Jumamosi iliyopita nilihudhuria kongamano la taasisi ya kiislamu lililofanyika kwenye msikiti wa Alfaruq mkoani Shinyanga.Mengi yalizungumzwa katika kongomano hilo ikiwa pamoja na kutoa msimamo wa baadhi ya waislamu kupinga kuhesabiwa sensa na kuto kumtambua kadhi mkuu pamoja na makadhi 15 walioteuliwa na Mufti mkuu wa Tanzania.
Kwa upande mmoja serikali inatuhumiwa kuukandamiza Uislamu kupitia Baraza Kuu la Waislamu Tanzania(BAKWATA),wamefika mbali zaidi kwa kuhoji hata nafasi za uongozi wa Taifa letu kwa misingi ya udini.Si nia yangu kujaribu kuzungumzia udini lakini hali hii imechochewa zaidi na chombo cha habari cha serikali kwa kutoa takwimu za kupika juu ya idadi ya Waislamu,Wakristo na Wasio na dini.
Chombo cha umma cha habari kinapotumika kama chambo cha kupika takwimu ni hatari kwa mustakabli wa taifa,kiasi cha Waislamu kutaka kujua nini hasa nia ya serikali kutaka kuwaminisha wananchi wake kwa takwimu hizo za kubumba.Ajabu na kweli leo katika kipindi cha jambo Tanzania,mkurugenzi wa TBC alitumia fursa hiyo kukanusha na kusema takwimu hizo hazikuwa sahihi na kuomba radhi kwa waumini wa dini yakiislamu.
Kwa kitendo hiki cha kuomba radhi ilihali hali ya hewa imekwisha chafuka na Waislamu kutishia kuto kuhesabiwa sensa inaiweka wapi umakini wa serikali iliyo sikivu.
Ikiwa sheria ya kimataifa ya takwimu za population ya watu duniani ina tamka wazi misingi ya kuhesabiwa ni pamoja na vipengele vya dini ,madhehebu na hata makabila,nini hasa kilichoisukuma serikali yetu kukiondoa kipengele hicho kinacho julikana kimataifa kama si samaki kujikaanga kwa mafuta yake mwenyewe
Tunahitaji serikali makini katika kuyapima mambo ambayo hayataleta mtafaruku wa amani hii tuliyo nayo kupotea.Ile dhana ya udini iliyokuwa ikinadiwa sana kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu sasa imeshika kasi kiasi cha kusababisha busara kupotea.Hatuwezi kuwa na viongozi wasio kuwa na hekima kwa kushindwa kuzuia ya mioyoni mwa na kutukana viongozi wa dini.
Kwa suala hil la sensa ya watu na makazi inabidi serikali ikubali kuwa imeteleza la sivyo tuachane nalo kwa serikali kujiandaa vizuri kuliko kupoteza pesa za kodi ya Watanzania kwa kukusanya takwimu ambazo hazitakuwa na ukweli wowote.Namaanisha kuwa kama serikali kwa kupitia wakuu wa Mikoa imesimama kidete kuwatisha wananchi wake watakao kataa kuhesabiwa una tegemea nini kama si machafuko ndani ya nchi na kukusanya takwimu zisizo sahihi kwa kudanganywa kwa makusudi na wananchi.
Ni bora serikali ikae chini na viongozi hao wa dini zote zilizo hapa nchi na kusikiliza hoja zao za msingi kuliko njia inayo jaribu kutumiwa hivi sasa ya kuwatisha wananchi.Siku zote hoja hujibiwa kwa hoja na si kwa vitisho,kwa staili ya vitisho inaashiria serikali kushindwa kuwaongoza wananchi wake kwa misingi ya kidemokrasia.
Ama kweli nimeamini zimwi likujualo halikuli likakwisha,matokeo haya yote ni ile dhambi ya kubaguana ambayo ikisha kukaa lazima utaisambaza kila kona.Udini uliotumika kama agenda kuu ya uchaguzi leo imezaa matunda na kuigeukia serikali iliyo kuwa dalali mkuu wa kuinadi sera hiyo.
Hekima itumike kuinusuru taifa letu,japo kuwa amani yetu ni ya bandia lakini kuna nchi zina itamani,chonde chonde tunataka amani halisia kuliko kuona viashiria vya uvunjivu wa amani ambao msingi wake mkuu ni serikali yenyewe.
Nawasihi wakae chini watafakari kwa kina na kurudisha vipengele ambvyo vinajulikani katika sheria za kukusanya takwimu za idadi ya watu na hali ya amani itakuwa shwari.Tusingependa Watanzania tuyazoe mabomu,tukiyazoea nchi haitakalika.Tuache hekima ichukue mkondo wake.