Mnabuduhe,
Nakunyambulia kutoka kitabu cha
Abdul Sykes:
''Nyerere alilipeleka tatizo hili kwa
Clement Mtamila, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya TANU.
Mtamila aliitisha mkutano wa Kamati Kuu nyumbani kwake mtaa wa Kipata na TANU ilijadili tatizo hilo. Miongoni mwa wajumbe wa kamati ile mbali na
Rupia na
Kambona walikuwa
Bibi Titi Mohamed na
Bibi Tatu bint Mzee. Kamati Kuu ya TANU ilimshauri
Nyerere ajiuzulu kazi ya ualimu. Tafarani hii ilitokea wiki chache tu baada ya kurudi kutoka Umoja wa Mataifa katika wiki za mwisho za mwezi Machi. Tarehe 23 Machi, 1955
Nyerere alijiuzulu ualimu. Ilikuwa adhuhuri
Nyerere alipokuja Dar es Salaam kutoka Pugu, akiwa si mwalimu wa shule tena. Inasemekana aliposhuka tu kwenye basi alikwenda moja kwa moja ofisini kwa
Abdulwahid katika soko la Kariakoo kumpasha habari rafiki yake.
Nyerere alikaa na
Abdulwahid katika nyumba yake namba 78 Mtaa wa Stanley. Baadaye kidogo
Nyerere alirudi kijijini kwake huko Musoma.
John Hatch alipokuja Dar es Salaam kwa mwaliko wa TANU
Nyerere alikuwa kwao kijijini. Tutaona hapo baadae kidogo jinsi mgeni huyu Mwingereza alivyomgutusha
Schneider Abdillah Plantan kuhusu TANU kuwashirikisha wanawake katika harakati za kudai uhuru.
Ilikuwa wakati
Nyerere yuko Musoma ndipo
John Hatch kutoka Chama cha Labour cha Uingereza alipokuja Tanganyika kama mgeni wa TANU. TANU ilifanya mkutano mkubwa sana Mnazi Mmoja na
Hatch akawahutubia wananchi. Inakisiwa takriban wanachama wa TANU na mashabiki wake jumla yao kiasi watu elfu ishirini walijitokeza kwenye mkutano huo.
Ali Mwinyi Tambwe alikuwa mkalimani wa
Hatch.
Denis Phombeah pamoja na katibu mkuu wa TANU,
Oscar Kambona vilevile walihutubia halaiki ile.
Hatch akiwa anaunga mkono ukombozi wa watu weusi aligundua kuwa TANU haikuwa na tawi la akina mama. Katika dhifa ya chai iliyoandaliwa na TANU kwa heshima yake,
Hatch alilieleza tatizo hili kwa
Schneider Plantan na
John Rupia.
Hatch alimwambia
Schneider kwamba ili kuwa na chama chenye nguvu TANU isiwaache akina mama nyuma.
Hatch alimwambia
Schneider kwamba huko Uingereza Chama cha Labour kilikuwa kimejikita kwa wanawake kama moja ya nguzo yake kuu.''
Kushoto: Bi Tatu bint Mzee, wa tatu Julius Nyerere, wa tano Bi. Titi Mohamed wakimsindikiza Nyerere safari
ya kwanza UNO 1955.
Kulia: Bi. Titi Mohamed, Clement Mtamila, Sheikh Suleiman Takadir na Julius Nyerere.
Mzee Mohamed
Wewe ni muongo sana, Nyerere ndie alikuwa rais wa TANU akiwa na uzoefu wa kimataifa akifahamiana na waingereza wengi na akiwemo John,
Nyerere ndie aliyeratibu na kuuleta ugeni huo Tanganyika, leo unasema alikuwa kijijini Mwitongo???
Aisee wewe ni muongo sijawahi kuona mzee wangu....
Hebu tujikumbushe hapa yaliyomo kwenye kitabu cha Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi.
_________________________________________________
Mwl. Julius Kambarage Nyerere, alipendwa na kuheshimika sana ndani na nje ya nchi. Mwaka 1985, aliamua kwa hiari yake mwenyewe, kuacha uongozi wa Taifa ili apumzike. Alizunguka nchi nzima kuwaaga Watanzania. Kwa mapenzi makubwa, wakampa zawadi za kila aina. Wananchi walionesha wazi huzuni waliyokuwanayo kwa uamuzi aliouchukua. Walimuaga wakilia machozi!
