SEHEMU YA PILI
SURA YA KWANZA
VITA KATI YA WAKUU.
VUNJO.
MPAKA hapa tulipofika tumesoma habari za Wachaga hata za wakati ule wakuu wa Kichaga walipojisimamisha kuwa watawala wa nchi ndogo ndogo. Basi, sasa tutaendelea na kusimulia habari ya majira watawala walipopigana wao kwa wao, na wakuu wengine waliokuwa na nguvu walipojimilikisha katika sehemu kubwa ya nchi.
Wakuu wa Vunjo walianzisha hali hii kwanza, nao waliwatangulia wengine kadiri ya vizazi kadhawakadha kabla hawajajaribu kufanya hivyo.
Wakuu wa Mamba. Labda Marawite mkuu wa Mamba alikuwa wa kwanza wa Kichaga kuweka na kuwafundisha askari kwa taratibu. Kisha kuwafundisha, aliwachukua, akaenda nao nchi ya Rombo, na huko aliwatiisha watu mpaka kufika nchi ya Mkuu. Marawite alirudi kwake na mateka mengi, na huku nyuma watu waliasi, lakini aliwaendea tena akawaadhibisha kwa kukatakata na kuharibu viunga vyao vya migomba.
Marawite alirithiwa na Mafuluke mwanawe ambaye alifanya vita na mkuu Iwite wa Marangu akamshinda, lakini baada ya muda kupita alipatana naye. Tena, Mafuluke alimsaidia Nyange wa Kilema ajipatie tena utawala wake na kumfukuza Musuo. Watu wa Msae na wa Kondeni walijiweka chini ya Marawite kwa hiari yao. Wakati ule, nchi ya Mwika pia ilikuwa sehemu ya Mamba, wala haikuwa utawala wa peke yake mpaka baadaye, na mkuu wake alikuwa Kyasimba ambaye ni baba wa mtawala wa sasa wa Mwika. Wakati alipokuwa akitawala mwanamke Mashina, Kyasimba aliasi akauawa vitani.
Pia Mafuluke alishughulika na mambo ya Kilimanjaro ya magharibi, maana alimsaidia Warsingi mkuu wa Uru kuwafukuza Wamachame waitoke nchi, na kwa kuwa alikuwa rafiki wa Warsingi alimsaidia pia kumpiga Iwere mkuu wa Kibosho. Hivi nguvu za Mafuluke zikajulikana kotekote; ikachukua muda mrefu kabla ya kutokea mkuu mwingine wa Kichaga aliyefanya nguvu yake ijulikane pande zote mbili, yaani mashariki na magharibi ya Kilimanjaro.
Malamia mwanawe Mafuluke alipopata umri wa kutosha, Mafuluke akajiuzulu, lakini Malamia aliishi miaka michache tu akafa. Malamia alipokufa, ndugu yake Ngawondo alikuwa mdogo tu, na kwa hivi Mafuluke akaushika tena utawala. Wakati huo watu wa nchi ya Mkuu waliasi, lakini walitiishwa upesi, wakaadhibiwa kwa kuharibiwa mashamba yao na viunga vyao vya migomba.
Mara Ngawondo alipopata umri wa kutosha kushika utawala, Mafuluke akajiuzulu tena. Ngawondo alikuwa mtu wa vita, akashughulika sana katika kuwafundisha askari wake, akawavisha ngozi nyeusi za ndama, kofia za ngozi na kanda mikononi na miguuni. Kila askari alijaribiwa uhodari wake kwa kupiga upindi, na wale walioshinda waliwekwa katika jeshi la pekee lililoitwa Wasaghara, ila wale waliosalia hawakupata jina wala kuruhusiwa kuwinda.
Basi, alipokwisha kuwafundisha askari wake hivi, Ngawondo alifanya vita na watu wa Kahe, Ugweno, na Waukuma, yaani Waarusha. Akaendelea kufanya vita na majirani zake wote, akajipatia sifa katika nchi nzima. Siku moja Ngawondo alifanya vita na watu wa nchi ya Mkuu waliokuwa wameasi tena, akateka ng'ombe wengine alioweka Mafuluke huko Mkuu. Basi, Mafuluke alikasirika, maana yeye hakutoa ruhusa Ngawondo afanye vita na Mkuu. Basi alipokutana na ng'ombe wanaletwa, alimwua mtu mmoja wa Ngawondo aliyekuwa akiwatangulia. Ngawondo alikuwa nyuma ya ng'ombe, naye alipopata habari ya tendo hili, alighadhabika, akawafukuza ng'ombe mbele kwa nguvu sana, wakamwangusha Mafuluke, wakamkanyaga, akaumia vibaya hata kesho yake akafa. Baada ya siku chache tu, Ngawondo mwenyewe akafa.
Hapo paliondokea ushindani juu ya mtu wa kuurithi utawala, maana Keenya mwana mkubwa wa Ngawondo alikuwa mtoto mdogo tu. Kweli, nduguye Ngawondo Lyombe alipendwa na watu, lakini waliogopa ya kuwa hatakubali kumwachia Keenya utawala hapo atakapopata umri wa kutosha. Basi, watu walifikiri sana wakapata shauri la kufaa. Mafuluke alikuwa amemwoa binti ya Iwite mkuu wa Marangu, na kwa kuwa Iwite alimwonea wivu Mafuluke kwa ajili ya nguvu zake, alimshawishi binti yake amwue mumewe kwa sumu. Lakini Mafuluke aliambiwa habari hizi na kijana mwanamke jina lake Mashina ambaye Iwite alimpa binti yake awe kijakazi chake. Basi, Mafuluke kwa kuwa alikuwa na shukrani, alimwoa yule kijana Mashina akapendwa sana na watu kwa sababu ya busara yake. Basi, hapo Ngawondo alipokufa, watu walimchagua Mashina atawale mpaka Keenya awe amepata umri wa kutosha, naye hata Lyombe alitoa nchi kwa hiari yake mwenyewe, akahama akaenda kukaa Uru. Kirumi, mwanawe Lyombe alirudi baada ya miaka kupita, akakaa Mamba tena.
Mashina alikuwa na busara, na watu wote wakamheshimu, lakini kwa kuwa ni mwanamke ilikuwa lazima aweke wanaume kuwaongoza askari wake vitani, na mmoja aliyesifiwa zaidi alikuwa Mawinje.
Mashina alikuwa mtawala mwenye nguvu wa mwisho wa Mamba, na katika wakati wa utawala wake, nchi yake ilishindana na wakuu wawili wenye maarifa mengi ya vita, ndio Rongoma na Horombo, ambao kila mmoja alipata kutawala nchi yote ya Vunjo.
RONGOMA.
