SoC02 Kubadilishwa mfumo wa elimu wa Tanzania

SoC02 Kubadilishwa mfumo wa elimu wa Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

M GABAGAMBI

New Member
Joined
Oct 2, 2020
Posts
2
Reaction score
1
Upo umuhimu mkubwa sana wa kubadilishwa mfumo wa elimu ya hapa nchini Tanzania kutokana kwa asilimia kubwa kutokidhi mahitaji ya jamii ya Watanzania wengi. Kwa kawaida elimu ya hapa nchini Tanzania imekuwa ikianzia kuanzia chini mpaka elimu ya juu, yaani shule za awali, shule za msingi, shule za sekondari, vyuo vya kati pamoja na vyuo vikuu.

Kila mwaka wanafunzi wakihitimu katika fani mbalimbali kwa ambao walifanikiwa kujiunga na vyuo vya kati na vyuo vikuu, lakini wanafunzi wengine ambao ni kundi kubwa wamekuwa wakihitimu elimu ya msingi na elimu ya sekondari na kushindwa kuendelea; yaani kutofikia kiwango cha ufaulu pia vile vile wapo ambao wamekuwa wakiacha shule pamoja na utoro kwa kiwango kikubwa kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili.

Wahitimu wengi ambao wamepata ujuzi katika vyuo vyetu vya ndani ya nchi ya Tanzania wamekuwa hawana sifa katika soko la ajira ndani na nje ya nchi,mbali na kujiajiri wao binafsi kwa sasa kimbilio lao kubwa limekuwa katika kujishughulisha kwenye shughuli za bodaboda, vibarua wa ujenzi, vibarua wa kufyatua tofali, mama ntilie, machinga, udalali, utapeli wa mtandaoni, kuosha magari, kupiga debe kwenye vituo vya mabasi ambapo wamekuwa wakijipatia kipato kisichokidhi mahitaji ya binafsi na pia hawalipi kodi kwa serikali.

Lakini pia lipo kundi kubwa ambao wamekuwa wakitumika kama vibaraka na wawekazaji wakigeni na wafanyabiashara wakubwa na kulipwa malipo kidogo na wengine wamekuwa wakitumika kwenye kufanya biashara zisizo za halali.

Madhara yake vijana wengi wamekuwa katika wimbi la kutokuwa na ajira kabisa na hata ambao wapo kwenye ajira kipato au mishahara yao ni midogo hivyo pia na hao wamekuwa wakishindwa kumudu majukumu ya familia zao hata wengine wamekuwa wakitelekeza familia na kukimbia majukumu, Kitu ambacho nguvu kazi ya taifa imekuwa ikipotea bure na hata hivyo vijana wengi wamekuwa katika kipindi cha kukata tamaa na kujihusisha na vitendo haramu.

Lengo la elimu hapa nchini Tanzania ni kuwawezesha vijana kujitegemea na kupata maendeleo ya kifikra na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Lakini imekuwa ndivyo sivyo kwa vijana wengi ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya kati,kwa asilimia kubwa vijana wanashindwa kuliletea maendeleo taifa la Tanzania na hivyo nguvu kazi zao zimekuwa faida kwa wageni, wageni ambao wenye mitaji mikubwa ya kifedha na kimawazo wamekuwa wakiwatumia vijana wa kitanzania na kuwaacha katika wimbi kubwa la umasikini ulio kithiri.

Miradi mikubwa ambayo ikiendeshwa hapa Tanzania kwa asilimia kubwa ni miradi ya wageni kutoka nje ya taifa la Tanzania, lakini pia imekuwa ikiendeshwa na watendaji wa kigeni kwa mfano miradi ya ujenzi, miradi ya kifedha (yaani taasisi za kibenki), miradi ya mawasiliano, miradi ya Afya, miradi ya kimazingira, miradi ya kilimo, miradi maji na umwagiliaji, miradi ya nishati hata pia katika michezo na burudani.

Kwa asilimia kubwa wawekazaji wakigeni wamekuwa wakiwatumia vijana wa kitanzania kama ndio soko lao la vifaa na teknolojia ambazo wamekuwa wakizivumbua na kutengeneza, kuanzia nishati, usafirishaji, burudani na michezo, bidhaa za kilimo.

Watanzania wachache ambao wamesoma shule za gharama ndani na nje ya nchi ndio wameweza kushika nafasi chache katika nafasi za juu katika makampuni na taasisi kubwa.

Lakini pia ni Watanzania wachache sana ambao wameweza kuanzisha miradi na taasisi kubwa zenye kuliletea maendeleo taifa la Tanzania.Wengi wao hao walioanzisha miradi mikubwa tegemeo lao kubwa ni kutoka kwa wafadhili wa kigeni,kusudi waweze kuendesha miradi yao.

Kwa kiwango kikubwa lengo la elimu tangu tulipopata Uhuru wa nchi yetu ya Tanzania bado hatujaweza kulifikia mpaka sasa. Japo serikali ya Tanzania imekuwa ikitenga bajeti ya mabilioni ya pesa katika sekta ya elimu lakini ni wasomi wachache sana ambao ndio wanaweza kujitegemea na kuiletea nchi ya Tanzania kwa kiwango kidogo sana ukilinganisha na nchi za ulaya,marekani, pamoja na Asia.
Imekuwa kawaida sana kwa miaka hii ya sasa (2000 na kuendelea) kwa mwanafunzi wa shule ya msingi kuhitimu darasa la saba bila kujua kusoma,kuandika na kuhesabu kwa lugha ya kiswahili.

Tathimini ya haraka elimu ya Tanzania imekuwa ikizalisha watu ambao ni wanasiasa wasiokuwa na tija katika maendeleo ya taifa la Tanzania. Kwa takribani mawazo au fikra na ndoto za wahitimu wengi wa vyuo ni kuwa wanasiasa wakiamini maisha mazuri na ya mteremko yapo katika siasa, hata hivyo tumejionea baadhi ya wanasiasa na viongozi wengi wa umma wamekuwa wakiingiza taifa la Tanzania katika kusaini mikataba mibovu na ya hovyo isiyokuwa na tija kwa taifa, wizi wa mali na fedha za umma, ubinafsishaji wa makampuni na viwanda vya umma, rushwa pamoja na kung'ang'ania madaraka,wenye kuliletea hasara taifa na kurudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi.

Ni vyema tukawa na elimu ambayo itakayo mwezesha kila mtu kujiajiri na kufanya kazi kwa weledi katika soko la ajira na kuweza kujitegemea na kupata maendeleo kwa kiasi ambacho kitapunguza ukali wa maisha kama ilivyo kwa sasa ukilinganisha na elimu ya sasa ambapo inaonekana kama ndicho chanzo cha umasikini. Kwa vile kuwepo kwa miaka mingi ya kusoma na kukaa darasani baada ya kuhitimu elimu, ajira hakuna na mhitimu anashindwa kujiajiri.

Wakati familia na serikali inatumia gharama kubwa kumsomesha mwanafunzi na pia muda mwingi amekuwa akiutumia akiwa shule na mwishowe kuhitimu bila na kuwa na sifa kwenye soko la ajira au kuwa na ujuzi wa kumwezesha yeye mwenyewe kujiajiri, Kwahiyo mwisho wa siku kiwango cha umaskini kinazidi kuongezeka kwake binafsi,kwa familia na kwa taifa.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom