Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeutaka uongozi wa chama hicho wilayani Urambo na mkoani Tabora kuhakikisha kuwa Mbunge wa jimbo la Urambo Mashariki ambaye pia ni Spika wa Bunge, Samuel Sitta, anapita katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, wakati wa ziara yake ya siku mbili wilayani Urambo mkoani Tabora.
Rai hii mpya inayotoa sura mpya ya Mkamba ambaye alitoa kauli kali hadharani akisema wazi kwamba Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho ina ubavu wa kumdhibiti Sitta, baada ya kuelezwa kwamba kiongozi huyo wa Bunge alikuwa amekaripia kwa kuruhusu mjadala wa wazi bungeni unaoelezwa kujeruhi serikali na chama tawala. Makamba akiwahutubia wananchi wa jimbo la Urambo Mashariki kwa nyakati tofauti, Makamba, alisema kuwa wananchi wa jimbo hilo wakimchagua Sitta hawatakuwa wamefanya makosa.
Ni kwa kuona umuhimu wake wabunge kwa pamoja wakamchagua kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na juhudi zake za kuleta maendeleo ya jimbo hili
zinaonekana pamoja na ujasiri na msimamo wake wa uongozi katika kuliongoza Bunge, alisema Makamba.
Makamba alimtaja Spika Sitta kuwa ni bakora ya kuwapigia wapinzani, hivyo anastahili kuwa kiongozi kutokana na uwezo wake kielimu na busara alizonazo, na kwamba haitakuwa vyema kama wananchi na viongozi wa CCM mkoani Tabora na Wilaya ya Urambo wakimpoteza.
Aidha, Makamba alipata fursa ya kuzungumza na mama yake mzazi Sitta, Ajati Zenna binti Said (84), nyumbani kwa Sitta.
Katika mazungumzo hayo, Makamba alimwambia mama huyo kuwa watu wabaya wamekuwa wakiwachonganisha wakidai kuwa Makamba na Sitta ni maadui, madai ambayo aliyakanusha na kuyaita kuwa ni maneno ya kisiasa.
Akizungumza na viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata na tarafa, Makamba alisema kumpoteza Sitta watakuwa wamepoteza mtu wa thamani.
Awali Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora, Iddy Ally Ahamed na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa, Hassan Wakasuvi, walisisitiza umuhimu wa Sitta katika jimbo hilo kutokana na juhudi zake za kupigania maendeleo kwa wananchi wake.
Makamba alisisitiza kuwa wabunge wanaozunguka sehemu mbalimbali
wakihamasisha jamii kupiga vita ufisadi wanasitahili kuungwa mkono, kwani bila kulisimamia tatizo hilo halitakwisha na wananchi wataendelea kupoteza haki yao kutokana na kutopata haki stahili.
Hatua ya Mkamba kwenda katika jimbo la Urambo Mashariki na kumpigia debe Sitta imekuja wiki kadhaa baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kumkemea Sitta kwa madai kuwa analiendesha Bunge kibabe kutokana na kuruhusu mijadala inayokidhalilisha chama hicho na serikali yake.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho walipendekeza Sitta anyang'anywe kadi na kufukuzwa uanachama.
Baada ya kikao hicho, Makamba alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akitamba kuwa uamuzi wa NEC ulikuwa sahihi na kwamba chama hicho kina ubavu wa kumdhibiti Sitta kwa sababu aliupata wadhifa wa Spika kupitia CCM.
Sitta amekuwa akishutumiwa na baadhi ya viongozi wa CCM kutokana na kushirikiana na baadhi ya wabunge wa chama hicho wanaovalia njuga vita dhidi ya ufisadi nchini.
Msimamo huu mpya wa Makamba unaokana siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, kuzungumza na wananchi kwa kujibu maswali yao laive kwa njia ya televisheni yaliyoulizwa kwa simu za moja kwa moja, barua pepe na ujumbe mfupi wa simu za mkononi.
Katika maswali hayo, Kikwete alisema wazi kwamba hakukuwa na mkakati wowote wa NEC kudhibiti wabunge wapambanaji wa ufisadi.
Hivi karibuni pia taarifa zimetolewa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba nchi wahisani zimetaka maelezo kutoka CCM kama kweli limeamua kudhibiti Bunge ili lisiiwe na makali dhidi ya serikali. Wahisani hao wanahisi kuwa kukatwa kwa makali ya Bunge fedha zao wanazotoa kama msaada hazitakuwa salama.
CHANZO: NIPASHE