SoC03 Kudhibiti matukio ya watu kujitoa uhai nchini

SoC03 Kudhibiti matukio ya watu kujitoa uhai nchini

Stories of Change - 2023 Competition

Mkuki13

New Member
Joined
Jun 7, 2023
Posts
3
Reaction score
2
Miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya kikatili lakini pia kumekuwa na matukio mengi ya watu kujitoa uhai, kitu ambacho kinaleta taharuki kubwa katika jamii na nchi kiujumla. Katika hili andiko nitaongelea zaidi upande wa kujitoa uhai na afya ya akili.


Afya ya akili ni nini?

Vitu gani husababisha mtu kujitoa uhai?

Kutokujiamini, kujikatia tamaa, kuumizwa na watu uliowaamini na kujiona uko mwenyewe yaani hauna msaada wala thamani. Lakini pia kuna imani au destuli kwa upande wa wanaume kustahimili maumivu na kujikaza kiume, hii nayo inamaliza wengi. Wengi wanaofikia maamuzi ya kujiua wanakuwa wamekosa mtu wa karibu wa kuwakumbusha thamani waliyo nayo, pia kuwa ni sawa wakati mwingine kwenye maisha kupitia shida na kuomba msaada kwa watu wa karibu maana binadamu tumeumbwa kutegemeana.


Kutokana na hali ya maisha kumekuwa na

msukumo mkubwa na vishawishi kutoka vyanzo mbali mbali, ikiwemo mitandao ya kijamii na jamii kiujumla. Watu wengi hasa vijana tunaishi kwa kutizama maisha ya wengine, bila hata kutaka kujua wao wanafanya nini ili kuishi hayo maisha. Kila mtu anataka kuishi kama Jayzee na Beyonce lakini ana kipato cha dola 2 kwa siku. Hii hupelekea kujiona haufai, hauwezi, au si wathamani kabisa.

Ukosefu wa ajira na kutokujiongeza kwa vijana nako huleta hali ngumu ya maisha ambayo hupelekea msongo wa mawazo. Imani tulizoamimishwa kuwa ukifika miaka 30 lazima uwe umeowa na una familia nazo huwapa mawazo vijana wengi ukizingatia namna ambavyo dunia inaenda kiuchumi hii inatakiwa tubadirishe fikra zetu.

Ukiangalia sasahivi mitaani kila mtu ana biashara zinazofanana, akili zetu zimefika mwisho kubuni vitu vipya? Na bado kijana huyu aliyekwama kubuni kitu kipya cha kumuongezea kipato anaamini anatakiwa alete watoto duniani ambao kila mtoto atakuja na baraka zake, mchezo wa bahati nasibu. Mtoto huyo huyo akija na baraka zake unapata changamoto hujui ale nini au avae nini, mwisho unamuacha yatima na yeye apambane kiume kwanzia umri mdogo.


Namna gani unaweza kutambua mtu anayetaka kujitoa uhai?

Kwa kawaida si rahisi kufahamu ikiwa hauna ukaribu na mtu huyo. Watu wenye ukaribu zaidi wanaweza kujua kwa kuona mabadiliko katika tabia ya mtu huyo, na namna anavyoongea. Endapo mtu anayetaka kuondoa uhai wake atakuwa anapitia msongo wa mawazo basi ni rahisi zaidi kutambua ingawa kuna wakati unaweza kuhisi ni jambo dogo na litaisha. Utaona anakuwa ni mtu wa kulalamika hata katika jambo dogo, anakuwa ni mtu wa kulia mara kwa mara, hupoteza hamu ya kula, atapenda kujua kutoka kwa watu wake wa karibu kama ikitokea hayupo, je? Atakumbukwa, au kuenziwa? Na atapenda kubaki mwenyewe mara nyingi ili kupata nafasi ya kufikiria njia rahisi na upenyo wa kutimiza jambo lake. Huyu mtu pia ikiwa umemkosea haogopi kukuondoa uhai kwakuwa ana amini hakuna kilicho bakia kwa upande wake.


Jinsi ya kumsaidia mtu huyu?

Kwanza inatakiwa umpe nafasi ya kukuamini, usimlaumu kwa chochote na mruhusu kuongea ya moyoni. Onyesha umakini wa kumsikiliza. Baada ya kumsikiliza ni vizuri kuweza kutafuta kwanza msaada katika mamlaka husika kabla ya kwenda kumshitaki mtu huyu kwenye vyombo vya sheria. Kwasababu kwanza inabidi apatiwe msaada na wataalamu wa afya ambao utaweza kumrudisha katika hali yake ya kawaida. Lakini pia ili kurudi katika hali ya kawaida inategemeana na utayari wa mtu huyu maana mtaalamu atatoa maelekezo tu ya kumfanya ajione wa thamani, ajiamini na awe shupavu ili kuweza kukabiliana na hali ngumu kimawazo.

