SURA YA 16
Jua la kwanza. Adamu na Hawa wanafikiri ni moto unaokuja kuwateketeza.
1 BAADA ya haya Adamu na Hawa hawakuacha kusimama pangoni, wakiomba na kulia, mpaka asubuhi ilipopambazuka.
2 Na walipoiona nuru imerudi kwao, walijizuia na khofu, na wakazitia nguvu nyoyo zao.
3 Kisha Adamu akaanza kutoka kwenye pango. Na alipoufikia mdomo wake, akasimama na kugeuza uso wake upande wa mashariki, na kuliona jua likichomoza katika miale inayowaka, na kuhisi joto lake juu ya mwili wake, aliogopa, na akafikiri moyoni mwake kwamba mwali huu wa moto umetoka ili kumpiga.
4 Kisha akalia, akajipiga-piga kifuani, akaanguka kifudifudi, akaomba ombi lake, akisema:--
5 “Ee Bwana, usinipige, usiniteketeze, wala usiuondoe uhai wangu duniani.”
6 Kwa maana alifikiri kwamba jua ni Mungu.
7 Ikawa alipokuwa bustanini, akasikia sauti ya Mungu, na sauti aliyoifanya bustanini, akamcha, Adamu hakuuona mwanga wa jua ung’aao, wala joto lake liwakalo halikumgusa mwili wake.
8 Kwa hiyo akaliogopa jua wakati miali yake ya moto ilipomfikia. Alifikiri kwamba Mungu alikusudia kumpiga kwa hayo siku zote alizokuwa amemwekea.
9 Kwa maana Adamu naye alisema katika mawazo yake, kama Mungu hakutupiga kwa giza, tazama, amelitoa jua hili na kutupiga kwa joto kali
10 Lakini alipokuwa akiwaza hivyo moyoni mwake, Neno la Mungu lilimjia na kusema:
11 "Ewe Adamu, inuka na usimame. Jua hili si Mungu; bali limeumbwa ili litoe nuru mchana, ambalo nilizungumza nawe pangoni nikisema, 'Kutapambazuka, na kutakuwa na nuru wakati wa mchana'
12 "Lakini Mimi ni Mungu niliyekufariji wakati wa usiku"
13 Na Mungu akaacha kuzungumza na Adamu.