Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
KISA CHA ALLY SYKES, DENIS PHOMBEAH NA KENNETH KAUNDA
TANGANYIKA NA MKUTANO WA WAPIGANIA UHURU KUSINI YA SAHARA 1953
SEHEMU YA PILI
Trevor Huddleston
Ally Sykes na Denis Phombeah walipoingia ndani ya jengo la uwanja wa ndege mjini Salisbury waliambiwa wasimame mwisho wa foleni nyuma ya abiria wazungu.TANGANYIKA NA MKUTANO WA WAPIGANIA UHURU KUSINI YA SAHARA 1953
SEHEMU YA PILI
Trevor Huddleston
Baada ya abiria wote Wazungu kukaguliwa na kutoka nje, wao waliambiwa waingie ndani ya chumba kimoja pembeni.
Afisa mmoja wa Uhamiaji Mzungu aliyeonekana kuwa mkali aliwapa hati zilizowataja kuwa ni wahamiaji wasiotakiwa na akawataka kutia saini kwenye hati hizo.
Yule Afisa wa Uhamiaji, Kaburu wa Afrika ya Kusini alikuwa mrefu takribani futi sita, alikuwa na bastola kiunoni na alikuwa ameshika rungu katika mkono wake wa kulia.
Baada ya kuona kuwa Ally Sykes na Denis Phombeah hawangetii amri yake, alizizuia pasi zao za safari na akawaambia waondoke pale kwenye jengo la kiwanja cha ndege na warudi kutoa taarifa kwake asubuhi iliyofuata.
Kwa kweli Ally na Phombeah walikuwa kama wa waliotupwa kusikofahamika.
Nje ya uwanja ule wa ndege wa Salisbury kiza kilikuwa kimetanda na hakukuwa na usafiri wa kuwapeleka mjini, kitambo cha takriban kilomita 12.
Hawangeweza kupitisha usiku ule pale kiwanja cha ndege hadi asubuhi iliyofuata kwa sababu eneo hilo lilichukuliwa kuwa eneo la usalama sana na Mwafrika yeyote ambaye angekutwa karibu na eneo hilo usiku angeweza kupigwa risasi pale pale.
Ally na Phombeah hawakuwa na chaguo jingine isipokuwa kuanza kutembea zile kilomita 12 kuelekea katikati ya mji.
Baada ya kutembea mwendo mfupi gari la posta ambalo lilikuwa likija kutoka uwanja wa ndege kuchukua barua lilisimama na dereva, Mwafrika, aliwapa msaada akiwaambia wapande garini upesi.
Aliwaambia kwamba alikuwa amewaona kule uwanja wa ndege na alishuhudia yote yalitokea na alijua hasa kile kitakachotokea kwao.
Ilikuwa kwa sababu ya hii ndiyo maana amekuja kuwachukua kuwafikisha mjinii.
Yule dereva aliwaambia kwamba Waafrika walipata kuuawa katika hali kama hiyo iliyowafika wao.
Yule dereva aliwachukua kwa mfanya biashara mmoja Mwafrika mashuhuri kwa jina la Charles Mzengele ambaye aliishi katika viunga vya Salisbury mahali pamoja pakiitwa Harare.
Baada ya kusikia mkasa wa wageni wake, Mzengele aliwaambia kwamba hangeweza kuwapatia mahali pa kulala mle nyumbani mwake kwa sababu ilikuwa kinyume cha sheria.
Waafrika hawakuruhusiwa kupata wageni bila ruhusa ya Jumbe.
Halikadhalika Waafrika hawakuruhusiwa kumiliki nyumba ndani ya mipaka ya manispaa ya Salisbury.
Mzengele alimpigia simu Jumbe wa eneo lake akieleza kuwepo kwa Ally na Phombeah nyumbani mwake.
Mjumbe akatoa amri kuwa hao watu wazuiwe hadi yeye atakapofika.
Alipofika Mrakibu aliwauliza Ally na Phombeah, kwa sauti iliyojaa dharau kama wao walikuwa Ally Sykes na Denis Phombeah.
