Inaendelea sehemu ya 3
Baada ya matukio hayo kupita maisha yaliendelea kama kawaida. Baadae baba yangu alikuja kupona ugonjwa wa akili uliokuwa unamsumbua. Baada ya kupona alienda kuuza eneo ambalo tuliliacha kule Bunda, akaja kununua eneo pale kijijini. Akafyatua na tofali na kuzichoma baadae akajenga nyumba ndogo ya vyumba viwili na sebule maarufu kama mgongo wa tembo na nyumba nyingine akajenga ya tope na bati zilizoezekwa kwa mtindo wa flat hujulikana zaidi kama "slope". Tukaanza kuishi pale, tuliendelea na maisha kama kawaida wakati huo nikiwa darasa la tano mwaka 2007, tukijikita hasa hasa kwenye shughuli ya kilimo. Na huo ndio mwaka ambao babu alifariki dunia (RIP). Niliendelea na shule hadi nikamaliza darasa la saba, baadae nikajiunga na sekondari katika shule ya kata iliyokuwa katika kijiji cha mbali kidogo na Kijiji chetu ambako ndio ilikuwa kata yetu. Ili kufika mahali kata ilipo ulikuwa unavuka kijiji kimoja katikati ndio unafika, umbali sio chini ya masaa matatu kwa mwendo wa mguu. Hivyo vijana ambao tulitoka vijiji vya mbali tulilazimika kupanga vyumba hapo katani, ili kupunguza umbali wa kwenda shule. Vyumba hivyo vijana waliita "ghetto" sio kama la Mangwair lakini lenye kapeti manyoya, mashine ya dry cleaner na kistudio cha kiaina. La kwetu lilikuwa na godoro lisilo na kitanda, vyombo vichache kwenye beseni, kibatari na vimadaftari vya kiaina hakuna duu ambaye lingeweza kumchengua.
Ilipita miaka mingi nikiwa sijashuhudia tukio lolote la kishirikina, kiasi kwamba hadi kumbukumbu za tukio lile zikawa zimeshafutika. Mambo yalikuja kubadilika nilipokuwa sekondari. Nikiwa ndio niko likizo ya mwisho wa mwaka kuingia kidato cha tatu. Nakumbuka ilikuwa likizo ya mwisho wa mwaka kama sikosei ni either ilikuwa mwezi wa 12 mwaka 2011 au tarehe za mwanzo wa mwaka 2012. Kulikuwa na mechi ya Arsenal sikumbuki vizuri ilicheza na timu gani, lakini ilikuwa ni mechi ya ligi kuu. katika ile mechi Arsenal ilishinda 2-1 magoli ya Arsenal yalifungwa na Van- Persie kwa penalty na Benayoun dakika za mwishoni. Kipindi hicho kocha wa sasa wa Arsenal Michael Arteta bado anakipiga uwanjani. Sasa mimi huwa ni shabiki wa damu wa hii timu tokea enzi za mzee Wenger. Sasa kama unavyojua mazingira ya kijijini kulikuwa hakuna umeme hivyo mechi tulikuwa tunaenda kuangalia centre yaani yalipo maduka. Kuna jamaa alikuwa na banda la video anatumia generator linalopiga kelele kama mziki wa Young Lunya. Kulikuwa na umbali kidogo kutoka nyumbani hadi huko madukani umbali kama wa nusu saa kwa mwendo wa mguu. Sasa wakati naenda kucheki mechi nilikuwa na washikaji zangu watatu, sasa mechi ilivyoisha nataka nirudi nyumbani nikawa siwaoni. Na ilikuwa ni usiku kama saa sita hivi, kumbe jamaa walichoka kuangalia mpira wakaondoka kimya kimya Sasa ikabidi nirudi peke yangu, maana kitongoji chetu hakikuwa na watu wengi wapenzi wa mpira. Hivyo wengine waliokuwemo mle bandani sio wa maeneo ya kwetu.
Njia tuliyokuwa tunapita ina miti vichaka na nyumba za mbalimbali. Nikaanza kutembea peke yangu usiku ulikuwa kimya Kweli Kweli ni sauti ya upepo na wadudu tu ndiyo vilisikika. Kuna sehemu nikafika huwa hakuna nyumba kwa umbali kama wa mita mia mbili hivi ila kuna miti mingi sana na vichaka vichaka. Wakati natembea nikawa nasikia vishindo vya mtu kwa nyuma, kama yuko nyuma yangu umbali mdogo tu anakuja. Nikageuka kuangalia sikuona kitu, niliogopa kidogo lakini nikaendelea na safari nikidhani labda ni mawenge ya usiku tu. Nilipoanza kutembea nikaanza kusikia tena, safari hii kwa karibu zaidi kuliko mwanzo ni kama mtu alikuwa yuko mita chache sana nyuma yangu. Aiseee! Mapigo ya moyo yalienda kasi sijapata kuona!. Haraka haraka nikageuka tena kuangalia lakini sikuona kitu. Aisee nilitimua mbio zaidi ya Hussein Bolt! Nilikimbia kwa mwendo kama wa dakika tatu, nikashangaa kwa mbele yangu nikamuona mtu anatembea. Nikasimama ghafla kusoma kumuangalia nilikuwa naogopa sana nisingemuamini yeyote tena. Nilivyomuangalia, nikabaini alionekana kama mwanamke bibi mzee sana anatembea polepole kwa kujivuta kizee amevaa nguo zilizoonekana nyeusi tii. Niliweza kuona vizuri kwa sababu alikuwa mita chache sana! Akili iliniambia ndio walewale Kuona hivyo nilibadili njia kwa kasi na kuanza kukimbia huku nikipita kwenye mashamba nikikimbia hovyo. Kwa sababu nilikuwa mwenyeji haikunisumbua kukimbia nikikatiza kuelekea uelekeo wa nyumbani.
Nilikimbia bila kuchoka umbali mrefu sana, wakati nakaribia sasa kufika home. Nikaikamata sasa barabara inayonyoka kuelekea nyumbani. Nikawa kama nimechoka kukimbia nikawa natembea ila kwa kasi Sana ! Nilishtuliwa na sauti ya mwanamke wa makamo ikiniita!
"We mtoto" alisema yule mwanamke tena kwa kiswahili
Nilishtuka na kuanza kupepesa macho ili nione ile sauti ilitokea wapi. Nilipigwa na butwaa nilipomuona mwanamke amechuchumaa pembeni ya barabara amevaa nguo nyeusi amejifunika hadi usoni huku akiniangalia.
" We mtoto haunisikii"
Mr the Dragon nikakaa kimya. Wazee wetu walitufundisha ukisikia unaitwa usiku hata na mtu unayemfahamu usiitike ovyo. Wakati mwingine wachawi wanaweza kutumia uchawi wao kuigiza sauti hata ya mtu unayemfahamu na wakakuita. Ukiitika tu wanachukua sauti yako inakuwa rahisi wewe kulogwa. Kwa hiyo nilichagua kukaa kimya. Sikuweza kukimbia ni kama mwili ulikuwa umepigwa ganzi.
"Wewe mtoto kwa nini unatembea tembea usiku"
Mimi kimya!
"Usirudie tena kutembea usiku,potea hapa haraka"
Aisee hizo mbio nilizotoka nazo nadhani ingekuwa ni kwenye mashindano ya Olympic mita mia ningeweza kuibuka na gold medal. Nilikimbia hadi nyumbani nikamkuta brother wangu ninayemfata amelala. Nilimgongea mlango akafungua nikaingia ndani.
"Mbona unahema hivyo"
"Nimekuja peke yangu nilikuwa nimeogopa nikawa nakimbia" niliamua kuficha
"We nae muoga sana" alisema huku akipanda kitandani kulala.
Na mimi nilipanda kulala, usingizi ulikuwa wa mang'amung'amu sana, usiku mzima nilifikiria mambo yaliyotokea siku hiyo. Tukio la kusimamishwa na yule mwanamke ndio lilinitisha zaidi. Yule mwanamke alikuwa anatisha vibaya mno. Niliwaza Yule mwanamke atakuwa nani lakini sikupata jibu, nilijaribu kuikumbuka sauti yake na kuangalia kama nilishawahi kuisikia pale kijijini lakini niliambulia patupu. Kesho yake niliendelea na kazi kama kawaida, sikumwambia yeyote kuhusiana na tukio lile. Kuna muda mama yangu alihisi kulikuwa na shida na kuniuliza kama kulikuwa na shida lakini niliamua kuficha, sikumwambia chochote.
Baada ya siku kadhaa shule ilifunguliwa, sasa ukawa muda wa kurudi kwenye kile kijiji ambako shule ilipatikana yaani katani. Nilitembea nikiwa na washikaji na mabinti tuliokuwa tunasoma nao hadi tukafika. Getto kwetu tulikuwa tunaishi mimi na marafiki zangu wawili, jumla tukawa watatu. Hao wote nilisoma nao tokea shule ya msingi Mwanono. Usiku nikiwa nimelala niliota ndoto moja iliyonitisha kidogo.
Niliota mimi ni mtu mzima kidogo ambaye nilikuwa nimeshaondoka kijiji cha Mwanono nikaenda mjini kuishi huko. Nikaishi miaka mingi bila kurudi pale kijijini, sasa siku hiyo nikawa nikawa ndio nimerudi sasa kwa ajili ya kusalimia ndugu jamaa na marafiki. Kwenye ndoto niliota nimeshushwa na bodaboda pale madukani Mwanono nikapokelewa Kwa bashasha na marafiki zangu kitambo hapo kijijini ambao niliwakuta pale centre. Tukaanza kupiga story mbalimbali, miongoni mwa mazungumzo jamaa wakaanza kuniambia Mwanono Sasa hivi pamebadilika pamekuwa mjini, itabidi tukutembeze ujionee. Wakati tukiwa tunaendelea na mazungumzo hayo alikuja pale msichana mmoja niliyemfahamu vyema akiwa na baiskeli akasema
" Nyie mnataka mumtembeze lini, mimi naanza kumtembeza leoleo, hebu Mr the dragon panda hii baiskeli nikubebe nikutembeze" alisema yule msichana
Bila hiyana wala kipingamizi nikapanda baiskeli akanibeba, halafu huyo binti akawa anaendesha. Aliendesha baiskeli kwa dakika kadhaa ikafika sehemu kulikuwa na kona, tulipokunja ile kona tulitokea kwenye mazingira ambayo nilikuwa mgeni kabisa. Nilijaribu kukumbuka pale itakuwa ni sehemu gani kwenye kile kijiji lakini sikupatambua kabisa. Kulikuwa na nyumba nzuri za kisasa na mama mandhari ya kuvutia Sana. Msichana yule aliendesha baiskeli hadi kwenye nyumba moja nzuri sana, kisha akaniambia ingia ndani. ile naingia ndani nikakuta kundi kubwa la watu
Ghafla nikashtuka kutoka usingizini. Niliposhtuka tu nilihisi maumivu mgongoni. Nikajishika nikawa nahisi maumivu ya kuchanwa chanwa mgongoni na kitu chenye ncha kali. Ilibidi niamke nikawasha kibatari kuangalia mgongoni
LAHAULAH!!! nilikuwa na Chale mgongo mzima zikiwa mbichi kabisa na damu kana kwamba ndio nimetoka kuchanjwa na nimepakwa dawa nyeusi na nyekundu. Wazo la kwanza lilikuwa kwenye ile ndoto niliyotoka kuota
Hasahasa msichana aliyenibeba kwenye baiskeli kwenye ile ndoto, ndio yule yule aliniambia mimi ni muoga wakati nilipoona wachawi nikiwa darasa la tatu miaka kama saba iliyopita.
Ndio yule aliyeniambia usiku ule nakimbia wachawi kurudi ndani, wao walienda kula nyama kwenye mkwaju wa kwa mzee Lugota. Yule Yule ambaye tulisoma nae darasa moja na sasa tunasoma darasa moja sekondari. Yule ambaye bibi yake ni mchawi anayeogopeka Kijiji kizima.
Itaendelea tena kesho majira na nyakati kama hizi
Usiku mwema.