Tuliposimulia habari za Kilema, tulifika mpaka wakati Kombo alipourithi ukuu. Katika utawala wake, Kilema iliingiwa na Ngaramite mkuu wa Marangu aliyesaidiwa na watu wa Chimbili na wengine wa Ugweno. Kombo alikimbia pamoja na watu wake wote mpaka Kirua alipotawala Mosha. Basi, ikatokea ya kuwa Mosha alimtamani mkewe Kombo, akajaribu kumshawishi ampe sumu mumewe na mwanawe Rongoma pia. Lakini yule mwanamke alikimbia, akarudi Kilema, na Kombo na watu wake wote walimfuata. Mara alipopata habari hii, Ngaramite aliingia tena Kilema pamoja na rafiki zake Wagweno. Kombo alitaka kukimbia tena, lakini mke wake alijipatia silaha, akawaongoza watu wa Kilema kuonana na adui, na hapo Kombo aliona haya, na yeye mwenyewe akaja akawaongoza. Watu wa Kilema walijipa moyo kwa kuwa wameona ushujaa wa yule mwanamke, wakapigana kwa nguvu nyingi sana wakawashinda kabisa adui zao.
Basi, baada ya hayo, Kombo alinuia kumpiga Mosha kwa kuwa alifanya tendo ovu lile wakati alipokuwa mgeni wake. Akampeleka mwanawe Rongoma Utaita ili apate msaada lakini alikawia sana, na huku nyuma yeye mwenyewe alipata msaada kutoka Ugweno akawashinda watu wa Mosha, akawaweka chini yake. Baada ya muda kupita Rongoma alirudi kutoka Utaita ameleta watu wa kupigana pamoja naye, na kwa kuwa nchi ya Kirua ilikuwa imekwisha wekwa chini ya baba yake Kombo, walifanya vita na Marangu iliyotawaliwa na Masanjuo, wakateka sehemu ya nchi ile.
Baada ya miaka michache kupita, Kombo alijiuzulu, na Rongoma mwanawe aliurithi utawala. Wakati huo huo Kilewo aliyekuwa mkuu wa Marangu akafa pia, na mara ile Rongoma alipeleka tarishi kuwakaribisha wanawe Kilewo waje kukaa pamoja naye ili apate kuwatunza, maana kwa kuwa ni mzao wa Mremi, alifanya kama anataka kuwa kaka yao. Silawe na Ishosho wana wawili wa Kilewo walikwenda Kilema wakapokewa vizuri, lakini walipotaka kurudi kwao, Rongoma aliwafanya wafungwa, kisha, aliingilia Marangu akajitangaza mkuu kwa haki, kwa kuwa ni mkubwa wa ukoo, uliotoka wakuu wa nchi zote mbili.
Sasa na tuache habari za matendo ya Rongoma, tupate kuchungua habari za sehemu nyingine, na kusimulia habari za matendo ya Horombo aliyekuwa mkuu, kushindana na Rongoma.
HOROMBO.
Tumesoma jinsi wakuu wa Mamba walivyowashinda watu wa Rombo. Katika siku zile hapakuwa na wakuu katika upande ule wa pili wa mlima, ila kulikuwa na watu wachache wachache tu walioongozwa na wakubwa wao, kama ilivyokuwa katika sehemu nyingine za Kilimanjaro kabla ya kusimamishwa wakuu. Katika nchi ya Useri tu kulikuwa mkuu, lakini Useri haikuwa sehemu ya milki ya Mamba. Mtu mmoja jina lake Moosinyi wa ukoo wa Kumba alikuja na wafuasi wake wakakaa Keni, na kijukuu chake jina lake Ukongi alipigana na Marawite wa Mamba kwa muda, na ingawa alishindwa, hata hivi alifanywa mkubwa wa nchi ya Chimbili chini ya Marawite. Chimbili ni nchi iliyo kati ya Mriti na Mkuu. Urio mwanawe Ukongi alimwasi Mafuluke, pia akashindwa baada ya vita vikali vya siku nyingi. Katika vita hivi nchi iliachwa ukiwa wala haikuwa na ng'ombe, lakini Mafuluke aliweka ng'ombe wake wengine kwa watu, na kwa miaka kadhawakadha walikaa kwa amani chini yake. Urio alikuwa na wana wawili, mkubwa alikuwa Msangaro na mdogo aliitwa Horombo. Msangaro alikuwa kijana mpole, lakini Horombo alikuwa mkali wala hawezi kutulia, akamwudhi sana baba yake kwa kuwaua ng'ombe waliowekwa kwao na watu wa Mamba na kuila nyama yake. Alikuwa na nguvu nyingi sana, tena mrefu kuliko wote wa nchi, na kwa hivi hapana mtu aliyethubutu kumchokoza. Katika ujana wake Horombo alijipatia sifa nyingi kwa sababu alimwua tembo peke yake, na watu wa Waalenyi walipokuja wakachukua nyama ya tembo yule, basi, hapo aliwanyang'anya ng'ombe zao wote akawachinja akafanya karamu. Matendo aliyoyafanya Horombo yaliwaogofya sana watu wa Keni mpaka walimwomba awe mkuu wao, maana waliona ya kuwa hakuna njia ila hii ya kupata amani katika nchi. Lakini watu wa nchi zilizo jirani, yaani Mriti, Mengeve, Chimbili, na Mkuu hawakumkubali Horombo, na kwa hivi alifanya vita nao akawanyang'anya ng'ombe wengi sana. Lakini ng'ombe wale aliowachukua, kwa kweli walikuwa ng'ombe za watu wa Mamba, na yule mwanamke Mashina alikuwa mkuu wa huko. Basi, mara alipopata habari ya matendo haya, alipeleka jeshi chini ya amri ya Mawinge kumwadhibu Horombo.
Horombo hakuogopa, lakini alijua ya kuwa hana nguvu ya kupigana na jeshi la Mamba, na kwa hivi yeye na watu wake wakarudi wakakaa mwituni. Baada ya muda kupita, askari wa Mamba walichoka kukaa siku zote tayari kwa vita, wakaanza kukaa kwa raha katika nyumba zilizoachwa tupu na Wakeni. Usiku mmoja walipokuwa wakifanya karamu katika nyumba zile, Horombo akaja na watu wake kwa werevu sana, wakazichoma moto nyumba, na watu walipojaribu kutoka nyumbani waliwaua. Hapana mtu mmoja aliyeokoka katika jeshi zima isipokuwa Mawinge, maana yeye alikuwa akikaa peke yake mbali kidogo na watu wake akikesha.
Baada ya hayo, vita vikaendelea miaka minane kati ya watu wa Mashina na watu wa Horombo. Hapana aliyeweza kumshinda kabisa mwenziwe, wala hapana mmoja aliyeweza kupita mlango uliojengwa kwenye korongo liitwalo Kishingonyi. Basi vita vikaendelea hivi mpaka Mashina akatambua ya kuwa nguvu za nchi yake zinapotea bure, akakubali Horombo awe mkuu wa nchi ya Rombo. Tena akafanya urafiki naye akachanjia na udugu uliodumu mpaka kufa kwake Mashina.
Basi, sasa Horombo alianza kutiisha nchi iliyo- kuwa mbele ya nchi ya Mkuu. Aliwahi kufanya bila shida mpaka alipofika Useri, na hapo Kafuria aliyetawala Useri na Ngasini alimzuia. Kafuria alipata askari zake walio bora Ngasini. Horombo hakuwahi kuitiisha Useri wakati huo kwa sababu mambo mengine yalitokea, ikawa lazima aende kwa haraka kumsaidia Mashina rafiki yake.