Baada ya Ally na Phombeah kujitambbulisha Jumbe akasema, ''Aha, nyinyi ndio mnajidai wapigania uhuru mnaotaka kuwatoa Waingereza toka Tanganyika, na sasa mmo njiani kwenda Lusaka kuendelea na upumbavu wenu !''
Yule Jumbe aliwachukua Ally na Phombeah nyumbani kwake na akawaambia walale usiku mzima ndani ya boma la ngíombe.
Nyuma ya boma hilo kulikuwako na kibanda ambamo waliwekwa nguruwe.
Uvundo kutoka lile banda la nguruwe ulikuwa hauvumiliki.
Ally Sykes na Denis Phombeah hawakuthubutu kutoka nje kupata hewa safi kwa kuwa walikuwa wamefungiwa kwa nje na pale penye uwanja wa ile nyumba palilindwa na mbwa wakali san aina ya Alsatian.
Ukweli ni kuwa Ally Sykes na mwenzie Denis Phombeah walikuwa kifungoni.
Usiku mdudu alimuingia Phombeah sikioni na sikio lilianza kumwasha sana maumivu yakawa hayavumiliki.
Ally hakuweza kufanya lolote kumsaidia rafiki yake.
Hakuweza kumwita yeyote kwa kuwa walikuwa wamefungiwa ndani na nyumba za wafanyakazi zilikuwa mbali sana toka kwenye yale mabanda ya ngíombe.
Mapema asubuhi yule Jumbe alikuja kuwafungulia na kuwaamuru waondoke waende zao.
Ally alimuuliza ikiwa angeweza kumpeleka Phombeah hospitali ili akatibiwe sikio lake. Mjumbe akamwambia Ally kwamba Waafrika walikuwa hawatibiwi hospitalini.
Ally na Phombeah wakiwa wamechoka sana walianza kutembea pole pole kuelekea uwanja wa ndege wa Salisbury.
Hawakutembea zaidi ya maili moja nara likatokea gari lile lile lililowachukua usiku wa jana na kuwachukua tena kuwapeleka uwanja wa ndege.
Hii ilikuwa zaidi ya nyota njema. Baadaye Ally alikuja kutambua kwamba Charles Mzengele alikuwa na habari zao zote hata kabla ya kupelekwa nyumbani kwake na yule dereva wa gari la posta.
Halikadhalika pia alijua kwamba toka uwanja wa ndege wangechukuliwa na kupelekwa kwake au kwa mtu mwingine kama yeye.
Mizengele alikuwa na nduguye kachero kijumbe mtoa habari (informer) akifanya kazi Special Branch ya walowezi.
Kulikuwa na uvumi kwamba Mzengele alikuwa akiwapeleleza Waafrika wanaharakati wa kisiasa na kupeleka habari hizo juu.
Inaaminika kwamba wapigania uhuru wengi walifungwa gerezani na baadhi yao hata wakapoteza maisha yao kutokana na matokeo ya kazi hiyo ya usaliti wa Mzengele.
Wazungu walowezi nao kama kuonyesha shukurani kwae kwa usaliti wake Mzengele alikuwa amepewa duka kubwa mjini Salisbury ambalo ndipo iliipokuwa ofisi yake.
Hili duka likiwa kiini macho kuficha kazi yale yailiyokuwa yakitendeka pale Mzengele akijijengea picha ya kuwa ni mfanyabiashara Mwafrika aliyefanikiwa.
Inasemekana Charles Mzengele aliendesha moja ya idara stadi, hodari na yenye nguvu kupita zote za upashaji habari nchi nzima.
Hii inaeleza kile kitendawili cha Ally na Phombeah kupewa lifti na dereva wa gari la posta pale uwanja wa ndege siku ile walipowasili kisha kupelekwa nyumbani kwa Mzengele na hatimaye kukabidhiwa kwa yule Mjumbe wa eneo lile usiku ule ule.
Vilevile inaeleza kule kupewa msaada kwa Ally na Phombeah na mtu yule yule asubuhi iliyofuata na kuchukuliwa hadi uwanja wa ndege kwa ajili ya kuondoshwa nchini.