Kumbukumbu muhimu ni hutuba yake, ya kuwaaga Watanzania, ya ter. 5 Novemba, mwaka 1985, kabla hajastaafu Urais aliyoitoa mbele ya wazee wa Dar es Salaam:
Mimi nimeanza siasa na wazee wa Dar es Salaam, na wazee wa Tanzania. Nimeanza nao mapema sana, mapema kweli. Nilirudi kutoka masomoni, Uingereza, Oktoba 1952, miaka thelathini na mitatu (33) nyuma. Wakati huo nikiwa kijana mdogo wa miaka thelathini na kidogo hivi (ushee). Niliporudi, nikakubaliana na wamisionari hapo Pugu (sekondari), nifundishe shuleni kwao. Lakini, nikiwa shuleni Chuo Kikuu nilijua. Niliishaamua kwamba maisha yangu yatakuwa ya siasa. Niliamua hivyo. Nitafundisha kwa muda wa miaka mitatu, nione hali inavyokwenda na kuzoeana na wenzangu kabla ya kuanza maisha ya siasa.
Niliporejea nchini, hapo Oktoba, nikaenda Butiama. Januari, nikarudi Dar es Salaam. Nikaanza kazi. Nikataka kujua habari za African Association. Mzee Mwangosi, anakumbuka. Yeye ndiye aliniambia habari za African Association. Alishaniambia habari hizo, tangu nikiwa Makerere, Chuo Kikuu, nikiwa mwanafunzi.
Pale (Makerere), mimi na wanafunzi wenzangu tulianzisha chama kinachoitwa, Tanganyika African Welfare Association (TAWA), cha wanafunzi wa Tanganyika, mimi nikiwa katibu wao. Hapa tukaona mambo yanakwenda vizuri kidogo.
Tukaona kwa nini TAWA iwe ya wanafunzi peke yao na si Tanganyika nzima? Kwa hiyo, nikawaandikia baadhi ya watu, Tanganyika. Nikasema, jamani eeh, tumeanzisha chama, kwa nini msianzishe huko matawi ya chama hicho?
Ndugu Mwangosi akapata barua hiyo. Alikuwa miongoni mwa waliopata barua hiyo. Akaniandikia (nikiwa Makerere), akasema: “Wewe, kwa nini unataka kuanzisha chama kipya? Kipo chama. Kipo chama cha TAA (Tanganyika African Association).”
Kwa hiyo, la maana si kuanzisha matawi, maana Chama kipo na matawi yameenea. La maana ni kwamba hicho chama chenu mfute, na muanzishe tawi la Tanganyika African Association.
Hivyo ndivyo tulivyofanya. Kwa hiyo, mimi nikawa katibu wa katawi la TAA, hapo Makerere. Niliporudi Tabora, na kuanza kufundisha pale St. Marys (sasa inaitwa Sekondari ya Milambo), nikachaguliwa katibu wa TAA wa jimbo ambalo makao yake makuu yalikuwa Tabora. Ulipofanyika mkutano wa TAA mjini Dar es Salaam, nilihudhuria nikiwa mjumbe kutoka Tabora. Kwa hiyo, nilikuwa naijua Tanganyika African Association. Nilipokuwa ninaondoka kwenda Ulaya kusoma, nilikuwa nimeishaonja shughuli za TAA. Sasa niliporudi, baada ya kukaa Pugu siku chache, nikaja mjini Dar es Salaam. Nikauliza nani wanaongoza TAA? Nikaambiwa kuna jamaa mmoja anaitwa Abdul Sykes. Sasa ni marehemu. Abdul ndiye alikuwa katibu wakati huo. Nilipelekwa na Kasela Bantu, ambaye naye aliteleza-teleza na hatunaye hapa (kwenye mkutano). Kasela Bantu alikuwa mwalimu mwenzangu. Tulifundisha pamoja Milambo. Nilipokuja Dar es Salaam, nikakuta anafanya kazi Redio (Tanganyika Broadcasting Corporation). Ni Kasela Bantu aliyenipeleka kwa Sykes.
Wakati huo, mambo yalikuwa yanasinzia kidogo. Kwa muda mfupi mwaka ule, tukafufua-fufua, hasa kutoka Januari. Kufika Aprili, TAA ikafufuka. Tukafanya mkutano hapo, Anautouglou. Kwenye mkutano huu, wakanichagua kuwa Rais wao, wa TAA. Ninasema yote haya, kwa shukrani kwa wazee. Jamaa hawa walikuwa watu wazima wa Dar es Salaam, na mimi kijana mdogo, Mzanaki, na Kiswahili changu si kizuri sana―cha matatizo.