Ule urafiki kati ya Mashina na Horombo haukumpendeza Rongoma, maana alishuku ya kuwa kwa namna hii watakuwa na nguvu kushinda zake. Basi, alimwagiza Mashina avunje urafiki na mapatano aliyoyafanya na Horombo, na Mashina alikataa kabisa. Basi, hapo Rongoma alifanya vita naye. Pigano kali sana likafuliza mahali palipoitwa Palenyengi, lakini hapana upande mmoja ulioshinda, na baada ya pigano hilo, vita vikaendelea kwa muda wa miaka sita, na vile vile hapana upande mmoja ulioshinda kabisa. Basi, Rongoma alipoona ya kuwa shauri lake halisitawi, alifanya jambo lisilofuata desturi ya vita. Usiku mmoja alituma kundi la watu, wakaingia Mamba kwa hila, wakamwua Mawinge mkubwa wa askari, wakamchukua Mashina amefungwa mpaka Kilema. Horombo alikuwa amefanya haraka kwenda kumsaidia Mashina rafiki yake, lakini alipofika aliona ya kuwa Mashina ana nguvu ya kuwazuia adui zake. Basi, akarudi kwake ndipo alipopata habari ya kukamatwa kwake, na mara ile alipeleka msaada ili kuzuia nchi ya Mamba isitekwe na Rongoma, lakini alipofika, aliona ya kuwa watu wa Mamba wamekwisha kujiweka katika mikono ya Rongoma, naye amemweka Tarimbo mke wa Ngawondo awe mkuu wa nchi ya Mamba. Horombo alifika mpaka Msae, na hapo alitaka Rongoma aje apigane naye. Kwanza watu wa Horombo walishindwa, wakakimbia na huku wanafukuzwa na watu wa Rongoma, lakini Horombo aliwatia moyo watu wake, wakasimama wakapigana, na watu wa Rongoma walishindwa wakakimbia. Kwa muda, vita vikaendelea, kisha, wakuu wote wawili walitambua ya kuwa hapana mmoja anayeweza kushinda kabisa, na kwa hivi walifanya mapatano, wakaweka mpaka pale penye korongo liitwalo Kishingonyi. Hapo walifanya kama ilivyokuwa desturi yao, yaani walizika mtoto wa kike na mtoto wa kiume wangali hai, na tangu wakati ule, Kishingonyi ni mpaka unaotenga nchi za Rombo na Vunjo.
Basi, sasa Horombo akarudi kufanya vita na Kafuria, akawahi kuteka sehemu ya nchi ya Useri, lakini Kafuria alifanya uhodari sana Ngasini akailinda nchi vizuri sana, wala hakushindwa huko kwa muda mrefu.
Basi, huku nyuma Rongoma alikwenda kuiingilia nchi ya Kirua, na hapo Kikare mwana wa Mosha alikuwa mkuu. Kikare alijaribu kupata mapendeleo mbele ya Rongoma akampa ng'ombe wote waliokuwa katika nchi, lakini hakupata kitu ila kuuawa na watumishi wa Rongoma.
Basi, sasa Rongoma alikuwa akitawala nchi zote toka korongo liitwalo Kishingonyi mpaka Nanga, akaogopwa kotekote. Hata Wamasai waliokuwa wakikaa uwandani wakamwogopa, na walipokwenda kufanya vita na Wagweno, aliwashurutisha warudishe ng'ombe zote walioteka, maana Rongoma aliwapenda Wagweno kwa ajili ya msaada waliompa Kombo baba yake.
Kombo babaye Rongoma alipojiuzulu, mwana wa Rongoma alikuwa amekwisha kuwa mtu mzima. Kombo aliishi mpaka wakati baada ya kufanya amani kati ya Rongoma na Horombo, na kwa hivi hakosi alikuwa mzee wa miaka mingi sana. Rongoma aliishi kadiri ya miaka kumi baada ya kufa kwake babaye.
Basi, baada ya vita na Horombo, miaka kumi ya amani ilifuata, na kwa muda huo Silawe na Ishosho na Mashina walikuwa wamefungwa Kilema. Mwisho, Rongoma alifanya shauri la kuwaua Silawe na Ishosho, lakini mwanawe alilichukia sana shauri hili ovu, na usiku uliotangulia ule uliofanywa kuwa usiku wa kuwaua, alijaribu kuwaokoa. Alikwenda kwa werevu mpaka nyumba waliyofungwa, akaona ya kuwa askari walinzi wamelala usingizi, basi akavunja ukuta wa nyumba. Ishosho alitambaa akatoka katika tundu lililofanywa, lakini Silawe alikuwa mnene, na kishindo alichofanya alipokuwa akijaribu kuongeza tundu ukutani, kiliwaamsha askari. Basi, hapo ikawa kumwacha Silawe, na kesho yake akauawa, lakini Ishosho alikimbilia Uru akapata ulinzi kwa mkuu Warsingi.
Rongoma alishuku matata akajaribu kumdanganya Horombo, akatoa habari ya kuwa anataka kumwoa Mashina, lakini siku iliyofuata ile aliyouawa Silawe, Mashina alinyongwa. Baada ya muda kidogo, Rongoma aliugua akafa. Imehadithiwa ya kuwa Mashina alijua ajali itakayompata, akamwambia Rongoma ya kuwa akimwua, basi roho yake haitatulia ila itamsumbua na kumtesa mpaka amtolee kafara ya barafu kutoka mlima Kibo. Basi, Rongoma alipoanza kuugua, alitoa kafara nyingi za ng'ombe kumtuliza roho ya Mashina, lakini zilikuwa bure, maana alizidi kuugua. Kisha, alimtoa mwanawe awe kafara, na hata hivyo akazidi kuugua. Hatimaye alikumbuka maogofya yale aliyoonywa na Mashina, akawatuma watumishi wengine walioaminiwa sana wapande mlima Kibo wakalete barafu, ambayo alisadiki kuwa ndivyo roho ya Mashina ilivyotaka. Watumishi wale hawakuthubutu kukataa kwenda, wala hawakuthubutu kwenda kupanda mlima Kibo, basi, walijificha mwituni mpaka kupata habari za kufa kwake Rongoma, ndipo walipothubutu kurudi kwao.
Kifo cha Rongoma kilifichwa muda wa miaka miwili, lakini baada ya muda huo, habari ikapata kujulikana kidogo kidogo, na Horombo alifanya haraka kutoka Useri kwenda Mamba, akawaruhusu watu wa huko wamrudishe Keenya kutoka Ugweno. Horombo akaendelea mpaka Marangu, na baada ya vita kidogo tu, alimfukuza Kirita nduguye Rongoma. Kirita alikimbilia Kilema akajiunga na watu wa mwana wa Rongoma aliyeitwa Tewuo. Basi, sasa watu hawa wakaja kufanya vita na Horombo, na vita vikali vikashikana, ikawa Horombo alikuwa karibu kushindwa, lakini mwisho aliwashinda kabisa Kirita na Tewuo. Hapo watu wa Kilema waliingiwa na hofu kuu, na usiku ule ule Tewuo pamoja na watu wengi na ng'ombe zote walitoka nchi ile wakahama kwenda Machame. Hawangaliweza kufanya hivi, lakini Horombo alikuwa amekaa mpakani ili watu wake wapumzike baada ya vita vikali. Basi, alipoingia Kilema aliona ya kuwa watu walio wengi wamekwisha kimbia, akachoma moto nyumba, akachukua mateka yaliyobaki, akarudi kwake. Tewuo na watu wake walipokewa na Rengwa mkuu wa Machame, akawapa nchi ya Kombo wakae huko. Basi, wakakaa huko muda wa miaka ishirini, maana Masaki mwanawe Tewuo alizaliwa huko, na waliporudi Kilema alikuwa amekwisha kuwa mtu mzima.
