Sura ya 16 inaendelea
Nimeshasema kuwa nilitegemea vyombo vya habari kuandika kashfa ile muda wowote ule. Lakini sikutegemea habari iliyokuja. Hakuna anayetakiwa kukumbushwa kuwa ni nani aliuawa huko Dallas, Texas mnamo tarehe 22 ya mwezi wa kumi na moja, 1963. Ndani ya saa moja baada ya mauaji, na huu ninakwambia ni ukweli mtupu-kila Imam wa Kiislamu alipokea maelekezo kutoka kwa bwana Elijah Muhammad-yalikuwa maelekezo mawili. Kila Imam aliamrishwa kutosema chochote juu ya mauaji yale. Bwana Muhammad alisema kuwa iwapo tutaulizwa tutoe maoni yetu, tuseme: “Hatuna maoni.”
Katika siku zile tatu ambazo hakukuwa na habari zozote isipokuwa za kuuawa kwa Rais, bwana Muhammad alikuwa na ratiba ya kuzungumza kwenye ukumbi wa Manhattan Centre, New York. Alihairisha kuja kuongea, na kwa vile tulikuwa tumeishalipia ukumbi na haikuwezekana kurudishiwa pesa zetu, bwana Muhammad aliniambia niongee badala yake, nami nikafanya hivyo.
Tokea siku ile, nimeangalia notisi za hotuba ile mara nyingi sana, ni hotuba niliyokuwa nimeiandaa zaidi ya juma
moja kabla ya kuuawa kwa Rais. Kichwa cha hotuba yangu kilikuwa, “Hukumu ya Mungu juu ya Marekani ya mzungu.” Ilielezea jambo nililozoea kuliongelea, “Utavuna utakachopanda” au jinsi ambavyo mzungu wa Marekani alivyokuwa akivuna alichopanda.
Kukawa na kipindi cha majibu na maswali. Ilikuwa haiepukiki kwa mtu kuniuliza, “Una maoni gani juu ya kuuawa kwa Rais Kennedy?”
Bila kupoteza hata sekunde moja, nilijibu kile nilichohisi kilikuwa kimetokea, “Yaani kitendo cha kuku kurudi nyumbani kulala
(Chickens coming home to roost).” Nilisema kuwa chuki ya mzungu haijaishia tu kuua watu weusi wasio na ulinzi, kwa kuwa imeachwa kuenea bila kuzuiwa, mwishowe imemdhuru mkuu wa nchi. Nilisema kuwa ni kitu kile kile kilichowapata Medgar Evers, Patrice Lumumba na mume wa bi Nhu.
Mara moja vyombo vya habari vilitangaza na magazeti kuandika:
Malcom X kutoka kwa Waislamu weusi: Chickens Come Home to Roost.’”
Hata leo ninapofikiria jambo lile najihisi kuchoka kabisa. Marekani kote, duniani kote, na hata watu mashuhuri zaidi duniani walikuwa wanasema kwa namna moja ama nyingine, na wengine kwa maneno makali kuliko mimi, walisema kwamba mazingira ya chuki yaliyopo Marekani yalikuwa ndiyo chanzo cha kifo cha Rais. Lakini Malcom X aliposema kitu kilekile, ikawa nongwa kubwa.
Ratiba yangu ya kumtembelea bwana Muhammad kila mwezi ilikuwa ni siku iliyofuata. Nilipokuwa kwenye ndege nilipatwa na hisia kuwa jambo fulani litatokea. Siku zote nimekuwa na hisia kali juu ya mambo.
Tulisalimiana na bwana Muhammad kwa bashasha. Lakini nilihisi kuna kitu hakiko sawa kwenye ucheshi wake wa kawaida. Kwa miaka mingi nilijivuna kuwa mimi na bwana Muhammad tulikuwa karibu sana kiasi kwamba nilijua alivyohisi kutokana na nilivyohisi, kama alikuwa na wasiwasi basi nilikuwa na wasiwasi, kama nilikuwa mtulivu basi nilifahamu naye alikuwa mtulivu. Sasa nilikuwa nahisi mkazo. . . .
Tulianza kwa kuongelea mambo mengine. Kisha akaniuliza, “Umeona magazeti ya leo asubuhi?”
Nilijibu, “Ndiyo, nimeyaona.”
“Hiyo ilikuwa ni kauli mbaya sana, nchi hii ilimpenda sana mtu yule. Nchi yote ipo katika maombolezo. Haukuwa wakati muafaka kusema yale. Kauli kama ile inaweza kuwapa wakati mgumu Waislamu wote.”
Kisha kwa kama sauti iliyosikika kutoka mbali, alisema, “Itanibidi kukuzuia kuongea kwa siku tisini zijazo ili Waislamu wote waweze kuepukana na kosa hilo.”
Nilipigwa na ganzi. Lakini nilikuwa mfuasi wa bwana Muhammad. Siku zote nilikuwa nawaambia wasaidizi wangu kuwa mtu yeyote aliye kwenye nafasi ya kutoa adhabu, yeye mwenyewe anatakiwa kuwa tayari kupokea adhabu.
Nilimwambia bwana Muhammad, “Nakubaliana nawe na niko tayari kutumikia adhabu hiyo kwa asilimia mia moja.”
Nilipanda ndege kurudi New York huku nikijiandaa kisaikolojia kuwaambia wasaidizi wangu wa Msikiti Namba Saba kuwa nimesimamishwa au “Nimenyamazishwa.”
Lakini kwa mshangao, nilipofika nilikuta wasaidizi wangu walikuwa tayari wamepewa taarifa. Na kilichonishangaza zaidi ni kuwa ujumbe wa telegram ulikuwa umetumwa kwa kila gazeti, redio na kituo cha televisheni cha New York. Kusambaza ujumbe huo ilikuwa ni kazi ya haraka na ya ufanisi kabisa kuwahi kuona ikifanywa na maafisa wa Chicago.
Simu zote nilizoweza kupatikana ziliita. London. Paris. AP., U.P.I. Na kila kituo cha redio na televisheni na magazeti yote walinipigia simu. Wote niliwaambia kuwa “Nilikosa kumtii Muhammad. Na nakubaliana kabisa na busara zake. Na pia kuwa nategemea kuendelea kuongea tena baada ya siku tisini.”
“Malcom X anyamazishwa!” vilisema vichwa vya habari.
Hofu yangu kubwa ilikuwa iwapo kashfa ile ikaibuka ndani ya siku tisini zijazo, basi sitakuwa na uwezo wa kuisemea nami nilikuwa ndiye Muislamu mwenye uzoefu zaidi katika kushughulika na vyombo vya habari ambavyo vingeikuza kashfa yoyote iliyotokea ndani ya Taifa la Kiislamu.