Nimekuja, natoka Ulaya, tena masomoni. Muda mfupi tu jamaa hawa wakaniamini haraka sana―katika muda wa miezi mitatu. Wakanichagua Rais wa TAA. Hapo ndipo nilianza shughuli mpya ya kuandika katiba ya TAA na kuipa madhumuni hasa ya shabaha ya kuleta uhuru.
Baada ya miezi kumi na mitatu (13), hapo mwaka 1954, tukaanzisha TANU. Jina hili lilipendekezwa na akina Abdul Sykes. Walikuwa wamelifikiria tangu zamani, walipokuwa askari vitani (Vita Kuu ya Pili ya Dunia) huko Burma. Miezi minne baada ya kuanza kazi Pugu, nikawa ninakuja Dar es Salaam, kwa miguu, kila Jumamosi. Baadaye, wazee wakanipa baiskeli, nikawa ninakuja mjini kukutana na wenzangu, kufanya mikutano.
Hivyo ndivyo tulivyofanya. Wazee wakaniamini upesi sana. Tukawa na uhusiano mkubwa sana. Wadogo wenzangu wengine walikuwa Abdul Sykes, Abass Sykes (mdogo wake), Dosa Aziz, (na wengine wengi) waliokuwa ni wazee.
Katika kuhutubia mikutano yangu, nilikuwa nikisema: “Wazee na Ndugu zangu!” Wazee hasa ndio walikuwa na mikutano ya awali ya TAA na TANU. Walikuwa na msimamo wa hali ya juu kabisa. Hawakuyumba hata kidogo. Vijana walikuwa na mashaka. Wengine walikuwa na vikazi vyao, waliogopa kuvipoteza. Nalo jambo lenyewe ni la hatari, la kuzungumzia uhuru! Unaweza ukakosa kazi, na wapo waliopoteza kazi. Wengine wakaacha kazi. Akina Rashid (Kawawa) waliona watoke kwenye shughuli hizo tuje tuungane katika chama.
Wazee wa Dar es Salaam, na baadaye wa nchi nzima, wakatuunga mkono, na kila nilipokwenda, watu wa kwanza walionielewa, walikuwa wazee.
Nilikwenda Songea mwaka 1955, mara baada ya kujiuzulu. Huko, wazee walinipokea na kunielewa. Nilianza safari za kuitembelea Tanganyika nzima. Nilikwenda Mbeya. Mkutano wangu, niliufanya na wazee kikundi kidogo cha wazee, ndani ya nyumba ya mtu.
Kwa mkutano huu wa Mbeya, wazee wakauliza: Unatafuta nini? Nikawaambia natafuta uhuru. Wale wazee, kwa sababu ya Vita vya Maji Maji, na wanakumbuka, kabisa. Wakaona, mimi ninatafuta jambo la hatari. Tulifanya mkutano wa makini kweli. Wakauliza: Wewe unawezaje kuleta uhuru? Wewe una njia gani kudai uhuru na usitiwe kitanzi na Waingereza? Tulielezana. Nikawaambia ninyi wazee, Waingereza wanawadanganya. Waingereza wametumwa na ule Umoja wa Mataifa, uliokufa (League of Nations), waje kuishika Tanganyika kwa muda tu; watusaidie, na wakati tutakapokuwa tayari, watuachie tujitawale. Waingereza wanafanya ujanja, hawasemi. Vita vimekwisha (vya Pili) na Umoja wa Mataifa mwingine, mpya (United Nations Organisation UNO), umewakabidhi Tanganyika kwa shabaha ileile. Sisi siyo koloni lao. Wamepewa dhamana tu.
Kwa hiyo, nikawaambia wazee, hakuna haja ya kumwaga damu. Tuwaseme tu! Tuwashitaki kwa waliowaleta hapa kwamba hawafanyi kazi yao, wamesahau kabisa!
Wazee wakauliza: “Eeh, inawezekana?” Nikasema, inawezekana. Kazi yetu ya kwanza, ilikuwa kuwaambia watu kwamba uwezekano wa kujitawala upo. Hilo lilikuwa la kwanza. Wazee walijua maana ya kujitawala. Walitamani kujitawala, lakini hawakujua waanzie wapi. Vijana hawakuwa na habari kwamba kujitawala kunawezekana. Kwa hiyo, kwa wazee sikuwa na matatizo. Wao hawakuwa na kazi, hawakumwogopa Mwingereza. Hawakuogopa kufukuzwa kazi. Baadhi walikuwa wafanyabiashara.
