Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
KUKUTANA KWANGU NA "DEEP THROAT" WA MADINA, HANDENI 2014
Angalia hiyo picha hapo chini.
Picha hii nimeipiga miaka saba iliyopita siku kama ya leo.
Picha imeanza kwenye ndevu kuja chini hakuna sura. Hivi ndivyo mwenyewe alivyotaka.
Alitaka sura yake isionekane. Kwa nini anajificha?
Huyu bwana kaja nyumbani kwangu mimi simjui lakini yeye ananijua na nilipomuuliza ananijuaje jibu lake lilikuwa, "Nani asiyekujua Sheikh Mohamed?"
"Wewe nani ndugu yangu?"
"Usitake kunijua mimi nimeelekezwa kwako na Waislam ili nikuekeze mambo mazito yaliyowafika ndugu zetu vijiji vya Lalago na Madina Wilaya ya Handeni."
Pale pale mimi nikampa jina ndani ya nafsi yangu nikamwita, "Deep Throat."
Deep Throat ndiye mtu aliyetoa siri ya Watergate iliyomfanya Richard Nixon ajiuzulu urais wa Marekani.
Hili jina lilinijia haraka kwani wakati huyu Deep Throat wangu ananifikia na kuniambia ana habari za Lalago na Madina nchi ilikuwa katika msisimko na taharuki kubwa.
Taarifa zilikuwa zimezagaa nchi nzima kuwa katika baadhi ya vijiji Tanga kuna kambi za ugaidi, zinazomilikiwa na Al Shabab, kuna mahandaki ya vita na silaha za kutungulia ndege.
Deep Throat wangu alikuja kunipa ukweli wa taarifa hizi na akaniambia kuwa yeye ni mmoja wa vijana waliokuwa wanaishi Madina lakini kakimbia huko baada ya kijiji kuvamiwa na kupita operesheni ya kamatakamata wakisakwa magaidi.
Deep Throat wangu akaniambia huko alikotoka ni hatari kuwa na muonekano wa Kiislam hasa kufuga ndevu na kuvaa kanzu fupi.
Akaniambia kuwa mabasi yanasimamishwa njiani na askari ukionekana na muonekano usiofaa unashushwa na kuwekwa chini ya ulinzi.
Deep Throat wangu alinieleza mambo mengi ya mauaji na misikiti kuchomwa moto.
Mwisho wa mazungumzo akaniambia kuwa katumwa kuja kwangu ili nieleze ukweli kupitia kalamu yangu.
Nilimuomba Deep Throat kabla sijanyanyua kalamu yangu kuandika anipatie ushahidi zaidi wa picha na sauti za waathirika wakieleza haya yaliyowafika.
Deep Throat akaniambia Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bi. Chiku Galawa amezungumza na wananchi wa Tanga kuhusu hali ya usalama wa mkoa wake kupitia Radio Nur FM, na kaeleza mengi ya kutisha.
Ndipo katika kuagana kwa miadi kuwa atanipatia ushahidi nilioomba nikamuomba nimpige picha.
Deep Throat akaniruhusu kupiga ndevu zake na alipokuwa anaondoka namsindikiza nikaona kanzu yake iko juu ya fundo za miguu.