Katika nchi ya Kirua, Kikare mwana mdogo wa Mosha alirithi utawala, ikawa Horombo kumwambia lazima ajiweke chini yake. Kikare alikataa, na mara Horombo akashika njia kwenda kuitiisha nchi yake.
Basi, sasa Horombo aliweza kutumia nguvu zake zote kutiisha nchi ya Useri, lakini hakufuata desturi yake na kuyaongoza majeshi yake mwenyewe, ila aliwapeleka wakubwa wa askari wapigane na Kafuria, akawaambia washambulie usiku bila kuonya watu. Basi, kwa kuwa alighafalika hivi, Kafuria alishindwa upesi sana, akakimbilia pamoja na watu wake mwituni akajilinda huko kadiri alivyoweza. Lakini baada ya muda alishindwa tena, na Malamia mwanawe alihama pamoja na watu wengi wakaenda Machame, wakakaa huko mpaka kufa kwake Horombo.
Basi, sasa mkono wenye nguvu wa Horombo ulitawala na kuweka amani katika nchi zote za Rombo na Vunjo, lakini kabla ya muda mwingi kupita, nchi ilivurugika na upuzi wa wakati ule. Wakubwa wote waliokuwa chini ya Horombo walikuwa na lazima kutoa ng'ombe wengine kila mwaka, ndio kodi, na Keenya mkubwa wa Mamba alilazimishwa vile vile. Basi, ikawa mtu mmoja jina lake Ndakawo mwana wa yule kijakazi wa Mashina, alitaka kushika ukubwa wa Keenya, akatoa habari ya kuwa ng'ombe aliopeleka Keenya wawe kodi kwa Horombo wametiwa uchawi ili kumwua Horombo. Basi, Horombo alipata habari akasadiki ya kuwa ni kweli, na mara ile aliingilia Mamba akamfukuza Keenya, na Keenya alikimbilia Ugweno. Huko Ugweno alikusanya jeshi la watu, akawatumainia sana hata alimwambia Horombo aje kupigana naye, lakini alishindwa upesi, na watu wa Ugweno walibaki wachache sana hata waliogopa kurudi kwao, na kwa hivi walijificha Marangu. Hapo, Keenya alimshawishi Ishosho kumsaidia kupigana na Horombo na hawa wawili walianza kuiweka nchi ya Marangu tayari kwa vita. Walijenga safu mbili za nyumba za mawe, wakafundisha askari wao kila siku. Mara Horombo alipopata habari ya mambo hayo, alikuja Marangu akawaamuru wajitoe katika mikono yake. Lakini Ishosho na Tewuo walikuwa na tumaini kuu, na licha ya kukataa kujitoa, walipeleka maneno ya ufidhuli kwa Horombo. Ikawa Horombo hakuleta askari wa kutosha pamoja naye kuwashambulia wakati ule, na kwa hivi alirudi kwake, lakini alikamata punda sitini akawachinja wote mpakani, akasema ya kuwa hii ndiyo alama ya kuwaonyesha namna atakavyowatendea na wao. Basi, kwa kuwa hawakushindwa pale, Ishosho na Tewuo walipata moyo, wakaondoka wakaingia nchi ya Mamba. Hapo kukawa vita vikali sana, na askari mia mbili wa Horombo waliuawa, na wengine walikimbia. Sasa adui zake walifikiri ya kuwa vita vimekwisha, wakaanza kujishughulisha kuokota na kukusanya silaha za watu waliouawa vitani, lakini huku nyuma Horombo alikuwa amewakusanya askari wengine wa Rombo na kuwaweka mafichoni, nao wakatoka ghafula wakawashambulia watu wa Marangu wakawachezea mpaka wakachoka sana, wala hawakuweza kuwafuatia wale watu wa Horombo waliokimbia.
Labda Horombo alikuwa akipigana na Wamasai wakati huo wakamshughulisha sana, hatujui, lakini hakuwashambulia watu wa Marangu tena kwa muda wa miaka miwili. Ndipo alipowashambulia akafanya jeshi lake sehemu tatu. Sehemu moja ilimshambulia Keenya, na moja nyingine ikamshambulia Ishosho mbali mbali. Lakini hawakusitawi, ikawa walikuwa karibu kukimbia, kumbe sehemu ile ya tatu ikatokea ikamshambulia Ishosho kwa nyuma yao. Sasa ikawa machinjo tu, na Ishosho mwenyewe aliuawa. Imesemwa ya kuwa mahali walipopigana palitapakaa mifupa mpaka siku za utawala wa Mareale. Keenya aliposikia habari za kuangamizwa Ishosho alishikwa na hofu, akakimbilia Machame, na hapo aliuawa na mkuu Rengwa.
Kwa muda wa miaka minne mitano iliyofuata Mamba haikuwa na mtawala, mpaka Horombo alipomweka Kuwese mwana mdogo wa Mafuluke awe mkuu. Baada ya miaka michache kupita, Kuwese aliuawa pamoja na Horombo katika vita vya mwisho alivyopigana na Wamasai.
Ishosho aliposhindwa, watu wa Marangu walijinyenyekea mbele ya Horombo, akawasamehe akawaambia wamlete mkubwa wanayemtaka wao. Basi, walimleta Shamtembonyi ndugu wa Ishosho na Horombo akamkubali. Shamtembonyi alikuwa mjinga, ndiyo sababu Horombo alimkubali, maana alijua ya kuwa hana haja kushuku kuwa atamwasi. Lakini kabla ya kupita siku si nyingi, watu wa Marangu walichoka upuzi wake, wakamwomba Horombo amweke Itosi ndugu yake mdogo badala yake, na baada ya kupita muda, Itosi alimwua Shamtembonyi ndugu yake.