Mzee John Rupia (marehemu), alikuwa mfanyabiashara na kaidi kidogo. Aliwahi kutishwa na kunyang’anywa leseni yake ya biashara. Akaambiwa akiendelea kushirikiana na kijana mwenda wazimu (Julius Nyerere), atanyang’anywa leseni moja kwa moja. Rupia aliwajibu: “Potelea mbali!”. Nasema yote haya ikiwa njia ya kutoa shukrani kwa wazee na imani yao kwa vijana wakati huo.
Imani hujenga imani. Na mambo haya makubwa ya nchi, kama hayana baraka za wazee hayaendi. Magumu sana. Wanasema ngoma ya watoto haikeshi! Mimi nilipata baraka za wazee tangu zamani. Tangu awali kabisa.
Siku moja, Dosa akanifuata Magomeni (Dar es Salaam). Akasema: “Leo wazee wanakutaka.” Wapi? “Kwa Mzee Jumbe Tambaza. Wanakutaka usiku.” Nikasema, haya, nitakuja. Nikaenda. Nikakuta wazee wameshakaa; wameniita kijana wao kuniombea dua. Mimi Mkristo(u), wao Waislamu watupu. Wakaniombea dua za ubani. Tukamaliza. Tulipomaliza wakasema kuna dua pia za wazee wao. Basi wakanitoa nje. Tukatoka. Zilizomalizika, zilikuwa za Kurani. Sasa, zikaja dua za wazee, za jadi. Walikuwa na beberu la mbuzi. Wamechimba shimo. Wakaniambia simama. Nikasimama. Beberu akachinjwa, huku naambiwa, “Twining (Twainingi) umekwisha!” (Edward Twining alikuwa Gavana wakati huo). Ndipo nikaambiwa: “Tambuka!” Nikavuka lile shimo. Hapo nikaambiwa na wazee: “Basi nenda zako; tangu leo Twainingi amekwisha!”
Sasa mimi Mkristo(u), hao Waislamu. Na mimi mkorofi-korofi katika mambo haya (ya kutambika). Lakini, tulikuwa tunaelewana na wazee wangu hao. Kwa hiyo, nilitambuka pale na kuambiwa: “Nenda nyumbani salama. Twaining hawezi tena!” Wazee wangu wengine, wanakumbuka. Tulikuwa tunakwenda Bagamoyo (kwenye makaburi). Kwenye makaburi kule, tunapiga dua huko kwenye makaburi na wazee wangu.
Baadhi yetu mtakumbuka safari moja, jamaa wa Kenya, hawa akina Tom Mboya (marehemu), walishitakiwa. Tukasema tuwasaidie. Tuwasaidie vipi? Tukasema tufunge. Tukaomba nchi nzima kufunga siku hiyo. Tufunge! Tukafunga. Hakuna kula. Na siku ya kufunga, tulikuwa na mkutano Bagamoyo. Tukaenda huko. Tukafanya mkutano hadi saa 12 (za) jioni.
Baada ya mkutano, tukaenda nyumbani kwa Mzee Mohamed Ramia (marehemu). Hapa ndipo tulikuwa tumefikia. Mimi nikamuuliza mzee: “Sheikh, una Aspro?” Akajibu: “Kwa nini unataka Aspro?” Nikajibu kuwa kichwa kinaniuma kweli kweli. Akasema, S”ubiri.” Tulisubiri hadi saa ya kufuturu. Tukafuturu vizuri. Mzee Ramia, akaniuliza: “Bado unataka Aspro?” Nikajibu, “Kichwa sasa hakiumi!” Kumbe ilikuwa njaa. Nawaelezeni haya kwa sababu huko tulikotoka, tulishikamana sana. Tulishirikiana sana na wazee.
Nyuma ya pazia, Mwl. Nyerere amebeba alama muhimu na rekodi za kipekee duniani. Alama hizo zinamfanya kuwa binadamu wa kipekee kabisa Afrika katika Karne ya Ishirini na Moja ( 21), alama hizo ni:
Alizaliwa tar. 13 Aprili, mwaka 1922, Butiama na kufariki tar. 14 Oktoba, mwaka 1999, London, Uingereza. Ni Rais wa kwanza Afrika kuachia madaraka kwa hiari yake mwenyewe.
