Mtoa Taarifa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2024
- 213
- 671
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) unawataarifu watumiaji wa kivuko MV. CHATO II HAPA KAZI TU kinachotoa huduma katika maeneo ya Chato, Mharamba, Izumacheli na visiwa vya jirani kuwa, kivuko hicho kimesimama kutoa huduma kuanzia majira ya saa nne na nusu asubuhi kutokana na kunasa kwa nyavu katika mitambo yake ya uendeshaji, nyavu hizo ni zile zinazotegwa na wavuvi wanaofanya shughuli za uvuvi wa samaki katika maeneo ambayo kivuko husika kinatoa huduma.
Wazamiaji wetu tayari wamezamia chini ya kivuko na wanaendelea na zoezi la uondoaji wa nyavu hizo ili kurejesha huduma ya kivuko husika na baada ya kumaliza zoezi hilo huduma za uvushaji abiria zinatarajiwa kuendelea kama kawaida.
TEMESA inawaomba abiria wote kuwa watulivu na wavumilivu wakati zoezi la kuondoa nyavu hizo likiendelea. Aidha, inawakumbusha wavuvi wanaofanya shughuli za uvuvi Ziwa Victoria ambalo vivuko vinatoa huduma kuacha kutega nyavu hizo katika njia za vivuko kwani ni uvunjifu wa sheria na inasababisha uharibifu wa mifumo ya uendeshaji wa vivuko na usumbufu kwa watumiaji wa huduma za vivuko.
TEMESA pia inawaomba radhi abiria kutokana na changamoto iliyojitokeza na inawakumbusha kuendelea kufuata maelekezo ya mabaharia wakati wote wanapotumia vivuko ili kuendelea kuwa salama.
Imetolewa na Kitengo cha Masoko na Uhusiano
TEMESA
04/12/2024