Hapo ndipo tunapokosea, kutumia mbavu katika kusuluhisha migogoro ya aina hii ni kuendeleza migogoro na jamii husika bila ulazima wowote, sitaki kuamini kuwa kwa kumteka/kumkamata Dkt. Ulimboka ndio migomo itakwisha huu ni ubabe ambao hauna nafsi katika nchi zenye demokrasia na utawala wa sheria. Ikitokea Dkt. huyo amedhurika katika kipindi hiki litokuwa doa kwa chama tawala na serikali yake.
Huu ndio ufisadi wa fikra. Pamoja na kuwa migomo hii ya madaktari inaendeshwa bila kuwa na mikakati madhubuti ya kuona kama inafanikiwa au la, bado pia serikali inashindwa kujipanga kuwashawishi kwa hicho wanachoamini na matokeo yake ni kuendeleza ubabe wa wenye dola ambao hawataki kufikiria na wasio na nguvu ya dola wanaodai haki yao ambao pia hawajui hatma ya hilo wanalolifanya.
Kukosekana kwa dhamira inayoeleweka zaidi ya kuamini tu kuwa watu wengi wakifa serikali itatusikiliza kwa sababu madaktari ni muhimu, bado ni tatizo katika migomo mingi ya tanzania na ndiyo maana hakuna mafanikio au yanakuwepo kidogo sana kwa kuwa kila upande unachotaka ni ubabe na siyo kuwa na dhamira madhubuti inayoeleweka na hata inayoainisha njia mbadala endapo iliyopo itashindwa katika kipindi fulani.