Ni Rais wa kwanza kuhama Ikulu na kwenda kuishi kwenye nyumba aliyoijenga kwa mkopo yake akiwa bado Rais.
Ni kati ya Marais aliyekuwa analipwa mshahara mdogo duniani, na pengine kati ya rais aliyewahi kulipwa mshahara mdogo barani Afrika mpaka sasa.
Ni Mtanganyika wa kwanza kusoma Chuo Kikuu nchini Uingereza, akiwa Mwafrika wa pili kupata Shahada nje ya Afrika: akisomea English, Political Economy, Social Anthropology, British History, Economic History, Constitutional Law, and Moral Philosophy.
Ni kiongozi aliyeisaidia China kuingia Umoja wa Mataifa na hutuba yake maarufu akisema kwamba,”Umoja wa Mataifa si serikali ya dunia, bali ni sehemu ambayo dunia nzima inakutana. Kwa hiyo, kumtoa China katika umoja wa mataifa ni kumtoa kuwa sehemu ya dunia.”
Ndiye mwanzilishi wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini (Anti Apartheid Movement), mwaka 1959, pamoja na Trevor Huddleston, nchini Uingereza.
Ni mmoja kati ya waanzilishi wa Umoja wa Afrika, 1963.
Amezisaidia nchi nyingi za Afrika kupata uhuru kuliko mtu mwingine yeyote katika historia ya ukoloni. Nchi hizo ni: Zambia (1964), Malawi (1964), Botswana (1966), Lesotho (1966), Mauritius (1968), Swaziland (1968) and Seychelles (1976) na baadae 1975, (Mozambique), (Angola), 1980 (Zimbabwe), 1990 (Namibia) na 1994 (South Africa).
Mwaka 2009, alitajwa na rais wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kama, Shujaa wa Waulimwengu Kuhusu Haki za Kijamii (World Hero of Social Justice).
Amepokea shahada mbalimbali kutoka Vyuo mbalimbali ambavyo ni: University of Edinburgh (UK), Duquesne University (USA), University of Cairo (Egypt), University of Nigeria (Nigeria), University of Ibadan (Nigeria), University of Liberia (Liberia), University of Toronto (Canada), Howard University (USA), Jawaharlal Nehru University (India), University of Havana (Cuba), National University of Lesotho, University of the Philippines, Fort Hare University (South Africa), Sokoine University of Agriculture (Tanzania) na Lincoln University (PA, USA).
Alipokea Tuzo ya Order of José Marti Cuba (1975), Order of the Aztec Eagle (Collar) Mexico (1975), Order of Amílcar Cabral, Guinea Bissau (1976), the Nehru Award for International Understanding (1976), the Third World Prize (1982), Order of Eduardo Mondlane Mozambique (1983), the Nansen Medal for outstanding services to Refugees (1983), Order of Agostinho Neto, Angola (1985), Sir Seretse Khama SADC Medal (1986), Joliot-Curie Medal of Peace (1988), the Lenin Peace Prize (1987), the International Simón Bolívar Prize (1992), the Gandhi Peace Prize (1995), Statesman of the 20th century by the Chama Cha Mapinduzi (2000), Order of the Companions of O. R. Tambo (Gold), South Africa (2004), Royal Order of Munhumutapa, Zimbabwe (2005), Most Excellent Order of the Pearl of Africa (Grand Master), Uganda (2005), Order of Katonga, Uganda (2005), National Liberation Medal, Rwanda (2009), National Liberation Medal, Rwanda (2009), Campaign Against Genocide Medal, Rwanda (2009), Order of the Most Ancient Welwitschi Mirabilis, Namibia (2010), Tanzania Professional Network Award (2011), Order of Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Tanzania (2011), National Order of the Republic (Grand Cordon), Burundi (2012) na Order of Jamaica, Jamaica.
Mwaka 2007, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alimpa tuzo ya Katongo ambayo ni Medali ya juu kuliko zote ya Jeshi la Uganda, kwa heshima ya upinzani wake dhidi ya ukoloni na serikali ya Idi Amin.