Wakati huo, Horombo alikuwa akijenga maboma katika nchi ya Keni kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya Msangaroa nduguye na wakuu wa askari zake. Wakati ule, Marinde alikuwa mkubwa wa askari aliyejulikana zaidi. Katika maboma hayo, Horombo alipatengeneza mahali pa kuwazika watu wote waliokuwa na nguvu katika nchi yake, maana alitaka kujua kwa hakika kuwa wamezikwa; wala hawakuitoka nchi yake ili wamfanyie matata. Mahali pengine katika boma lake kubwa ni mahali walipofanya kazi wahunzi waliofua chuma cha kutengenezea silaha. Mahali pengine bomani huitwa "mahali ра masikitiko," ndipo mahali walipokuja watu wa Useri kutoa vyungu vyao kuwa kodi, maana walikuwa wamekwisha toa kila kitu walichokuwa nacho vikabaki vyungu vyao tu, na huyu mkuu alividai hata vyungu vyao. Ipo miti mikubwa mingi nje ya boma, ndiyo iliyopandwa na watu wa Marangu kwa amri ya Horombo. Watu wote wa Vunjo na wa Rombo walishurutishwa kufanya kazi ya kujenga maboma hayo, na hasa watu wa Marangu, maana hao walikuwa waoga, na kila mara vita vilipotokea kati kati ya Horombo na Wamasai, hao watu wa Marangu walijaribu kuepuka wasiingizwe vitani, kwa hivi Horombo aliwadharau akawafanya watu wa kazi badala ya kuwa askari. Wengine wa Marangu lakini walikuwa mashujaa, ndio wale waliongozwa na Nderima nduguye Itoshi, na Nderima alipata sifa hata Horombo alimfanya kuwa mkuu wa nchi ya Samanga iliyo katika Marangu. Lakini baada ya kufa kwake Horombo, Itoshi aliitwaa Samanga akamwua Nderima. Basi sasa Horombo aliitawala nchi yote toka Gasini mpaka Nanga, ambayo ilikuwa nchi kubwa kupita nchi yo yote iliyotawaliwa na mkuu ye yote kabla yake Horombo na baadaye. Lakini hata sasa Wamasai walitembeatembea katika nchi za nyandani, wakashindana naye juu ya malisho waliyotaka kwa ng'ombe zao.
****
Baada ya kushindana sana, Horombo aliteka kundi kubwa la ng'ombe za Wamasai, akawaambia ya kuwa hawawapati tena mpaka wakubali kutoka katika nchi za nyandani. Wamasai walikataa kuondoka, na baada ya muda mfupi wakaja kupigana na Horombo. Walipigana vita vikali kwa siku kadhawakadha, kisha, Wamasai walirudishwa mpaka mto Rombo. Na Wamasai wale waliokuwa katika nyanda za Marangu walirudishwa vile vile, na kwa muda wa miaka mingi hapana Wamasai waliothubutu kuingia katika nchi za Horombo. Baada ya kushindwa mara ya kwanza Wamasai waliomba amani, na Horombo akapatana nao kwa sharti ya kuwa wasipite mpaka kuja kusini ya mto wa Rombo. Lakini Wamasai walilivunja agano hili mara nyingi, na kwa hivi ikawa lazima Horombo kupigana nao mara kwa mara, na vita vya Horombo na Wamasai viliendelea miaka kadhawakadha, hata husemwa kwa muda wa miaka kumi na mitano.
Huku nyuma Wamasai waliongezeka katika nyanda zilizo chini ya Useri, na Kafuria akawa anatafuta njia ya kujilipiza kisasi juu ya Horombo, akawatumia Wamasai katika kupata mradi wake. Basi, akawapelekea ujumbe waje kumsaidia kupigana na Horombo. Wamasai walitaka sana, lakini walikuwa hawana moyo kupigana na Horombo peke yao, basi Kafuria alifanya shauri. Alipata kwao ng'ombe dume thelathini, na kwa hao akanunua mikufu mingi ya chuma akaipeleka kwa Wamasai waliokuwa katika nchi za mbali, iwe zawadi ya kushuhudia mali waliyo nayo Wachaga. Shauri hili lilisitawi, na Wamasai wengi sana toka pande zote wakaja kwenye nchi chini ya Shira.
Wakati huo huo Kikare mwana wa Mosha aliyekimbia Uru wakati wa utawala wa Rongoma, alirudi Kirua, na mara Horombo alipopata habari alipeleka mwanawe Mapusu pamoja na jeshi kumtaka Kikare ajitoe. Basi, hapo Mapusu alipata habari za jeshi la Wamasai akampelekea baba yake taarifu ili kumwomba ruhusa ya kuwashambulia. Kwanza Horombo alisitasita, lakini baadaye akakubali, maana alikusudia kumpa mwanawe nafasi kuonyesha ushujaa wake, na tena yeye mwenyewe aliazimu kuwashambulia Wamasai na jeshi jingine kutoka upande mwingine. Walakini Mapusu alitamani sana kujipatia sifa, akawashambulia Wamasai kwa jeshi dogo tu alilokuwa akiliongoza peke yake. Basi watu wake wakashindwa kabisa na yeye mwenyewe aliuawa vitani pamoja na askari zake wote ila wawili tu, ndio waliorudi kumwambia Horombo habari. Imehadithiwa ya kuwa Horombo alipowaona wanakuja, alisema: "Ninyi mmekuja kuniambia ya kwamba mmemwacha mwana wa mkuu maiti. Vyema, nimesikia." Na pale pale akawaua wote wawili mwenyewe.
Sasa jeshi kubwa la Wamasai lilitapakaa kwenye uwanda wa Chimbili, na watu wote walijaa hofu, tena walikuwa wamechoka vita vya daima. Lakini Horombo alisema "Watu hawa wametupa ng'ombe wengi katika siku zilizopita, na sasa wamekuja kutupa zaidi." Akawakusanya askari zake wote akawaahidia ya kuwa vita hivi vitakuwa vya mwisho kupigana na Wamasai. Wamasai walishauriwa na watu wa Kafuria, wakagawanya jeshi vikosi vitatu, na kimoja lazima kiende kwa nyuma ya watu wa Horombo. Horombo naye aliligawanya jeshi lake vikosi vitatu, na kikosi cha kwanza kiliongozwa na Kuwese wa Mamba, akafaulu kuangamiza kabisa kikosi cha kwanza cha Wamasai. Horombo mwenyewe alishambuliwa na askari wenye nguvu wanne waliochaguliwa kusudi, lakini aliwaua wote wanne peke yake. Kikosi cha pili cha Wamasai kilishindwa pia. Basi, karibu na jioni, kikosi cha tatu cha Wamasai kilikuwa kimewahi kufika nyuma ya Wachaga, wakateka ng'ombe wengine wa Horombo. Horombo aliwaongoza watu wake kupigana nao, wakawaua wengi. Basi, ikawa usiku ulipoingia, wakaacha kupigana. Imesimuliwa ya kuwa uvundo wa maiti ulikuwa mbaya sana hata watu hawakuweza kupata usingizi. Basi, kulipokucha vita vikashikana tena, wakapigana vikali. Panapo saa tisa, watu wengine wa Horombo walijaribu kumshawishi atafute mahali ра salama kwa sababu wamepungua sana, lakini alikataa. Baada ya kupita muda kidogo, sana, mkono wake wa kushoto ulivunjwa kwa pigo la rungu lililotupwa, na kwa hivi hakuweza kuishika ngao yake na kujilinda, na kwa kuwa alikuwa mtu mrefu tena mkubwa, adui zake waliweza kumfanya shabaha kweli kweli, nao hasa nia yao ilikuwa kumwua. Basi ikawa baadaye kidogo alipigwa mshale wa mbavuni, na mara akaonekana kuruka juu hewani, kisha akaangukia mahali penye miamba.
Usiku ukaingia, na watu wa majeshi ya pande zote mbili walikuwa wamechoka kabisa, wakaanza kurudi nyuma. Katika upande wa Wachaga watu wengi waliokuwa wakubwa na mashujaa walikuwa wamekwisha kufa, pamoja na Horombo, na Kuwese wa Mamba, na karibu wakubwa wote wa askari, na askari wengi sana. Lakini Wamasai walipata hasara zaidi, nao walikimbia usiku wakaacha ng'ombe wale waliowakamata. Basi, ikawa ingawa Wachaga walipata hasara nyingi mno, lakini kwa kweli walikuwa wameshinda.
