SHINYANGA, 28 OKTOBA, 2010*
WAKATI mchakato mzima wa zoezi *la upigaji kura likifika ukingoni imebainika kuna vituo hewa vya kupigia kura vilivyoandaliwa katika Jimbo la Shinyanga mjini.
*
Hali hiyo isiyokuwa ya kawaida imewafadhaisha wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani kutokana na kutumika kwa baadhi ya majina ya wapiga kura wa vituo vingine kwenye vituo hivyo hewa.
*
Kutokana na kubainika kwa mapungufu hayo yenye kila sura ya kuvuruga au kuiba kura katika zoezi la uchaguzi wa Oktoba 31, baadaye wiki hii Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Shinyanga kimemwandikia barua msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika jimbo la Shinyanga.
*
Kituo kimoja kati ya vitu vilivyothibitishwa na waandishi wa habari kubeba mapungufu hayo ni kile cha namba 00018940 cha Chekechea Misheni ambapo wapiga kura walioorodheshwa katika daftari la kupigia kura kwenye kituo namba tatu majina 264 yamerudiwa kuandikwa pia katika kituo namba mbili jambo ambalo limewashangaza wengi na kuweka dhana ya kuwepo kwa vituo hewa katika orodha ya Tume ya Taif ya Uchaguzi (NEC).
*
Baadhi ya majina yaliyobainika kuandikwa mara mbili katika vituo tofauti ni yale yanayoanzia na herufi MW mpaka ZU katika kituo namba tatu kikiwa na wapiga kura 334 na yale yanayoanzia herufi KE mpaka ZU katika kituo namba mbili chenye idadi ya wapiga kura 494.
*
Baadhi ya majina yaliyobinika kubeba udanganyifu huu ni pamoja na Bi. Veronica Paulo Nyanda mwenye shahada namba 11037634, Bi. Veronica Michael Shigulu (11061105), Bi. Veronica Philipo Alphonce (46588250) na Bi. Veronica Philipo Massawe (11042211) yakiwa yameandikwa kituo namba mbili na pia kuonekana kama yalivyo katika kituo namba tatu.
*
Wakati huohuo Katibu wa CHADEMA mkoani Shinyanga, Bw. Nyangaki Shilungushela akizungumzia hali hiyo alisema kitendo hicho kimewapa wasiwasi kuwa kuna mpango muovu wa kuchakachua kura au kuongeza idadi ya kura hewa mara baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika kwa kutumia namba na idadi ya wapiga kura vituoni ambao majina yao yameandikishwa mara mbili.
*
Alisema tayari wamekwisha kumwandikia msimamizi wa uchaguzi kulalamikia kitendo hiki kinachoonesha kuna vituo hewa vilivyoandaliwa.
*
Hali hii imejitokeza hapa mjini je, huko vijijini hali ikoje ambako wananchi wengi si wafuatiliaji wa mambo? alihoji Shilungushela.
*
Kwa upande wake msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika Jimbo la Shinyanga mjini, Bw. Festo Kangombe amekiri kuwepo kwa hali hiyo na kueleza kuwa tayari ofisi yake imeishawasiliana na NEC ambao wanashughulikia tatizo hilo kabla ya siku ya upigaji kura.
*
Alisema baada ya kubaini mapungufu hayo hawakuwa na jinsi ya kufanya bali kubandika majina hayo vituoni kama yalivyo ili kuwatendea haki watu wengine ambao majina yao hayakuwa na matatizo ya kujirudia kweenye orodha.
*
Ni kweli tatizo hilo lipo hata sisi tulilibaini mapema, lakini tayari tumeishawasiliana na Tume ya uchaguzi ambao ndiyo wenye dhamana na daftari hilo la wapiga kura, hivi sasa wanalifanyia kazi, na marekebisho yatafanyika kabla ya siku ya upigaji kura, lakini hata siku hiyo patakuwepo na watu maalum wa kutoa maelekezo, alieleza Bw. Kangombe.
*
Kama itashindwa kufanyiwa marekebisho, ambayo hakuna shaka kuwa yatahitajika baada ya kuchunguza pia vituo vyote vya kupigia kura nchini, hii itakuwa kashfa ya aina yake kwa NEC ambayo itaondoa imani ya wananchi na hata Mataifa kwa NEC.Mwisho