SoC02 Kisu cha Ngariba

SoC02 Kisu cha Ngariba

Stories of Change - 2022 Competition

Nabii koko

Member
Joined
Aug 16, 2022
Posts
21
Reaction score
15
_89386239_tools_1.jpg

Giza totoro la usiku wa manane liliendelea kukumbatia kibanda alimoswekwa Marina, binti wa miaka kumi wa mzee Pakishu. Hakuwa amepata usingizi tangu aliposokomezwa humo na baba yake. Angepataje usingizi wakati KISU CHA NGARIBA kilikuwa kimeachama meno nje, tayari kufurahia kalamu ya kutafuna nyama yake alfajiri baada ya usiku huo?

Akili yake ilikuwa maili nyingi kukumbuka mabishano yaliyokuwepo kati yake na mama yake asubuhi ya siku hiyo na kumfikisha alipo sasa.

"Ehee... unaweza kukumbuka tulichoongea jana usiku kabla ya kulala?" Mama aliuliza.

"Mama bwana yani sihemi, kila wakati habari ni zile zile za juzi. Haya, ulinieleza juu ya faida za tohara kwa mwanamke!"

"Ndio hivyo, tohara itakuepusha na mimba za utotoni pamoja na magonjwa ya kuambukizwa kupitia ngono." aliongea huku akimshikashika kichwani.

"Pia utabaki kuwa bikira hadi utakapoolewa, baba'ko atatajirika kwa ng'ombe kutokana na bikira yako.

"Kwa hiyo anataka kutajirika kupitia mimi?" Marina alijikuta ameongea bila kutegemea. Alikutana na kofi zito lililomfanya apoteze mawasiliano kichwani kwa muda.

"Pumbavu! Unataka kuniaibisha? Hivi hujui kuwa kukeketwa ni dawa kwa baadhi ya magonjwa pia? Halafu, ni heshima kwa familia yetu sote. Nilikwishakweleza, hii ni mila yetu tumeikuta, lazima tuidumishe! Halafu, ukikeketwa utaweza kutimiza ndoto zako vizuri, unasikia?" Marina alitikisa kichwa kukubali kwa shingo upande. Aliendelea..

"Jana baba'ko alifika shule kukuombea ruhusa kuwa unaumwa. Utakaa nyumbani kwa takribani majuma mawili." Alimaliza kwa sauti kavu.

"Lakini mi siumwi, naa... mwalimu alisema..."

Hakumalizia, alikatishwa kitu kizito cha bapa mithili ya ubao kilichotua shavuni pake kutokea nyuma. Nyota nyota zilimulika. Alijaribu kutofautisha ladha ya kiganja kilichompitia sasa na kile alichopigwa mwanzo akabaini kuwa hiki kilikuwa kitamu zaidi. Alikuwa ni baba yake ayeliyekuwa nyuma yake kwa sekunde kadhaa akifuatilia mazungumzo yao. Alimwadjibu vikali na kumtupa lumande alimo sasa.

Akiwa katikati ya tafakuri hii sasa, Marina alisikia sauti ya chini ikiita jina lake. "Marina!" Nalangu aliita kwa mara nyingine kwa sauti ya chini asije akasikika na baba yake. Nimekuletea chakula mdogo wangu," aliongea na kupenyeza sahani ya chakula kupitia nafasi chini ya mlango. "Sina namna ya kukutorosha hapa kwa sasa. Funguo ya kufuli hii anayo baba. Ila...mpango wetu uko palepale kama tulivyoongea mchana. Nitahakikisha nakusaidia", aligeuka na kutokomea gizani.

Nalangu alishakeketwa akiwa na miaka mitano hivyo hakutaka yaliyomkuta yeye yasimfike mdogo wake. Kwa bahati mbaya alipaswa kuondoka yeye na mama yao ifikapo alfajiri kwenda kumkeketa Marina. Atafanyaje?
****** * ****
Alfajiri ilifika. Marina alihesabu sekunde tu kukifikia kisu cha ngariba.

Mabinti wapatao sita wenye umri kama wake walikuwa wamejitandaza juu ya vumbi uwanjani wakisubiri huduma. Marina alikuwa mwishoni.

Mstari ulibakiwa na watu watatu, zamu ya Marina ilinukia.

Alitupia macho kule alikokuwa amekaa dada yake muda wote. Hakumwona. Aliyemwona ni mama yake mzazi akiwa hana hata chembe ya huruma. Muda aliokubaliana na dada ulikuwa ndio huu. "Mbona haonakani?" alijisemesha, mapigo ya moyo yaliongezeka.

Nalangu alikuwa amemuaga mama yake kuwa anakwenda kumsafisha mwanae aliyejisaidia na hatakawia. Kabla ya kuondoka pia alimwomba mama kuwa yeye ndiye amsindikize Marina kwenda ndani kwa ngariba akakubali.

Wasiwasi ulimwingia Marina kwani sasa kwenye foleni alibaki peke yake. Akiwa katika taharuki mara ghafla alisikia...
"Mwingine aje!" moyo ulimruka huku akijihi si kama ganzi mwili mzima. Hawezi kutoroka kwani alikuwa katikati ya umati wa wanawake waliokuwa wakishuhudia.

Mpango wake uliokuwa ni kwamba atajifanya amebanwa na haja hivyo dada yake atamsindikiza na kumtorosha watakapofika chooni. Kisha dada atarudi na kupiga kelele za kuomba msaada wa kumtafuta Marina kwamba amemtoroka. Ni kama ibilisi aliingilia mbinu yao kwani hadi sasa dada hakuonakana. Marina atafanyaje? Huku nyuma baada ya kuona Nalangu hayupo na zamu imefika, mama aliinuka tayari kumshikisha Marina kwa ngariba yeye mwenyewe.
****** * *****
Kulikuwa kumeshapambazuka. Marina alijitupia ndani ya nyumba ya mwalimu wake bila hodi akitweta huku akidondosha matone ya damu. Kama bahati kwake, mwalimu Shija alikuwa ndio kwanza anajipatia kifungua kinywa mezani kabla ya kwenda kazini.

Hali ile ilimkata mate mwalimu akaachia kikombe na kumfuata Marina. Alisikiliza kisa chote toka mwanzo. Mwisho mwalimu alipiga simu kwa mkuu wake kuomba ruhusa, akamwacha mkewe akiuguza jeraha la Marina na kuwafuata wazazi wake.
****** * *****
Baada ya mgogoro mkubwa kati yao,
mwalimu Shija aliwatishia wazazi wa Marina kuwa alikuwa ametoa taarifa polisi juu ya unyama waliopanga kumfanyia binti yao ili kuwaweka sawa wamsikilize. Aliendelea ...

"Kama nilivyosema, hakuna faida yoyote ya kumkeketa msichana zaidi ya hasara tu wazee wangu. Unapomkeketa mwanao,
*Unamuathiri kisaikolojia. Hawezi kusahau kamwe yale maumivu anayoyapata wakati wa ukeketaji.

*Pili, anaweza kuambukizwa magonjwa kama UKIMWI na mengine kwa kuwa mangariba wengi hutumia kisu ama wembe mmoja kuhudumia watu wengi bila kuchukua tahadhari.

*Tatu, mnaweza kumpoteza mtoto kutokana na kutokwa damu nyingi baada ya kukeketwa.

*Mtoto huyo anapokuwa mtu mzima, pia anaweza kupoteza maisha wakati wa kujifungua. Hii ni kwa sababu wengi waliokeketwa hupata shida ya kujifungua na hivyo kupasuliwa ama kuchanika hatimaye kuvuja damu nyingi.

*Ukeketaji pia unaathiri taaluma ya mtoto kwa sababu atapoteza muda mwingi kusubiri apone na kushiriki sherehe baada ya kupona. Alipoeleza hoja hii Mzee Pakishu alitazamana na mkewe kuonesha waliguswa mahali. Aliendelea...

*Kiungo kinachoondolewa mwilini kina kazi kubwa katika tendo la ndoa. Mwanamke hapati msisimko wowote anapokutana na mwenzi wake wakati wa tendo.

*Mwisho, kumkeketa msichana ni kumpa ulemavu wa kudumu. Hivyo naweza sema sio kila mila ni nzuri, nyingine tunapaswa kuziacha kwani mababu zetu hawakufanya tafiti za kutosha juu ya ukeketaji na kuishia kushadadia faida ndogo tu bila kuangalia madhara.

Ili kumuepusha mtoto asijiingize kwenye mapenzi katika umri mdogo cha muhimu ni kumpa elimu ya jinsia. Pia, tusitegemee kutajirika kupitia watoto wetu. Tufanyeni kazi kwa bidii tutafanikiwa. Mwisho kabisa naomba mniahidi kwamba kuanzia sasa mtaachana na hii mila, na Marina atakuwa salama. " Alimaliza.

"Tunashukuru kwa elimu hiyo mwalimu. Tumekuelewa, ila mimi nitakuahidi iwapo tu nawe utawazuia polisi wasije," aliongea mzee Pakishu ikionesha wasiwasi kidogo. Mwalimu aliweka mambo sawa akaaga na kuondoka.

Ilkuwaje baada ya zamu ya kumkeketa Marina kufika na mama yake kuinuka tayari kumkabidhi kwa ngariba?

Pale mama alipoinuka tu Nalangu naye alitokea na kumuwahi kabla yake. Mama alimwacha aendelee. Kumbe wakati alitoka muda ule kwenda kumsafisha mtoto na kuchelewa kuja, alibadili mbinu. Alizunguka nyuma ya nyumba ya ngariba na kifungua mlango wa nyuma kwa ajili ya kutorokea.

Aliporudi, alimchukua Marina na kumwongoza kufuata korido iliyowapeleka hadi mlango wa kutokea upande wa pili. Dakika takribani tano zilipopita kukiwa kimya, alikuwa na uhakika Marina amefika mbali. Alirudi na kupiga yowe kuomba msaada kwamba Marina amemchoropoka na kukimbia kwani mlango wa nyuma haukufungwa.

Waliokuwa na uwezo walijaribu kumtafuta bila mafanikio wakaacha. Hivyo Marina alinusurika na KISU CHA NGARIBA. Ile damu ilyokuwa ikimvuja ilitoka katika kidole baada ya kujikwaa alipokuwa akikimbia na kucha kung'oka.




vifaa_1.jpg
Female-Genital-Mutilation_1.jpg
 
Upvote 0
Back
Top Bottom