Habari za kufa kwake Horombo zilipofika kwake, Manyaki mke wake mpenzi alijinyonga kwa hofu ya mambo yatakayowajia, pia akawanyonga watoto wake wawili wadogo. Lakini ikatokea ya kuwa Horombo alipoanguka hakufa pale pale, na Mfumo mwanawe alikwenda mahali pale akamkuta bado yu hai lakini karibu kukata roho, akamkata kichwa chake akakichukua kwao, maana aliogopa ya kuwa adui watakuja na kufanya vivyo na kukichukua kichwa cha Horombo kiwe ukumbusho.
Horombo amepata sifa kuwa ni hodari, tena shujaa mkubwa wa watu wote wa Kichaga, akafa katika kupigana na adui wa watu wote wa kabila lake. Nchi ya Horombo ilikuwa kubwa kuliko nchi aliyotawala mkuu ye yote wa Kichaga, lakini tutaona ya kuwa utawala aliousimamisha haukudumu siku nyingi baada ya kufa kwake.
MAMBO MENGINE YALIYOTOKEA ROMBO NA VUNJO BAADA YA KUFA KWAKE HOROMBO.
Mara alipokufa Horombo, ufalme aliousimamisha ulivunjika. Watu wa kila sehemu ya nchi yake wa- kajiwekea mkuu wao wenyewe, na hata katika nchi ya Chimbili, yaani toka Mriti mpaka Mkuu, wana wa Horombo walishindana wao kwa wao juu ya ukuu. Watu wa nchi iitwayo Mkuu waliasi kwa waziwazi, lakini Kisuma mwanawe mkubwa Horombo aliwashawishi ndugu zake wengine washirikiane naye, wakawatiisha watu wa Mkuu kwa muda. Huyu Kisuma alikuwa na nguvu hata akaweza kujitia katika mambo ya Vunjo na kumtoza faini mkuu wa Marangu kama tutakavyosoma halafu, tena mpaka wakati aliotawala Rindi aliushika utawala wa nchi kutoka Kishingonyi mpaka mto Tumi. Lakini Rindi alipotawala, sehemu zilizobaki za nchi za Horombo zilitengana na kutekwa, na husemwa ya kwamba Kisuma alikufa kwa huzuni.
Nguvu za Horombo zilipokwisha, Wamasai walirudi tena katika nyanda, na watu wa Rombo wanalilia hasara ya nchi hizo za malisho mpaka sasa. Hata hivyo zilipotea kwa sababu ya upuzi wao, maana badala ya kumtegemeza mkuu mmoja awezaye kupigana na kuwapatia haki zao, waliwaruhusu watu wajisimamishe ovyo ovyo mpaka kila kilima kilikuwa na mkubwa wake. Basi nchi ilitengana, ikawa nchi ndogo ndogo zisizo na nguvu, kama hali ile iliyokuwa nayo wakati wa zamani walipokuja watu kukaa kwanza katika nchi za Kilimanjaro.
Katika nchi ya Mamba Kuwese alirithiwa na Maricha ndugu yake. Maricha alikuwa mwoga, lakini alifikiri ya kuwa akipata msaada wa Waswahili wengine waliokuwa na bunduki, ataweza kumshinda Kisuma. Lakini alishindwa, na Waswahili wale waliomsaidia waliuawa, na Maricha pamoja na watu wengine wa Mamba walikimbilia Kirua. Kwa muda mrefu kufuata mambo hayo, Mamba ilikuwa haina mkuu, na nchi ilitawaliwa na Kisuma mpaka Kisamaka alipopata msaada wa Itosi wa Marangu akajifanya mkuu wa Mamba akawafukuza Warombo. Warombo walijaribu kuiteka Mamba mara mbili tena, lakini kila mara walishindwa.
Itosi aliendela kutawala katika Marangu mpaka akaugua akafa. Kifo chake kilifichwa na mkubwa wa askari Sarika kwa muda wa kadiri ya miaka miwili, naye ndiye aliyeushika utawala, lakini watu walipopata habari, ikawa Sarika lazima kukimbia, na Salego nduguye Itosi aliushika utawala mahali pa Ndaalio mwana wa Itosi, maana Ndaalio alikuwa mtoto bado. Salego alitawala kwa muda wa miaka ishirini, ndipo Ndaalio akataka haki yake. Salego alipata mapendeleo mbele ya wazee, lakini Ndaalio alipendwa na askari na vijana. Sehemu mbili za watu zilikuwa karibu kupigana, lakini Oshami mkubwa wa askari wa Salego alimtangazia Ndaalio ukuu, na kwa hivi shauri lilikatwa. Basi, Salego alihama akaenda kukaa na Kisamaka, akamwoa dada yake. Alijaribu kushawishi Kisamaka kwenda kufanya vita na Ndaalio, lakini alikataa kwa sababu watu wa Marangu walimsaidia alipopigana na Horombo na Kisuma. Lakini hata hivyo, vita vikatokea, maana Mamganga mama yake Kisamaka alitaka kumsaidia mume wa binti yake, yaani mkwewe, akawashawishi watu wengi wa Mamba kuingia katika nchi ya Marangu, na yeye mwenyewe aliliongoza jeshi mpaka kufika mpakani, kisha akawapa amri Salego na mwanawe mdogo Ndelaiyo. Kisamaka alipoisikia habari hii alikasirika, na husemwa ya kuwa alimwomba Mungu jeshi liangamizwe. Mama yake Ndaalio aliwatia watu wa Marangu moyo kushindana na watu wanaowashambulia, ila aliwaagiza wasiwaue Salego na Ndelaiyo. Basi, watu hao walioingia Marangu waliweza kuingia kidogo, lakini walishindwa katika pigano la kwanza, nao walipotaka kukimbia waliona haiwezekani kwa kuwa kila njia imezibwa. Basi walikimbia huko na huku kwa muda wa siku nne, kisha jeshi zima liliangamizwa. Salego na Ndelaiyo walikamatwa, lakini mama yake Ndaalio aliwaokoa wasiuawe, wakapewa ruhusa kurudi kwao.
Basi, hapo Ndaalio aliwapa watu ruhusa kuingia katika sehemu zile za nchi za Mamba Salego alipopata wafuasi wake, lakini kwa amri ya mama yake hapana mtu aliyeuawa.