Unapompeleka mtu huyu kwenye vyombo vya sheria kabla hajapatiwa matibabu inaweza ikamuathiri zaidi kwasababu atahisi amesalitiwa, atajihakikishia kuwa kweli kumbe yeye hana thamani na pia hii inaweza kujenga chuki kwa watu wake wa karibu ambayo itampelekea kufanya vitendo vibaya kutokana na hali atakayoipitia akiwa ana adhibishwa.


Nini kifanyike kupunguza vitendo vya kujitoa uhai na kuimarisha afya ya akili?

Kwanza inabidi jamii kwanzia kwenye ngazi ya familia turudishe ushirikiano kama zamani. Tujenge tabia ya kusikilizana, ikiwezekana kila familia wapate muda angalau mara moja kwa wiki kuweza kuongea na kuambiana mambo yanayo msumbua kila mmoja na wajue namna ya kusaidiana, hii itapunguza kuweka vitu moyoni.

Kama wazee wetu walivyoishi kwa ujamaa na kuchukuliana iliwasaidia kuepuka vitendo kama hivi kwasababu hakuna mtu alijiona yuko mwenyewe nali kila jambo walisaidiana kulitatua kimawazo, kwa vitendo na mengineyo.

Leo tumezidisha utandawazi hadi maisha yamekuwa kama adhabu. Tukumbushane kila mara kuwa kila mtu ni wa thamani kwa nafasi yake na tuweze kuheshimu utafutaji wa kila mmoja, tutoke kwenye mifumo ya daktari, mhandisi, mwanasheria na wengine ndo wamuhimu kuliko machinga. Kila mmoja ana nafasi yake na umhimu wake katika jamii na serikali kiujumla. Pili, tuache tabia za kuiga maisha ya wengine na turidhike na ya kwetu kwakuwa haujui mangapi huyo unayemtamani anapitia, imemgharimu nini kufika hapo alipofika.

Maisha yana fumbo kubwa na siri nzito. Tatu, jamii hasa wazazi waelewe kuwa zama tunazoishi si sawa na walizoishi wao. Ni sawa kuwa na familia na watoto pale unapoona uko tayari na angalau kuna mwanga kwenye maisha yako.

Siku hizi hatuishi kwa kubahatisha bali kwa mipango, ndivyo dunia inavyoenda. Kwanini ulete watoto kwenye hali ambayo wewe binafsi haikufurahishi? Unatafuta watu wa kuteseka nao? Kuzaa bila maandalizi ni adui mkubwa wa mafanikio na ni chanzo cha kujilaumu, kujutia na msongo wa mawazo.

Nimeona watu wengi wakaribu wanavyohangaika sababu tu walizaa kwa kubahatisha, wengine wanatamani wangejua mapema ugumu wa kulea mtoto ukiwa haujajipanga lakini hakuna namna ya kumrudisha mtoto alikotoka inabidi wapambane.

Katika upande wa afya ya akili serikali inabidi iongeze nguvu kutoa elimu juu ya afya ya akili kwasababu wengi bado hawajui nini afya ya akili. Kuna jamii bado inaamini ni mambo ya ugaibuni lakini jamii hizo hizo zinaathiriwa sana na mambo haya. Elimu itolewe kuanzia ngazi za wanafunzi wa shule ya msingi na kuendelea, kwa kuwa vizazi vingine tayari vimekwisha kuathiriwa na mfumo wa wazee wetu mabadiliko yatakuja lakini yatachukua muda.

Lakini tukikazania vizazi vya chini itakuwa rahisi kufikia lengo kwasababu watakuwa katika mfumo mpya wa kufikiri na mitazamo mipya. Hivyo watakuwa ni wenye kujitambua, kujiamini na hii itasaidia kupunguza vitendo vya kikatili na kuimarisha afya ya akili kwa jamii zetu.

Upatikanaji wa huduma za matibabu na wataalamu wa afya ya akili urahisishwe katika vituo vya afya na pia yawepo makundi maalumu kwa ajili ya watu wasio na familia au watu wa karibu kukutana na kuelezeana shida zao kwa kuwa kuongea kunasaidia sana kupunguza machungu moyoni.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom