Kongole sana Muleba Ibin Kagera kwa kujisimamia vizuri

Kongole sana Muleba Ibin Kagera kwa kujisimamia vizuri

Mohamed Ismail

JF-Expert Member
Joined
Mar 16, 2014
Posts
224
Reaction score
236
Anaandika Mo Mlimwengu.

Wakati tunasoma shule kuna watu walikuwa hawana juhudi za kuzingatia masomo na wengi wao walikuwa ni watoro hata darasani. Walikuwa na nidhamu mbaya kwa walimu wao. Lakini ilipofika kipindi cha matokeo wote walikuwa makini kufuatilia matokeo yao. Na walivyopata matokeo mabaya walikuwa na visingizio kibao. Wengine wataishia kusema baraza la mitihani halina usawa, wengine wanapendelewa watoto wa walimu na wengine waliishia kusema wamerogwa. Nani alikuambia ukipanda bangi utavuna mchicha. Yote ni kuonyesha kila mtu anataka mambo mazuri.

Wakati Rais wetu Dr Samia Suluhu Hassan akiwa Mwanza akihitimisha mbio za Mwenge. Ilikuwa ni sherehe kubwa, tulishuhudia burudani za kutosha na sherehe hizo ziliambatana na kutolewa zawadi kwa watu ambao walifanya vizuri kwenye kusimamia miradi kwenye maeneo yao. Kazi ya mwenge ni kumulika ndani na nje ya mipaka yetu na usiishie kumulika tu uwe ni ishara ya kuleta amani, upendo na utuondolee dharau na chuki.

Muleba ni wilaya iliyoongoza kwa kufanya vizuri kwenye usimamizi wa miradi lakini haikuishia hapo na Kagera ukawa mkoa ambao umeongoza kwa kufanya vizuri. Kumbe mchuma janga hula na wa kwao. Kitendo cha pongezi hizi kutolewa na Rais wetu imekuwa furaha kwa wana Muleba wote na wana Kagera wote. Kuna furaha mtu unaipata kuona nyumbani kwenu kunasemwa kwa mambo mazuri. Mlimwengu mimi sikubahatika kuwa Mwanza lakini nilikuwa kwenye TV sambamba na waliokuwa uwanjani kushuhudia hitimisho la Mwenge.

Niliona Mkuu wetu wa mkoa akiwa na furaha furi furi isiyo na kifani akiwa uwanjani. Nikamshuhudia DC wetu pamoja na Mkiti wa Halmashauri wetu wakiwa na tabasamu pana kupokea tuzo mbele ya Rais. Nilifurahi mno kuna mtu nilkuwa nimekaa naye karibu ambaye siyo mwenyeji wa Kagera. Niligeuka ghafla kuwa mkalimani na kumuambia hizi zawadi zinatolewa wilayani kwetu. Nikamuambia huyu ni DC wangu nyumbani na nikamuambia na hayo mazuri wanayopongezwa nayo yamefanyika nyumbani.

Kwenye simu zetu za smartphones nilishuhudia wakazi wengi wa Muleba kwenye whatsapp status wamejaza picha za viongozi wetu wakiwa wamebeba tuzo. Ni shayiri dhahiri watu wanapenda mambo mazuri ndani ya wilaya zao na mikoa yao. Hizo tuzo hazikutolewa kwa mkandarasi, hizi tuzo hazikutolewa kwa wananchi. Hizi tuzo zilitolewa kwa viongozi ambao wamepewa mamlaka ya kutusimamia. Ndio maana inapotokea ndivyo sivyo na hao ndio huwa tunawapa lawama. Nilifurahi kuona viongozi wangu wa Chama nao wakifurahia tuzo hizo.Kwa sisi tuliopitia masomo ya ualimu tulifundishwa kutolewa kwa tuzo au pongezi huwa ni kuhamasisha mtu aendelee kufanya vizuri ili na wakati mwingine afanye vizuri zaidi ya alichofanya mwanzo.

Mwisho naomba niwapongeze viongozi wote wa Mkoa wa Kagera na hususani wilaya ya Muleba. Lakini nitakuwa mchoyo wa pongezi kama sitawashukuru zaidi wananchi wa Muleba ambao wamekua chachu ya maendeleo ya wilaya yetu. Ukifanya vibaya utakosolewa na ukifanya vizuri utapongezwa na hii imepelekea watu wawe na nidhamu ya utendaji wa kazi katika maeneo yao. Na hii ndio maana yangu ya kusema pongezi kwa Muleba ibin Kagera kwa kujisimamia vizuri. Na hii ndio maana ya Muleba itajengwa na wana Muleba wenyewe.

NB: Zile Takwimu za kwamba Mkoa wetu uko nyuma kiuchumi. Hii nayo inatuumiza sana. Tuna hamu sana ya kupokea tuzo nyingine ya Mkoa ambao umepanda kwa kasi kiuchumi.
 
Back
Top Bottom