Kisamaka alifadhaika mno kwa msiba aliouleta mama yake juu ya nchi yake, akataka kumwua, lakini wazee walimshauri asifanye hivi ila apelike wajumbe kuomba amani. Basi, kama ilivyokuwa desturi alipeleka wajumbe, yaani mzee mmoja amefuatana na mtoto wa kike na mtoto wa kiume wanaongoza kondoo aliyevikwa majani ya msale. Kwa desturi ya Kichaga, wajumbe wa namna hii hawawezi kudhuriwa hata kidogo, na mtu akiwadhuru huwa amefanya kosa lililo kubwa sana. Hata hivyo, Sariko alionana nao akawaua, na mama yake Ndaalio alikasirika mno. Kisamaka aliposikia habari akafikiri ya kuwa sasa hakuna hata tumaini kidogo la kupata amani, akapeleka ujumbe Rombo kuomba msaada kwa Mjumo, mwana mdogo wa Horombo ambaye alimchukia Kisuma kwa kuwa alimwua baba yake. Basi, Mjumo pamoja na wakubwa wengine wa Rombo walimpelekea habari Ndaalio ya kuwa Kisamaka yu chini ya ulinzi wao, na ya kuwa wakimdhuru, basi, lazima watakuja na kupigana na Marangu. Ndaalio alikubali kufanya amani, lakini aliweka sharti ya kuwa Mlawi mwanawe Kuwesa afanywe mkuu wa sehemu moja ya Mamba. Wakati huo huo watu wa nchi ya Msae wakajitenga na Mamba, wakajiweka chini ya mtu jina lake Mrimia. Kwa hivi Mamba ikawa imetengwa sehemu tatu, na kila sehemu ilikuwa na mkuu wake.
Sasa Mlawi alitaka msaada wa Ndaalio kumtoa Kisamaka, kwanza alikataa, lakini baadaye alipeleka kundi la askari katika nchi ya Mamba wakauzunguka mji wa Kisamaka. Waliwaua watu wengi, lakini Kisamaka alijitega mlangoni ameweka silaha tayari, na hapana mtu aliyethubutu kumshambulia. Basi, hapo wale watu walizunguka nyuma ya nyumba yake wakaichoma moto, na moto ulipofika karibu naye, Kisamaka aliruka juu ya mgongo wa fahali mkubwa mweusi akatokea mlangoni ghafula. Mtu mmoja wa Ndaalio alimtupia mkuki, ukampenya mwilini, na alipoanguka, wale wengine walijitupa juu yake wakampiga tena na tena kwa mikuki yao. Katika nyumba hiyo mke wake Kisamaka aliunguzwa mpaka akafa. Basi, hapo askari wa Marangu waliteka nyara nchi ya Kisamaka, na sehemu ile iliyotawaliwa na Mrima, wakamtangaza Mlawi mkuu wa nchi yote ya Mamba. Tendo ovu hilo liliwakasirisha wakuu wa Rombo wakadai fidia kwa ajili ya kila mtu wa Mamba aliyeuawa, tena walidai ng'ombe zote waliochukuliwa warudishwe. Ndaalio aliogopa ya kuwa Warombo wakija kumshambulia, basi na Wakilema nao watamshambulia upande mwingine, akakubali shauri lao. Hapo Warombo walidai ng'ombe 500, mbuzi 500, na majembe 500. Ndaalio alimwomba Mlawi alipe sehemu kwa kuwa alikuwa akimsaidia yeye, Mlawi hakuweza kulipa, lakini alikubali kutoa sehemu ya nchi iliyo upande wa magharibi. Nchi hiyo isipokuwa sehemu ile ya Chero imekuwa chini ya wakuu wa Marangu tokea wakati huo.
Kwa muda huo wote, Tewuo na watu wake walikuwa wakikaa katika nchi ya Machame walikokimbilia, lakini walipata mali nyingi sana, na kwa hivi watu wa Machame waliwaonea wivu. Tena Tewuo na watu wake waliingia katika vita vilivyofanywa na Rengwa juu ya jirani zake, na kwa kuwa walikuwa hodari sana, ikawa Wamachame kuwachukia kama kwamba ni adui zao. Rengwa mwenyewe hakuwaogopa, lakini alipokufa, Mamkinga mwanawe alikubali shauri la kuwaua. Wakati huo huo Horombo alikufa, na mara wale Wakilema waliposikia habari hii waliomba ruhusa kurudi kwao. Lakini walishuku ya kuwa hawataruhusiwa, na kwa hivi walitengeneza mashauri yao kwa siri, wakapata ruhusa ya Kasenga mkuu wa Kibosho kupita katika nchi yake. Tewuo alikusanya ng'ombe zao walio wazuri wakawaacha wengine, na siku moja usiku walitoka katika nchi ile. Lakini Wamachame waliwafukuza wakakutana nao mpakani. Sasa ikawa Mamkinga kuogopa kwenda mbele zaidi, asishambuliwe upande mmoja na Wakilema na upande wa pili na Wakibosho. Basi, hivyo ndivyo walivyorudi kwao wale Wakilema baada ya miaka mingi. Waliikuta nchi yao ukiwa inatumiwa na watu wa Marangu kama mahali pa kuwindia tu. Wamarangu walijaribu kuwazuia, lakini Wakilema walikuwa hawana mahali pengine kwenda wakapigana vikali sana, na kwa hivi Wamarangu waliona ni bora kuwaacha waingie katika nchi yao tena wakakae kwa amani. Baada ya muda kupita, Tewuo alikufa, na Masaki mwanawe aliirithi nchi.
Tendo la kwanza la Masaki lilikuwa kufanya vita na nchi ya Kirua. Ikawa Kikare akajiuzulu katika nchi ile, na Marengo mwanawe wa pili aliurithi utawala. Pengine Marengo huitwa Momino. Marengo alikuwa mtawala mwema akafanya mambo mengi kuwalinda watu wake wasiwe na shida, na wakati wa utawala wake unakumbukwa kuwa wakati wa neema katika nchi, lakini wema alioufanya ulilipwa uovu. Mara Mrumi mtoto wake alipotoka jandoni akafanya shauri la kuutwaa utawala na vijana wengi wa hirimu yake walipatana naye. Tena wazee wengine walikuwa upande wake kwa sababu walimwonea chuki Marengo kwa kuwa aliwashurutisha kuwapa watu maskini ng'ombe wao wengine ili wasiwe na shida. Basi, Marengo alipoona ya kuwa watu wanaomfuata Mrumi mwanawe wamezidi, alimkimbilia Masaki wa Kilema. Mara ile, Masaki aliingia nchi ya Kirua, na ingawa kwanza alirudishwa nyuma, lakini alipata msaada wa Wagweno, wakawashinda watu wa Kirumi, na Kirumi na watu walio wengi walikimbilia kwa Salia mkuu wa Moshi.
Baada ya hayo, Marengo aliona ya kuwa hapana watu wanaomfuata, akaona ni vizuri zaidi kumweka Leminyi mwanawe awe mkuu wa nchi. Leminyi alikuwa amekimbilia Machame wakati alipotawala Mamkinga, na Marengo akashika njia yake kwenda kumleta, lakini alipokuwa akipita katika nchi ya Moshi alikamatwa akarudishwa Kilema. Basi, sasa watu walimwonya ya kuwa watamwua asipokubali kujiuzulu na kumweka Kirumi mwanawe awe mkuu, na hivyo ikawa hana budi kukubali.
