidini, ndiyo maana alilizungumza kwa adabu na kwa heshima ili kuepuka kuingia kwenye malumbano. Alisema alitarajia maaskofu wangetafakari angalizo lake kwa makini, lakini kwa bahati mbaya hawakufanya hivyo; badala yake wakamkejeli, wakamtukana na wengine kudiriki kumwita kuwa fisadi.
Hawa walioniita mimi fisadi ni vyema wakaenda kuungama na kufanya toba maana wamefanya dhambi kubwa kuniita fisadi
walitaka nisihoji hiki walichofanya, hilo linawezekana wapi?
Kama kuna hoja ni vyema waijibu, wasitutishe tunaohoji kwa kutuita mafisadi, hivi ni nani ndani ya Kanisa hilo anaweza kusimama na kusema historia yake kuwa ni msafi kuliko mimi? Wasifikiri kama watu hatuwajui mambo yao, tunayajua, ila hatutaki kuyasema. Mimi sijaiba kitu cha mtu hata siku moja, bahati mbaya Mwalimu Nyerere (Julius) hayupo angenishuhudia, alisema.
Mwanasiasa huyo alikwenda mbali zaidi kuwa wakati viongozi wa dini wanachambua maoni yake, kuna baadhi ya watu walitumia fedha chafu kuwahonga baadhi ili wamtukane na kumchafua mbele ya jamii.
Najua kuna watu waliohongwa wanichafue, ila nawasikitikia zaidi waliokuwa wanatoa hizo fedha chafu, kwani mwisho wao unakuja, watasema wapi wamezitoa fedha hizo, alisema mwanasiasa huyo bila kufafanua kwa kina suala hilo.
Kingunge ambaye kabla ya kuanza mazungumzo yake alitoa historia yake ya uongozi ndani ya chama na serikalini na namna alivyoshiriki kuijenga nchi hii tangu mwaka 1954, alisema analifahamu Kanisa Katoliki tangu enzi za Mkoloni na jinsi lilivyokuwa linatumia nguvu kuwakamata wale waliolipinga.
Wakati nasoma Msimbazi nikiwa kidato cha pili, walitaka kunifukuza shule, kisa nilihoji sababu ya Padri Mzungu kututukana sisi wanafunzi weusi, niliepuka kufukuzwa kwa sababu Makamu Mkuu wa Shule hakuwa Mkatoliki.
Tunakumbuka uasi wa Padri Martin Luther, ulitokana na mabavu ya Kanisa hili, walitaka kinachozalishwa katika nchi za Ulaya kipelekwe Vatican, Padri akahoji, wakataka kumkamata akawakwepa
sasa hawa wasiturudishe huko nyuma, sasa hivi hili haliwezekani ni lazima tukemee wanapokiuka misingi yetu ya kitaifa, alisema.
Alisema yeye alitoa ushauri juu ya waraka baada ya kuusoma, kwani asingekuwa ameusoma asingezungumza bungeni. Aliwashukuru wale ambao walimuunga mkono akiwamo Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad, kuwa ni mtu makini mwenye msimamo, ndiyo maana akaupinga Waraka huo.
Kingunge alisema yeye akiwa mzee ndani ya CCM na mzee katika nchi, anapoona kuna jambo ambalo linahatarisha amani na mshikamano wa Taifa ni lazima akemee. Alisema waasisi wa Taifa hili walilijenga kwa kutumia siasa na si dini wala kabila.
Dini haiunganishi watu, inatenganisha watu ndiyo maana waasisi wa Taifa hili wakatumia siasa, alisema Kingunge na kusisitiza kuwa laiti Mwalimu Nyerere angekuwa hai, Kanisa lisingethubutu kutoa Waraka huo.
Alisema vyama vya siasa ndivyo vyenye kazi ya kutunga Ilani na si Kanisa, kwani halijaandikishwa kama chama cha siasa. Watuambie hili Kanisa ni chama cha siasa au kama wana chama chao cha siasa waseme, ndiyo maana wanashauri kwenye Ilani yao kuwa Katiba ya nchi iandikwe upya. Kingunge aliwashangaa hata viongozi wa Serikali aliosema wanashabikia waraka huo wa Kanisa.
Hawa nawashangaa sana
hawajui CCM ilikotoka, ndio maana wanazungumza mambo wasiyoyajua, ni heri wanyamaze kuliko kiongozi mkubwa serikalini kuunga mkono waraka ule. Alisema Kanisa hilo wanachotaka kufanya ni kurithisha watoto udini, jambo alilodai kuwa ni hatari kubwa kwa Taifa na yeye akiwa mzee, kamwe hatakubali nchi ipelekwe kwenye udini.
Kwa kweli nimesikitika sana na jinsi maaskofu walivyonitendea, ila nitaendelea kuwaheshimu kwani wana majukumu makubwa ya kidini, ila sitakubali watupeleke kwenye udini, alisisitiza mwanasiasa huyo.
Akichangia Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni, Kingunge alilitaka Kanisa Katoliki kufuta waraka na ilani lilivyovisambaza kwa maelezo kuwa vinahatarisha amani ya nchi na kuligeuza Taifa kuwa sawa na Lebanon.
Baada ya kutoa maoni hayo, Kingunge aliandamwa na wanasiasa, wanazuoni na wachambuzi wa mambo ya siasa, kwa maelezo kuwa waraka huo hauna dosari kwani ulikuwa unatoa elimu kwa waumini ya namna ya kuchagua viongozi waadilifu. Katika hali isiyotarajiwa, Kingunge alisema viongozi ndani ya CCM wamejaa ubinafsi, jambo ambalo alisema linaathiri kwa kiasi kikubwa uongozi wa nchi.
Alisema ubinafsi huo umesababisha nidhamu ndani ya CCM kushuka na ndiyo maana viongozi wa chama hicho wanajibizana hadharani. Mwanasiasa huyo mkongwe alisema chanzo cha nidhamu kushuka ni kutokana na viongozi wa chama hicho kutanguliza maslahi binafsi zaidi na kuacha kuwatumikia wananchi.
Ukiwa mbinafsi nafasi ya kuwajali wenzako haipo, uongozi bila mizania unafuta sura ya kuwatumikia watu wengine, unakuta kiongozi anafikiri ya kwake tu
mimi nitapata nini?, alisema.
Kuna walioingia kwenye chama kwa malengo ya kupata vyeo, hao ni lazima wafanye mambo ya ajabu ili wapate uongozi, kwani ndilo lengo lao, alisema. Aliongeza kuwa kushuka nidhamu kwa viongozi hao kunafanya hata vikao vya chama visiwe vya siri tena kwani ndio wako mstari wa mbele kutoa siri kwa wanahabari.
Zamani nidhamu ilikuwepo, huwezi kusikia watu wanajibizana ovyo kama ilivyo sasa, tulikuwa tunasemana kwenye vikao zaidi, lakini leo hii nidhamu hakuna viongozi wetu wamejaa ubinafsi, hilo halipo tena, alisema.