Baadae nilikuja kufahamu kuwa kunyamazishwa kwangu kulienda mbali kuliko nilivyofikiria. Sikuzuiwa tu kuongea na
vyombo vya habari, bali sikuruhusiwa hata kufundisha ndani ya Msikiti wangu Namba Saba.
Baadaye likatoka tangazo ndani ya Taifa la Kiislamu kuwa nitarudishwa ndani ya siku tisini,
“Iwapo atatubu.”
Kwa mara ya kwanza hili lilinifanya nianze kuwa na mashaka. Nilikuwa nimetubu kabisa. Lakini kwa makusudi kabisa, Waislamu walikuwa wakionyeshwa kuwa nilikuwa nimeasi.
Sikupambana mtaani kwa miaka mingi na kuwa mjinga. Nilifahamu nilipokuwa nategwa.
Siku tatu baadaye nilipata habari kuwa afisa mmoja wa Msikiti Namba Saba ambaye alikuwa msaidizi wangu wa karibu sana, alikuwa akiwaambia baadhi ya ndugu wa Msikiti pale kuwa, “Kama mngefahamu alichofanya Imam Malcom X, mngeenda kumuua kwa mikono yenu.”
Na hapo nikafahamu wazi. Kama ambavyo kila afisa ndani ya Taifa la Kiislamu alifahamu, kwamba tishio la kuuawa liliweza kutolewa na mtu mmoja tu.
***
Kichwa changu kilikuwa kama vile kinavuja damu kwa ndani. Nilihisi ubongo wangu umeharibika. Nilienda kumuona Dr. Leona. A. Turner ambaye alikuwa daktari wa familia yangu kwa miaka mingi, alikuwa anafanyia kazi yake huko East Elmhurst, Long Island. Nilimuomba anichunguze ubongo.
Alinichunguza na kusema kuwa nilikuwa kwenye mkazo mkubwa na nilihitaji kupumzika.
Mimi na Cassius Clay(Muhammad Ali) hatuko pamoja leo hii. Lakini siku zote nitamshukuru kuwa katika kipindi hiki, alipokuwa huko Miami akijifua kupigana na Sonny Liston, alitukaribisha, mimi, Betty na watoto kwenda huko kama wageni wake-ikiwa kama zawadi ya miaka sita ya ndoa yangu na Betty.
Nilikutana na Cassius Clay mnamo mwaka 1962 huko Detroit. Yeye na kaka yake Rudolph walikuja kwenye mgahawa mdogo wa wanafunzi uliokuwa karibu na Msikiti wa Detroit, wakati huo Elijah Muhammad alikuwa karibu kuhutubia mhadhara mkubwa. Kila Muislamu alivutiwa na ndugu wale. Cassius alinifuata na “Kunipa tano.” Na kujitambulisha kama ambavyo alivyokuwa akijitambulisha baadaye duniani, “Naitwa Cassius Clay.” Alijitambulisha kama vile ninapaswa kuwa nafahamu yeye ni nani. Basi nikafanya kama vile namfahamu. Lakini ukweli ni kuwa mpaka wakati ule nilikuwa sijawahi kumsikia kabisa. Tulikuwa watu wa dunia mbili tofauti kabisa. Ukweli ni kuwa Elijah Muhammad alikuwa ametuzuia Waislamu kushiriki aina yoyote ile ya michezo.
Muhammad alipokuwa anaongea, ndugu wawili wale waliongoza katika kupiga makofi. Hilo lilimpendeza kila mtu kwa kutokuwa kwao wanafiki—haiwezi kusemwa walikuwa wanatafuta mashabiki maana eneo la mwisho duniani kwa mtu kwenda kupata mashabiki wa ndondi ilikuwa ni kwenye mihadhara ya Waislamu.
Kutoka siku hiyo, nikawa nasikia hapa na pale kuwa Cassius alikuwa akihudhuria Misikiti na migahawa ya Kiislamu kwenye miji mbalimbali. Na kila ilipotokea nilikuwa nikihutubia sehemu ambayo yupo na aliweza kufika basi alihudhuria.
Nilipendezwa sana naye. Tabia yake ilimfanya kuwa mmoja wa watu wachache sana niliowahi kuwaalika nyumbani kwangu. Betty pia alipendezwa naye. Na watoto wetu walimpenda sana. Cassius alikuwa kijana aliyeweza kumpendeza mtu yeyote, mwenye urafiki, nadhifu na mnyenyekevu. Alikuwa ni mtu makini sana hata kwa mambo madogomadogo. Kwa jinsi alivyokuwa anajitia hamnazo kwenye umma nilihisi kuwa alikuwa na mpango wa kumuwezesha kushinda, na alikiri hilo kwa kuniambia kuwa alikuwa na mpango wa kucheza na akili ya Sonny Liston ili aingie ulingoni akiwa na hasira, asiyejifua vizuri na mwenye kujiamini kupita kiasi—akitegemea ushindi wa haraka kama kawaida yake. Si tu kwamba alisikiliza ushauri, bali aliuomba pia. Mwanzoni nilimsisitiza jinsi ambavyo mafanikio ya mtu maarufu yanavyotegemea anavyofahamu na kuelewa tabia na malengo halisi ya watu wanaomzunguka. Nilimuonya kuhusu “mbweha-wajanja” kama alivyowaita wanawake vijana na warembo waliomzonga; nilimwambia Cassius kuwa hao hawakuwa “Mbweha-wajanja” walikuwa mbwa mwitu hatari. Hii ilikuwa ndiyo safari ya likizo ya kwanza ya Betty tokea tumeoana. Watoto wetu watatu walicheza na kurukaruka na
bingwa aliyepigania mkanda wa uzito wa juu.
Sijui ningefanya nini iwapo ningebaki New York katika nyakati zile tete—nikiwa nimezingirwa na simu zilizoita muda wote. Kutoka kwa waandishi wa habari, na wengine wote waliokuwa na shauku ya kufurahia anguko langu.
Nilikuwa nimepata mshtuko wa kihisia. Nilikuwa kama mtu aliyekuwa kwenye ndoa nzuri kwa miaka kumi na miwili, na kisha ghafla asubuhi moja wakati wa kifungua kinywa mwenza wake akamsukumia karatasi za talaka.
