Lycaon pictus
JF-Expert Member
- Jan 31, 2021
- 9,189
- 16,128
- Thread starter
-
- #21
SURA YA IX
KUMALIZIKA KWA DARAJA YA MTO WA TSAVO
KUMALIZIKA KWA DARAJA YA MTO WA TSAVO
WASIWASI WOTE ulipotuondokea pakawa hapana tena shaka juu ya simba, kazi iliendelea upesi mno, na daraja ya Tsavo ikawa karibu kumalizika. Katika kujenga misingi, na nguzo zilipozidi kwenda juu, tukawa twafikiri namna ya kunyanyua yale mawe mazito na kuyapandisha juu. Hatukuwa na winchi (mashine ya kuyainulia), na kwa sababu hiyo nikashughulika kutengeneza majukwaa ya mataruma mawili ya reli yenye kimo cha futi thelathini thelathini. Mataruma haya, kwa juu yakafungwa pamoja na kwa chini yakatanuliwa kwa nafasi ya futi kumi kumi, tukayakita katika magogo makubwa ya miti. Hekima hii ilitufaa, nasi tukawa twapandisha yale mawe kwa kuvuta kamba katika roda, baada ya kuyafunga huku chini; naam baada ya muda mfupi tu tukamaliza kazi yetu ya kujenga.
Kazi yetu ya pili ikawa ni kupima urefu ule tuutakao wa futi sitini kati ya nguzo kwa boriti za chuma. Kwa kuwa sikuwa na winchi wala magogo ya kutosha kuvutia boriti za chuma na kuzilaza sawasawa, nikapata fahamu za kutengeneza nguzo za kujishikiza kati ya kila tao, zilizojengwa kwa magogo ya miti namna ya kihero. Zikachukuliwa boriti kubwa za miti zikalazwa toka huku kwenye nguzo za mawe mpaka kwenye vile vihero, halafu zikapangiliwa reli; kisha zile boriti za chuma zikavutwa juu sawasawa hali ya kuwa zimo katika mabehewa yake zilimoletewa kutoka Mombasa.
Kisha zikanyanyuliwa katika yale mabehewa, tukatekua zile nguzo na ile boriti ikateremka sawasawa taratibu. Ile boriti ya pili ilipokwisha wekwa tayari, hatukusubiri mara tukaanza kuunga reli, hapo tena nikawa na hamu mno ya kuona gari la moshi la kwanza likijaribu kupita juu ya daraja ile.
Ajabu niliyoona ni kuwa baada ya siku au mbili hivi tangu kumalizika ile daraja na kuondolewa ile mihimili ya katikati, ilinyesha mvua kubwa ajabu. Mto ukaanza kujaa upesi upesi nao mara ukafurika, maji yakawa mfano wa gharika, ukang'oa miti mizima mizima na kuibingirisha kama vitakataka. Mto ukazidi kujaa nami nalisimama juu ya daraja yangu mpya nikitazama daraja mbili ndogo ndogo za troli tulizozijenga kwa sababu ya kutuletea mawe na mchanga kama zitasalimika au vipi. Kutahamaki nikaona zege la mataruma ya reli na ghasia nyingine ambazo nilijua ni troli vikipitishwa yosa yosa kwenye gurufa ya mto kwa mbali kidogo. Kuona hivyo nikadhani kuwa pengine ni troli inavuka kwa juu. Ilivyokuwa, nikaona inazidi kuja kule nilikokuwa nayo imejaa maji tele kabisa. Moyo wangu ulishtuka kidogo nilipoona daraja ya pili nayo ikikumbwa nalisikia mshindo mkubwa ajabu, kumbe ni mbao zikibabaduliwa na kuvunjwa, hizo zikaelemezwa upande wangu, kusiachwe hata alama ya daraja. Mkumbo huo hakika ulikuwa mkubwa kwani hata zile reli zilipondekapondeka kwa kunyongwa na mashina ya gogo ya miti kama kwamba ni nyuzi za simu.
Ghasia zote hizo za daraja hizo mbili zikawa zinachukuliwa na maji kwa kasi na kugongana na zile nguzo za daraja kubwa. Ama nalifadhaika sana bali kwa tumaini la moyoni juu ya kazi niliyofanya, hakika nikaona daraja yangu salama, na mara nikaona ghasia nyingine za zile daraja zilizokumbwa zikipitishwa kati ya matao ya nguzo na kwenda kwa kasi kabisa wa moja mpaka baharini.
Naam, naliyashuhudia hayo yakitendeka hali moyo umejaa furaha kabisa kwa kazi yangu njema niliyoifanya. Hatukukaa sana mara tukaingiliwa na vituko vingine Tsavo. Kwani ingawa tulisalimika na simba, sasa tunahangaishwa na chui, mafisi, mbwa wa mwitu, shume, na wanyama wengine wengi wa mwituni. Wanyama hawa walitutia hasara nyingi juu ya makundi ya kondoo na mbuzi waliokuwa wamefugwa kwa ajili ya maziwa na kitoweo. na watu walikuwa wakifurahi mno kama mmoja wao atanaswa mtegoni.
Katika wanyama wasumbufu, chui ametia shani kwani yeye haui kwa sababu ya kutaka kula bali kiasi cha mchezo tu: nami nalikuwa na chuki nao mno tangu siku ile yule mmoja alipokuja usiku akaua kundi zima. Wakati ule wanyama wangu walitimu kadiri ya thelathini wa kila aina ambao naliwafuga kwa ajili ya maziwa na kwa sababu ya kitoweo, wamefungiwa katika kibanda kimoja cha nyasi kando kidogo ya boma langu.
Usiku mmoja tulifadhaishwa mno kwa ghasia nyingi humo kibandani, bali kwa kuwa wakati ule ulikuwa kabla ya nyamaume hawajauawa, hakuna aliyethubutu kutoka kuangalia sababu ya udhia huo. Basi palipita muda mrefu kabla ya vituko vyote havijamalizika kabisa. Nilipotoka kwenda kule kibandani kutazama yaliyotokea, maskini, nikaona si mbuzi wala si kondoo, kila mmoja amenyooka twaa, mkavu wa juzi na kutazama tena nikaona hakuna aliyeliwa ila kukatwa kooni tu. Katika kuzidi kuangalia nikaona kuwa kile kibanda kilitobolewa tundu pana, na kwa ishara ya nyayo zilizoenea pale pote nikajua kuwa hakuna mnyama mwingine ila chui. Kwa jeuri yake hakuna hata mnyama mmoja aliyemla, ila wote aliwauma na kuwaua tu, kiasi cha kufurahisha moyo wake.
Nikatumai kuwa bila ya shaka, usiku atarudi kuja kula nyama zake. Kwa sababu ya dhana hiyo ile mizoga nikaiacha vile vile ilivyolala, nikatafuta mtego madhubuti wa chuma uwezao kumzuia chui hodari, nikautia mle kibandani nikaufunga kwa mnyororo mrefu wa kutosha kuburutika hata nje. Tukakaa kimya kabisa mle bomani mwangu, giza likaanza kufungamana, tukawa twasikiliza chui apige kelele atakapokuwa ameshikwa na mtego mle kibandani. Katikati ya usiku tukasikia mchupo wa nguvu na papo hapo tukasikia mlio wa hasira na kuchugachuga. Wakati wote huo nalikuwa nimekaa na bunduki yangu tayari pamoja na taa ikiwaka, nami kusikia hivyo nikatoka upesi huku nimeandamiwa na askari wangu mmoja amechukua ile taa.
Kiasi cha kukikabili kile kibanda, yule chui akaturukia kwa ghadhabu kiasi cha urefu wa ule mnyororo, hivi yule askari akaogopa mno akakimbia pamoja na ile taa akaniacha gizani kabisa. Giza la usiku huo lilikuwa zito mno kama la usiku wa jana nami sikuweza kuona chochote; walakini nalijua upande gani wa kupigia bunduki, nami kiasi cha kuielekeza ikanitoka risasi.
Kwa kiasi nilichoweza kuona, nalimwona akichugachuga nje na ndani mle bandani. Nikapiga kelele kuwaambia watu kuwa nimemwua, nao wote wakatoka nje pamoja na taa zote wakaja nazo. Akaja msimamizi wangu mmoja wa Kihindi, naye pia akasema kuwa atataka kujilipiza kisasi kwa kuwa baadhi ya mbuzi wengine walikuwa wake. Papo hapo akachomoa bastola yake akamwelekeza nayo yule chui hali amekwisha kufa, akafunga macho, akammiminia risasi nne mara moja. Hakuna hata moja iliyompiga mnyama yule bali aliwatisha wenzake waliokuwa wakitazama na mara hiyo wakatawanyika huko na huko. Asubuhi yake, kwa bahati pakapita kikosi cha Wakamba, ambao sina shaka walishikwa mno na njaa, wakanishauri niwape ruhusa ya kumchuna, wao wapate kuchukua ile nyama yake. Kwa kweli sikusita kuwapa ruhusa na kwa muda wa dakika chache ngozi ikawa imekwisha chunwa tena vizuri kabisa, kisha wao wenyewe wakaanza kunyang’anyana ile nyama.