Mitaa, barabara, majengo, vituo, shule, vyuo na vitu vilivyopewa jina lake; Daraja la Nyerere Kigamboni, Julius Nyerere University of Kankan, in Kankan, Guinea, Nyerere Drive, Gaborone (1.6 km) in Botswana, Nyerere Avenue, Mombasa (1.5 km) na Nyerere Road, Kisumu (2 km) nchini Kenya, Julius Nyerere Street, Windhoek (1.1 km) nchini Namibia, Julius Nyerere Street, Durban (0.5 km) nchini South Africa, Nyerere Road, Kitwe (1.4 km) nchini Zambia, Julius Nyerere Way, Harare (1 km) nchini Zimbabwe, Julius Nyerere International Airport, Julius Nyerere International Convention Centre, Nyerere Day- Public Holiday (14/10), Nyerere Cup, Nyerere Road, Unguja, Zanzibar (6.5 km), Nyerere Secondary School, Mwanga District na J.K. Nyerere Secondary School, Moshi, Kilimanjaro Region, Mwalimu J. K. Nyerere Secondary School, Mbozi District, Mbeya Region, Nyerere Memorial School, Korogwe, Tanga Region, Nyerere High School Migoli Iringa Region, Nyerere Secondary School, Unguja, Zanzibar, Mwalimu Nyerere Foundation, Mwalimu Nyerere Museum Centre na Mwalimu Nyerere Memorial Academy- Tanzania.
Baadhi ya vitabu alivyoviandika ni, Freedom and Unity (Uhuru na Umoja), Freedom and Socialism (Uhuru na Ujamaa), The Arusha Declaration, Education for self-reliance, The Varied Paths to Socialism, The purpose is man, Socialism and development, Freedom and Development (Uhuru Na Maendeleo), Ujamaa, Crusade for Liberation, Education for Self-Reliance, Uongozi na Hatima ya Tanzania, na Tujisahihishe.
Pamoja na kujulikana kama Baba wa Taifa la Tanzania, Nchi za Kusini mwa Afrika zinamtambua kama Baba wa Ukombozi wa Nchi za Kusini.
Pamoja na kujua lugha ya Kiswahili na Kiingereza kwa Ufasaha, pia alifahamu lugha ya Kigiriki na Kilatini.
Julius Nyerere ameandikwa kwenye kitabu cha Enyclopidia kama mtu pekee duniani katika historia ya Karne ya 21, aliyeweza kuwafanya watu wa makabila, dini, asili na historia tofauti kujiona kama watu wamoja.
Binadamu pekee aliyeasisi Muungano wa aina yake duniani wa Tanganyika na Zanzibar (wa serikali mbili) na kisha kuikalia kijasusi Zanzibar kwa Nusu Karne.
Yote aliyoyaanza tangu utoto wake, makuzi yake, harakati zake, utuuzima wake, uzee wake, yalifikia kikomo tar. 14 Oktoba, mwaka 1999, alipoaga dunia kwenye kitanda cha Hospitali ya Mtakatifu Thomas, mjini London, alikokwenda kwa matibabu. Kabla hajafariki dunia, aliwakumbuka Watanzania wake akisema: “Najua nitakufa, sitapona ugonjwa huu. Ninasikitika kuwaacha Watanzania wangu, najua watalia sana. Lakini nami nitawaombea kwa Mungu.” Naam, Watanzania wake walilia sana, walipopata taarifu za kifo chake. Mwili wake ulipoletwa nchini, waliomboleza kwa uchungu mno. Mwl. Julius Kambarage Nyerere alizikwa kijijini kwake, Mwitongo Butiama, kwa heshima zote na wananchi wa Tanzania na wmataifa mbalimbali wakiwemo viongozi mashuhuri, waliokuja kwa ajili ya mazishi.
Ni dhahiri, msingi wa yale yote aliyoyaamini na kuyasimamia, utaendelea kudumu ndani ya mioyo ya kizazi chake, kizazi hiki na vizazi vijavyo kutokana na mchango mkubwa alioutoa akiwa muasisi na Baba wa Taifa katika kujenga taifa la Tanzania. Huyo ndiye mtoto aliyezaliwa siku ya mvua, na kupewa jina la mzimu wa mvua, KAMBARAGE; mwana wa Chifu, Nyerere Burito na Mgaya wa Nyang’ombe. Ni dhahiri, tar. aliyozaliwa 13 Aprili, mwaka 1922, Mgaya hakujua kwamba ajifungua mtoto ambaye angekuja kuwa kiongozi mashuhuri sana Afrika na duniani, aliyewapenda binadamu wote na kuwatumikia Watanzania kwa moyo wake wote, akili na nguvu zake zote.