Nilihisi kama kuna kitu fulani cha asili kiliharibika, labda jua au nyota. Lilikuwa ni jambo kubwa kwangu kiasi kwamba akili yangu ilishindwa kulikubali. Kwenye kambi ambayo Cassius alikuwa akijifua, na kwenye Motel ya Hampton House ambako familia yangu iliishi, niliongea na mke wangu na watu wengine, na ukweli ni kuwa nilikuwa naongea maneno ambayo hayakuwa na maana yoyote. Chochote nilichosema kilitoka kwenye sehemu ndogo tu ya ubongo wangu, sehemu kubwa ilikuwa imejawa na mambo zaidi ya elfu yaliyotokea katika miaka kumi na mbili iliyopita . . . mambo yalivyokuwa Misikitini . . . jinsi tulivyokuwa pamoja na familia ya bwana Muhammad. . . nyakati tuilizokuwa pamoja na Waislamu wengine—kibinafsi, nikiwahutubia na katika mijumuiko ya kijamii . . . na nyakati nilipohutubia umati uliokuwa na wazungu ndani yake, na kuongea na vyombo vya habari.
Pale kwenye kambi ya Cassius Clay niliongea na waandishi kadhaa wa habari za michezo, niliwaambia tena na tena kuwa nilianza kuona habari ya kuwa nitarudishwa baada ya siku tisini kuwa ni uongo. Lakini kisaikolojia sikuwa tayari
kukubaliana na ukweli: kwamba mimi na Taifa la Kiislamu tulikuwa tumepeana talaka ya moja kwa moja. Unaelewa ninachomaanisha? Sahihi ya jaji kwenye karatasi inaweza kuwaachanisha wanandoa—lakini kwao wote, kama walikuwa na ndoa nzuri, itawachukua miaka mingi sana kuachana kisaikolojia.
Sikuweza kuepuka mbinu na hila za wazi kutoka Chicago za kuniondoa kabisa kutoka katika Taifa la Kiislamu kama
siyo kutoka duniani kabisa. Nilianza kuuona kabisa mpango wao wa kunitoa.
Muislamu yoyote atakuwa alifahamu kuwa kauli yangu ya “Kuku kurudi nyumbani kulala” ilikuwa ni kisingizio tu cha kuandaa mpango wa kunitoa. Na hatua ya kwanza ilikuwa tayari imeishatimizwa. Waislamu waliaminishwa kuwa nilikuwa nimemuasi bwana Elijah Muhammad. Sasa niliweza kuona jinsi hatua ya pili itakavyokuwa. Nitaendelea kusimamishwa na baadaye kutengwa moja kwa moja. Hatua ya tatu itakuwa kuwachochea Waislamu fulani wasiojua ukweli waniue ikiwa kama kutimiza wajibu wao wa kidini, au kunitenga kabisa hadi nipotee kwenye macho ya umma.
Mtu pekee aliyefahamu hali halisi alikuwa ni mke wangu. Sikuwahi kuwaza kuwa nitakuja kumtegemea mke wangu kama nilivyokuja kumtegemea Betty. Si kwamba tulikuwa tunazungumza sana. Betty hakusema chochote, lakini niliweza kuona kuwa kuna jambo linamzonga japo anaonekana mtulivu. Nilifahamu kuwa alikuwa mtumishi
muaminifu wa Allah kama nilivyokuwa. Na nilifahamu kuwa atasimama nami kwa hali yoyote ile.
Maneno ya kifo hayakuniogopesha. Kwa miaka kumi na miwili niliyokuwa na bwana Muhammad, nilikuwa tayari kujitolea maisha yangu wakati wowote ule kwa ajili yake. Kitu ambacho kwangu kilikuwa kibaya kuliko kifo ilikuwa ni usaliti. Niliweza kuelewa kifo, lakini sikuweza kuelewa usaliti—hasa kutokana na uaminifu nilioonyesha kwa Taifa la Kiislamu na kwa bwana Muhammad. Katika miaka kumi na miwili iliyopita, iwapo bwana Muhammad angetenda kosa na kuhukumiwa kifo, ningejaribu kusema mimi ndiye niliyetenda ili kumuokoa na ningeenda kwenye kiti cha umeme kama mtumishi wa bwana Muhammad.
Basi nikiwa kwenye ile kambi ya Cassius Clay kama mgeni wake, nilijitahidi kutoa matatizo yangu binafsi akilini na kukazia matatizo ya Taifa la Kiislamu. Bado nilikuwa napambana kujiaminisha kuwa ni kweli bwana Muhammad alikuwa anatimiza unabii. Maana kiukweli kabisa niliamini kuwa kama bwana Muhammad siyo Mungu, basi hakika alisimama pembeni ya Mungu.
Lakini kilichovunja imani yangu ilikuwa ni kitendo cha bwana Muhammad. Badala ya kukiri mbele ya wafuasi wake yale aliyotenda kama udhaifu wa kibinadamu au utimizo wa unabii—kitu ambacho niliamini kabisa kuwa Waislamu wangekielewa au walau wangekubaliana nacho, yeye akataka kuficha aliyofanya.
Hilo ndilo lilikuwa pigo kubwa zaidi kwangu.
Hapo ndipo nilipoanza kutambua kuwa nilimuamini bwana Muhammad kuliko imani yake juu yake yeye mwenyewe.
Na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuanza kujifikiria mimi mwenyewe baada ya kutoweza kufanya hivyo kwa miaka kumi na miwili.
Niliondoka Florida kwa muda mfupi ili kuwarudisha Betty na watoto nyumbani kwetu huko Long Island. Nilipata habari kuwa maafisa wa Chicago walikuwa wamechukizwa na kitendo changu cha kwenda kwenye kambi ya Cassius Clay. Walihisi kwamba Cassius hana nafasi yoyote ya kushinda. Na kwamba mimi kujihusisha naye kutawaabisha Waislamu. (Sifahamu kama bingwa leo hii anakumbuka kuwa magazeti mengi yaliandika habari za kabla ya pambano isipokuwa gazeti la
Muhammad Speaks. Japokuwa Cassius alikuwa ndugu wa Kiislamu lakini gazeti la Kiislamu halikuona umuhimu wa kuandika pambano lake.)
Nilirudi tena Miami, nikiamini kuwa ni mpango wa Allah kunifanya mimi nimsaidie Cassius kuuonyesha ulimwengu ukuu wa Uislamu—kuonyesha kuwa akili huzidi nguvu. Sihitaji kukukumbusha jinsi watu walivyodhihaki uwezekano wa Cassius Clay kumpiga Liston.
