Kilango amvaa Kingunge
2008-08-29 09:34:01
Na Simon Mhina
Wabunge wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bi. Anne Kilango Malecela (Same Mashariki) na Alloyce Kimaro (Vunjo) wamesema mwanasiasa mkongwe nchini, Bw. Kingunge Ngombale Mwiru ana mawazo mgando na kumtaka atofautishe CCM ya mwaka 77 na hii ya sasa.
Aidha wamesema kauli ambazo Bw. Kingunge ametoa jana, zinaashiria kwamba anazeeka vibaya na atamaliza vibaya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Nipashe kwa njia ya Simu jana, wabunge hao ambao wapo mstari wa mbele kupambana na ufisadi, walisema wameshangazwa na kauli za Bw. Kingunge kwamba wanachokifanya ni kujitafutia umaarufu.
Jana Mzee Kingunge alikaririwa na vyombo vya habari akidai kuwa anawashangaa baadhi ya wabunge wa CCM wanaokiponda chama chao kwa kujifanya kutetea maslahi ya umma.
Bw. Kingunge alitoa kauli hiyo mjini Dodoma wakati anapokea maandamano ya wananchi waliokuwa wanapongeza hutuba ya Rais aliyoitoa Bungeni hivi karibuni.
Kingunge alikaririwa akiwaonya wabunge hao waachane na umaarufu wa `kwenye magazeti` kwa vile umaarufu wao umetokana na CCM.
Bi. Kilango, alisema Mzee Kingunge asingetoa kauli hizo kama hana anachofaidi kwa mafisadi.
Alimuomba Bw. Kingunge awataje hao wabunge wanaodhoofisha CCM kwa tabia yao ya kupinga ufisadi.
``Yaani Mzee Kingunge haoni madhara ya wabunge wa CCM kuwaachia wapinzani kutetea maslahi ya taifa peke yao? Mzee wetu huyu sio tu anaua chama, lakini hatua yake yakutetea mafisadi kinyume kabisa na msimamo wa Mheshimiwa Rais unatuachia maswali mengi kuliko majibu. Kingunge hawezi kuwatetea mafisadi, kama asingekuwa anafaidi matunda ya ufisadi,`` alisema.
Bi. Anne alimtaka Mkongwe huyo awaache wabunge watekeleze wajibu wao waliotumwa na wananchi.
``Nyerere angefufuka akamsikia Kingunge akiwakemea watu wanaopinga uovu, angemnasa kibao,`` alisema.
Hata hivyo, Mbunge huyo alisisitiza kwamba kauli za Bw. Kingunge hazitawakatisha tamaa na wataendeleza mapambano kwa lengo la kuifanya CCM iendelee kuheshimika nchini.
Alisema watu wenye mawazo mgando kama Kingunge ndio wanakuwa vyanzo vya kuanguka vyama tawala kwenye nchi za Kiafria.
``Huyu Mzee (Kingunge) ana lake jambo, kwanza inaonekana haitakii mema serikali ya Rais Kikwete ambayo imetumia muda mwingi kupamba na ufisadi kwa kuunda tume nyingi,``alisema.
Kuhusu kuweka mbele maslahi ya CCM, Bi. Malecela alisema maslahi ya chama hicho yameongezeka baada ya baadhi ya wabunge kupinga ufisadi.
Naye Mbunge Kimaro, alimtaka Bw. Kingunge apumzike kwa amani na asidandie magari ya kasi.
``Mimi nampenda Kingunge, nawapenda wazee kama yeye. Tunawaenzi na tunawahitaji, lakini wanapofikia mahali pa kutetea dhuluma, tunawaomba wakae pembeni,`` alisema.
Bw. Kimaro alisema madai ya Kingunge ni matokeo ya watu kung\'angania madaraka na kulewa nyadhifa katika sehemu moja muda mrefu.
``Mwambieni Kingunge maneno yake sio ya kweli, hakuna Mbunge wa CCM mwenye nia ya kukidhoofisha chama chake, wanaodhoofisha ni mafisadi pamoja na yeyote anayetaka kuwakingia kifua kama anavyofanya... Maneno na kejeli zake hazitatuvunja moyo tunaendelea. Habari ndiyo hiyo,`` alisema.
Mbunge huyo alisema Kingunge amechoka na wala hana jipya, hivyo ameshindwa kutambua alama za nyakati kuwa CCM ya mwaka 77 si hii ya sasa.
Alisema ndani ya CCM kuna watu ambao wamejiunga nayo kwa nia ya kujitajirisha, hivyo watu pekee wa kukemea hali hiyo ni wabunge.
``Kingunge hataki mabadiliko kwa vile hana jipya, mimi namheshimu ndio maana namuomba akae pembeni ale pensheni yake,`` alisema.
Bw. Kimaro alisema nia ya wabunge wanaochachafya mafisadi ni kukitetea chama chao na kuifanya CCM irejee kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi (wanyonge) kama yalivyo madhumuni ya kuanzishwa kwake.
Alisema inasikitisha kuona kwamba Kingunge haoni tatizo la ufisadi nchini, badala yake anaona wabunge wanaopinga ufisadi ndio maadui.
Alisema kwa vyovyote mafisadi wameishiwa nguvu, sasa wameamua kumfanya Bw. Kingunge kuwa nabii wao wa kuwasemea, baada ya wao kubanwa pande zote.
``Ukweli ndio unaojenga siku zote. Rais amezungumzia tatizo la ufisadi katika EPA, Waziri Mkuu naye amekiri ufisadi ndani ya Richmond, yote hayo Kingunge hayaoni? Tunadhani anayaona, ila huenda kuna faida anayoipata kwa hao mafisadi,`` alisema.
* SOURCE: Nipashe