Wakati huo wote, mkuu mwenye haki ya Kirua alikuwa Masaki, lakini sasa amani iliyofanywa kati ya Marangu na Kilema ilivunjika, na siku za maisha yake zilizosalia zilikuwa za vita alivyofanya na Ndaalio. Vita hivi vilianzishwa namna hii;- Mwizi aliyejulikana sana alikuwa amekamatwa akiiba katika Marangu, na watu wakamfukuza mpaka Kilema, na huko wakamwua. Basi, tendo hili lilikuwa kama kudharau nguvu ya mkuu wa Kilema katika nchi yake mwenyewe, ikawa fitina kuzuka. Watu wa Kilema walianza kuibaiba ng'ombe za watu wa Marangu, na watu wa Marangu waliibaiba ng'ombe za watu wa Kilema, na mambo haya yakaendelea hata yakawa kama vita vya chini chini. Kweli, wakuu wawili wa nchi zile hawakutoa ruhusa mambo hayo yatendeke, lakini hata hivyo walikuwa kama wametoa ruhusa kwa sababu walikubali kupokea sehemu za mateka yaliyotekwa. Wakati huo ilikuwa desturi ya vita ya kuwa wanawake wasidhuriwe, ila watembee-tembee bila hofu; lakini sasa ikawa wanawake wengine kuuawa katika safari zile walizofanya za kuiba ng'ombe. Basi, Masaki alitambua ya kuwa mambo hayo ni mabaya kuliko vita vya wazi, akamwambia mkuu wa Marangu ajifanye tayari kwa vita, akaingia Marangu. Marangu. Lakini alishindwa akafukuzwa. Basi, hapo watu wa Marangu waliingia katika nchi ya Kilema, nao vile vile walishindwa na kufukuzwa. Basi, vivyo hivyo vita vikaendelea, wala hapana upande mmoja ulioshinda. Sasa Masaki alipata msaada wa askari kwa mkuu mmoja wa Wataita, na askari hao walifanya hasara nyingi katika jeshi la Marangu, maana walitumia mishale yenye sumu, na kwa hivi wakaweza kufanya hasara nyingi kuliko watu wa Kichaga. Lakini Masaki hakupata faida nyingi katika vita hivi, maana Wataita walikataa kushambulia tena kwa kuwa wamekwisha kupata mateka waliyotaka, tena habari walizochukua kwao juu ya utajiri wa nchi ya Kilema ziliwafanya Wataita wengine wakubali kumsaidia Ndaalio. Ikawa Kilema kuingiliwa tena, ikatekwa, na Wataita wakarudi kwao tena. Masaki aliwakaribisha tena Wataita waje kumsaidia, na Ndaalio akafanya vile vile, ikawa Wataita wakaja wakapigana kila upande, wakateka mateka mengi wakarudi kwao tena, na kwa hivi hakuna mkuu mmoja aliyepata faida katika vita walivyofanya wakuu hao wawili, ila Wataita.
Masaki aliwakaribisha Wataita waje tena kumsaidia, na safari hii Ndaalio aliwakaribisha Warombo na Wataita wengine waliokuwa wakikaa karibu na Taveta, waje. Hao Wataita walikuwa askari mashuhuri, na wengine wao walikuwa na bunduki. Basi, walipigana, mkubwa wao akauawa, na mara Wataita walijitoa katika vita, na Wamarangu walikuwa hawana budi kurudi nyuma pia. Vita hivi vilikuwa vya mwisho. Nchi zote mbili zilikuwa zimechoka, mali zimekwisha, na watu wakawa maskini kabisa, wala hakuna upande mmojawapo uliopata faida hata kidogo. Basi, katika msiba huu uliowapata, kwanza Masaki aliwakusanya watoto wa kike akawaamuru kupanda kilima kiitwacho Ngangu na kuwalaani adui zao, kisha, Ndaalio naye aliwakusanya watoto wa kike wote wa nchi yake nao wakafanya vile vile. Tendo hili lilikuwa mwisho wa vita, maana watu waliona ya kuwa ni tendo la kuogofya sana, wakasema vita lazima viishe. Baada ya muda kidogo kupita Ndaalio akafa, na baada ya muda kidogo Masaki naye alishikwa na ndui akafa, basi sasa misiba ya nchi zote mbili ilizidi.
Ndaalio alipokufa hakuacha mrithi ila ndugu zake wanne, na katika ndugu hao, Marangu na Kinabo ndio waliojulikana zaidi baadaye. Hapana mmoja katika ndugu hao aliyeonekana kuwa atafaa kuwa mtawala, na kwa hivi watu walimchagua Msanjo mama yake Ndaalio awe mkuu wao. Msanjo alikuwa mtawala mpole mwenye busara, akafanya mapatano na wakuu wote wa Vunjo, kwanza waondoe desturi iliyoitwa Kilya Shigu, na tena ya kuwa ni marufuku mkuu mmoja kujaribu kumwua mkuu mwingine. Lakini utawala wake haukudumu kwa amani. Wana wawili wa Masaki walikuwa wakikaa Kilema, ndio Seiya na Fumbo, lakini kwa kuwa walikuwa wadogo bado, watu walimchagua mtu jina lake Makindara atawale. Baada ya muda kupita Seiya alikufa, na watu walifikiri ya kuwa Makindara ndiye aliyemwua kwa uchawi, na kwa hivi aliuawa. Sasa Maambo nduguye alishika utawala, naye alikuwa mtu wa vita akawakaribisha Waarusha waje wamsaidie kushambulia Mamba. Lakini Waarusha wakaja wakateka nyara si Mamba tu, ila na Kilema pia, kisha, wakaenda zao. Sasa watu wa Kilema walifikiri ya kuwa wakimweka mkuu, hapo hapatakuwa na vita, maana haikuwa desturi ya mkuu kwenda vitani mwenyewe, na kwa hivi walifanya shauri la kumweka Fumba awe mkuu wao.
Maambo na wasaidizi wao Waarusha waliposhambulia Mamba, yule mwanamke mkuu Msanjo aliwapeleka askari zake katika nchi ya Mlawi wakawafukuza Waarusha, wakawaua wengi na kuteka ng'ombe waliowachukua. Baadaye Waarusha wakarudi wakaingia Marangu, na kwa kuwa wakati huo ndugu zake Ndaalio walikuwa wakishindana wao kwa wao, basi watu hawakujaribu kuwazuia Waarusha. Lakini hata hivi, askari walilinda nyumba ya Msanjo kwa hiari yao, na kwa hivi ingawa Waarusha waliteka ng'ombe wengi sana kila mahali, lakini ng'ombe za Msanjo walikuwa salama. Sasa ikawa ndugu zake Ndaalio kusema ya kuwa Msanjo alikuwa amefanya shauri na Waarusha waje kuteka ng'ombe za nchi, na ya kuwa nchi imepata hasara kwa sababu ilitawaliwa na mwanamke. Basi, kwa maneno haya waliyosema, watu wakaanza kumwasi Msanjo, na baadaye aliona afadhali akimbie, akakimbilia Msae. Lakini, watu walimfuata wakamwomba arudi pamoja nao. Ndugu zake Ndaalio waliendelea kushindana wao kwa wao juu ya nani atakayekuwa mkuu, ikawa Mlawi akafanya haraka akaja kumsaidia Msanjo. Watu wa Marangu wakamwambia Mlawi ya kuwa hawana nia ya kumdhuru Msanjo, waliyotaka ni yeye kumchagua mmoja wa ndugu zake Ndaalio awe mkuu wao. Basi, Msanjo alimchagua Kinabo, na Mlawi alimsaidia kumweka imara ingawa watu wengi hawakulipenda shauri hili.