Safari hii nilikuja na picha za Floyd Patterson na sonny Liston kutoka kwenye kambi zao za kujifua, wakiwa na makasisi wakizungu kama washauri wao wa kiroho. Cassius Clay, akiwa kama Muislamu, hakuhitaji kuambiwa yale ambayo Ukristo wa kizungu umemfanyia mtu mweusi wa Marekani. “Hili ni pambano juu ya kweli,” nilimwambia Cassius. “Ni pambano la kwanza la ulingoni kati ya Msalaba na Mwezi. Ni vita ya kisasa ya kidini. Mkristo na Muislamu wakikabiliana huku televisheni zikiuonyesha ulimwengu mzima kinachotokea!” Nilimwambia Cassius, “Unafikiri Allah amepanga yote haya ili wewe utoke ulingoni bila ushindi?” (Utakuwa unakumbuka kuwa wakati wa kupima uzito wa mabondia, Cassius alikuwa akipiga kelele, “ushindi wangu umetabiriwa! Siwezi kupigwa!”)
Washauri wa Sonny Liston walimfanya apambanie zaidi “uchangamano” kuliko kujifua kupambana na Cassius. Mwishowe akawa amefanikiwa kupanga nyumba kubwa kwenye eneo la wazungu. Nyumba hiyo ilimilikiwa na mmiliki wa timu ya Baseball ya New York, Dan Topping. Baadhi ya jioni mimi na Cassius tulikuwa tukitembelea maeneo ya watu weusi. Watu weusi wale walibaki midomo wazi, wakishangaa kuwa alikuwa kati yao badala ya maeneo ya wazungu kama ambavyo mabingwa wengi weusi walivyopendelea. Mara kwa mara Cassius aliwashangaza watu weusi wale kwa kuwaambia, “Nyie ni watu wangu. Ninapata nguvu zangu kwa kuwa kati ya weusi wenzangu.”
Kitu alichokuja kukutana nacho Sonny kilikuwa si cha kawaida—kitu kutoka kwa mtu anayemuabudu Allah na asiyeogopa chochote.
Katika viti zaidi ya elfu nane vilivyokuwepo ndani ya ukumbi wa mikutano wa Miami, nilipata kiti namba saba. Siku zote namba saba imekuwa namba yangu ya bahati.
Imefuatana nami maisha yangu yote. Nilichukulia hilo kama ujumbe kutoka kwa Allah kuwa Cassius Clay alikuwa anaenda kushinda pambano. Mbali na Cassius, pia nilikuwa na wasiwasi juu ya ndugu yake Rudolph ambaye alikuwa anafanya pambano lake la kwanza la kulipwa kwenye pambano la utangulizi.
Cassius alimuangalia ndugu yake akimshinda mtu mmoja mweusi kutoka Florida aliyeitwa “Chip” Johnson. Alikuwa amekaa nyuma ya ukumbi kwa utulivu na amevalia suti. Baada ya miezi mingi ya vioja na vituko vya wakati wa kupima uzito, sasa alikuwa na utulivu wa ajabu. Utulivu huu ulitakiwa kuwashtua wachambuzi wa michezo waliyemtabiria kupigwa vibaya.
Basi Cassius akapotea, kwenda kuvaa kwa ajili ya kumkabili Liston. Kama tulivyokubaliana, nilijumuika naye katika kuomba Baraka za Allah. Mwishowe wakawa ulingoni na Liston, kila mtu kwenye kona yake. Nilikunja mikono yangu na kuwa mtulivu kabisa, kamera za televisheni zingeweza kukufanya uonekane mpumbavu unapokuwa unashangilia pambano.
Pambano lilienda kama Cassius alivyopanga isipokuwa kwa kemikali fulani iliyomuingia machoni na kumfanya asione vizuri kwenye raundi ya nne na ya tano. Aliweza kuepuka makonde yenye nguvu ya Liston. Kufika raundi ya tatu, Liston ambaye umri ulikuwa umeanza kwenda alianza kuchoka, alikuwa amejifua na kujiaminisha kuwa atamaliza pambano ndani ya raundi mbili tu. Mwishowe Liston akapoteza pambano. Siri ya matokeo ya pambano lile la kihistori ilikuwa ni kuwa miezi kadhaa kabla ya usiku wa pambano, Clay alikuwa ameishamshinda Liston kiakili.
Pengine hakujawahi kuwa na sherehe ya bingwa mpya iliyokuwa na utulivu kama ile. Mfalme kijana wa ulingoni alifika kwenye Motel niliyoishi. Alikula aiskrimu na alikunywa maziwa na mcheza mpira mashuhuri, Jimmy Brown, rafiki wengine na baadhi ya waandishi wa habari. Kutokana na usingizi, alilala kidogo kitandani kwangu kisha baadaye akaenda kwenye makazi yake.
Asubuhi iliyofuata tulipata kifungua kinywa pamoja, baada ya hapo alifanya mkutano na waandishi wa habari na kutoa tangazo lililokuwa kichwa cha habari duniani kote, alitangaza kuwa yeye ni “Muislamu Mweusi.”
Lakini ngoja nikuambie kitu kimoja kuhusu hilo. Cassius hakujitangaza kama “Muislamu Mweusi.” Waandishi wa habari ndiyo walioandika hivyo, alichowaambia ni kuwa: “Naamini katika dini ya Kiislamu, nikimaanisha naamini kuwa hakuna Mungu isipokuwa Allah na Muhammad ni mtume wake. Hii ni dini ileile inayoaminiwa na watu zaidi ya milioni mia saba ambao si weupe huko Afrika na Asia.”
Hakuna kitu cha ajabu katika mambo yote yaliyofuata kama kitendo cha Floyd Patterson kutangaza kuwa; akiwa kama Mkatoliki anataka kupambana na Cassius Clay ili mkanda wa ubingwa wa juu usiwe mikononi mwa Muislamu. Kilikuwa kitendo cha kusikitisha sana kutoka kwa Mkristo mweusi aliyechotwa akili, akiwa tayari kumpigania mzungu
ambaye hataki kabisa kujihusisha naye. Kama majuma matatu mbele, magazeti yakaandika taarifa kuwa huko Yonkers, New York, Patterson alikuwa anauza nyumba yake ya dola 140,000 kwa pungufu ya dola 20,000. Alikuwa “Amechangamana” kwenye mitaa ya wazungu ambao walifanya maisha yake kuwa ya taabu sana. Hakuna aliyemtendea kirafiki, na watoto wao waliwaita watoto wake “Niggers.” Jirani yake mmoja alikuwa amemfundisha mbwa wake kwenda kujisaidia kwenye uwanja wa Patterson. Mwingine alijenga uzio ili watu weusi wasionekane. “Nilijaribu lakini haikuwezekana,” Patterson aliviambia vyombo vya habari.
