Kula huku kula gani, kula bila ya kunawa?
Kula huku kula gani, kula bila kupumua?
Kula huku kula gani, kula bila kuchagua?
Kula huku kula gani, vya watoto navyo mwala?
Kula huku kula gani, mikono yote miwili?
kula huku kula gani, mbona nyinyi si makuli?
Kula huku kula gani, mwala hadi pilipili?
KUla huku kula gani, vya watoto navyo mwala?
Kula huku kula gani, kula huku mwacheua,
Kula huku kula gani, na meno mmekenua,
Kula huku kula gani, huku mnajisheua,
Kula huku kula gani, vya watoto navyo mwala?
Kula huku kula gani, mwala huku mwavimbiwa,
Kula huku kula gani, na harufu mnatowa,
Kula huku kula gani, na jasho hilo mwalowa,
Kula huku kula gani, vya watoto navyo mwala?
Kula huku kula gani, mwagawiana sinia,
Kula huku kula gani, zamu mnajipangia,
Kula huku kula gani, mwala tena mwarudia,
Kula huku kula gani, vya watoto navyo mwala?
Kula huku kula gani, mnakula hadi mbegu,
Kula huku kula gani, mwayala hata magugu,
Kula huku kula gani, huku mwatuita ndugu,
Kula huku kula gani, vya watoto navyo mwala?
Kula mmeshakwishakula, sasa muda wa kulipa,
Vya wanetu mmekula, kulipa na mtalipa,
Mlidhani tumelala, wajanja mkatukopa,
Vya kwenu hatutavila, na kura hatutawapa!
Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
Naogopa kuwa ubeti wa mwisho hauwakilishi hali halisi kama beti nyengine zinanavyofanya.
Naogopa kuwa bado tutawapa kura zetu hao hao kwani si ndio tunaowaita mashujaa? Mashujaa hao ni kazi kubwatukia Richmong na Meremeta huku wakjiundia milo sasa hata maendeleo ya majimbo wao ndio wawe walinzi ili wateke vyao mapema.
Si tunawajuwa Tunaowaita Mafisadi lakini kwenye chaguzi "mashujaa wetu " wanakuwa mbele kuwaokoa.
Nionavyo mimi Vya wenetu wameshakula na hawana haja ya kutukopa kwani wanajuwa kuwa sisi ni mitaji yao na ikija 2010 tutawapa tena. Kwani hao mashujaa wetu si wao wanaomiliki makampuni ya kutunyonya mbona tunanyamaza kimya?