Kisa cha ''wachawi watatu'' katika Macbeth ndani ya ukumbi wa mjadala wa kura tatu Tabora 1958

Kisa cha ''wachawi watatu'' katika Macbeth ndani ya ukumbi wa mjadala wa kura tatu Tabora 1958

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
Leo FB imenirushia kumbukumbu ya mkutano wa Tabora kuhusu Uchaguzi wa Kura Tatu wa mwaka wa 1958.

Uchaguzi huu nimeueleza kwa kirefu katika kitabu cha Abdul Sykes na katika mihadhara kadhaa niliyopata kufanya.

Vilevile nimeandika kitabu ''Uamuzi wa Busara,'' (2007) kuhusu Kura Tatu.

Leo sitaki kujirudia ila napenda tuwaangalie wahusika wakuu wa Kura Tatu katika staili ya ''Dramatis Personae.''

Hii ''Dramatis Personae,'' ni orodha ya wahusika katika michezo ya William Shakespeare, ukifungua kitabu tu unakutana na orodha ya majina yao.

Tunaanza na Julius Nyerere Rais wa TANU.

Mwalimu alitaka sana TANU iingie katika Kura Tatu lau kama TANU nzima ilikuwa haitaki.

Sheikh Suleiman Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU.

Sheikh Suleiman ndiye tunaweza kusema alikuwa kiongozi wa wapinzani wa Kura Tatu ndani ya TANU.

Sheikh Takadir baada ya kurudi kutoka Tabora TANU ikiwa imepiga kura ya kushiriki Kura Tatu alimkabili Nyerere uso kwa macho ndani ya mkutano wa Halmashauri Kuu pale New Street (Lumumba Avenue) na akamwambia maneno makali kiasi hakuna mtafiti yeyote wa historia ya TANU hadi leo aliyekuwa na ujasiri wa kuyaandika maneno yale.

Siku ile Mwalimu alilia.

Adhabu ya Sheikh Suleiman Takadir ilikuwa kufukuzwa uanachama wa TANU na nafasi yake ya Mwenyekiti wa Baraza la Wazee akachukua Mzee Iddi Tulio.

Zuberi Mtemvu yeye alikuwa ''siasa kali,'' sera yake ilikuwa Afrika kwa Waafrika na Kura Tatu masharti yake ilikuwa Mwafrika ampigie kura Mzungu, Muasia na Mwafrika.

Hapa sasa tunaingia katika kisa cha watu naweza kuwaita, ''The Three Musketeers,'' au tunaweza kuwaita, ''The Three Conspirators,'' ukipenda, ''The Three Witches,'' yaani, ''Wanga Watatu,'' mfano wa wale ''Three Weird Sisters,'' katika, ''Macbeth,'' ya William Shakespeare.

Mimi nimelipenda jina hili la ''Wanga Watatu,'' kupita yote kwa kuwa katika hawa ''wachawi,'' watatu, wawili walikuwa wapinzani wa Kura Tatu, Mwalimu Kihere na Sheikh Rashid Sembe.

Lakini walipokutana na Nyerere na kufanya kikao Mwalimu aliwabadilisha fikra wakaunga mkono Kura Tatu.

Hawa ni Mwalimu Nyerere, Mwalimu Kihere na Sheikh Rashid Sembe wapangaji wa mpango wa ushindi Mkutano wa Tabora wa kuwashinda wapinzani wote wa Kura Tatu waliokuwa wakiongozwa na Sheikh Suleiman Takadir.

Kilichofuatia ndani ya ukumbi wa mkutano Tabora timu hii ya watu watatu kama wanga wafanyavyo ikawa kama vile wamewavamia wajumbe majumbani kwao wakawanyunyuzia dawa ya kuwageuza mawazo.

Mkakati huu uliokuwa unaongozwa na hawa wazalendo watatu ulishinda.

Waingereza wanasema, ''Carried the day.''

Leo tumebakia na simulizi.

Hii ndiyo historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika katika ukweli wake.




Kushoto ni Sheikh Suleiman, John Rupia na Julius Nyerere nyuma yao
ni vijana wa Bantu Group wahamasishaji wa umma na walinzi wa viongozi
wa TANU.



+2
 
Back
Top Bottom