***
Agizo la kwanza la kuuawa kwangu, lilitolewa kupitia afisa wa Msikiti Namba Saba ambaye alikuwa msaidizi wangu wa karibu. Msimamizi wangu mwingine wa karibu wa zamani alipewa jukumu na kutekeleza jambo hilo. Alikuwa ni ndugu mwenye uzoefu na vilipuzi; alielekezwa ategeshe bomu kwenye gari langu ambalo litalipuka mara tu nikiliwasha. Lakini inaonekana ndugu huyu aliona jinsi nilivyokuwa muaminifu kwa Taifa la Kiislamu hivyo hakutekeleza amri ile, na badala yake alinifuata. Nilimshukuru kwa kuokoa maisha yangu. Nilimwambia ukweli ya yaliyokuwa yakiendelea huko Chicago. Alipatwa na mshangao mkubwa sana.
Ndugu huyu alikuwa na ukaribu sana na ndugu wengine kutoka Msikiti Namba Saba ambao wangeweza kutumika
kuniua. Alisema kuwa atachukua jukumu la kuwaelimisha wote ili wasije kutumika vibaya.
Agizo hili la kuuawa kwangu ndilo lililosababisha nianze kukubali talaka ya kisaikolojia kati yangu na Taifa la Kiislamu.
Kila nilipokuwa—mitaani, maeneo ya biashara, kwenye lifti, kwenye magari nk, nilianza kuona sura za Waislamu niliowafahamu, na nilifahamu kuwa yeyote kati yao anaweza kuwa anasubiri apate nafasi nzuri ya kunimiminia risasi.
Nilikuwa naumiza kichwa juu ya nini cha kufanya. Haikuwezekana kutenganisha maisha yangu na harakati za mtu mweusi wa Marekani. Jamii ilinichukulia kama “Kiongozi.” Kwa miaka mingi nilikuwa nimewashambulia wale walioitwa “Viongozi” wa watu weusi kutokana na kasoro zao. Sasa ilinipasa kujitafakari na kujiuliza iwapo nina sifa za kuweza kumsaidia mtu mweusi katika mapambano yake ya kupigania haki. Nilikuwa na uzoefu wa kutosha kuelewa kuwa ili kuratibu na kusimamia kitu chochote na kikafanikiwa, unatakiwa kwanza kuchunguza hali halisi na kweli za msingi.
Kwanza kabisa nilijua kuwa nina mtaji wa kujulikana kimataifa. Hakuna kiasi cha pesa ambacho kingeweza kununua hilo. Nilifahamu vyema kuwa iwapo nitasema jambo lolote linalostahili kuwa habari watu watalisoma na kulisikia, pengine hata duniani kot—kutegemeana na jambo lenyewe. Pia ndani ya jiji la New York, ambako ingekuwa ndiyo sehemu yangu ya kazi, nilikuwa na wafuasi wengi ambao hawakuwa Waislamu. Wafuasi hao wamekuwa wakiongezeka tokea siku ile niliyowaongoza Waislamu kuandamana kwenda polisi wakati walipompiga ndugu yetu Hinton. Mamia ya watu weusi wa Harelm waliona hilo, na maelfu wengine walisikia jinsi ambavyo tulionyesha kuwa watu weusi wanaweza kutimiza jambo lolote iwapo watamkabili mzungu bila woga. Tokea siku hiyo, Harlem yote ilijionea jinsi polisi walivyowaheshimu Waislamu. (Hicho ndicho kipindi ambacho inspekta wa polisi msaidizi wa kituo namba 28 aliponiambia, “Hakuna mtu anatakiwa kuwa na nguvu kiasi hicho.”)
Kwenye miaka iliyofuata nilipata ushahidi mbalimbali unaaonyesha kuwa asilimia kubwa ya watu weusi wa New York waliitikia yale niliyosema, kutia ndani wengine wengi sana ambao hawawezi kukiri hilo hadharani. Kwa mfano, karibu mara zote nilipohutubia mihadhara ya mitaani, nilikusanya watu mara kumi hadi kumi na mbili ya wale waliokusanywa na “Viongozi” wengine wa watu weusi. Nilifahamu kuwa kwenye jamii yoyote, kiongozi wa kweli ni yule anayestahili kufuatwa kutokana na matendo yake. Wafuasi wa kweli wanakuja wenyewe kwa hiari yao. Nilifahamu kuwa tatizo kubwa la “Viongozi” wa watu weusi wenye majina makubwa ni kukosa kwao kueleweka na watu weusi walioishi maeneo ya maghetto. Wangewezaje kueleweka wakati muda mwingi waliutumia “kuchangamana” na wazungu? Nilifahamu kuwa watu wa maghettoni walifahamu vyema kuwa kiroho sikuwahi ondoka maeneo ya maghetto, na hata kimwili sikuondoka zaidi ya ilivyolazimu. Nilikuwa na silika za kighetto; kwa mfano, niliweza kuhisi iwapo mkazo haukuwa wa kawaida kwenye hadhira ya watu wa maghettoni. Na niliweza kuongea na kuelewa lugha ya maghettoni. Kulikuwa na kisa kimoja ambacho kilinijia akilini kila mara nilipomsikia mmoja wa “viongozi wa watu weusi” wenye majina makubwa akidai kuwa anaongea kwa niaba ya watu weusi waishio maeneo ya maghetto.
Siku moja baada ya mkutano kwenye mitaa ya Harlem, nilipokuwa naongea na mmoja wa “Viongozi” hawa kutoka mjini-kati, tukafuatwa na mpambanaji mmoja wa mitaa ya Harlem. Sikuwahi muona mpambanaji yule hapo kabla. Alituongelesha kwa sekunde kadhaa akitumia lugha ya mtaani hasa, kisha akaendelea na safari yake kwenye barabara ya saba.
“Kiongozi” yule kutoka mjini-kati alibaki anamuangalia mpambanaji yule kama vile amemsikia mtu akiongea Kihindi. Aliniuliza alichoongea nami nikamwambia.
Ninachotaka kumaanisha ni kuwa, nikiwa kama “kiongozi,” ninauwezo wa kuongea kwenye vinasa sauti vya vyombo vya habari kama ABC, CBS , NBC au chuo cha Harvard na Tuskegee; ninaweza kuongea na watu weusi wa “daraja la kati” na watu weusi waishio maeneo ya maghetto(watu ambao viongozi wengine hawaishi kuwazungumzia) na kwa vile nami niliwahi kuwa mpambanaji, nilielewa vyema kuliko wazungu wote na vyema kuliko karibu “viongozi” wote wa watu weusi—kwamba mtu mweusi hatari kuliko wote ndani ya Marekani ni mpambanaji kutoka maeneo ya maghettoni.
Kwa nini nasema hivyo? Mpambanaji kwenye msitu wa maghettoni anaheshimu mamlaka ya mzungu kwa kiasi kidogo kuliko mtu mweusi yoyote katika Amerika ya Kaskazini. Mpambanaji wa maghettoni hana kitu chochote ndani yake kinachomzuia kufanya lolote. Hana dini, hana wazo la maadili, hawajibiki kama raia, haogopi chochote. Ili aishi, muda wote yuko macho akitafuta mtu wa kumnyonya, muda wote anatafuta binadamu dhaifu kama mnyama Chororo-kaya afanyavyo. Mpambanaji wa maghettoni siku zote na muda wote ni mtu wa vurugu. Kila anachofanya anajitoa mzimamzima.
Na kinachomfanya mpambanaji wa maghettoni awe hatari zaidi ni “picha” inayopendeza anayowaonyesha vijana wa maghettoni walioacha shule. Vijana hawa wameona jinsi wazazi wao walivyotaabika kutafuta maisha au jinsi walivyokata tamaa ya kupambana kwenye ulimwengu wa mzungu wa kibaguzi na usio na uungwana. Wanaamua kuwa ni bora wawe kama wapambanaji ambao wanawaona wamevalia “nadhifu” na kuonyesha pesa, na kutojali yoyote wala chochote. Hivyo vijana wa maghettoni wanaanza kuvutiwa na maisha ya wapambanaji, maisha ya madawa, wizi, ukahaba—kwa ujumla uhalifu na ukosefu wa maadili.
Mara ya kwanza nilipoona hatari ya vijana hawa iwapo watachochewa kufanya vurugu niliogopa sana. Mchana mmoja wakati wa majira ya joto nilihudhuria mkutano mmoja kwenye mitaa ya Harlem ambao ulikuwa na vijana hawa wengi sana. Nilikuwa nimealikwa na viongozi “makini” wa watu weusi ambao kwa kawaida walikuwa hawaongei nami; nilifahamu kuwa walitumia tu jina langu ili kuvuta watu. Nilipofika jukwaani, niliuambia umati ule kuwa ukweli ni kuwa sitakiwi pale, jina langu limetumika tu kuvuta watu, kisha nikashuka.
Sijui kwa nini nilifanya vile! Wale vijana wakaanza kughadhabika na kupiga kelele. Ndani ya muda mfupi barabara zikawa zimefungwa na umati wenye hasira. nilipanda juu ya gari na kupunga mkono nikiwataka watulie. Walitulia, kisha nikawaomba waondoke nao wakafanya hivyo. Huo ndiyo wakati ilipoanza kusemwa kuwa nilikuwa mtu mweusi pekee ndani ya Marekani aliyeweza ‘Kuzuia machafuko ya watu wa rangi tofauti au kuyaanzisha.’ Sijui kama ninaweza kufanya lolote kati ya hayo. Lakini nafahamu kitu kimoja: kwa dakika chache zile nilijifunza kuheshimu moto uliopo ndani ya wapambanaji na vijana wanawaowahusudu—watu wa maghettoni ambao mzungu wa kaskazini amewafungia humo kwa miaka mia moja.
Majira ya joto ya mwaka 1964 huko Harlem, Rochester na katika majiji mengine, yametoa picha ya kitu kinachoweza kutokea—na ni picha tu sababu vurugu zote zile zilitokea kwenye maeneo ya watu weusi tu. Ukiacha watu hawa wa maghettoni wenye hasira wachochewe sawasawa na tukio fulani, na kisha walipuke hasira na kutoka kwenye maeneo yao hadi kwenye maeneo ya wazungu! Ndani ya jiji la New York ukiwaruhusu watu weusi wenye hasira watoke Harlem na kuvuka bustani ya Central Park, au chukulia Chicago South Side, ikiwaacha watu weusi wale waingie mjini-kati. Ukiwaacha watu weusi wa Washington D. C waingie barabara ya Pennsylvania. Detroit tayari imeshuhudia maandamano ya amani ya watu weusi zaidi ya laki moja—fikiria kuhusu hilo. Bomu la kijamii la watu weusi liko karibu kila jiji, Cleveland, Philadelphia, San Francisco, Los Angeles . . . kote huko hasira ya mtu mweusi inatokota.
***
Nimetoka nje ya mada na kuzungumzia baadhi ya matukio yaliyonifundisha kuheshimu hatari iliyopo maeneo ya maghetto. Nilikuwa najaribu kuelezea jinsi nilivyochunguza sifa zangu kwa makini iwapo ninafaa kuwa “kiongozi” huru wa watu weusi.
Mwisho wa uchunguzi wangu nikafikia hitimisho kuwa uchaguzi juu ya jambo hilo ulikwisha fanyika. Umati wa watu wa maghettoni uliniamini na kuniona kama kiongozi miongoni mwao. Nilifahamu vyema kuwa watu wa maghettoni humuamini yule tu ambaye ameonyesha kuwa hawezi kuwauza kwa mzungu. Na si tu kuwa sikuwa na nia ya kuwazua, lakini jambo hilo halikuwa hulka yangu.
Niliiona changamoto ya kuunda taasisi ambayo itasaidia kutibu ugonjwa wa mtu mweusi wa Amerika ya Kaskazini— ugonjwa unaomfanya aendelee kuwa chini ya miguu ya mzungu.
Mtu mweusi wa Amerika ya Kaskazini alikuwa mgonjwa wa kiakili kutokana na jinsi alivyokubali na kufuata utamaduni wa mzungu kama kondoo.
Mtu mweusi wa Amerika ya Kaskazini alikuwa mgonjwa kiroho sababu kwa karne kadhaa ameukubali Ukristo wa mzungu—Ukristo unaomwambia Mkristo mweusi asitarajie undugu wa kweli kati ya binadamu wote, bali avumilie ukatili wa wale wanaojiita Wakristo wakizungu. Ukristo umewafanya watu weusi wasiweze kufikiri sawasawa.
Umemfanya mtu mweusi afikirie kuwa; iwapo hana viatu na hana chakula-“Tutapata viatu, na maziwa na asali, na samaki wa kukaanga Mbinguni.”
