Winga anayeteleza Mrisho Ngassa alifunga kwa mara ya pili katika michuano ya Chalenji wakati bao lake la pekee lilipoiangushia Burundi kipigo cha tatu mfululizo katika mechi zote tatu, na kuipeleka Kilimanjaro Stars katika robo fainali.
Ngassa, ambaye bao lake pekee liliizamisha Zanzibar Heroes katika mechi ya 'ndugu wa damu' Jumanne, alikuwa nyota tena jana wakati alipomalizia vyema kazi nzuri iliyofanywa na Juma Nyosso aliyempa pasi safi Mussa Hassan 'Mgosi' aliyempasia mfungaji.
Katika mechi ambayo Stars ilitawala mchezo katika kipindi cha kwanza kabla ya kugeuziwa kibao kipindi cha pili hasa baada ya goli hilo lililofungwa katika dakika ya 48, wachezaji wa Kili Stars walicheza kwa tahadhari kubwa wakijua hatma yao imeshikwa na timu hiyo iliyokuwa na hasira za kufungwa mechi zote mbili za kwanza.
Wakati dakika 45 za kwanza zilipomalizika, ubao wa matokeo ulisomeka 0-0 na kipindi cha pili kilipoanza iliwachukua Kili dakika tatu tu za kwanza "kucheka" na nyavu.
Burundi waliokuwa tayari wametolewa katika michuano hiyo walionekana kucheza bila ya "presha" na waliliandama goli la Kili Stars kama nyuki na kama si kukosa umakini kwa Geterethe Dizina, mambo yangekuwa tofauti.
Akiwa katika nafasi ya wazi ya kufunga huku wenzake wakijiandaa kushangilia goli la kushawazisha katika dakika ya 89, Dizina alipiga kichwa nje mpira wa krosi 'tamu' aliyotumbukiziwa na Nahimana Cloud wakati kipa wa Kili Mwarami akiwa katika nafasi ambayo asingeweza kuokoa.
Licha ya kutawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza, Burundi ndio waliokuwa wa kwanza kubisha hodi langoni kwa Kili baada ya mshambuliaji Didier Kayumbagu kukosa goli la wazi kwa kupiga shuti pembeni dakika 2 tu tangu mechi ianze.
Hata hivyo, Stars ilijibu mashambulizi dakika mbili baadaye wakati shuti la Danny Mrwanda lilipotua mikononi mwa kipa wa Burundi Vladimir Niyonkuru.
Dakika ya 5 Ngassa alikosa goli baada ya kuwatoka mabeki wa Burundi na kupiga shuti lililopaa juu ya goli kabla ya Burundi nao kukosa goli katika dakika ya 12 wakati Abdulrazak alipopiga shuti pembeni wakati goli likiwa wazi baada ya kipa wa Kili Stars Mwarami Mohammed kuangukia upande wake wa kushoto.
Kwa ushindi huo Kili Stars imetinga hatua ya robo-fainali pamoja na Uganda, Zambia na Rwanda, na hata kama Zanzibar Heroes itaifunga Uganda katika mechi ya kufunga Kundi C, Bara itasonga mbele kama mshindi bora wa tatu.
Timu 2 kutoka katika kundi miongoni makundi matatu ya michuano hiyo zinaingia moja kwa moja hatua robo-fainali na timu mbili zilizofanya vizuri zaidi zitaungana na timu hizo ili kukamilisha idadi ya timu nane zitakazocheza robo-fainali.
Zambia ilimaliza kwa kishindo jana baada ya kushinda 6-0 dhidi ya Djibouti, ambayo ilifungwa 5-0 na Ethiopia kabla ya kuchapwa 2-0 na wenyeji Kenya katika Kundi A. Zambia imeshinda mechi zote tatu ikiwa imefunga magoli 9 huku ikiwa haijafungwa hata goli moja.
CHANZO: NIPASHE
sasa watanzania tusahau yote ya nyuma tumumpe support maximo.
excessive criticism is not helpful