Kuna ukweli wowote kwenye hili kuwa kuketi kwa muda mrefu sehemu moja pasipo kutembea au kujishughulisha na kazi yoyote ni hatari kwa afya?
- Tunachokijua
- Afya ya binadamu inaweza kuimarishwa kwa kula mlo bora, kufanya mazoezi yanayoongeza utimamu wa mwili, kuepuka tabia hatarishi zinazoongeza nafasi ya kupatwa na magonjwa pamoja na kuweka mkazo kwenye afya ya akili.
Mambo haya kwa pamoja hupunguza mzigo wa kupatwa na magonjwa nyemelezi, huokoa pesa nyingi zinazoweza kutumika katika kurekebisha afya iliyoharibika kwa kufuata aina mbalimbali za tiba, huongeza nafasi ya kuishi umri mrefu zaidi pamoja na kuwezesha utekelezaji wa majukumu binafsi ambayo huchangia kuongezeka kwa pato la mtu binafsi na taifa kwa ujumla wake.
Kuketi kwa muda mrefu ni hatari kwa afya?
Baada ya kuanzishwa kwa mada hii na mdau, JamiiForums imezungumza na wataalam wa afya ya binadamu pamoja na kufuatilia tafiti mbalimbali za afya ambapo imebaini mambo yafuatayo;
- Ni kweli kuwa kuketi sehemu moja kwa muda mrefu pasipo kunyanyuka au kujishughulisha na jambo lolote linalokufanya uhame kutoka sehemu hiyo kwenda sehemu nyingine sio salama kwa afya.
- Huongeza nafasi ya kupatwa na magonjwa sugu
- Magonjwa yanayoweza kutokea huwa na athari nyingi kwa afya ikiwemo kutengeneza utegemezi, kushindwa kutekeleza majukumu ya kila siku au hata kusababisha kifo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyo ya kuambukiza huchukua uhai wa takriban watu milioni 41 kila mwaka duniani, kadirio la 74% ya vifo vyote duniani hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari mapema.
Ushauri
Uwapo ofisini au sehemu yoyote unayotumia muda mwingi kuketi, wataalam wa afya hushauri uzingatie mambo haya;
- Tembea kidogo kila baada ya dakika 30 za kuketi
- Simama unapokuwa unazungumza na simu au ukitaka kuangalia TV
- Tumia ngazi za kawaida kutembea badala ya kupanda lift kila mara
- Fanya mazungumzo na wenzio mkiwa sehemu ya wazi inayoweza kuruhusu matembezi kuliko kuketi kila mara ofisini