Mtu mweusi wa Amerika ya Kaskazini alikuwa mgonjwa kiuchumi na hilo lilinaonyeshwa wazi na jambo moja: akiwa kama mteja, alipata kidogo kuliko anachostahili, na kama mzalishaji, alitoa kidogo zaidi. Mtu mweusi wa Marekani anatuonyesha picha halisi ya tegemezi—chawa mweusi ambaye yupo kwenye kiini macho kuwa anapiga hatua sababu yupo kwenye chuchu za ng’ombe mnene ambaye ni Marekani ya mzungu. Kwa mfano, kwa mwaka watu weusi hutumia dola bilioni 3 kwa ajili ya magari, lakini Marekani hakuna muuza magari mweusi wa maana. Kwa mfano, asilimia arobaini ya Scotch Whisky ghali zinazoingizwa nchini hushuka kwenye makoo ya mtu mweusi anayetafuta hadhi; lakini viwanda pekee vya pombe vinavyomilikiwa na mtu mweusi vipo bafuni au mahali fulani huko porini. Au kwa mfano jambo la aibu linaloendelea katika jiji la New York. Ndani ya jiji hili kuna watu weusi milioni moja lakini biashara za watu weusi zilizoajiri zaidi ya watu kumi hazifiki ishirini. Ni kwa sababu watu weusi hawamiliki na kudhibiti biashara kwenye maeneo yao ndiyo maana hawana jamii imara. Mbaya kuliko yote ni kuwa mtu mweusi wa Amerika ya Kaskazini alikuwa mgonjwa kisiasa. Amemruhusu mzungu amgawe kwenye upumbavu wa “mrepublikani” mweusi na “mdemokrati” mweusi, “mliberali” mweusi na “mhafidhina” mweusi . . . wakati kura milioni kumi za watu weusi ndizo zingeweza kuwa zinaamua siasa za Marekani—maana kura za wazungu zimegawanyika sawa sawa kati ya warepublikani na wademokrati. Sanduku la kura ndipo mahali pekee ambapo mtu mweusi anaweza kufanya harakati zake kwa heshima, na kwa kutumia nyenzo na nguvu ambayo mzungu anaielewa, anaiheshimu, anaiogopa na kukubaliana nayo. Ngoja nikuambie kitu! Iwapo kamati ya wapiga kura weusi ingewaambia wanasiasa “wenye chuki kali” dhidi ya watu weusi, “Tunawakilisha kura milioni kumi,” mtu huyo mwenye chuki angeruka na kusema, “Unaendeleaje rafiki? Karibu ndani!” iwapo watu weusi wa Mississippi wangepiga kura kama kikundi kimoja, Eastland angejidai kuwa mliberali kuliko Jacob Javits—au vinginevyo asingeweza kusalia madarakani. Unafikiri ni kwa nini mwanasiasa huyo mbaguzi anapambana kufanya watu weusi wasiweze kupiga kura?
Kama kuna kikundi cha watu kinaweza kupiga kura kwa pamoja na kuamua matokeo ya uchaguzi na kinashindwa kufanya hivyo, basi kikundi hicho kinaumwa kisiasa. Kuna wakati wahamiaji waliufanya ukumbi wa Tammany kuwa mahali penye nguvu sana katika siasa za Marekani. Mwaka 1880, meya wa kwanza Mkatoliki mwenye asili ya Ireland alichaguliwa kuongoza jiji la New York, na kufikia mwaka 1960, Marekani ikawa na Rais wa kwanza Mkatoliki mwenye asili ya Ireland. Iwapo watu weusi wa Marekani wangepiga kura kama kitu kimoja, wangekuwa na nguvu zaidi ya hizo.
Siasa za Marekani zinaongozwa na maslahi ya vikundi mbalimbali na uwezo wa kushawishi. Ni kundi gani ambalo maslahi yao yanatakiwa kushugulikiwa haraka, kundi gani linahitaji kupiga kura kwa pamoja zaidi ya watu weusi? Chama cha wafanyakazi kinamiliki ndani ya jiji la Washington moja ya majengo makubwa yasiyo mali ya serikali—jengo ambalo lipo mahali ambapo wanaweza kuona kila kitu kinachoendelea kwenye ikulu ya Marekani, na hakuna hatua yoyote ya kisiasa inayochukuliwa bila ya kupitia ushawishi wao. Makampuni makubwa ya mafuta yanapata ruzuku kupitia ushawishi. Mkulima, kupitia ushawishi wake amekuwa kikundi kinachopokea ruzuku kubwa kuliko vyote ndani ya Marekani, sababu ni kuwa mamilioni ya wakulima hawapigi kura kama wademokrati, warepublikani, waliberali au wahafidhina, bali wanapiga kura kama wakulima.
Madaktari wanaushawishi wenye nguvu zaidi katika Washington. Walipigania maslahi yao na kufanikiwa kuzuia mpango wa Medicare uliohitajiwa na mamilioni ya watu. Kwa nini kuna vikundi vyenye ushawishi vya walima ngano, mbogamboga, wafugaji wa ng’ombe, na hata cha Wachina!
Nchi ndogo kabisa ambazo watu hawajawahi kuzisikia zina watu wao wenye ushawishi ndani ya Washington, wakiwakilisha maslahi yao.
Serikali ina idara zinazoshughulika na vikundi vinavyopambana kuonekana na kusikika. Idara ya kilimo inashughulika na mahitaji ya wakulima. Kuna idara za elimu, afya na ustawi wa jamii. Kuna idara ya mambo ya ndani ambayo ndani yake inashugulika na mambo ya Wahindi. Je mkulima, daktari na Mhindi ndiyo matatizo makubwa yanayoikabili Marekani leo hii?Hapana—ni mtu mweusi! Kulitakiwa kuwe na idara yenye ukubwa wa Pentagoni, ikishughulikia kila aina ya matatizo ya watu weusi.
Watu weusi milioni ishirini na mbili! Wameitumikia Marekani kwa miaka mia nne, tokea vita ya uhuru, wamepambana na kufa katika vita zote; wamekuwepo ndani ya Marekani kabla ya wahamiaji wa mwanzo, na miaka mingi kabla ya mafuriko ya wahamiaji—lakini leo hii wako chini kwenye kila nyanja.
Ikitokea kesho kila mtu mweusi kati ya watu weusi milioni ishirini na mbili akatoa dola moja ili kujenga jengo lao ndani ya jiji la Washington. Na kila asubuhi, kila mbunge apokee ujumbe unaomjulisha matakwa na matarajio ya mtu mweusi wa Marekani—sauti ya matakwa ya mtu mweusi inatakiwa kuwa kwenye kila sikio la kila mbunge.
Nguzo zinazoendesha nchi hii ni nguvu za kiuchumi na kisiasa. Mtu mweusi hana nguvu za kiuchumi—na itamchukua muda mrefu kuwa nazo. Lakini sasa mtu mweusi wa Marekani ana nguvu za kisiasa kuweza kubadili mustakabali wake ndani ya siku moja tu.
***
Taasisi niliyokuwa naiwazia kuunda kichwani mwangu ili kumsaidia mtu mweusi kupata haki zake kama binadamu, kumtibu maradhi yake ya kiuchumi, kisiasa na kiroho ilikuwa ni kubwa sana. Lakini kama unataka kujenga kitu chochote cha maana, unatakiwa kuanza na mpango wa maana.
Taasisi niliyopanga kuunda ilikuwa tofauti kabisa na Taifa la Kiislamu kwa sababu ilikuwa ya watu weusi wa dini zote, na itaenda kutimiza kile ambacho Taifa la Kiislamu lilihubiri tu.
Tetesi zilienea kwa kasi, hasa kwenye miji ya mashariki— nimepanga kufanya nini? Kitu cha kwanza kufanya ilikuwa kuvutia watu ambao wako tayari. Kila siku, ndugu wanaharakati, watu wa vitendo ambao walikuwa nami katika Msikiti Namba Saba, walikuwa wanatangaza kujitoa kutoka Taifa la Kiislamu na kujiunga nami. Kila siku nilipata uungwaji mkono kutoka kwa watu weusi ambao hawakuwa Waislamu, na cha kushangaza walikuwepo wengi kutoka kwa watu weusi wa “daraja la kati” na “daraja la juu” yaani wenye “kujiweza,” watu waliochoshwa na na hadhi za uongo. Watu walianza kuwa na mshawasha: “Lini utaitisha mkutano, lini tutajipanga?”
Nilikodi ukumbi wa dansi kwenye hoteli ya Theresa kwa ajili ya mkutano wetu wa kwanza. Hoteli hiyo ilikuwa kwenye makutano ya mtaa wa 125 na ya barabara ya saba, moja ya maeneo ya Harlem yenye pilika nyingi.
Gazeti la Amsterdam News liliandika habari za kikao chetu na kusema kuwa tulipanga kuanzisha Msikiti wetu kwenye hoteli ya Theresa. Barua, simu na ujumbe wa telegram kutoka nchini kote vilifika hotelini pale vikinitafuta. Ujumbe wao mkubwa walisema kuwa kitu hiki ndicho watu walichokuwa wakikisubiria. Watu ambao sikuwahi hata kuwasikia walionyesha imani kubwa sana kwangu kwa namna iliyonigusa sana.
Watu wengi walisema kuwa sheria kali za kimaadili za Taifa la Kiislamu zilikuwa kikwazo kwao, hivyo walitaka kuungana nami.
Daktari mmoja aliyekuwa anamiliki hospitali ndogo, alinipigia simu akitaka kujiunga. Wengine wengi sana walituma michango yao hata kabla hatujatangaza sera zetu hadharani. Waislamu kutoka miji mingine waliniandikia barua kuwa watajiunga nami. Wengi wao wakidai kuwa “Taifa la Kiislamu halifanyi chochote” . . . “Taifa la Kiislamu lilikuwa linajikongoja sana.”
Wazungu wengi nao walitupigia simu na kutuandikia barua wakitaka kutoa michango na kuuliza iwapo wanaweza kujiunga. Jibu lilikuwa ni hapana, hawawezi kujiunga, ni watu weusi tu ndiyo waliruhusiwa, lakini kama waliweza wangeweza kuchangia fedha kwa ajili ya harakati zetu za kutatua tatizo la ubaguzi wa rangi ndani ya Marekani.
Mialiko ya kuhutubia ikaanza kumiminika—asubuhi moja ya Jumatatu tulipokea mialiko ishirini na mbili.
Nilishangazwa sana kuona idadi isiyo ya kawaida ya mialiko ilitoka kwa wachungaji wa Kikristo wazungu.
Niliitisha mkutano na waandishi wa habari. Nilikaa mbele ya kinasa sauti, Taa za kamera zilimulika huku na kule. Waandishi wa habari, wanaume, wanawake, wazungu, weusi—wakiwakilisha vyombo vya habari vilivyofika duniani kote, walikaa wakiniangalia, wameshika kalamu zao na vitabu vyao tayari kuandika.
Nilitangaza kuwa: ‘Nitakwenda kuanzisha na kuongoza Msikiti mpya ndani ya jiji la New York, na utaitwa Muslim Mosque Inc(Msikiti wa Waislamu, Inc.” Hilo lingetupa msingi wa kidini na nguvu ya kiroho ambayo ni muhimu ili kuondoa mambo yanayoharibu maadili ya watu katika jamii yetu.
“Msikiti wa Waislamu, Inc utakuwa na makao yake makuu kwa muda kwenye hoteli ya Theresa, katika Harlem. Utakuwa ndiyo kambi kwa ajili ya harakati za kutokomeza ukandamizaji wa kisiasa, unyonyaji wa kiuchumi na mmomonyoko wa kijamii ambao kila siku unawakabili watu weusi milioni ishirini na mbili wa Marekani.” Baada ya hayo waandishi wa habari wakaanza kuniporomoshea maswali.
***
Haikuwa rahisi kama ninavyosimulia. Nilitembelea mara nyingi nilitembelea maeneo mbalimbali huku nikiwaza kuwa baadhi ndugu zangu wa zamani walikuwa na mawazo kuwa wataonekana mashujaa ndani ya Taifa la Kiislamu iwapo wataniua. Nilifahamu fikra za wafuasi wa Elijah Muhammad; niliwafundisha wengi jinsi ya kufikiri. Nilifahamu vyema kuwa hakuna mtu anayeweza kukuua haraka kuliko Muislamu iwapo atahisi kuwa hilo ndilo Allah anamtaka afanye.
Kulikuwa na jambo lingine kubwa nililotakiwa kufanya. Nilikuwa nalo kichwani kwa muda mrefu sana nikiwa kama mtumishi wa Allah. Lakini lilihitaji pesa ambazo sikuwa nazo. Nilipanda ndege hadi Boston. Kwa mara nyingine nilimgeukia dada yangu Ella. Japo kuna nyakati nilimkasirisha Ella toka nitoke Michigan nikiwa kijana mshamba, lakini Ella hajawahi kutoka karibu yangu.
“Ella,” nilisema, “Ninataka kwenda Mecca kuhiji.” Ella alisema, “Unahitaji kiasi gani?”
Mwisho wa sura ya 16